Ijumaa ya tarehe 21 Julai 2017 itachukuwa muda mrefu kwangu kusahaulika. Kwenye ukurasa wa Facebook, mtumiaji mmoja alikuwa ametuma taarifa iliyoandikwa na dawati la michezo la mtandao wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusu nchi yangu, Zanzibar, kuvuliwa uwanachama wake iliokuwa imeupata siku 128 hapo kabla kwenye Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Kwanza niliipita habari hiyo ghafla kama siijui, lakini kisha nikarudi kuisoma kwa kina neno kwa neno. Ilikuwa taarifa fupi na nzito. Licha ya kuwa kwangu mhariri na mtangazaji wa shirika la habari la kimataifa kwa takribani miaka saba sasa na kwamba BBC yenyewe ni shirika la habari la kimataifa, nilijikuta siiamini habari hiyo.
Nikaenda kwenye mtandao wa CAF, kisha kwenye akaunti binafsi ya Twitter ya mkuu wake, Ahmad Ahmad wa Madagascar, na mote humo sikukuta taarifa hizo. Hadi muda huo, bado kwenye mtandao wa CAF kulikuwa na bendera na jina la Zanzibar kwenye orodha ya wanachama, tena chini ya bendera na jina la Tanzania.
Hata hivyo, nikaituma tena ripoti hiyo ya BBC kwenye ukurasa wangu wa Facebook, nikiambatanisha na wasiwasi na matarajio yangu. Niliomba na kupenda ile iwe ni habari ya uzushi tu, ambayo punde ingelitamkwa kuwa si kweli.
Siku hiyo pia, nikiwa mhariri wa zamu, nilikuwa nimefikiwa mezani pangu na habari ya wafanyakazi wa kigeni wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia nchini Tanzania kutakiwa kuondoka mara moja. Muda mchache baadaye, mkurugenzi wa Acacia jijini London akakanusha ripoti hiyo ya shirika la habari la Reuters, akisema kilichotokea ni kuhojiwa kwa wafanyakazi wake wawili tu, na sio kufukuzwa nchini Tanzania.
Kwa hivyo, nikawa naomba kimoyokimoyo na hii ya Zanzibar kuvuliwa uwanachama wa CAF itamkwe kuwa haikuwa ya kweli. Lakini hadi siku ya pili yake mchana, habari ilikuwa imebakia hivyo hivyo, huku wahusika wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wakitajwa kutokuwa na habari ya jambo hilo. Ikimaanisha kuwa aidha hawakuwa wamearifiwa kwa taratibu rasmi au walikuwa wanadanganya. Na bado, moyoni mwangu nikawa nataka kuamini kuwa kutokuwa kwao na taarifa kunamaanisha kuwa jambo lenyewe halipo.
Sijui kama unazielewa hisia hizi, lakini mchangiaji mmoja wa ukurasa wangu wa Facebook aliniandikia faraghani akizifananisha na za mzazi aliyepotelewa na mwanawe katika mazingira ya kutatanisha. Mzazi huyu huwa haamini kuwa mwanawe hatapatikana tena. Hata kama miaka mingi itapita, bado huwa anadhani kuwa kuna siku mwanawe atarejea akiwa mzima, salama usalimini.
Ndizo hisia zangu ambazo hadi naandika makala hii, masaa 24 baada ya kupokea taarifa ya kupotea Zanzibar kutoka ramani ya CAF. Kuna kitu kinanifanya nisitake kuamini ukweli kuwa tumeshatolewa. Hisia tu.
Naam, ni hisia tu. Hisia si lazima ziwe uhalisia. Ingawa baadhi ya wakati, sadfa huzigeuza hisia zetu kuwa ukweli. Hayo ndiyo yale yaitwayo makarama. Bahati mbaya kwangu ni kuwa miye si mja wa makarama, na hivyo mara kadhaa hisia zangu hazikumbwi na rehema ya sadfa zikawa ukweli. Zanzibar yangu imeondoshwa kwenye CAF.
Huo ndio uhalisia uliopo mbele yangu na ndio ambao nitaujadili hapa, baada ya kuipata barua rasmi Rais wa Chama cha Soka cha Zanzibar, Ravia Idarus Faina, na Kaibu Katibu Mkuu wa CAF, Essam Ahmed, siku hiyo hiyo ya tarehe 21 Julai. Nitaachana kabisa na hisia zangu binafsi za mzazi aliyepotelewa na mwanawe.
Uhalisia namba moja ni kauli ya Ahmad Ahmad inayosema hivi: “Zanzibar imeondolewa kwenye uwanachama wa CAF kwa kuwa ni wanachama wa FIFA tu ndio ambao wanaweza kuwa pia wanachama wa CAF.”
Uhalisia namba mbili ni sababu ya ziada iliyomo kwenye Kifungu Na. 4(4) cha Katiba ya CAF ambacho kinalilazimisha shirikisho hilo “kukitambua chama kimoja tu cha kitaifa kwa nchi.”
Na uhalisia huo namba mbili ndio unaopigilia msumari kwenye wa namba tatu, unaosema kuwa “uwakilishi wa kitaifa uliopo sasa unaotambuliwa na FIFA na CAF ni ule wa Shirikisho la Soka la Tanzania.” Hapo anakusudia Shirikisho la Soka la Tanzania Bara (TFF).
Huo ndio uhalisia uliopo kwenye uamuzi wa CAF iliyokutana Rabat, Morocco, na kuiondolea Zanzibar uwanachama wake ilioupata tarehe 16 Machi 2017 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Sasa tuje kwenye uchambuzi wa uhalisia huu, kuangalia ambapo sisi Wazanzibari tulijikwaa na sio tulipoangukia.
Ukweli ni kwamba vyombo vya kimataifa vinaitambua Tanganyika (ninaiita Tanganyika kwa makusudi, maana ushahidi unathibitisha kuwa ndiyo inayojiwakilisha kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania). Ukweli huu ndilo jinamizi kubwa kwenye nafasi, maslahi na taswira ya Zanzibar ndani na nje ya mipaka yetu, maana siasa ya Tanganyika nje ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Zanzibar ni muakisiko tu wa siasa yake ya ndani.
Nimeandika mara kadhaa – na daima nitaandika hivi hivi madhali hakuna kilichobadilika – kwamba Tanganyika inaamini kwa dhati kwamba ukitaka kuwa na Muungano imara (soma Tanganyika imara), basi lazima uwe na Zanzibar dhaifu. Kinyume chake ni kuwa unapokuwa na Zanzibar imara, basi ujikubalishe kuwa na Tanganyika (Muungano) dhaifu. Huu ni ukweli mchungu, lakini ndio uhalisia ulivyo.
Na wala hili jambo halijaanza leo kwenye la uwanachama wa CAF tu. Limekuwa hivyo ndani ya hii inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na limekuwa hivyo pia nje yake. Chimbuko lake lilianzia hata mwezi mmoja haujatimia tangu kuwekwa saini kwa Makubaliano ya Muungano, pale Mwalimu Julius Nyerere alipoanza kuipopotowa Zanzibar nguvu zake kwa kutunga sheria ya kuzibatiza jina la Muungano shughuli zote za Tanganyika ambazo hazikuwa katika yale Mambo 11 ya Muungano, tunayoambiwa walikubaliana na Mzee Abeid Karume.
Kati ya sheria hizi ni ile iliyoitwa The Transitional Provision Decree (N0. 1) ya mwaka 1964, ambayo iliwapa uhamisho wafanyakazi wote wa serikali ya Tangayika na kuwa wa serikali ya Muungano. Kwa sheria hii, iliyochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la tarehe 1 Mei 1964, ndipo taasisi kama vile Mahkama Kuu ya Tanganyika zilipogeuka kuwa Mahkama Kuu ya Tanzania.
Kisha wiki mbili tu baada ya hapo, yaani tarehe 15 Mei 1964, akachapisha sheria nyengine iliyoitwa The Transitional Provision Decree (No. 2) iliyoelekeza kuwa “kila pale penye neno au kumbukumbu inayosomeka Tanganyika sasa pasomeke Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”
Kwa hivyo, hata lile agizo lililokuwemo katika Katiba ya Muda kwamba “Tanganyika and Zanzibar are one United Sovereign State” baadaye likaja kubadilika na sasa ikawa “Tanzania is one State and is a Sovereign United Republic”, ambayo ndiyo iliyomo hadi sasa, na ndiyo inayotumika kuifanya Zanzibar isiwe na chake mbele ya jumuiya za kimataifa, hata kama ushirikiano wa kimataifa si jambo la Muungano.
Kwa kutumia mwanya huu, kila kitu cha Zanzibar kinakuwa kimsingi na kiutekezaji ni cha Tanganyika kwa jina la Muungano, hata kama kijuujuu kitasemwa na kuoneshwa kinyume chake. Vyote na chochote cha Zanzibar si chake.
Ndio maana ukaona, kwa mfano, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaunda wizara zake, kisha anachanganya mambo yasiyokuwa ya Muungano na ya Muungano kwenye wizara moja, kama hilo la Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Masuala ya Afrika Mashariki, ambamo ndani yake ni Mambo ya Nje tu lililo la Muungano. Ndivyo pia ilivyo pia kwa Wizara ya Mambo ya Muungano na Mazingira, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, na kadhaa wa kadha.
Anaweza pia kuunda wizara isiyohusiana kabisa na Mambo ya Muungano na ambayo, kwa hivyo kimsingi inakuwa ya Tanzania Bara tu, lakini akamteuwa Mzanzibari kuwa waziri, kama vile Dk. Hussein Mwinyi alivyowahi kuwa waziri wa afya na sasa Profesa Makame Mbarawa alivyo waziri wa ujenzi.
Kizungumkuti hiki hakifanywi kwa bahati mbaya. Kipo kwa makusudi, maana kwa jicho la ndani la Dodoma ni kwamba kuna nchi moja tu, kuna serikali moja tu na kuna chama kimoja tu. Hii ndiyo falsafa ya mwasisi wa huo unaoitwa Muungano wenyewe, Mwalimu Nyerere, na ambayo inatekelezwa kivitendo na wafuasi wake, miongoni mwa Watanganyika na miongoni mwa Wazanzibari pia.
Kwa hivyo, kwenye hili la CAF, tulipojikwaa sisi Wazanzibari tunaotaka kuiona nchi yetu ikisimama kwa miguu yake yenyewe kwenye mambo yake yote yasiyokuwa ya Muungano, sio kwenye kiherehere chetu cha kujipeleka CAF kabla ya kutoka FIFA, kama inavyojieleza barua ya kufukuzwa kwetu, bali ni kwenye kutokulimaliza kwanza lililosababisha kila chetu kikawa si chetu wenyewe – kutolimaliza la siasa za Muungano kuelekea nchi yetu.
Kama kweli tunataka kuiona Zanzibar ikiwa mwanachama wa jumuiya yoyote ya kimataifa, kama kweli tunataka kuiona Zanzibar ikisimama kwenye mambo yake yote yasiyo ya Muungano, tunapaswa kwanza kukimaliza kizungumkuti kilichomo kwenye Muungano wenyewe. Je, tuko tayari?
Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: CAF, FIFA, mpira wa miguu, soka, Tanzania, Zanzibar
