Waziri wa Habari wa Tanzania Bara, Dk. Harrison Mwakyembe, amewatolea wito wasanii kutokujihusisha na mambo ya siasa kwenye kazi zao, akiwaonya kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwaweka mahala pabaya.
Akijibu hoja ya Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule, ambaye pia mwanamuziki anayetambulika kwa kina la Profesa Jay, kuwa wasanii wakiimba nyimbo za siasa kuihoji serikali wamekuwa wakinyanyaswa, ila wakiimba nyimbo za kuisifia tu wanaachwa, Mwakyembe alisema kuwa wasanii hawatakiwi kuimba nyimbo za siasa na kama wanataka kuzungumzia siasa basi wagombee udiwani au ubunge.
Waziri huyo aliyewahi kuwa mwandishi wa habari na pia mwandishi wa kazi za fasihi, amewashangaza watu pale aliposema hakuna mwanamuziki yeyote duniani aliyefanikiwa kwa kuikandia serikali.
“Nimetembelea nchi kama Nigeria na wasanii waliofanikiwa kama wakina P Square, Tiwa Savage, David, ni wasanii wenye mafanikio, lakini hawajapata mafanikio hayo kwa kuitukana serikali,” amedai Waziri Mwakyembe.
“Muziki ni entartainment industry (tasnia ya burudani) na sio political indusrty (tasnia ya siasa) na hata Afrika Mashariki wasanii kama Chamilione na akina Diamond na Ali Kiba wana mafanikio lakini hawaimbi siasa,” alihoji Mwakyembe kwa mujibu wa mtandao wa Jamii Forum ambao umeweka vidio yake.
Akitilia mkazo hoja yake ya kuwa wasanii wanaoimba siasa hufikwa na matatizo, waziri huyo alimtolea mfano msanii wa Nigeria, Fella Kuti, “aliyeimba siasa na akaishia pabaya.”
Filed under: BURUDANI Tagged: bunge, Joseph Haule, muziki, mwakyembe, Profesa Jay, siasa, wasanii
