Katika kile kinachoonekana ni muamko wa uhamasishaji wa maandamano kupitia mitandao ya kijamii ukiendelea, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amewaonya watu wanaopanga kushiriki maandamano hayo ya Aprili 26 watapata matatizo makubwa watajikuta wakiwa vilema.
Kamanda Muruto aliyasema hayo juzi mbele ya vyombo vya habari, alipowafikisha kwa wanahabari watu wawili wanaotuhumiwa kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano.
“Watakaoingia barabarani siku hiyo watapata matatizo makubwa kwani wengine watajikuta wakiwa vilema. Hivyo, ni vyema kuitumia mitandao katika kuhamasisha maendeleo badala ya kuhamasisha mambo ya kijinga,” alisema Kamanda Muroto .
Kamanda Muroto aliwataja watu hao waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwamba ni dereva wa Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF), Amandus Manchali na Yuda Mbata ambaye ni mkulima mkaazi wa Bahi.
Aidha, Kamanda Muroto amewaasa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuitumia kwa faida ya taifa kuhamasisha maendeleo.
Kamanda Muroto aliwafananisha watu wanaoandaa maandamano hayo kama watu walioshiba na kuvimbewa ambao wamesahau nchi ilipotoka ambao wanaweza kuhamishia choo ndani ya nyumba zao.