Mkononi mwangu nina kitabu kiitwacho ‘A Golden Opportunity? Justice & Respect in Mining’ (Fursa ya Dhahabu? Haki na Heshima kwenye Madini) cha mwaka 2008. Waandishi wake ni wawili – Mark Curtis na Tundu Lissu.
Ni matokeo ya utafiti uliofanywa na wawili hao wakiwa chini ya Baraza la Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na uchapishaji wake kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Kikristo la Norway.
Ndani ya kitabu hiki, namuona Lissu mpambanaji na mtaalamu akipigania rasilimali za nchi yake kwenye eneo la madini, akitetea haki za wananchi wanyonge wa kawaida, na akiipa changamoto serikali pamoja na wawekezaji kuacha ukatili, dhuluma na unyanyasaji dhidi ya wakaazi wanaozunguka au waishio katika maeneo zilipo rasilimali hizo za madini.
Simuoni Lissu msaliti wala Lissu mkurupukaji wala Lissu mpinga maendeleo kama, kwa bahati mbaya sana, wanavyotaka kutuaminisha maadui zake. Bali ndani yake, namuona Lissu mzalendo aliyetulia, mwenye maarifa na uwelewa wa anachokisimamia na anayeiona Tanzania inayopaswa kuwa na haki na usawa na neema na maendeleo.
Naacha ripoti hii hata sijaimaliza kufika kwenye mapendekezo, nageukia mitandao ya kijamii – Facebook, Instagram, Twitter, Facebook, YouTube na blogu za Tanzania. Mote nakutana na sura na habari kuhusu Lissu. Asilimia 99 ni maelezo, ufafanuzi, ushuhuda na maombi ya kumtakia apone haraka.
Namo humo simuoni Lissu aliyetengwa na watu, bali namuona Lissu aliyezungukwa na umma unaompenda na kumuhusudu. Hata wale ambao kisiasa ni mahasimu wake, nawaona japo hivyo kwenye maandishi ya mitandaoni, wakisimama naye. Wanamtakia afya ya haraka. Wanalaani janga alilokutanishwa nalo – risasi zaidi ya tano mwilini kati ya risasi zikaribiazo 40 alizorushiwa.
Nafungua televisheni za kimataifa – CNN, Al Jazeera, BBC, ABC. Nasoma magazeti ya kimataifa pia kuanzia majirani zetu wa Afrika Mashariki hadi Amerika na Ulaya. Hali ni sawa kwenye redio za ndani na za kimataifa. Habari ni Lissu.
Sifikirii kuwa hao watu waliopachikwa jina la ‘wasiojuilikana’ na au waliowatuma walifahamu awali namna ambavyo mashambulizi haya ya aibu yangeliweza kumyanyua zaidi mtu ambaye tangu hapo alishanyanyuka juu katika medani za mapambano ya haki, sheria na demokrasia.
Kiwango cha risasi zilizotumika, hapana shaka, kilikusudiwa hasa kiumalize uhai wa Lissu papo hapo na kuizika hadithi nzima ya mwanaharakati huyu mwenye kipawa cha ajabu. Lakini ukweli ni kuwa, hata kama zingefanikiwa kuyakatisha maisha yake siku ile (Mungu apishe mbali), basi zingeshindwa – kama ambavyo zimeshashindwa sasa – kumlaza chini Lissu.
Matokeo ya ‘upuuzi’ huu uliotendwa na yeyote aliyeutenda ni kuwa kile walichotaka kukizamisha, ndicho sasa wamekiibua. Kwa mfano, hadi risasi zinamiminwa kwenye gari la Lissu mnamo Alhamis ya tarehe 7 Septemba, wengi wetu – mimi nikiwa mmoja wao – hatukuwa tumesoma kazi za Lissu alizozifanya kabla ya kuingia kwenye ubunge.
Ni baada ya jaribio hili la kuuondoa uhai wake, ndipo tukaanza kusaka na kuchakuwa makabrasha ya kutaka kumfahamu zaidi Lissu anayepigania roho yake kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, Nairobi. Ndipo hapo tunakutana na maandiko kadhaa yanayoelezea alama alizowacha mwahala mote alimokanyaga shujaa huyu. Mojawapo ni hiki kitabu cha Golden Opportunity.
Wengine kwa kuona kuwa Lissu anawatoka mbele ya macho yao, wakageukia kuperuzi mtandao wa YouTube kumuangalia na kumsikiliza tena na tena yale ambayo aliyasema kipindi cha huko nyuma na hata cha karibuni zaidi.
Ukweli ni kuwa Google imepata sana matangazo ya bidhaa za wateja wake kupitia vidio za Lissu ndani ya kipindi hiki cha juma moja kuliko wakati mwengine wowote huko nyuma.
Mwandishi mmoja wa kujitegemea anayeendesha chaneli yake mwenyewe ya YouTube tangu mwaka 2014, ameniambia kuwa kwa mara ya kwanza alifikisha watazamaji 100,000 kwa vidio moja ndani ya masaa matano, baada ya kuweka vidio ya Lissu siku ya tarehe 8 Septemba, siku moja baada ya mashambulizi.
Binafsi nilikutana na Lissu kwa mara ya kwanza mwaka 2006 katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, ambapo vuguvugu la Katiba Mpya lilikuwa limeanza kupitia muungano wa vyama vya CUF, TLP, CHADEMA na NCCR-Mageuzi. Siku hiyo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa anazindua vuguvugu la kudai katiba mpya, na miongoni mwa waliohudhuria alikuwa ni yeye, Lissu.
Nakumbuka kuwa mchango wake siku hiyo uliwavutia wengi, hasa kwenye suala la Muungano na nafasi ya Zanzibar. Msimamo ulikuwa – na mara kadhaa baada ya hapo amekuwa akiurejea – kwamba Tanganyika inautumia Muungano kuikalia Zanzibar bila ridhaa ya Wazanzibari.
Ushauri wake ulikuwa lazima Wazanzibari wadai mabadiliko ya katiba ili kuubadilisha muundo wa Muungano kutoka ukaliwaji wa sasa na kuwa ushirikiano wa heshima baina ya majirani wawili wenye udugu wa damu na kihistoria. Nikiwa muumini wa Uzanzibari, nilimuamini hapo hapo, maana alikuwa anakisema kile ambacho nimekuwa nikikiamini siku nyingi.
Mara nyengine ilikuwa mwaka 2014 kisiwani Pemba, baada ya kuvunjika kwa Bunge Maalum la Katiba. Vuguvugu la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakati huo lilikuwa kwenye upya wake. Viongozi wa UKAWA walikuwa kisiwani Pemba kama sehemu ya kampeni yao kuwahamasisha wananchi kupinga kuandikiwa katiba mpya isiyokuwa na matakwa yao, mimi nilikuwa huko kwa mapumziko.
Kwa mara nyengine, alipewa jukumu la kuuzungumzia Muungano wa Tanzania, naye kwa mara nyengine akauita jina lake halisi – ukaliaji. Kwenye mkutano huo uliofanyika viwanja vya Gombani Kongwe, niliwashuhudia wazee wa Kipemba wakilia machozi kwa namna Lissu alivyokuwa akiwachoma kwa maneno yake.
Baada ya mara hizo mbili, mara nyengine kadhaa nimewasiliana naye kwa njia ya simu kikazi, nikimuomba kufanya mahojiano naye au kuwa mshiriki wa vipindi ninavyoandaa redioni. Na mote, ni nadra sana kunikatalia, labda awe na dharura kubwa sana.
Katika mazingira hayo yote niliyobahatika kukaribiana naye, Lissu aliniondolea shaka juu ya uwezo, uweledi na uzalendo wake. Alikuwa akikisema anachokiamini na kukisimamia. Na huyu ndiye Lissu anayejiuguza sasa, baada ya wabaya wake kutaka kuutoa uhai wake!
Kule visiwani Zanzibar wakati wa utawala wa Dk. Salmin Amour Juma aliyekuwa akijiita Kamando, wapinzani walikuwa wakimtania: “N’lidhani kamando wa chuma, kumbe kamando wa udongo. Tutamtoa ikulu, tukampeleke Kidombo!” Walikuwa wakikusudia kumdogosha Rais Salmin.
Lakini hata kwa maadui wa Lissu, sasa wanajuwa kuwa huyu sio tu ni wa chuma asiyevunjika, bali pia ni wa dhahabu asiyeshushika hadhi yake.
Kwa umadhubuti aliosimama nao kabla ya risasi za Alhamis, kwa mahaba aliyomiminiwa na umma wa Watanzania baada ya risasi hizo, na kwa dhamira aliyoisimamia maishani mwake mote, yote haya, yanamfanya mwanasheria, mwanasiasa na mwanaharakati huyu kuwa wa dhahabu.
Na hivyo ndivyo atakavyobakia ama awe hai au amekufa – Lissu wa dhahabu!
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHALISI la tarehe 18 Septemba 2017.
Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: CHADEMA, demokrasia, golden opportunity, haki, madini, Tanzania, Tundu Lissu
