Ilipoishia tuliona Abdull alivyoanza chuo na kukutana na marafiki wengi akiwemo Kassim, pia akakutana na Fartuun. Jioni moja wakati wakitoka chuo waliamua kufuatana na story mbili tatu zikawa zinaendelea. Sasa endelea….
Waliamua kutembea kwa miguu, wakidai wanafanya mazoezi ya kupunguza mafuta mwili, hatimaye kila mmoja akamuacha mwenzake na kuelekea njia ya nyumbani kwao.
Abdull hakuwa na mawazo sana na Fartuun,ingawa alimpenda pia lakini hofu na ugeni wake katika mji ule ni jambo lilokuwa likimrudisha nyuma sana. Siku zote aliamini familia ya Fartuun ilihitaji kijana mwenye pesa nyingi sana, tena awe Msomali na sio wa kuja, ili kumuoa binti yao. Hayo ndiyo mawazo yalioyokuwa yakizunguka kichwa cha Abdull.
Lakini kwa Fartuun hali ilikuwa ni tofauti mno, mara nyingi kichwani alikuwa akizongwa na mawazo ya kujiuliza Abull ni mwanaume wa aina gani, mbona kama hamuelewi!
Kama kawaida yao usiku uingiapo huzungumza kwa siku kwa dakika kadhaa kabla ya kulala, hata Talib alianza kunusa nusa harufu ya mdogo wake kuchelewa kulala kwa sababu ya maongezi kwenye simu, ingawa hakujua anazungumza na nani.
Usiku ule Fartuun alimuuliza Abdull, ni lini ataenda kumtembelea nyumbani kwao, Abdull akataka kukwepa swali lile kwa kusema kwamba watapanga lakini alielezwa wakati ule ndio walihitajika kupanga .
“Basi wiki ijayo unakuja kwetu. Right?”
“Sawa”, alijibu huku akivuta pumzi nzito na kuigeuza simu upande mwengine wa sikio.
Mazungumzo na vicheko viliendelea hadi usingizi uliposhinda sauti zao, lakini kulikuwa na jambo moja lililoanza kumuudhi Fartuun. Awali alikuwa akipendezwa sana na jinsi Abdull alivyo na aibu, lakini kadiri siku zinavyokwenda alianza kuchoka na kukerwa na aibu hizi.
Kama mwanamke alitamani mwanaume ndio azungumze suala la mahusiaano kati yao, lakini siku zilikatika Abdull hakuwa anaonekana hata na nia ya kufanya hivyo. Fartuun alishajitahidi vituko na mbinu lakini bado alikuwa anaendelea kukwama.
Wakati mwengine alikuwa anazongwa na mawazo kwamba Abdull hakuwa anampenda ndio maana hadi wakati ule hajamwambia kitu, lakini ni mawazo ambayo daima hakutaka yatamalaki kichwani mwake.
Asubuhi ya siku ya pili walikutana katika mjengo mlo wa chuo chao, walikubaliana kukutana hapo mara baada ya kutoka vipindi vyao vya asubuhi.
“Hivi mimi ni nani kwako? Fartuun alimuliza Abdull wakati wakiwa wameketi wanapata kifungua kinywa.
“Ni marafiki…”
Ni jawabu ambayo ilionekana kumkera sana Fartuun, akamwangalia Abdull usoni kwa jicho kali, kisha akaendelea kuchota chakula na kupeleka mdomoni.
“Mchumba wako wa Pemba ni mzuri kuliko mimi eee?
Ni swali lililonfanya Abdull kucheka lakini kwa Fartuun hakukuwa na la kumchekesha alibaki tu akimwagalia Abdull kwa jicho la hasira kidogo.
“Mbona umebadilika hivyo, na maswali ya ajabu ajabu.!
“Okay, najua cha kufanya”, alinena Fartuun bila ya kujibu chengine na akamuaga Abdull na kuondoka kuelekea darasani.
“Sikuelewi unajua…”, yalikuwa ni maneno ya mwisho ya Abdull kwa Fartuun wakati akifunikwa na viambaza vya madarasa akielekea darasani. Lakini Fartuun hakugeuka na kujibu cochote.
Wiki ikakaribia ukingoni na ahadi ya kwenda kumtembelea ndio ikawa imewadia. Fartuun anaishi katika eneo la Dagmada lipo pembezoni kabisa mwa bahari ya hindi.
Baba yake Fartuun anaitwa Aweys ni mfanyabishara tajiri na maarufu sana katika mji wa Mogadishu, akiishi na familia yake ya watoto watatu wawili wakiume na mmoja wakike ambaye ndiye Fartuun.
Mmoja wa Kaka yake Fartuun alibahatika kuoa lakini mke wake alifariki siku za karibuni wakati anajifungua mtoto wake wa kwanza, hivyo alipoteza maisha yeye na mtoto wake pia, kaka mwengine bado alikuwa hajaoa.
Mchana wa siku ya Jumapili Abdull alifika nyumbani kwao Fartuun kwa maelekezo ya mwenyeji wake, getini alikutana na walinzi wawili, waliojidhatiti kwa silaha na mashine ya kugundulia silaha.
Alipoingia ndani kulikuwepo Baba yake Fartuun, mama yake na kaka zake wawili wa kiume , alipofika aligundua mazingira ambayo yalitayarishwa maalumu kama kuna mgeni wa heshima anakuja, kana kwamba kila mmoja alitegemea na kusubiria mgeni huyo.
Alikaribishwa vizuri mno, kila mmoja akitabasamu wakati wa kupeana mikono hadi mwenyewe akashangaa, yalikuwa ni makaribisho ya kana kwamba anajuulika vizuri sana na familia ile.
Alianza wa kupata hofu mwisho moyo wake ukatulia na kukubali matokeo yoyote yatakayo kuja mbele yake. Baada ya salamu alikaribishwa sebuleni,akawa anazungumza na baba yake Fartuun pamoja na kaka zake kuhusu maendeleo yake ya chuo.
Fartuun na Mama yake pamoja na binti mwengine, ambaye Abdull aliamini ndiye mfanyakazi wao wa ndani, walikuwa wanatayarisha chakula ingawa shughuli zao hakuziona , alikuwa kawapa mgongo, akizisikia tu sauti za sahani na vijiko.
“Unategemea maisha yako yatakuwa hapa au utarudi nyumbani kweu..?, ghafla Mzee Aweys alimtupia swali lililomuacha kinywa wazi kwanza.
“Inategemea na usalama wa hapa…hali ikitulia nitabaki..ikichafuka tutafute penye usalama…”
Swali hili lilimfanya Abdull agundue kwamba Fartuun alikuwa tayari ameshaiyeleza familia yake, baadhi ya mambo kuhusu yeye.
Baada ya dakika kadhaa mlo wa nguvu ukaekwa katika meza ya chakula, iliyopo pembeni kidogo ya sebule. Kimya ndicho kilichotawala katika dakika zote za kula, ni utamaduni uliomfurahisha sana Abdull, kwani mwenyewe kikawaida hapendi kuzungumza wakati wa kula.
Baada ya hapo, familia ikarudi sebuleni, kisha Mzee Aweys akamkaribisha mwanawe Fartuun na kumwambia uwanja ni wake. Hofu ya Abdull ilifufuka kidogo kwani hakujua nini kitaenda kutoka kinywani mwa Fartuun.
Fartuun alisimama akiwa anatabasamu, huku moyo wa Abdull ukisema kwamba ni utambulisho tu hakuna jengine. Fartuun alianza kwa kukwamgua koo lake, ishara kuna jambo zito ambalo alitaka kulisema .
“Wazazi wangu na Kaka zangu, huyu ndiye mchumba wangu kwa jina la Abdull-llatif Seif ambaye nimekuwa nikiwaeleza ..”
Bila ya kuchelewa Abdull akameza mate mazito, yaliyochezesha hadi koromeo lake na kulifanya litoe sauti, baada ya hapo akohoe kidogo, aliamini anampa ishara Fartuun kwamba kakosea katika utambulisho anao utoa.
“Tumekubalia kufunga ndoa…nimemleta mumuone mnikubalia kuolewa na yeye kwa hali yoyote aliyonayo na mtupe baraka zenu..”, Fartuun alimaliza na kukaa kitako.
Jasho jembamba lilikuwa linatiririka ,moyo wake ukazidisha mapigo, kwani hadi Fartuun anamaliza yeye alikuwa haelewi anaanzaje wala anamalizaje, akabaki katika bumbuwazi la ajabu sana, akitoa tu macho.
Sekunde hazikukatika sana kabla Mzee Aweys hajamuuliza Abdull kwa upande wake ana lipi la kusema, kwani familia yote ilikuwa haina kipindamizi chochote juu ya jambo lile. Abdull akajiuliza ikiwa akatae au akubaliane na Fartuun.
Kilichoelezwa na Fartuun sio makubaliano yao ya kuja kumtembelea, wala si jambo ambalo wamewahi hata kulizungumza, alijihisi kusukumiziwa mzigo mzito ambao aliona unaumiza nyama za ubongo wake kwa kuwaza na kuwazua.
Hamaye bila ya kuchelewa akakubaliana na kila kilichosemwa na Fartuun, akakubali huku akimuangalia Fartuun ambaye alikuwa ameinamisha kichwa chini kama muumini aliyekuwa katika dua nzito. Baada ya Abdull kutoa jibu la kukubali, akamuona Fartuun anainua kichwa na kuacha bonge la tabasamu huku akinfinyia Abdull jicho.

Siku nyingi zilikuwa zimeshakatika za urafiki wa Abdull na Fartuun, kikao kile kilifanyika ikiwa ni mwezi mmoja tu ulibaki kabla ya kumaliza chuo, familia ilikubali suala la ndoa waanze kulizungumza mara baada ya kumaliza masomo yao. Lakini walimsisitiza Abdulla aje na Kaka yake kabla ya chuo hajamaliza, ili na yeye familia imtambue.
Uchumba rasmi kati ya Abdull na Fartuun ulianza hapo, hata Abdull alipokuja kumuuliza Fartuun kwa ukali kwanini aliamua kufanya vile. Aliishia tu kumuonea huruma kwani alitoa jawabu huku machozi yakimtoka.
Fartuun alilalamika kwamba Abdull hakutaka kumuelewa kwamba anampenda.
“Unadhani ulitaka mimi nifanye nini?,
“Kama hunitaki na hutaki tufunge ndoa …sawa nataenda kuwaambia..”, aliendelea kulalama huku machozi yakimtoka.
Kuna wakati Abdull alikuwa anakubali moyoni mwake, kwamba hana uwezo mzuri wa kumkabili mwanamke, licha ya Fartuun kufanya jambo ambalo hakumpa Abdull taarifa kabla, lakini ilikuwa ni nafuu pia kwake.
Mapenzi yao yakanawiria na kukuwa, lakini Talib hakuwa anajua kinachoendelea. Hata kule Abdull alikoombwa ampeleke bado alikuwa hajampeleka.
Kazi ya uvuvi na bishara ya kuuza samaki iliendelea vizuri , katika kipindi hiki cha mwisho wa masomo kwa Abdull, Talib alijaribu kumpa muda ili ashughulike na masomo yake kwanza.
Ingawa hali ya usalama ya mji wa Mogadishu haikuwa salama sana, lakini haikufanya watu kuacha kufanya yao. Wasomali walishavizoeya vita kwani vilianza zamani mno.
“Abdull , leo nataka tuzungumze kidogo…”, yalikuwa ni maneno ya Talib
“Sawa..nikirudi chuo tutazungumza..”
Baada ya siku kusonga kwa kasi, zilikuwa ni siku za mwisho chuoni huku akifanya mitihani ya kumalizia.
Baada ya ahadi ya kuzungumza atakaporudi chuoni. Ndipo muda ulipowadia wakaenda kukutana katika mgahawa ambao mara ya mwisho walikaa pamoja na rafiki yao Ismail, na wao wakaamua kuketi pale pale ili wazungumze.
“Inaonekana mazungumzo yanapokuja katika mgahawa huu, yanakuwa mazito kidogo..”, alisema Abdull huku akivuta kiti kukaa.
Wakaagiza Chai ya maziwa na vitafunwa, kisha mazungumzo yakaanza kama walivyoahidiana.
Talib alianza kumkumbusha Abdull safari yao kutoa Pemba kupita Mombasa hadi walipofika Somalia, huku akisisitiza ule unyama uliotendeka hadi wao wakawa wakimbizi.
Kilele cha mazunguzo ya Talib ni kumshawishi Abdull, walipize kisasi kwa kile kilichotokea, alinena kwamba wakati wa jicho kwa jicho na pua kwa pua, ulikuwa umeshafika.
“Sasa hicho kisasi tunaenda kukifanya kwa nani?
“Kwa kiongozi aliyepo madarakani…”
“Mbona kazi ngumu..”
Ni kiongozi gani wanaenda kulipiza kisasi? Je, uchumba wa Abdull na Fartuun utafikia wapi? Mpango wao utafanikiwa? Tukutane wiki ijayo…..