Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Sudan: Mapinduzi bado kukamilika

$
0
0

NADHANI ni kweli kwamba madikteta wote ni vichaa. Hakuna dikteta mwenye akili timamu. Ndiyo maana ninakubaliana na mwandishi wa Kituruki Mehmet Murat Ildan kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa dikteta ila kichaa.

Yalinijia hayo nilipokuwa nikiwafikiria madikteta wawili watatu wa Kiafrika wakiwa pamoja na Omar Hassan al Bashir wa Sudan aliyepinduliwa na jeshi Alhamisi iliyopita.

Kuanguka kwa al Bashir kumenikumbusha ile kadhia niliyowahi kuisimulia katika ukurasa huu siku al Bashir alipojaribu kuniadhiri kadamnasi jijini Khartoum.  Siku hiyo, akiwa bado mtawala wa kijeshi, alitangaza mpango wa kutayarisha uchaguzi wa mwanzo tangu aipindue serikali ya waziri mkuu Sadiq al Mahdi 1989. Nilikuwa mbele yake alipokuwa anauizindua mpango wake.

Nilimuuliza iwapo alikuwa na azma ya kuchuana na wagombea wengine katika uchaguzi wa mwanzo wa urais. Jawabu yake haikunipendeza.

“Mtazameni huyu, nani anautaka urais?” Alinijibu  kama kwa dharau hivi. Wiki chache baadaye nilishtuka niliposikia kuwa aliamua kugombea uchaguzi wa urais kwa niaba ya chama chake cha National Congress.

Na Ahmed Rajab

Chama hicho, kilichokuwa kikitamba katika medani ya siasa za Sudan, hivi sasa kimezuiwa na jeshi kisishiriki katika serikali ya mpito itayoundwa lakini kinaweza kikagombea uchaguzi utapofanywa. Kwa sasa kamati maalum itaundwa kuzishika mali za hicho chama kikichokuwa kikitawala hadi majuzi tu.

Hatua hiyo ni moja ya maazimio yaliyokubaliwa kwenye mkutano uliofanywa Jumapili iliyopita baina ya jeshi na vyama vya upinzani pamoja na asasi za kiraia na Jumuiya ya Wataalamu. Hata hivyo, Jumuiya hiyo imesema kwamba haikuridhika na matokeo ya mazungumzo hayo.

Kupinduliwa kwa al Bashir kumezidi kunithibitishia ukweli wa dhana ya mwandishi Ildan kuhusu udikteta na umajununi. Asingekuwa na wazimu wa kung’ang’ania madaraka al Bashir asingepinduliwa. Angeliondoka madarakani kwa heshima kama Field Marshal Abdel Rahman Swar al Dhahab aliyeushika urais tangu Aprili 6, 1985 hadi Mei 6, 1986.

Swar al Dhahab aliingia madarakani katika mazingira  yanayofanana na ya sasa. Maisha yalikuwa magumu, wananchi walikuwa haweshi kuandamana dhidi ya utawala wa kijeshi wa Jenerali Ja’afer Nimeiry aliyeingia madarakani 1969 baada ya kuipindua serikali ya kiraia ya Rais Ismail al Azhari.

Nimeiry alizidi kujitatiza kwa kutawala kimabavu na kwa kuitumbukiza nchi yake katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya serikali na wenyeji wa Sudan Kusini. Uchumi ulizidi kuwa mgumu kwa kufuata sera za Mfuko wa Fedha za Kimataifa (IMF).

Aprili 6, 1985 Nimeiry alikuwa kwenye ziara rasmi Marekani alikokwenda kuomba msaada wa fedha. Huku nyuma, Khartoum, waziri wake wa ulinzi, Swar al Dhahab alimpindua, bila ya kumwaga damu, katika mapinduzi ya kijeshi. Swar al Dhahab alifanya uungwana wa kuwarejeshea raia hatamu za serikali mwaka mmoja baada ya kupindua.

Al Bashir hakuwa na uungwana huo. Aliipindua serikali iliyochaguliwa ya waziri mkuu Sadiq al Mahdi baada ya serikali hiyo kuanza mashauriano na waasi wa Sudan Kusini. Ajabu ya mambo ni kwamba miaka kadhaa baadaye mnamo 2005 al Bashir alifanikiwa kuvikomesha vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe na kuwezesha pafanywe kura ya maoni ambayo hatimaye iliigawa sehemu ya kusini iwe taifa huru la Sudan Kusini.

Majeshi yalichagua tarehe 6 Aprili kumpindua mwanajeshi mwenzao al Bashir wakiigiza tarehe ambayo Swar al Dhahab alimpindua mwanajeshi mwenzake Nimeiry.

Al Bashir, kama alivyokuwa Nimeiry kabla yake, alifanya mengi yaliyoiumiza Sudan. Wote walisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyowaua maelfu kwa maelfu ya wananchi wenzao.

Historia itamkumbuka al Bashir kwa mengi lakini kubwa kwa kuwa Rais wa mwanzo aliyekuwa madarakani aliyeshtakiwa na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) kwa shtuma ya kusababisha mauaji ya watu wasiopungua 300,000 huko Darfur.

Aligombana na washirika wake akina al Turabi, Ghazi Salah al Din al Atabani na waziri wa zamani Hassan Osman Riziq. Kwa vitendo vyake na misimamo yake al Bashir amekuwa na maadui ndani na nje ya nchi.

Nimekuwa nikikumbuka aliyowahi kunambia dikteta mwingine wa Kiafrika nilipomaliza kuzungumza naye katika Ikulu ya nchi yake.  Aliniuliza: “Ukitoka hapa [nchini mwake] utaelekea wapi?” Nilimwambia Khartoum.

“Unamfuatia nini mkorofi yule al Bashir?” Aliniuliza huku akikunja uso. Sikutaka kujua zaidi kwanini alimwita al Bashir “mkorofi”.  Ilikuwa wazi kwa swali lake na ile iitwayo lugha ya mwili wake kwamba al Bashir hakuwa shetani wake.

“Kumbe wanajuana, wakorofi kwa wakorofi.” Nilijiambia kimoyomoyo. Bahati mbaya sikupata fursa ya kuwa na al Bashir faraghani nikamchuma kuhusu huyo dikteta mwenzake, ambaye jina lake ninalihifadhi.

Kwa hakika, mengi yamekuwa yakinienda kichwani tangu wananchi wa Sudan walipomiminika barabarani kuanzia Desemba mwaka jana wakiutikisa utawala wa al Bashir.  Kumbukumbu zangu za Sudan ni nyingi, pia za siasa za Sudan na za wanasiasa wa Sudan.

Wanasiasa hao ni pamoja na Mansour Khalid, aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje, John Garang aliyekuwa kiongozi wa wapiganaji wa Sudan Kusini, Joseph Lagu ambaye ni muasisi wa Anyanya, jeshi la waasi wa Kusini Sudan na Hassan al Turabi.

Wengine ni masahibu wangu wa muda mrefu Ahmed Suleyman, aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha Sudan, Ahmed Ibrahim Diraige, mwenye siasa za mrengo wa kushoto na aliyewahi kuwa gavana wa Darfur pamoja na Shawgi Mallasi, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa chama cha Ba’ath.

Mallasi akimhusudu Saddam Hussein, aliyekuwa rais wa Iraq na kiongozi wa chama ndugu cha Ba’ath nchini mwake. Alivutiwa na Saddam kiasi cha kuwa akimuiga Saddam namna alivyokuwa akichana nywele. Nikipenda kumtania kuhusu kiroja hicho.

Siku moja ingawa ilikuwa wazi kwamba alitafirika kwa huo utani wangu alitabasamu na kunambia: “Wewe Ahmed nitakuua ukiandika mambo haya.”

Ninaikumbuka mara yangu ya mwanzo kuizuru Sudan mwaka 1968.  Siku hizo nchi hiyo ndiyo iliyokuwa kubwa kwa eneo kushinda nchi yoyote nyingine barani Afrika.

Nilikuwa njiani kurudi London nikitokea Tanzania na Uganda. Nilijipa kama wiki kukaa Khartoum na kuuzuru mji wa Omdurman kabla ya kuelekea Saudi Arabia kwa siku chache, kupitia  Port Sudan nilikohisi kama nilikuwa ndani ya tanuri kwa joto.

Ndege yetu ilipotua Khartoum, nililiona jiji zima likiwa barabarani. Nakumbuka maelfu kwa maelfu ya vichwa vya watu waliokuwa wakindamana na mabiramu yao.

Umma huo haukuwa na imani na serikali ya ubia iliyokuwa madarakani chini ya waziri mkuu Muhammed Ahmed Mahjoub na iliyokishirikisha chama chake cha National Unionist Party (NUP) na kile cha Umma cha Sadiq al Mahdi.

Mahjoub, aliyekuwa mwandishi na mshairi, alichaguliwa kwa mara ya kwanza awe waziri mkuu 1965 lakini alilazimishwa ajiuzulu. Serikali ya mwanzo ya Sudan huru ilipinduliwa 1958 na Jenerali Ibrahim Abboud lakini kwa sababu ya shida za kiuchumi na machafuko ya kisiasa mwaka.  Mapinduzi hayo hayakumwaga damu.

Abboud aliselelea madarakani bila ya kutimiza ahadi za kurejesha serikali ya kiraia.  Umma ulichoka na kufikia mwishoni mwa Oktoba 1964 baada ya machafuko na mfululizo wa migomo jeshi lililazimika kuyaacha madaraka. Yaliyojiri wakati huo yanafanana na ya sasa.

Maandamano na migomo iliyomg’oa madarakani Jenerali Abboud, kama maandamano na mgomo nilioushuhudia mara yangu ya mwanzo kufika Sudan, ilikuwa ikiongozwa na wafanyakazi pamoja na wafuasi wa chama cha Kikomunisti cha Sudan kilichokuwa na nguvu kubwa siku hizo.

Siku hizi chama hicho, chenye kuongozwa na Muhammed Mukhtar al Khatib bado kina sauti katika siasa za Sudan lakini sicho kinachowaongoza waandamanaji wenye kupinga utawala wa kijeshi.

Umma uliomiminika katika barabara za miji ya Sudan ulilishinikiza jeshi liyaunge mkono madai yake. Hatimaye lilimpindua al Bashir. Lakini aliyeshika mahala pake waziri wa ulinzi Luteni-Jenerali Ahmed Awad Ibn Auf alidumu madarakani kwa siku moja na saa kadhaa tu.

Alibidi ajiuzulu kwa sababu wapinzani hawakumtaka. Wapinzani wanamuona yeye na al Bashir kuwa kitu moja. Baraza la kijeshi linalotawala sasa linaongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhani ambaye wengi wanamuona ni afadhali kushinda Ibn Auf. Lakini hata yeye wapinzani hawamtaki. Hawataki mwanajeshi yeyote aongoze utawala wa nchi.

Mtu mwengine mzito aliyelazimishwa na jeshi astaafu ni Meja-Jenerali Salah Abdallah “Gosh”, aliyekuwa hadi Jumapili iliyopita mkurugenzi wa idara ya ujasusi na usalama wa taifa.

Inasemekana kwamba Februari mwaka huu, Gosh alikutana kwa siri na Yossi Cohen, mkuu wa shirika la ujasusi la Israel, Mossad, mjini Munich, Ujerumani. Walikutana, kwa msaada wa Misri, pembezoni mwa mkutano wa kimataifa kuhusu mambo ya usalama. Lengo lilikuwa ni kupanga mkakati wa kumfanya Gosh awe rais pale al Bashir atapoanguka. Gosh ana mahusiano mazuri na shirika la ujasusi la Marekani, CIA.

Nchi za Saudi Arabia, UAE na Misri zilitaka Gosh amrithi al Bashir. Kwa mambo yalivyo Sudan sasa nchi hizo zinaonesha zimeondokea patupu kuhusu suala hilo.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 17 Aprili 2019. Mwandishi anapatika kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab


Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles