Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Maalim Seif una mkate gaeni

$
0
0

Leo nimetafuta muda nikasoma kwa kituo taarifa iliyochapishwa hivi karibuni na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia tasnia ya ubunifu na uvumbuzi linaloitwa kwa Kiingereza World Intellectual Property Organisation [WIPO] inayohusu maendeleo ya teknolojia katika upande wa Artificial Intelligence [kwa hakika nimeshindwa kupata tafsiri yake sahihi ya Kiswahili].  Hata hivyo kwa kifupi ni jinsi mashine zinavyoweza kufanya kazi ya kutumia “akili” ya kikomputa.  Wenyewe wanasema huu sasa ndio umeme wa karne ya 21.

Kwa kutumia “akili” hiyo, mashine zinaweza sasa kusoma maandishi ya mkono, kutafsiri lugha moja kwenda nyengine na mambo mengine kadhaa ambayo ni ya ajabu kwa kweli.  Kilichonivuta hisia ni kwamba taasisi za taaluma za China zinaongoza katika taaluma hii.  Naam China hii ambayo nchini kwetu tunadhani tunafafanana nayo kisiasa.  Tunayodhani bado inasimama katika uono wa miaka ile ya China yetu sisi Afrika.  

Lakini nikapata muda pia kudurusu maandiko mawili ya kihistoria muhimu kwa Zanzibar.  Moja ni lile liloandikwa na Anne Bang linaloeleza historia ya Zanzibar kama kitovu cha elimu, taaluma na wanataaluma wa zama za miaka ya 1900 na ushei.  Andiko hili la MEETINGPLACE ZANZIBAR, linaeleza jinsi mwanazuoni maarufu mwenye mizizi ya kihadhrami Bwana Ahmad Ibn Sumayt alivyojenga mtandao hadi kwa wanazuoni wa Uturuki akina Bwana Fadhil Pasha na wengine waliohama Hadhramaut kuja Zanzibar na kuifanya Zanzibar kuvuma kwa utukufu wa Elimu.  

Aidha, andiko la Wesley Gilbert linalosomeka Our Man in Zanzibar.  Andiko hili linaeleza kwa uchambuzi mkubwa jinsi Marekani ikiwa dola ya kwanza ya kigeni, ilivyoanzisha ubalozi wake Zanzibar mwaka 1835 na kuteua Balozi wake wa mwanzo mfanyabiashara Bwana Richard Waters aliyetokea Salem, Massachusetts na jinsi Kijiji cha Selemu, Unguja kilivyopata jina hilo kutoka kwa Balozi huyu.  

Kubwa zaidi, inaeleza biashara kubwa iliyokuwa ikifanyika baina ya Zanzibar na Marekani hadi kuwashitua Waingereza ambao walimtuma Captain Hart kutoka Bombay kuja Zanzibar kuchunguza urafiki wa Marekani na Zanzibar.  Waingereza nao wakalazimika kuingia Mkataba wa urafiki na Zanzibar miaka miwili baadaye.

Suala la msingi hapa hivi kuna uhusiano gani wa hadithi nilizotangulia kuzieleza na msingi wa makala hii?  

Uhusiano ni mkubwa

Kwanza, ni ukweli unaojaribu kufifilizwa kwa nguvu kubwa.  Ukweli kwamba Zanzibar kama dola iliyoungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano ina historia ya aina yake ambayo ingeweza kutumika kuendeleza mema ya historia hiyo.  Zanzibar kama kitovu cha taaluma na biashara haipingani na siasa wala Muungano.  Bali ingeweza kutumika kama kito cha uzuri wa Muungano na kama kielelezo cha umoja wa Zanzibar ndani ya tofauti zilizotokana na historia.  

Profesa Makame Mbarawa, akiwa waziri wa mawasiliano wa Tanzania alipigania mawasiliano kuwa jambo la Muungano.

Badala yake juhudi kubwa zinafanyika kufuta hilo.  Ukiuliza hakuna mwenye majibu ya vita hivi vya kupambana na fahari hii ya Zanzibar.  Kinachotia moyo, tena sana, ni ule muamko wa watu wengi wa Zanzibar na muungano wa hisia zao za kulinda kwa Imani yao ya dhati fahari na utukufu wa nchi yao.

Pili, Zanzibar ina mustakbala wake ambao upo majaribuni.  Mustakbala sio wa kizazi cha leo bali vizazi vijavyo.  Bila ya kuwa na maamuzi juu ya mustakbala wao na bila ya kuwa na kauli juu ya mustakbala wao, hawatafaidi maendeleo ya makubwa ya dunia katika nyanja mbali mbali. Kwa mfano hili la maendeleo ya teknonolojia.  Zanzibar ina vijana waliotapakaa dunia nzima wenye vipawa vya aina yake katika fani ya teknolojia.  

Inasikitisha hata hivyo, kwa mfano, katika Katiba Inayopendekezwa, Mzanzibari msomi Profesa Mbarawa Mnyaa ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kushawishi Wazanzibari wa chama chake wakubali Mawasiliano liwe jambo la Muungano.  Na naam, likaingizwa katika Orodha ya Muungano.  Nilipopata fursa ya kuwafafanulia hatari ya jambo hilo kuwa la Muungano, pamoja na wao kukubali hatari hiyo, lakini ushauri ulipita sikio la kulia ukatokea la kushoto [au kinyume chake].  Mawasiliano ndio uchumi wa dunia tunakoelekea.  Ndio maisha.  Afya, usafiri, kilimo, elimu, huduma za fedha zote zitategemea mawasiliano.  Unawezaje kutoa nyenzo hiyo muhimu tena bila kuweka ufafanuzi wala mipaka.?

Tatu, Zanzibar ni mkusanyiko wa dunia.  Kila mtu yupo. Wa rangi, kabila, asili, dini na mila na desturi mbali mbali.  Ndio maana hata aliyewahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar Sir John Grey aliwahi kusema mfumo wa Zanzibar wa kisheria unafanana na watu wake.  Ni mseto maalumu.  Maana sheria za kiingereza zinatumika, za asili zinatumika, za kihindu na za kiislamu za madhehebu yote zinatambuliwa na kutumia Zanzibar; Ibadhi, Sunni, Khoja zote ni sehemu ya sheria zao.  Mchanganyiko huu ni ndio uzuri na fahari ya Zanzibar.  

Unaposikia mmoja akianza kusema Machotara na Wahindi si kwao Zanzibar inashangaza.  Inabidi umkumbushe tu mambo matatu kwa haraka labda atarudi katika mstari: Mosi, kwamba mji wa Chake Chake wa awali kabisa ambao hadi mwaka 1914 ulikuwa na nyumba karibu 200 ulijengwa katika ardhi iliyotolewa Wakfu na bwana mmoja wa kiarabu Bwana Nassor bin Khalef mwaka 1825 hata kabla Sultani hajahamia Zanzibar.  Pili, kwamba nyumba ya kwanza iliyotaifishwa Zanzibar mwaka 1964 kupitia Legal Notice No. 5 la 1964 ilijengwa na Tayabhali Karimjee kwa matumizi yake binafsi na hadi leo ipo pale Migombani na ndio makazi rasmi ya Serikali.  Tatu, kwamba wengi wanaojifanya ndio wenye Zanzibar ya leo, wazazi wao au wao wenyewe waliomba uraia wa Zanzibar mwaka 1961 na 1962.  Orodha ya majina yao ipo katika magazeti rasmi ya Serikali ya miaka hiyo.  

Dhamira ya dhati yahitajika

Katika hali hiyo, Zanzibar inahitaji dhamira ya dhati kabisa ya kuunganishwa.  Dhamira ya kuondoa hisia ya kuwa kuna wenye Zanzibar na wengine wapo kwa ihsani ya wenye Zanzibar ambao hawaonekani kuwa na ihsani.  Dhamira ya kujenga misingi ya umoja inayoendana na uhalisia uliopo kwamba Wazanzibari ni wamoja.  

Wananchi wakiwania kumpa mkono Maalim Seif Sharif Hamad, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Julai 2010, Fuoni Zanzibar.

Wengi wa Wazanzibari wa leo wanalijua hilo na wana hamu na hilo.  Wanahitaji viongozi wenye dhamira ya kweli, wenye maono na wanaoamini katika hilo.  Viongozi ambao wanatambua umoja wa Wazanzibari haugombani hata kidogo na umoja na mshikamano wa Watanzania wasiokerwa na maendeleo ya Zanzibar na waoamini kwamba maendeleo ya Zanzibar ni faida kwa Tanzania yote.  

Unapokuwa na viongozi ambao wanawabagua watoto na wajukuu zao kwa misingi ya itikadi na nasaba katika mambo ambayo ni haki yao ya msingi kama vile ajira, chambilecho Rais Magufuli, watu si wajinga, wanaona, wanatambua na wanaweza kupambanua.

Ndio maana, nikasema Maalim Seif una mkate gaeni, usiuache ukaungua.  Matarajio ya Wazanzibari katika hayo niliyoyaeleza ndio mkate wenyewe.  Imani yao kwa kiongozi anayeweza kusimamia matarajio hayo ndio yatayoamua siasa na mustakbala wa Zanzibar. Sio sura, sio rangi, siyo bendera, siyo nguvu wala chama.

Lakini kutafuta, kudai na kusimamia jema, siku zote kuna dhoruba, maafa na mikiki, wakati mwengine ya kukatisha tamaa kabisa.  Kama kutafuta jema ni rahisi, basi ingekuwa rahisi kazi ya Mitume wa Mungu, maana waliteuliwa na Mungu kusimamia kazi ya Mungu.  Hata hivyo walikutana na dhoruba, mpaka baadhi ya wakati ikabidi Mungu mwenyewe awaliwaze na kuwapa moyo.  Waswahili wana msemo “Mpishi ndiye Apyaye”.  Lakini kovu za kuungua huko katika upishi wa jema ndiyo nuru, ndio haiba, ndio heshima na ndio kito cha ufalme wa kila mtafuta jema.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Othman Masoud Othman, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambaye kwa sasa yuko safarini Geneva, Uswisi. Mwenyewe anapenda kujitambulisha kama Mwanasheria Mkuukuu.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles