Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuber Kabwe, amekuwa kiongozi wa karibuni kabisa wa upinzani nchini Tanzania kutiwa nguvuni na jeshi la polisi, kwa sababu ambayo bado hazijafahamika. Zitto, ambaye alikuwa kwenye ziara maalum ya kichama mkoani Morogoro, alikamatwa huko usiku wa Alhamis (22 Februari 2018).
Katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa uchambuzi huu, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Othman Masoud, alizungumzia nadharia ya mtego wa komba akiufananisha na namna viongozi wa Zanzibar wanavyoiingia wenyewe nchi yao kwenye maangamizi kwa muktadha wa majibu yao kwa Waziri wa Sheria wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, juu ya hadhi, mamlaka na nafasi ya taasisi ya urais na katiba ya Zanzibar, na pia akagusia wasifu wa Profesa Kabudi kama amjuavyo yeye. Katika sehemu hii ya pili, anaanza kulinganisha kati ya kile walichokipitisha viongozi wa Zanzibar kwenye Katiba Inayopendekezwa na kile wanachojifanya kumsuta sasa Profesa Kabudi. – Mhariri
Viongozi Wetu na Uchu wa Kipande cha Ndizi
Suala la kujiuliza ni kwamba je, ugeugeu wa wazi wa baadhi ya viongozi ambao wamekua mstari wa mbele kumtuhumu Profesa Kabudi ni wa kiasi gani na je, umekuwa na tija kwa Zanzibar? Au ndio uliompa silaha Profesa Kabudi kugeuka kwa tija ya Tanganyika?
Kwanza, tuangalie mifano michache tu. Mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kumlaumu Profesa Kabudi, ndiye aliyetoa pendekezo la kuongeza kifungu kinachosema Zanzibar ni miongoni mwa nchi katika nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar. Pendekezo hilo lilikubaliwa baada ya kueleza matukio kadhaa ya jinsi viongozi wa Serikali ya Muungano wanavyoidhalilisha Zanzibar ndani na kimataifa, akitoa mifano iliyomsibu yeye binafsi nje ya nchi.
Na kiongozi mwengine aliwahi kusema ndani ya Baraza la Wawakilishi kwamba laiti Wawakilishi wenzake wangeliisoma Katiba ya Muungano na kuifahamu, basi wangelishukuru kwamba bado angalau Zanzibar ina Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama. Kwa Katiba ilivyo, alisema, Zanzibar haina chake.
Na Othman Masoud Othman
Pili, wakati wa mchakato wa Katiba Inayopendekezwa kule Dodoma, mmoja wa viongozi wakuu wa sasa wa Baraza la Wawakilishi – kwa kushirikiana na wajumbe wenzake wa Kamati ya Uandishi – aliwahi kupeleka mbele ya kikao kilichoongozwa na mmoja wa viongozi wakuu wa Serikali ya sasa hivi, mambo 17 ambayo walihisi yanaibana Zanzibar katika Katiba Inayopendekezwa, lakini wajumbe wa Tanzania Bara wakiongozwa na Andrew Chenge waliyakataa katakata tena kwa ufedhuli kabisa. Aliwasilisha hoja hiyo kwa masikitiko hadi machozi yakamtoka, akikumbusha jinsi alivyodhalilishwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba wa Tanzania wakati wa mchakato wa “Katiba Inayopendekezwa.“
Baada ya mjadala mrefu, mambo 8 waliyakubali kwa kauli moja kuwa hayo ndio yawe “deal breaker” katika mchakato, yaani kwa vyoyote vile Zanzibar isiyakubali. Msimamo huo ulipata idhini ya “Serikali” ya Zanzibar.
Cha kushangaza, nadhani kipande cha ndizi kilifanya wajumbe wafatwe usiku kule Dodoma na kubadili upepo. Yaliyovuma kule Dodoma ni kuwa kumbe kipande cha ndizi chenyewe kilichotumika ni ahadi ya kupewa ugombea mwenza kwa mmoja wa viongozi wa Zanzibar wenye ushawishi na uamuzi uliotoka kutoka kwa mmoja wa wagombea watarajiwa wa Tanganyika.
Kumbe wala haikuwa ndizi bali tojo, wengine huita fumbufumbu. Wote wakageuka – wakageuka kauli zao, wakageuka misimamo yao na wakageuka hata hisia kwamba walikuwa wamekwenda kule kuwatetea wananchi wa Zanzibar ambao, kama Katiba Inayopendekezwa ingelipita, basi uhuru, historia, mila na hata silka zao zingebaki katika huruma ya mtawala. Zanzibar ikatoswa.
Katiba Inayopendekezwa na Maafa Dhidi ya Zanzibar
Tatu ni vyema tuangalie, kwa muhtasari tu, kile ambacho viongozi ambao leo wanamlaumu Profesa Kabudi walikikubali kiendelee milele dhidi ya Zanzibar kwa kupitia Katiba Inayopendekezwa. Kwa ufupi wao walishakubali kuidhalisha Zanzibar kwa kiwango cha kuiangamiza Zanzibar kwa kukubali Katiba Inayopendekezwa.
Waliyoyakubali dhidi ya Zanzibar kupitia Katiba Inayopendekezwa hayawezi hata kuwekwa katika mizania moja na aliyoyasema Profesa Kabudi, hasa ikizingatiwa kwamba aliyoyasema Profesa Kabudi ni maoni yake ndani ya Bunge, wala sio Katiba, sio Sheria, sio Kanuni wala Muongozo. Yale waliyoyakubali wao ni Katiba ya Taifa ambayo yasingeweza kubadilishwa isipokuwa kwa utaratibu ambao wao na wananchi wote wa Zanzibar hawana mamlaka nao. Ndio maana, mimi ninasema ilikuwa Katiba ya Kuiangamiza Zanzibar.
Miongoni mwa mambo waliyoyakubali chini ya Katiba Inayopendekezwa ni kama yafuatayo:
Mamlaka ya Rais wa Muungano kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na sehemu nyengine
Kwa mujibu wa [IBARA YA 2(2)] inaposomeka na ibara ya 83 ya Katiba Inayopendekezwa, Rais wa Muungano anakuwa na mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu [wadi na shehia]. Chini ya mamlaka hayo, anao uwezo wa kuongeza na kupunguza mikoa, anao uwezo wa kuiunganisha mikoa na kuwa mkoa mmoja. Chini ya mamlaka hayo, hakuna kinachomzuia Rais wa Muungano kuifanya Zanzibar kuwa mkoa mmoja au hata wilaya mmoja.
Waliokubali hilo walikuwa wakijua historia ya suala hilo. Kwamba Katiba ya Zanzibar ya 1979 iliwahi kuweka kifungu kama hicho kwa sababu ya mfumo wa chama kushika hatamu, ambapo katibu wa mkoa wa chama alikuwa pia ndiye mkuu wa mkoa. Hivyo Rais wa Zanzibar hakuwa na mamlaka peke yake kuunda mkoa, kwani akiunda mkoa wa kiserikali alikuwa anaunda mkoa pia wa kichama.
Hata hivyo, mfumo huo ulipoondolewa, Katiba ya Zanzibar ya 1979 ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria namba 9 ya 1982 ambayo ilirejesha mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu mikononi mwa Rais wa Zanzibar. Walioikubali Katiba Inayopendekezwa wakati wakijua kuna kifungu kama hicho, sijui walikusudia kumshikisha nani hatamu dhidi ya Zanzibar?
Ukuu wa Katiba ibara ya 9
“[9(1) Katiba hii ni Sheria Kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba hii.”
Kifungu hichi cha Katiba Inayopendekezwa kinazua masuala kadhaa ya msingi ambayo kwa mtu anayesimamia maslahi ya Zanzibar hawezi kukibali. Maswali hayo ni pamoja na:
Katiba ya Zanzibar nayo ni Sheria sawa na Sheria nyengine kwa madhumuni ya ibara ya 9(2) ya Katiba Inayopendekezwa? Kwa mujibu wa ufafanuzi uliowahi kutolewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Katiba ya Zanzibar ilichukuliwa kuwa sawa na sheria nyengine na hivyo haikutakiwa kupingana na Katiba ya Muungano, yumkini hata katika mambo yasiyo ya Muungano, kama kwamba Katiba ya Zanzibar inatokana na Katiba ya Muungano wakati inatokana na Hati ya Muungano;
Je, Katiba Inayopendekezwa ikipita, kifungu cha 2A cha Katiba ya Zanzibar kinachotamka kuwa Zanzibar ni nchi kitahitaji kurekebishwa au kitabatilika wenyewe kwa kufuata masharti ya ibara ya 9(2)?
Ibara ya 9(4) ya Katiba Inayopendekezwa inaeleza kuwa sheria, mila na desturi lazima zifuate Katiba hiyo [inayopendekezwa]. Je, sheria ni pamoja na Sheria za Kiislamu na je, matumizi ya Sheria za Kiislamu ni suala la Muungano?
Je, mila na desturi za Zanzibar ambayo ndiyo sehemu ya utamaduni wa Zanzibar zinafungwa na ibara ya 9(4)? Kama ni hivyo, mila na desturi za Zanzibar zitaendelea kuwa salama iwapo zitapingana na Katiba Inayopendekezwa?
Kama Katiba Inayopendekezwa ndiyo kuu kwa mambo yote, je, kutakuwa na haja ya kuwa na Katiba ya Zanzibar? Na kama itakuwepo, itakuwa na nguvu ya kikatiba au sheria sawa na sheria nyengine?
Pamoja na hatari hiyo ya kuathirika mno maslahi ya Zanzibar, bado kifungu hicho kilikubaliwa na wale ambao leo wanamlaani Profesa Kabudi.
Kwenye mfululizo huu wa vipindi vya Lima na Zaima, tunakuletea maarifa juu ya namna bora zaidi ya kutayarisha kitalu chako cha miti kwa ajili ya kupata miche bora ya shambani kwako, maana bila ya kuwa na mche bora, huwezi kupata mti unaozaa matunda kama unavyotarajia.
Kufuatia mauaji mengine ya kikatili dhidi ya diwani wake, Godfrey Luena, sasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewataka wanachama wake popote walipo kujilinda wenyewe dhidi ya mashambulizi yanayofanywa na watu ‘wasiojuilikana’, sambamba na kulitaka jeshi la polisi kueleza kwa nini lisitiliwe shaka kwa kifo cha Luena wa Kata ya Namwawala, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya hivi leo wametoa tamko lifuatalo kwa ushirikiano na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya wenye uwakilishi Tanzania na kuungwa mkono na Mwakilishi na Mabalozi wa Norwei, Kanada na Uswisi.
“Tunashuhudia kwa wasiwasi muendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayotishia nidhamu ya kidemokrasia na haki za Watanzania, katika nchi iliyojizolea umaarufu mkubwa duniani kwa utulivu, amani na uhuru.
“Tumesikitishwa na kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi mwisho wa juma lililopita Akwilina Akwilini Bafta, anayeombolezwa nchi nzima. Tunakaribisha wito wa Rais Magufuli wa uchunguzi wa haraka. Vilevile, tunatoa wito wa uchunguzi wa kina katika vifo vyote vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu. Tunatoa pole za dhati kwa familia zao zote.
“Tuna wasiwasi na ongezeko la ripoti za ukatili katika miezi ya hivi karibuni, kama vile: jaribio lililohatarisha maisha ya Mbunge Tundu Lissu; kupotea kwa watu kama mwandishi wa Habari Azory Gwanda; pamoja na mashambulio yaliyopoteza uhai wa viongozi wa serikali, wawakilishi wa vyombo vya usalama na wananchi yaliyotokea Mkoa wa Pwani ndani ya miaka miwili iliyopita.
“Tunaungana na watanzania katika kuziomba mamlaka husika, kutunza amani na usalama wa michakato ya kidemokrasia, nchi, watu wake na kuheshimu utawala wa sheria bila udhalimu.”
Chama cha Wananchi (CUF) kisiwani Pemba kimetoa onyo kali dhidi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa, Prof. Ibrahim Lipumba, kwamba asijaribu kukanyaga kisiwani huko kuendesha kile kinachoitwa “kongamano la vijana” kwenye ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo, Chake Chake, siku ya Jumamosi ya tarehe 24 Februari 2018. Chama hicho pia kimelitahadharisha jeshi la polisi, ambalo limempa ruhusa hiyo Lipumba, kwamba litabeba lawama kwa chochote kitakachotokezea. Zaidi angalia vidio hii ya Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Chake Chake, Saleh Juma.
Nimesoma barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, yenye tuhuma na vitisho vingi dhidi ya CHADEMA.
Bila kutoa ushahidi wowote na kwa kutegemea taarifa za upande mmoja tu, Msajili Mutungi ameituhumu CHADEMA kwa kufanya siasa za kibabe na vurugu na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa.
Msajili Mutungi anastahili kujibiwa hadharani na kukumbushwa mambo kadhaa. Inaelekea amejisahau sana au anafikiria Watanzania ni wajinga wasioelewa mambo yake.
Msajili wa Vyama vya Siasa amekosa sifa na uadilifu (moral authority) ya kunyooshea kidole CHADEMA au chama kingine chochote cha upinzani kuhusiana na jambo lolote linahusu Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.
Na Tundu Lissu
Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, nchi yetu imeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Vyama vya Siasa ukifanywa na Magufuli mwenyewe, mawaziri pamoja na wateule wake wengine na Jeshi la Polisi.
Mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, ambavyo ni haki ya vyama vya siasa kwa mujibu wa Sheria hiyo, imepigwa marufuku na Magufuli bila uhalali wowote. Msajili Mutungi hajawahi kukemea ukiukwaji huo wa sheria wala kutetea haki ya vyama vya siasa.
Viongozi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, wameuawa, wametekwa nyara na kupotezwa, wamepigwa risasi katika majaribio ya kuuawa, wameteswa, wamekamatwa na kushtakiwa kwa kesi za uongo.
Msajili Mutungi amekuwa bubu na kiziwi asiyesikia wala kukemea uonevu na ukandamizaji huu dhidi ya vyama anavyovisimamia.
CCM na serikali yake zimetoa hongo kurubuni madiwani, wabunge na viongozi wengine wa vyama vya upinzani kujiuzulu nafasi zao. Yote ni makosa ya maadili kwa mujibu wa sheria. Msajili Mutungi hajawahi kuliona hilo.
Polisi wameua mwanafunzi wa chuo aliyekuwa kwenye dala dala. Wamepiga risasi za moto na kujeruhi watu wengi bila sababu yoyote ya msingi.
Badala ya kukemea matumizi haya ya nguvu iliyopitiliza, Msajili Mutungi anaitishia CHADEMA iliyokuwa inadai haki yake ya kuwa mawakala kwenye vituo vya kura.
Tunajua kwa nini Msajili Mutungi hajawahi kuona makosa ya watawala wakandamizaji bali anaona makosa ya wanaokandamizwa tu.
Amefungwa macho na kuzibwa masikio na maboriti na mabanzi ya cheo chake. Ni msaka tonge anayejipendekeza kwa Magufuli ili aendelee kuwa kwenye nafasi aliyo nayo. Asitutishe.
Kwa vile anadai tumetenda makosa ya jinai, basi asubiri Mahakama zifanye maamuzi juu ya tuhuma hizi.
Yeye hawezi akawa mtoa tuhuma na jaji wa tuhuma hizo hizo. Nasikia amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, anatakiwa kuyafahamu haya.
Sasa diwani wetu huko Kilombero ameuawa kinyama. Kwa vile ni wa CHADEMA, wauaji wake ni ‘watu wasiojulikana’ na Msajili Mutungi na Jeshi la Polisi watafanya kama walivyofanya kuhusiana na wale waliojaribu kuniua kwa risasi lukuki September 7 ya mwaka jana: Nothing!!! Tusubiri na tuone kama Msajili Mutungi atatoa kauli yoyote kuhusu mauaji haya ya diwani wa CHADEMA.
Katika mazingira haya ya uonevu na ukandamizaji mkubwa, ni vyema kujikumbusha maneno ya Nelson Mandela ya mwaka 1953:
“Hakuna njia rahisi ya ukombozi mahali popote, na itabidi wengi wetu tupite mara kadhaa katika bonde la uvuli wa mauti kabla hatujafikia kilele cha matarajio yetu.”
Tangu Magufuli aingie madarakani, ametuingiza katika bonde la uvuli wa mauti. Mauaji haya na ukandamizaji huu dhidi ya vyama vya upinzani ndio bonde la uvuli wa mauti lenyewe.
Tutalipita bonde hili mara kadhaa kabla ya kupata ukombozi wa pili wa nchi yetu. Lakini tutalivuka. Hii ndio gharama halisi ya ukombozi mahali popote na katika zama zote.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Nassor Ahmed Mazrui, kimeikanusha vikali barua iliyotolewa na jeshi la polisi mkoa wa kusini Pemba, likidai kupokea barua ya CUF kuridhia kufanyika kwa kongamano kwenye ukumbi wa Makonyo, Chake Chake kisiwani Pemba hapo kesho (Jumamosi, 24 Februari 2018).
Hii hapa chini ndiyo taarifa rasmi ya CUF iliyotolewa na Mazrui:
“CUF – Chama cha Wananchi kimepokea taarifa ya ujio wa Ibrahim Lipumba kisiwani Pemba siku ya Jumamosi tarehe 24 Februari 2018, kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chake Chake Pemba kwa barua yake ya tarehe 23 Februari 2018 kwa Ofisi ya Wilaya ya CUF Chake Chake.
Makao Makuu ya CUF Zanzibar haijapeleka barua yoyote kuhusu ujio wa Lipumba kwa Jeshi la Polisi kama inavyodaiwa na barua hiyo ya Polisi.
CUF – Chama cha Wananchi kinatambua kuwa Lipumba sio kiongozi na wala sio mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa rasmi na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Chama cha Wananchi – CUF kinaamini kuwa ziara hiyo ni uchokozi wa makusudi unaofanywa na kibaraka Lipumba akishirikiana na Jeshi la Polisi. Ziara hii imekuja baada ya kufeli Jaribio la uvamizi wa Makao Makuu ya CUF Mtendeni ambalo lilikuwa na dhamira ovu sana kwa Chama.
Lengo la ziara hii ni kuwafanya wananchi, kama lilivyokuwa lile la uvamizi wa Makao Makuu Mtendeni, kututoa katika kupigania haki yao ya Ushindi Mkubwa iliyoporwa baada ya Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015.
Chama cha Wananchi-CUF kinawataka wanachama, viongozi na wapenzi wa CUF waliopo Pemba kuwa watulivu kuendelea na shughuli zao za maisha za kawaida na kupuuza kabisa ujio huo wa Lipumba.
Kama tulivyoshinda uchokozi wa kuvamiwa Makao Makuu Mtendeni tukashinde tena kwa kutokukubali kutolewa katika mstari kupitia uchokozi huu anatumiwa kibaraka Lipumba kupitia ziara yake hii ya Pemba.”
Katika sehemu ya piliya uchambuzi huu, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Othman Masoud, alianza kuvichambua vifungu vya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa kwa shangwe na kutetewa na wana-CCM wa Zanzibar mjini Dodoma. Kwenye sehemu hii, anaendelea kuvichambua vifungu hivyo. – Mhariri.
Mfumo wa Serikali Mbili [Ibara ya 73]
Ibara ya 73 ya Katiba Inayopendekezwa imeweka bayana mfumo huo. Ibara ya 75 imeweka bayana zaidi kuwa Serikali ya Muungano itasimamia mambo yote ya Muungano kwa Jamhuri ya Muungano yote na mambo yasiyo ya Muungano kwa Tanzania Bara. Mambo muhimu ya kuzingatia katika ibara hii ni kama yafuatayo:
Ibara ya 112 inaeleza kuwa mamlaka ya kuamua juu ya sera zote ni ya Serikali ya Muungano;
Ibara ya 114 inayohusu muundo wa Baraza la Mawaziri, ukiachia Rais wa Zanzibar hailazimishi kuwe na Waziri kutoka Zanzibar katika Baraza hilo;
Katika uteuzi wa Waziri Mkuu chini ya ibara ya 110 haulazimishi kushauriana na Rais wa Zanzibar;
Katika uteuzi wa mawaziri chini ya ibara ya 115, Rais wa Muungano anashauriana na Makamu wa Kwanza na Waziri Mkuu lakini Rais wa Zanzibar ambaye ni Makamu wa Pili hahusiki katika uteuzi;
Hakuna ibara inayoweka utaratibu wa namna ya kuihusisha, kuishauri au kuishirikisha Zanzibar katika kufanya maamuzi yoyote yanayohusu masuala ya Muungano;
Hakuna mfumo maalum wa kuunda Wizara za Muungano;
Hakuna bajeti wala mapato yaliyoainishwa kwa mambo yasiyo ya Muungano wala hakuna mfumo wa matumizi unaopaswa kutenganisha baina ya mapato na matumizi ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano;
Hakuna mfumo wa kikatiba unaoipa haki Zanzibar kupinga maamuzi ya kisera yatayofanywa na Serikali ya Muungano ambayo ni kinyume na maslahi ya Zanzibar;
Hakuna mfumo wa kikatiba unaoibana Serikali ya Muungano kufanya maamuzi yoyote yale kwa faida ya upande mmoja hata bila kuishirikisha Zanzibar na bila ya ridhaa ya Zanzibar;
Matokeo ya jumla ya mapungufu hayo ni kuwa Serikali ya Muungano iliyoundwa bila ya kuishirikisha Zanzibar inao uwezo wa kufanya maamuzi ya kisera na ya kiutawala bila ya ridhaa ya Zanzibar. Serikali ya Muungano inaweza kutumia rasilimali za Muungano kwa faida ya upande mmoja bila ridhaa wala kuishirikisha Zanzibar. Chini ya mfumo wa Serikali mbili unaojengwa na Katiba Inayopendekezwa, Zanzibar haimo katika Muungano bali ni sawa na iliyomo katika mahusiano ya kimahamiya (Protectorate).
Uhalali wa Rais wa Muungano kwa Upande wa Zanzibar [Ibara ya 89(6)]
Ibara ya 89, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kuwa mgombea wa Chama au mgombea binafsi. Chini ya ibara ya 89(6), mgombea urais atatangazwa ameshinda iwapo atapata zaidi ya asilimia hamsini ya kura zilizopigwa. Chini ya Katiba Inayopendekezwa, mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ni makubwa ikiwemo yale ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu.
Masharti haya yanazua maswali muhimu yafuatayo:
Kama Zanzibar ni mshirika sawa katika Muungano, kwa nini isiwe na sauti hata kidogo katika kumchagua mtu wanayemkabidhi mamlaka ya utaifa wao;
Iwapo kama Rais wa Muungano na chama chake hawakupata kura hata moja Zanzibar, uhalali wake wa kutekeleza mamlaka makubwa ya kiutawala kwa watu ambao hawakukuchagua unatokana na nini?
Iwapo Zanzibar – ambayo ni mshirika katika Muungano – haikubaliani na usimamizi wa Rais katika masuala yao yaliyopo chini ya Muungano, ina haki gani ya kikatiba au ya kisheria ya kumdhibiti Rais huyo ikiwemo tabia ya Rais huyo kuonyesha dhahiri kuikandamiza Zanzibar?
Hicho ni kielelezo tosha kuwa Zanzibar haimo katika Muungano kama mshirika bali kama mahamiya. Lakini pamoja na hayo, viongozi hao waliyakubali masharti hayo ya Katiba inayopendekezwa.
Mamlaka ya BUNGE [Ibara 134]
Ibara ya 134 ndio inayoimaliza kabisa Zanzibar. Ibara hiyo inaeleza utaratibu wa namna 3:
Kwanza, chini ya 134(1)(a)- aya hii inahusu utaratibu wa kupitisha Miswada ya inayohusu ama:
Sheria ya mambo yasiyo ya Muungano; au
Sheria ya Mambo ya Muungano yaliyomo katika Nyongeza ya Kwanza; au
Sheria ya Kubadili Katiba
Utaratibu utaotumika ni kwa kupitishwa Mswada huo ikiwa utaungwa mkono na Wabunge walio wengi.
Pili ni ibara ya 134(1)(b) – aya hii inahusu utaratibu wa kupitisha sheria inayohusu ama:
Kubadili masharti ya Katiba [ni dhahiri kuwa sharti hili limejirudia kwani ni sawa na sharti la ibara ya 134(1)(a) iliyoelezwa hapo juu];
Kubadili masharti ya jambo lililotajwa katika Nyongeza ya Pili ya Katiba [ni mambo mawili 2- kubadili masharti ya Katiba ya Muungano yanayohusu Mambo ya Muungano na kuongeza au kupunguza jambo la Muungano]
Utaratibu ni utakaotumika ni kupitishwa iwapo Mswada huo utaungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wa kila upande.
Tatu ni ibara ya 134(1)(c) – ibara hii inahusu utaratibu wa kupitisha sheria kwa mambo yaliyotajwa katika Nyongeza ya Tatu ambayo ni mambo matatu. Kwanza ni Muundo wa Jamhuri ya Muungano, pili, kuwepo au kutokuwepo Jamhuri ya Muungano na tatu ni kubadili masharti ya ibara ya 134. Utaratibu utaotumika ni wa kura ya maoni itayoungwa mkono na nusu ya wananchi wa kila upande.
Ibara hii ya Katiba Inayopendekezwa kwanza imerejea masharti ya ibara ya sasa ya 98 ya Katiba ya Muungano ambayo imekuwa ikipingwa na Zanzibar katika nyaraka, ripoti na maandiko yote. Imekuwa ikipingwa kwa sababu kadhaa lakini muhimu ni kama zifuatazo:
Inainyima kauli Zanzibar kama mshirika katika Muungano katika kuamua sheria za Mambo ya Muungano, ambazo kwanza zimependekezwa na Baraza la Mawaziri ambalo Zanzibar haina ushiriki, lakini sheria hizo ndio zinazoamua haki za kila upande katika Muungano;
Inawafanya wabunge wa Zanzibar wasiwe na kazi yoyote katika Bunge la Muungano;
Inakamilisha dhana ya kuwa Zanzibar si mshirika katika Muungano bali imo kama mahamiya.
Mifano ya namna Zanzibar ilivyoathirika na mamlaka haya ya upande mmoja katika kutunga sheria za pamoja ipo mingi sana na ndio miongoni mwa mizizi ya fitna za Muungano. Miongoni mwa Sheria za Muungano zilizotungwa bila ya ridhaa ya Zanzibar au kwa kutozingatia maoni ya Zanzibar ni pamoja na Sheria ya Tanzania Revenue Authority ya 1996, Sheria ya Benki Kuu ya 1995, Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu na Sheria ya Money Laundering ambayo ilipelekea SMZ na SMT kutofautiana katika kikao cha SADC kilichofanyika Botswana na hatimaye kupelekea Zanzibar kutunga sheria yake ya Anti-Money Laundering.
Pamoja na Ibara hii kutumika vibaya dhidi ya Zanzibar huko nyuma, ibara hii sasa imekwenda mbali zaidi kwa kuutia kufuli mfumo huu wa ajabu na kandamizi wa Muungano kwa kuulinda kuwa hauwezi kubadilishwa mpaka kwa kura ya maoni. Sijui kama kuna namna mbaya ya kukosa uadilifu kuliko mtu aliyepewa dhamana kutetea maslahi ya nchi na watu wake, kuwafunga katika dhulma ya wazi kiasi hichi. Na bado viongozi wakakubali masharti hayo.
Mambo ya Muungano
Kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ikilalamika katika mambo ya Muungano kwa sababu zifuatazo:
Wingi wa mambo ya Muungano [kiasi cha 34 kwa sasa];
Kukosa ufafanuzi wa mambo ya Muungano;
Mambo ya Muungano kuikosesha Zanzibar nyenzo za kiuchumi
Mambo ya Muungano chini ya Katiba inayopendekezwa ni 21. Mambo yote hayana ufanunuzi. Kwa mfano elimu ya juu. Unaposema Elimu ya Juu maana yake ni nini. Ni udhibiti tu au ni pamoja na mitaala, uanzishaji wa taasisi za elimu ya juu au ni pamoja na utoaji wa elimu ya juu. Jambo jengine muhimu lililoingizwa katika Orodha ya mambo ya Muungano bila ya kuwa na hata ufafanuzi ni Mawasiliano.
Kwa hakika katika ulimwengu wa leo mtu anapoinyima nchi au hata uchumi wake haki ya kudhibiti Mawasiliano anakuwa wa ajabu kabisa. Ripoti kadhaa za Benki ya Dunia zimeonyesha mchango wa Mawasiliano katika chumi za nchi na uchumi wa dunia kwa jumla.
Aidha, kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuunganika kwa teknolojia [covergency of technology] mawasiliano ndio hatma ya nchi zote. Tulipofikia sasa kila kitu kinafanywa kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano, kuanzia miamala ya fedha, usafiri wa teksi na karibuni hata friji lako nyumbani litaweza kuagiza kile kilichopungua ndani ya friji. Unajiuliza hivi waliokubali Katiba Inayopendekezwa walikubali kwa uchu wa kipande cha ndizi tu au kwa sababu ya ugonjwa mbaya zaidi ya huo?
Kukosekana kwa ufafanuzi katika Katiba juu ya mambo ya Muungano ndiko kuliko ipelekea Zanzibar ikose haki zake katika Kampuni ya Simu ya Tanzania [TTCL] wakati ilipobinafsishwa pamoja na kwamba Serikali zote mbili zilikubaliana kwa maandishi katika Ripoti ya Muafaka wa Serikali Mbili kwamba haki ya Zanzibar ipatiwe ufumbuzi.
Jambo jengine ambalo limeingizwa katika Mambo ya Muungano bila ufafanuzi na linaiangamiza Zanzibar ni katika nyenzo za kiuchumi hasa kodi.
Kwa mfano, Kodi ya mapato ndiyo nyenzo kuu ya kuendesha uchumi wowote wa kisiwa ambacho hakina rasilimali. Kodi ya mapato ndiyo nyenzo ya kuvutia mitaji na ndio nyenzo kupata mapato hata katika rasilimali za nchi.
Jambo hilo limerejeshwa katika Orodha ya Muungano kupitia Katiba Inayopendekezwa bila ya ufafanuzi wa aina yoyote. Maana yake Zanzibar ilipangiwa iendelee kubaki bila ya nyenzo hiyo muhimu ya uchumi milele.
Pamoja na kutokuwepo mabadiliko yoyote ya maana katika Mambo ya Muungano viongozi hao waliyakubali masharti hayo.
Kura ya Maoni Kubadili Muundo wa Muungano [ibara ya 134(1)(c) na Nyongeza ya Tatu
Katiba Inayopendekezwa imejenga misingi ya dhulma na kukosekana usawa na haki za washirika wa Muungano, jambo ambalo linawafanya watu wa upande mmoja wauchukie Muungano. Kwa upande wa pili, inawalazimisha dhulma hiyo iendelee mpaka pale anayedhulumu atapokubali kubadili dhulma hiyo kwa kupitia kura ya maoni
Hii ni dhulma kubwa dhidi ya Zanzibar. Haiingii akilini kwamba mtu ambaye ana kazi ya kuitetea Zanzibar akubali dhulma hiyo na kutaka kuirasimisha.
Ilipoishia shemu ya kwanza! Tuliona jinsi Abdull na Talib ambao ni ndugu walivyotoka Dodoma na kufika Dar es Salaam, baada ya mapumziko ya siku chache wakaelekea Zanzibar katika kisiwa cha Unguja. Huko wakaanza maisha, Abdull akiishi km mgonjwa wa akili na Talib akiwa na mtangamano mzuri na jamii inayomzunguka. Yote haya wanayafanya wakiwa na sababu maalum. Ndipo siku moja Abdull akiwa Forodhani akaikumbuka ile safari ya kukimbia Pemba na kukimbilia Mombasa, Kenya akiwa na kaka yake huyo…..Sasa endelea
Walipofika Nyali, Mombasa walianza maisha kwa kulala pembezoni mwa vibaraza vya nyumba za watu, wakati mwengine hufukuzwa na wenye nyumba hizo. Kula yao walikuwa wanaipata kwa kuomba omba masokoni au kutafuta mabaki mabaki ya samaki kutoka katika vyombo vya wavuvi.
Baada ya siku chache walipata akili ya kuomba kwa mmoja wa wavuvi awachukue baharini ili na wao wapate chochote kitu cha kutia mdomoni na kuhifadi mfukoni. Mzee Jabir hakuwa mkorofi, kila mmoja alimjua kwa wema wake, aliwakubalia ombi lao na kuanza kuwachukua katika shughuli zake za kivuvi.
“Hivi mnatokea wapi Mombasa hii?”, ilikuwa ni alfajiri ya awali Mzee Jabir akiwa na ndugu wawili tayari kuondoa nang’a ili kuingia baharini kwa ajili ya kuanza shuguhuli kusudiwa.
“Hatutokei Mombasa Mzee’;
“Kwahiyo mnatokea wapi?
“Kisiwa cha Pemba’
“Aaaa poleni sana, tunayasikia yanayotokea huko kipindi hiki… tumepishana na majahazi mengi tu wengine wakikimbilia Somalia”,alisema Mzee Jabir
Muda ule ulikuwa ni saa kumi na moja za jioni ndipo wavuvi wengi walipendelea kuelekea baharini kwa kipindi kile,kutokana na mahesabu yao ya kivuvi.
Na Rashid Abdallah
Siku zilianza kukatika, na maisha ya uvuvi yaliwawezesha ndugu wawili kupata chumba cha kulala na kujikimu milo yao, lakini hawakuwa wanahifadhi chochote mifukoni mwao. Hali ya maisha bado haikuwa laini kwani uvuvi wao wa dau lililokosa hata mashine, ulikuwa unawawiya vigumu kwenda kwenye maji makubwa ambako ndiko wangepata samaki wengi.
Baada ya mwezi kadhaa kukatika na hali bado haikuwa nzuri katika shughuli za kivuvi, ndipo walipopewa wazo la kuondoka na kukimbilia katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyopo kaskazini-mashariki mwa Kenya katika eneo la Garrisa.
Walikubaliana na wazo hilo kutoka kwa Mzee Jabir, kwani aliamini wangepokelewa kwa sababu kila mmoja alikuwa ameshasikia kile kilichotokea Zanzibar hasa katika kisiwa cha Pemba.
“Basi safari njema… huko pengine mtapata msaada mzuri zaidi”, Mzee Jabir alikuwa anawaaga Abdull na Talib, mapema asubuhi ,mara baada ya kuwatafutia gari la mizigo ambalo lingewafikisha Garrisa.
Safari ya kufika huko haikuwa nyepesi lakini hatimaye walifika Garrisa mchana mmoja wa siku ya Jumatano. Kisha wakapanda gari nyengine ya kuomba iliyokuwa inaelekea Dadaab.
Kambini walipokelewa mara baada ya maswali mengi mno, maofisa wa pale waliamini hali imekuwa shuari katika visiwa vya Zanzibar, hivyo walikuwa na maswali mengi mno hadi kukubali kuwapokea. Lakini hatimaye walipokelewa na kusajiliwa kama wakimbizi.
Katika kambi ya wakimbizi unafuu wa maisha unapatikana kwakuwa tu mnapata malazi ya bure na chakula cha bure, huduma nyengine pia zikiwa bure, kama afya, elimu na shughuli zinazowazunguka wakimbizi.
Kwa sababu Daadab ni kambi inayohifadhi wakimbizi wengi wa Kisomalia, hata lugha maarufu kambini pale ilikuwa ni Kisomalia, ingawa na Kiswahili hakikuachwa nyuma kikiwa na wazungumzaji wachache.
Waliishi katika hema moja na vijana wawili wa Kisomalia, ambapo mmoja wao alikuwa anaelewa Kiswahili vizuri tu. Nyakati za usiku kabla ya kulala, zilikuwa ni nyakati za kusimuliana maisha ya kila mmmoja aliyopitia hadi kufika pale.
Mohammed ambaye ndiye alijua Kiswahili vizuri , kabla ya vita havijapamba moto kule Somalia alikuwa anakwenda Mombasa mara kwa mara na Baba yake kwa shughuli za kibiashara.
Mohammed aliwasimulia mkasa wa kukosa familia yake. Ilikuwa ni siku ya jioni ya saa kumi, akiwa na familia yake wakisubiri chakula kilichokuwa kikiandaliwa na Mama yake katika nyumba yao iliyoko katika mji mdogo ulio nje kidogo ya jiji la Mogadishu, Somalia. Mohammed akiwa amempakata mdogo wake wa kiume aliyekuwa na miaka takribani sita.
Nyakati hizo ndipo kombora ambalo hajui hata lilitokea upande gani, lilipiga nyumba yao na kuifanya familia yote kuwa maiti isipokuwa yeye tu, alikosa mkono wake wa kushoto.
Mikasa kama ya Mohammed ni mingi sana katika kambi ya Dadaab. Abdull na Talib walianza kuzizoeya simulizi za namna ile. Maisha yaliendelea na siku zikikatika. Baada ya kuzoeyana na watu kadhaa na wao hawakuacha kujifunza lugha ya kisomali .
Maisha yalirudi kuwa ya furaha kwa kiasi fulani kwao, walitangamana vizuri na jamii ile, jioni hucheza mpira na kujumuika katika shughuli nyengine za eneo lile. Pia wakapata rafiki mwengine kwa jina la Ismail.
Miezi ilisonga wakiwa na rafiki yule wa Kisomalia. Kwa sababu Mohammed hakuwa mtokaji sana nje, kutokana na ulemavu aliokuwa nao, hivyo Ismail akawa ndiye rafiki yao mkubwa wakiwa nje.
“Pale Mogadishu hali imetulia kidogo sasa hivi, kuna biashara zangu tutaenda kufanya”, Ismail alikuwa akijaribu kuwashawishi Talib na Abdull, waondoke katika kambia ya Dadaab na waende Somalia.
Ismail alikuwa anawashawishi vijana hawa muda mrefu tangu kujuana nao, akiwaeleza kwamba maisha hayawezi kusonga mbele katika kambi ya wakimbizi, hivyo ni lazima wapate sehemu watakayo kuwa huru kufanya mambo ya kimaendeleo.
Ni maneno yaliyoingia akilini kwa ndugu wawili na hatimaye wakaamua kung’oa nanga zikiwa zimebaki siku tatu tu kabla ya rafiki yao Mohammed kufunga ndoa na binti mmoja wa Kisomali kutoka pale pale kambini.
Walipanda gari moja ambalo husafirisha watu kimagendo kuingia Somalia, kikawaida magari haya yalikuwa yanafika tu mpakani mwa Kenya na Somalia, hayakuwa yanavuuka kuingia mpaka wa nchi nyengine kati ya nchi hizo mbili.
Walikaa kutwa nzima katika msitu wakisubiri kiza kiingie ili wavuke mpaka kuingia Somalia, baada ya gari walilopanda kuwashusha na kuondoka. Walisubiri kiza kiingie kwani waliogopa wasije kukamatwa na wanajeshi wa Kenya au Somalia, na kuwatuhumu wanaingia Somalia kwenda kujiunga na kundi la Alshabab.
Kiza kilipoingia ndipo walipotoka na kuanza safari ya kuvuka mpaka.
“Ismail, wewe Ismail..”, Talib alikuwa anamuita Ismail aliyekuwa wa mwanzo kutoka mbele.
“Shii”, lakini alitoa ishara ya kidole katika mdomo wake, kumuashiria anyamaze na asiinue sauti. Walikuwa wanapita karibu na kizuizi cha jeshi la Somalia.
Wakiwa na nguo nyeusi wakitembemba udama udama, wakijificha na miti ya eneo hilo, hatimaye waliweza kupita salama katika eneno lile la kizuizi.
“Ulikuwa unasemaje?, aliuliza Ismail kwa ukali kidogo
“Chakula kinaelekea kuisha sasa tutatembeaje na njaa?
“Baada ya saa moja na nusu tutakutana na kijiji hapo mbeleni…usiwe na wasi wasi”, alieleza Ismail kisha kuwapa ishara wasonge mbele.
Usiku mzima ulikuwa ni wakutembea, lile saa moja na nusu waliloahidiwa lilikatika wala hakukuwa na kijiji chochote karibu. Hadi ilipofika saa kumi na moja alfajiri ndipo walipofika katika kijiji kimoja ndani ya Somalia.
Waliomba maji na chakula kutoka kwa wanakijiji hao, walikuwa wameishiwa na kila kitu.
Ilikuwa ni safari ya kupita katika ardhi isiyo na rutuba wala neema ya miti mingi. Wakati wanaingia kijijini , Ismail aliwaeleza kwamba safari yao imekuwa nzuri zaidi kwa sababu wamekwepa miale ya jua, kama wangesafiri mchana.
Halikuwa tatizo kwa Abdull na Talib kuwasiliana na Wasomali, walikuwa wanajua Kisomali tangu walipojifunza Dadaab.
Walionana na wenyeji wa kijiji na kuomba kupumzika katika msikiti mdogo ulioezekwa bati chakavu.
Majira ya saa sita za mchana kila mmoja akiwa katika usingizi mzito, walishituliwa na milio mizito ya risasi zilizokuwa zikilia nje kidogo ya kijiji kile, lakini milio ile ilizidi kusogelea kijiji kila dakika zisongapo.
“Vipi tunafanyaje sasa?, aliuliza Abdull kwa hofu kubwa
Ngoja nikaangalie kama kuna upenyo wa kutokea tutaondoka sasa hivi..”, alijibu Ismail huku akitoka na kuwaacha ndugu wawili msikitini pale, mioyo ikiwaenda mbio.
“Anaonekana haogopi!”, alisema Talib huku anachungulia nje kupitia dirisha la msikiti.
“Wamezoeya..”
Baada ya dakikia mbili Ismail alirudi na kuwataka wabebe mikoba yao, ili waondoke. Akidai kuna gari nje inaelekea Mogadishu amewaomba wenye gari na wamekubali.
Waliondoka mbio mbio na kukimbilia katika gari la pick up kisha likaanza kuondoka taratibu kukiwa na watu wengine katika gari, pia kulikuwa na bendera nyeupe imepachikwa ikipepea kutoka katika gari lile.
Iliwachukua takriban siku nne hadi kufika katika mji wa Mogadishu, njiani walikuwa wanapishana na wabeba silaha, ilikuwa inawabidi wapumzike kwa baadhi ya nyakati ili kukwepa mapigano mbele yao. Wakati fulani walikuwa wanashambuliwa licha ya bendera nyeupe iliyoashiria hawapo katika vita.
Saa mbili za jioni wakaingia Mogadishu, Ismail akiwa na Talib pamoja na Abdull. Muda mwingi wa safari ndugu hawa walikuwa kimya, hadi Ismail akawa anawashangaa, lakini kumbe ilikuwa ni hofu iliyojaa mioyoni mwao.
Ndugu wawili wakiwa na mwenyeji wao, wakashuka Xamar Jabjab, katika jiji la Mogadishu, eneo linalopepewa na mawimbi ya bahari kwa ukaribu wake, pia ni dakika chache tu kuifikia bandari kuu ya Mogadishu.
Je! safari hii ya kuelekea Mogadishu itakuwa na manufaa yoyote kwa ndugu wawili, au ni kujitia katikati ya tanuri la vita? Alichowaeleza Ismail ni cha kweli, pindi wakifika Mogadishu? Kilichowakimbiza Pemba ni kipi? Fartuun ni nani?
Kwenye sehemu ya tatuya uchambuzi huu wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, mwandishi alimalizia kuchambua baadhi ya ibara za Katiba Inayopendekezwa vinavyoiangamiza kabisa Zanzibar, licha ya kupitishwa kwa mbwebwe kubwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutokea CCM upande wa Zanzibar, ambao wengine leo hii wanamkejeli Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi, kwa kukitafsiri kile walichokipitisha kwa hiyari na ushawishi wao wenyewe kwenye Katiba Inayopendekezwa. Sasa endelea na sehemu hii ya mwisho.
Profesa Kabudi na Dhana Inayopotoshwa
Nimehisi ni wajibu kutanabahisha kwamba, pamoja na kwamba siungi mkono hata kidogo aliyoyasema Profesa Kabudi kwa vile si sahihi na hayaendani na wajibu wake wa kitaaluma na hata wa kimaadili na kiuongozi, lakini ni vyema kutafuta wapi tulipojikwaa na turekebishe. Profesa Kabudi alianza kwa kuipotosha dhana nzima ya Muungano wa Tanzania pale alipoufananisha na Muungano wa India na Ethiopia.
Na Othman Masoud Othman
Kwanza nchi hizo sio za Muungano bali ni za mfumo wa Shirikisho la kugawana mamlaka [federal arrangement]. Pili, shirikisho la nchi hizo halikutokana na muungano wa dola huru (sovereign states). Tatu, msingi mkuu wa kugawana madaraka baina ya Serikali ya Muungano (Shirikisho) na Serikali shiriki ni kile kiitwacho ugatuzi (devolution).
Kwa upande wa Muungano wa Tanzania, kwanza, umetokana na muungano wa dola huru, pili, dola hizo ziliungana kwa mkataba maalum wa kimataifa na tatu, msingi mkubwa wa kugawana madaraka baina ya Serikali ya Muungano na Serikali Shirika ya Zanzibar ni Mkataba wa Muungano, ambao uliweka mfumo wa kuhamisha madaraka (assignment of sovereign powers) kwa msingi kwamba, kwa yale madaraka yasiyohamishiwa katika Muungano, kila upande utakuwa na mamlaka kamili )exclusive powers).
Naamini kumbukumbu bado zipo jinsi nilivyofafanua katika kikao cha mawaziri wa pande mbili kule Dodoma juu ya upotoshwaji wa dhana ya Muungano katika Katiba Inayopendekezwa kwa kutaka kuingiza dhana ya devolution badala ya ile ya power assignment and exclusivity iliyoasisiwa na Mkataba wa Muungano, ambao unaeleza kwa ufasaha dhana hii.
Hata Mzee Rashid Kawawa alipokuwa akiwasilisha Mswada wa Sheria ya Kuridhia Muungano katika Bunge la Tanganyika, alitumia maneno fasaha sana katika dhana hii. Alisema wazi kuwa chini ya Mkataba wa Muungano, Zanzibar itatoa baadhi ya mambo yake na kuyaweka chini ya usimamizi wa pamoja wa Serikali ya Muungano. Kwa hivyo, chini ya msingi huo, Rais wa Muungano hawezi kuwa na residual power kwa mambo ambayo si ya Muungano kama Profesa Kabudi anavyotaka tuamini.
Pili, Profesa Kabudi anapokataa kwamba hakuna migongano katika katiba mbili, sijui anachukua wadhifa gani katika taaluma ya sheria. Maadili ya taaluma yanahitaji kuheshimu maamuzi ya mahkama za juu za nchi. Mahkama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi mbili tofauti – ile ya Seif Sharif vs SMZ [1998] TLR 48 na ile ya Machano na wenzake 17 [SMZ vs ALI [2000]1 EA 216 – imeeleza bayana kwamba ipo migongano ya wazi na ya msingi katika katiba mbili na kushauri hatua zichukuliwe kuondoa migongano hiyo.
Tatu, migongano ya kikatiba haiwezi kuondolewa kwa kuisuluhisha kwa kupora madaraka upande mmoja na kuyapeleka upande mwengine. Dawa ya migongano ni kurekebisha katiba. Mifano ipo mingi. Katiba ya Switzerland ya 1874 ilibadilishwa mwaka 1999. Ajenda kubwa iliyopelekea kubadilishwa, pamoja na mambo mengine, ni kutokuwepo bayana jinsi Serikali za Kantoni zitavyoshiriki katika mambo ya nje hasa pale sera na maamuzi ya Serikali ya Muungano yanapoathiri maslahi ya Kantoni. Katiba mpya ya 1999 iliweka bayana na kwa lugha fasaha suala hilo kupitia ibara za 55 na 56.
Aidha, Kanuni ya residual powers haiwezi kutumika kutengeneza mamlaka ambayo tokea asili yake anayedai mamlaka hayo hakupewa na Katiba au Sheria za nchi. Kutokana na kanuni hii inayodhibiti matumizi ya residual powers katika mahusiano baina ya mamlaka za nchi, ndio maana haikutumika katika muungano wa Uingereza. Pamoja na Uingereza na Scotland kuwa na miungano miwili; ule wa kifalme wa 1603 (Union of Crowns) na ule wa mkataba wa 1707 (Articles of the Union), lakini Mfalme James Stuart baada ya kuwa mfalme wa nchi zote mbili, za Scotland na England, alishindwa kuziunganisha nchi hizo mbili kwa kutumia mamlaka yake kama mfalme, ingawa yeye mwenyewe alihisi ana mamlaka hayo kwa kanuni ya residual powers.
Katika kulitekeleza hilo alifikia hata kutengeneza bendera mpya ya Muungano (Union Jack), lakini wenzake walimtanabahisha kwamba hana mamlaka ya kutumia residual powers za ufalme kwa suala hilo chini ya mfumo wa kikatiba wa nchi hizo. Ndio maana muungano wao rasmi ilibidi usubiri kwa zaidi ya miaka mia moja na hatimaye ukaanzishwa kwa kupitia mkataba wa muungano wa 1707, ambao ndio unaoipa Scotland haki ya kupiga kura ya maoni kuamua kama wanataka bado kuendelea kuwemo katika muungano kila wanapoamua kufanya hivyo. Kama Muungano huo ungeanzishwa na Mfalme Stuart kwa residual powers, Waskochi leo wasingekuwa wanafaidi uhuru wa kuamua juu ya hatma yao. Ni vyema kwa Wazanzibari nao kutahadhari sana na hichi kirusi kipya cha Muungano cha residual powers kinachotaka kupandikizwa na Profesa Kabudi.
Siamini kwamba mwalimu wangu hayafahamu haya na zaidi ya haya niliyoeleza. Labda wale viongozi wetu wa Zanzibar waliotuingiza katika mtego wa komba ndio inawezekana wanapata shida kuyafahamu haya na hata wanapofahamishwa, kwa kuwa wazi uchu wa kipande cha ndizi kinawakosesha tafakuri.
Hitimisho
Malumbano hayajawahi kuisaidia nchi yetu kutatua kero yoyote. Malumbano juu ya Muungano yamekuwa yakiendelea tokea mara tu baada ya Muungano kuasisiwa. Mwisho wa malumbano hayo, ni Zanzibar ndiyo inayopoteza, ndiyo inayozidi kuumia. Hakuna marekebisho ya maana yaliyofanyika, kwa vile ni dhahiri kwamba Muungano uliasisiwa juu ya ajenda ya siri na umekuwa ukilindwa juu ajenda na itikadi ya siri.
Viongozi wa Zanzibar ndio wenye wajibu wa kusimamia maslahi ya Zanzibar katika mahusiano haya. Inapotokea baadhi yao kuangalia maslahi yao badala ya maslahi ya nchi, ndipo Zanzibar inapoangamia.
Laiti ingekuwa katika mtego huu anayeangamia ni yule aliyefuata kipande cha ndizi tu, tungesikitika kwa vile ni mwenzetu lakini tungeweka tanga, tukatawanyika tukaendelea na mengine. Lakini, kwa bahati mbaya, mtego huu wa komba ulioingizwa Zanzibar ni tofauti. Katika mtego huu, komba anakula ndizi yake akaondoka, lakini kinachoangamia ni nchi na vizazi; dahri na milele. Bila ya shaka huu ni mtego mbaya zaidi.
TANBIHI: Hii ndiyo sehemu ya nne na ya mwisho ya mfululizo wa makala za Mwanasheria Othman Masoud Othman akiichambua dhana ya mtego wa komba na maangamizi ya Zanzibar kwenye Muungano yanayofanikishwa na wale wale waliopewa dhamana ya kuilinda Zanzibar. Tafadhali changia maoni yako kupitia hapa ama kwenye mitandao yetu ya kijamii. – Mhariri
Licha ya kwamba maafa ya Januari 2001 visiwani Zanzibar yamepita, lakini ukweli ni kuwa yamebakia hadi leo ndani ya nafsi na miili ya watu. Mmojawapo ni Bi Fathiya Zahran Salum ambaye siku ya tarehe 26 Januari 2001 imebakia kuwa na alama kubwa kwake na kwa mustakbali wake. Lakini alisimama na anaendelea kusimama hadi leo. Sikiliza simulizi yake hapa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC) ndio maadui wakubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akitabiri kwamba katika siku zijazo taasisi hizo zenye dhamana ya kusimamia uchaguzi zitaiingiza nchi kwenye maafa makubwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa wananchi wanaushinikiza uongozi wa chama hicho kuwaruhusu kutumia njia zao wenyewe kujilinda na kulipiza kisasi dhidi ya mauaji na mateso yanayofanywa kwao kutokana na sababu za kisiasa, lakini yeye na viongozi wenzake wanawazuwia kwa kuwa wanaamini kwenye ustaarabu na kuheshimiana.
Kama ambavyo polisi wana haki ya kukukamata kwa kufuata masharti ya kisheria, basi pia nawe una haki ya kupatiwa dhamana haraka iwezekanavyo kwa masharti hayo hayo ya kisheria. Msikilize Rais wa Chama cha Wanasheria cha Zanzibar (ZLS), Omar Said Shaaban, kwenye mfululizo huu wa Zaima Sheria.
Kiongozi wa kundi la Wazanzibari 40,000 waliofunguwa kesi kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rashid Salum Adi, anasema anakhofia usalama wa maisha yake na sasa ameuomba Umoja wa Mataifa kumpa ulinzi yeye na viongozi wenzake ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye kesi hiyo.
Katika barua aliyouandikia Umoja wa Mataifa na nakala yake kuonekana na Zaima Media, Adi anasema serikali na vyombo vyake, ambao ni walalamikiwa kwenye kesi hiyo inayoanza rasmi tarehe 8 Machi 2018 mjini Arusha, wameanza kutumia mbinu za kutaka kuwazuwia kufika mahakamani.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amefichua njama zilizopangwa kwenye tukio la uvamizi wa vyombo vya dola katika makao makuu ya chama chake yaliyopo Mtendeni, Mjini Unguja, wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi leo kwenye ofisi hizo, Maalim Seif amesema ushirikiano mkubwa wa wananchi na viongozi ndio ambao umezuwia njama hizo kushindwa.
Katika tukio hilo, polisi waliwaambia walinzi na viongozi wa chama hicho kuwa walikuwa na taarifa kuingizwa silaha kwenye ofisi hizo na hivyo walikwenda kupekuwa kuzitafuta.
Shirika la kutetea haki za binaadamu la LHRC nchini Tanzania linasema kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini humo ni miongoni mwa taasisi zilizoshindwa kutimiza majukumu yake kisheria kwenye chaguzi ndogo za hivi karibuni, na hivyo kuwa moja ya vyanzo vya machafuko yaliyopelekea vifo na uvunjwaji mkubwa wa haki za binaadamu.
Kampuni ya Kimataifa ya VAULT yenye Makao Makuu yake mjini Washington Marekani imeonesha nia ya kutaka kuweka Miradi ya Kiuchumi katika Ukanda wa maeneo huru ya Kiuchumi uliopo Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya VAULT Tawi la Tanzania Bwana Said Ali Said amesema Uongozi wa Kampuni hiyo umefikia uamuzi huo kutokana na maumbile mazuri ya Hifadhi ya Misitu pamoja na Fukwe za kuvutia watalii.
Bwana Said amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa VAULT iko tayari kuanza miradi yake wakati wowote kuanzia sasa iwapo itapata fursa hiyo ikilenga zaidi hapo baadae kujenga Hoteli yenye Hadhi ya nyota tano pamoja na ukumbi wa kimataifa wa mikutano.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya VAULT amesema katika hatua za awali za miradi yao imepanga kutoa ajira zaidi ya wananchi 300 wazalendo wa maeneo ya ukanda wa Micheweni kwa lengo la kuwa karibu na wananchi hao.
Naye Mwakilishi wa kampuni hiyo kutoka Washington nchini Marekani Bwana Hirsi Dirir amesema taasisi za uwekezaji pamoja na zile za miradi ya kijamii nchini Marekani zimelenga kusaidia wananchi wenye kipato cha chini katika mataifa mbali mbali duniani.
Balozi Seif akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wawili wa Kampuni ya kimataifa ya VAULT uliofika Ofisini kwake Vuga kumueleza nia yao ya kutaka kuwekeza kwenye Ukanda wa maeneo huru ya kiuchumi Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali imefarajika na muelekeo wa uwekezaji huo katika ukanda wa Micheweni ambao ni jambo zuri kwa vile litasaidia kutoa ajira kwa vijana wa Zanzibar.
Balozi Seif ameushukuru na kuupongeza Uongozi wa Kampuni ya VAULT kwa uamuzi wake wa kutaka kuwekeza kwenye ukanda wa Micheweni na kuushauri kuangalia uwezekano wa kuipa kipaumbele Miradi ya Uvuvi kwa vile visiwa vya Zanzibar vimezunguukwa na bahari sehemu zote.
Kwenye mfululizo huu wa makala za Nuru ya Tiba, leo Sheikh Sultan Al Mendhry anafafanua neema nne ambazo mwanaadamu anapokuwa nazo, huwa rahisi kwake kufanyiwa hasadi na akadhurika kwazo.