Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Algeria: Darasa za bure barabarani

$
0
0

KATIKA maktaba yangu nina kitabu, kijitabu kwa hakika, chenye kufundisha namna ya kufanya mashambulizi ya kigaidi katika miji kwa lengo la kupindua serikali. Kinaitwa “Minimanual of the Urban Guerilla” na kimeandikwa na Carlos Marighella, mwanasiasa na mpiganaji wa vita vya mwituni wa Brazil aliyefariki Novemba 1969.

Na Ahmed Rajab

Marighella alikuwa mfuasi wa itikadi ya Kimarx na Kilenin. Alikiandika kijitabu hicho kwa Kireno muda si mrefu kabla hajafariki. Nilikinunua changu mara tu baada ya kuchapishwa tafsiri yake kwa Kiingereza 1970.

Alipokuwa akikiandika kijitabu hicho kulikuwa na msisimko miongoni mwa wanaharakati wa mrengo wa kushoto kote duniani pamoja na katika nchi za Kiafrika zilizokuwa zikitawaliwa na Ureno. Msisimko huo ulikuwapo pia miongoni mwa wanaharakati wa nchi za Ulaya.

Nchini Ufaransa, kwa mfano, wanafunzi na wafanyakazi walikwishaonyesha wanachoweza kufanya walipoitikisa serikali ya Rais Charles de Gaulle kwa maandamano na migomo mwaka 1968.

Che Guevara na nadharia zake zilikuwa zimewavaa vijana wa mrengo wa kushoto katika Ulaya na Amerika ya Kusini.

Che na Marighella walikuwa na lengo moja lakini walishauri matumizi ya mbinu tofauti za kuleta ukombozi. Che akitaka mapigano ya ukombozi yafanywe katika sehemu za mashambani, vijijini. Marighella, kwa upande wake, akishauri yafanywe katika miji. Na ndio maana kijitabu cha Marighella kikipendwa sana na wanaharakati wa Ulaya.

Siku hizi wanaharakati na wapinzani wa tawala za kimabavu katika nchi za Kiafrika wanapaswa kuyaangalia kwa makini, kuyatalii na kuyazingatia yanayojiri Algeria.

Katika kipindi cha kama wiki sita sasa wananchi wa huko, kwa vitendo vyao, wamekuwa wakitudarisisha juu ya kupambana na mfumo wa utawala uliochakaa na kufanya mapinduzi baridi. Si kwa bunduki, si kwa panga, si kwa majambia. Si kwa mkupuo mmoja; lakini hatua kwa hatua.

Wamemiminika barabarani mamilioni kwa mamilioni. Utafikiri Algeria nzima iko nje barbarani. Silaha zao ni mabiramu na maneno: kaulimbiu za kutaka mageuzi. Hadi sasa hapakumwagika damu, ila jasho tu la waandamanaji na machozi ya furaha wanapopata fanikio.

Hilo ni funzo moja la awali kabisa la waandamanaji hao kwamba waliazimia kupata muradi wao kwa njia za amani. Si kwa mapigano.

Wananchi walianza kuandamana kwa mara ya mwanzo Februari 22 mara tu baada ya Rais Abdelaziz Bouteflika (“Boutef” kama anavyoitwa mitaani) kutangaza kwamba atagombea tena, kwa mara ya tano, uchaguzi wa urais. Wananchi walighadhibika. Walihisi walikuwa wanatukanwa na rais asiyejiweza kwa maradhi na aliyetaka kuwatawala kwa muhula mwingine wa tano.

Umma ulilazimika umiminike barabarani kwa sababu waliamua kujichukulia wenyewe hatua ya kupambana na Bouteflika hasa kwa kuwa vyama rasmi ya upinzani vimepwaya. Takriban vyote vimenunuliwa na mtandao wa Bouteflika.
Wapinzani wa kweli wamebidi waikimbie nchi wende kuishi uhamishoni badala ya kukubali maridhiano ya kitaifa, ambayo wanayaona kuwa si ya dhati na yaliyojaa unafik.

Mwanzoni, vuguvugu la waandamanaji lilikuwa halina jina lakini sasa lina jina, “Harakat rachad” (Vuguvugu la rashad) lakini viongozi wake bado hawajulikani. Waandamanaji hawataki kuwa viongozi. Na bora wasiwe kwa sababu wakichomoza wataojulikana kuwa ndio viongozi kuna hatari kwamba wanaweza wakakamatwa au, kama dhaifu, wakanunuliwa.

Bouteflika alijaribu kuwatuliza waandamanaji kwa kuwaahidi kwamba hatogombea tena urais kwa mara ya tano. Wananchi hawakuridhika. Wakaendelea kuandamana.

Halafu Bouteflika akauahirisha uchaguzi. Hatua hiyo pia haikuwatuliza waandamanaji. Wakaanza kumshikilia ajiuzulu.

Boutef akajaribu tena kuwatuliza kwa kuwaahidi ya kwamba atajiuzulu kabla ya kumalizika muhula wake Aprili 28. Waandamanaji hawakuridhika. Walimtaka ajiuzulu halan, mara moja.

Wakati huohuo, mtandao wa kisiasa wa Bouteflika wa wale waliokuwa wakimuunga mkono, ulianza kumomonyoka.

Mwishowe ndipo alipotangaza Aprili 2 kwamba anajiuzulu urais. Si hayo tu lakini siku ya pili yake aliwabembeleza wananchi wenzake wamsamehe.
Yote hayo yalishindwa kuwatuliza waandamanaji. Wakaanza kudai kwamba mfumo mzima wa kisiasa, uliochakaa na kuchoka, ubiruliwe juu chini.
Wakati mmoja Rais wa zamani Liamine Zeroual, mwenye kuheshimika sana nchini humo, alisema kwamba aliombwa lakini alikataa kuongoza serikali ya mpito baada ya kujiuzulu Bouteflika.

Maandamano ya wananchi, ambayo hadi sasa yanaendelea kufanywa kila Ijumaa, yamejaa pia mizaha na ngoma. Watu wa kila aina wamekuwa wakiandamana: watoto kwa watu wazima, vijana kwa vizee, wanawake kwa wanaume, wauza samaki, walala hoi na wenye kuweza kujikimu kimaisha, wanafunzi na wakufunzi, maprofesa na madereva, wafanyakazi na wasio na ajira.

Maandamano yalipokolea, hata polisi nao walijiunga nayo. Baadhi yao walionekana wakibeba mabiramu yenye maandishi dhidi ya serikali.
Hebu funga macho ulifikirie jeshi la polisi la Tanzania linavyofanya panapokuwa na harufu tu ya maandamano ambayo ni haki wanayopewa Watanzania na katiba ya nchi.

Pamoja na maandamano yao, watumishi wa serikali ya Algeria na wafanyakazi wengine wamekuwa wakigoma na wengine wamezishikilia sehemu zao za kazi.
Hiyo ni nguvu kubwa ya kitaifa na imewashtua watawala. Mkuu wa jeshi Ahmed Gaid Salah akaanza kuiona hali halisi ikimkodolea macho. Ndipo alipoona hana hila ila kumtoa mhanga Bouteflika.

Kwa hivyo, kwa ufupi, yaliyotokea ni haya: Bouteflika alilazimishwa na Salah ajiuzulu, akajiuzulu. Salah naye alilazimishwa na umma uliojaa barabarani amuondoe Bouteflika, akamuondoa.

Na si jeshi tu lililompa mgongo Bouteflika. Hata chama kinachotawala cha FLN, chama kilichopigana na kumwaga damu kupigania uhuru wa Algeria, na kilicho madarakani tangu Algeria iwe huru 1962 nacho pia kimemgeukia Bouteflika.
Hebu kifikirie Chama cha Mapinduzi (CCM) kikichukua hatua kama hiyo. Haitokuwa dhoruba itayovuma Tanzania bali kimbunga cha kisiasa.

Baada ya Bouteflika kuanguka Waalgeria sasa wanataka mfumo mzima wa utawala ung’oke pamoja na waliokuwa wapambe wa Bouteflika, akiwemo Salah pamoja na serikali mpya aliyoiteua Bouteflika kabla hajajiuzulu.
Yote hayo yakifanikiwa Waalgeria watakuwa wamefanya mapinduzi lakini kabla ya kufikia huko wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Kwa sasa changamoto kubwa inayowakabili wapinzani wa serikali ni jinsi ya kuondoka barabarani na kujiingiza katika mchakato wa kuleta mageuzi ya mfumo wa utawala. Makundi mapya yaliyochomoza tangu Februari yalipoanza maandamano dhidi ya Bouteflika yanahitaji kujumuika pamoja na asasi za kiraia na jumuiya za kisiasa ili zishiriki pamoja na upande wa serikali na chama kinachotawala katika mchakato huo wa mageuzi.

Wanaweza wakawaiga jirani zao wa Tunisia ambao wakati wa maandamano yao yaliyompindua Rais Zine el Abidine Ben Ali mwaka 2011 waliunda kamati kadhaa za kutetea mageuzi ya kisiasa na wakati huohuo wakiendelea kuandamana.

Watunisia walifanikiwa kuunda Tume Huru ya Uchaguzi iliyosimamia uchaguzi wa baraza la kutunga katiba. Katiba mpya iliidhinishwa Januari 2014 na uchaguzi huru wa mwanzo wa bunge na wa urais ukafanywa mwishoni mwa 2014, takriban miaka mine baada ya kuanza maandamano dhidi ya Ben Ali.

Ingawa serikali imetoa rai ya kutaka pafanywe mkutano wa kitaifa kuuzingatia mustakbali wa Algeria, waandamanaji wanataka mkutano huo uwahusishe wadau wote na makundi yote sio wanasiasa wakongwe tu na vyama vyao.

Katika mazingira kama yalivyo ya Algeria ya leo, waandamanaji na wapinzani wanahitaji kuwa na mkakati mmoja wa pamoja utaowawezesha kuendelea na hakarati zao na wakati huo kuuparaganya utendajikazi wa dola. Na hapo ndipo penye umuhimu wa vyama vya wafanyakazi na jumuiya za wataalamu kushirikishwa kikamilifu katika maandamano na madai ya waandamanaji.

Jambo la kutia moyo ni kuwaona baadhi ya wafanyakazi wanaoandamana wamekuwa wakidai mageuzi si katika mfumo wa utawala wa taifa tu lakini pia katika shirikisho kuu rasmi la vyama vya wafanyakazi lenye kubarikiwa na serikali.

Kwa muda mrefu katibu mkuu wake Abdelmadjid Sidi-Said amekuwa akikosolewa kwa kujipendekeza kwa watawala. Sasa wafanyakazi wanataka naye pia aondoke kwenye uongozi wa shirikisho lao. Wanataka wao wenyewe wawe viongozi wa kupigania maslahi yao.

Jeshi la Algeria ni uti wa mgongo wa nchi hiyo. Likiweza likajiheshimu kwa kutowakandamiza waandamanaji na baadaye likajitoa kabisa katika siasa basi litakuwa linalifanyia jamala kubwa taifa lao. Likianza vitendo vya kijinga vitavyosababisha umwagaji wa damu basi litageuka zimwi litalolila mpaka kulimaliza taifa hilo. Huo hautokuwa mustakbali mzuri kwa wananchi waliojitolea kufanya mapinduzi kwa njia za amani.

Mapinduzi haya tunayoyashuhudia yakiibuka Algeria ni kumbusho kwamba kweli watawala wanaweza, kwa muda fulani, wakazikandamiza ghadhabu za umma lakini hawawezi kamwe kuzizima.

Ni kumbusho pia kwamba watawala wanaweza wakawanunua vibaraka wawili watatu wanaojipendekeza kwao lakini katu hawawezi kuununua umma mzima, unapokuwa umejawa na ghadhabu za kutaka mageuzi.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 9 Aprili 2019. Anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab


Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles