Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all 854 articles
Browse latest View live

Aliyeupeleka Muungano mahakamani ahofia maisha yake

$
0
0

Kiongozi wa vuguvugu la Wazanzibari linalohoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rashid Salum Adi, ameuomba Umoja wa Mataifa kumpa hifadhi ya usalama wake wakati huu kesi yao ikikaribia kutajwa kwenye Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki mjini Arusha.


RC Kusini Pemba akasirishwa na matokeo ya Kidato IV

$
0
0

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman, amesema kufanya vizuri kwa skuli tatu tu kati ya zaidi ya 20 katika mitihani ya Kidato cha Nne 2017 ndani ya mkoa wake ni jambo la aibu na linalopaswa kuchukuliwa hatua kali kulirekebisha ili lisijirejee. Angalia ripoti ya Kauthar Is-haq kutoka kisiwani Pemba.

 

 

Hakuna mdharau ukweli aliyewahi kubakia salama

$
0
0

Ndugu zangu, nimeona tamko la Wizara ya Mambo ya Nje likieleza kuwa Balozi mbalimbali za Ulaya na Marekani ambazo hivi karibuni zimetoa kauli ya kukosoa mwenendo wa Serikali “hazijui hali halisi ya usalama wa nchi”. Kauli hii imenishangaza mno!

Nchi yetu imekuwa na tabia ya kijinga sana, kwamba serikali inaamini kuwa wao ndiyo wana hati miliki ya maono, mitizamo, halo halisi na mwelekeo wetu. Mtu yeyote anapotoa maoni na mtizamo wake juu ya nchi anaitwa “ametumwa”, “ana wivu”, “analeta chokochoko” “si mzalendo”, “ni mtu hatari” na mengineyo.

Katika historia ya dunia, wamiliki wa ukweli ni wananchi, wamiliki wa maono, mitizamo, mwelekeo na sisi ni nani – ni wananchi. Ndiyo maana mwananchi atakwambia “sina ajira”, mtawala atasema “huyo mvivu tu”, mwananchi atasema “sijavuna chochote shambani”, mtawala atajibu “serikali hailimi, usipovuna kufa kwa njaa”, mwananchi atasema “polisi wanatuua bila sababu”, mtawala atajibu “wanatimiza wajibu wao”.

Na Julius Mtatiro

Majibishano hayo kati ya mwananchi na mtawala yakupe picha halisi kuwa ukweli una mwenyewe, na mwenyewe ni mwananchi wa kawaida. Mtawala hawezi kuwa mkweli, dunia nzima! Watawala wakweli ni wale tu ambao nchi zao zina mifumo na vyombo huru ambavyo vinaweza kumwajibisha mtawala, vinaweza kufanya uchunguzi huru n.k.

Mauaji makubwa ambayo yanaendelea kutokea Tanzania, hali ya chuki na maneno ya kibabe kutoka kwa Rais na wasaidizi wake, mdororo na hali mbaya ya uchumi, mihimili ya dola (Bunge na Mahakama) kudhibitiwa na Rais, Vyombo vya habari huru kugeuzwa vituo vya propaganda za serikali au vichague kufungiwa…

Tume za Uchaguzi (ZEC na NEC) kugeuka kuwa matawi kindakindaki ya CCM, Jeshi letu la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa kugeuzwa kuwa vyombo vya kutumikia matakwa ya wanasiasa wa CCM na Serikali yake badala ya kuwa vyombo vya kulinda taifa zima na watu wake n.k. ndiyo hali halisi ya maisha ya Tanzania.

Hali halisi hii lazima isemwe na mabalozi wote, taasisi zote huru za kitaifa na kimataifa, viongozi wa dini zote, vyama vya siasa na kila mtanzania. Ukweli huu mkuu wa hali halisi ya maisha ya Tanzania hauwezi kubadilika kwa “tamko” la Wizara ya Mambo ya Nje, wala Tamko la Msemaji wa Serikali wala Tamko la magufuli.

Ukweli huu utasemwa kinyume chake na wamiliki halali wa ukweli (wananchi), ikiwa serikali itaamua kusimamia haki na matakwa ya ukweli unaomilikiwa na wananchi. Hakuna namna serikali itabadilisha hali hii kwa matamko bila vitendo.

Otherwise nawasihi watanzania, tuendelee kusema ukweli, tuieleze serikali ukweli, nawakumbusha kuwa hakuna serikali iliyoendelea kupuuza ukweli na ikabaki salama. Nawakumbusha tena kuwa malalamiko makubwa na manung’uniko ya sasa ni sehemu muhimu ya hatua za umma kujirejeshea haki na miliki zake.

Kwa kadri serikali inavyoendelea kudharau kelele hizi na ukweli huu, ndivyo inavyozidi kubaki na watu wachache wanaoiunga mkono (hasa Majeshi na wana CCM wenye vyeo).

Nyerere aliwahi kusema serikali zisisubiri wanaozipinga wawe wengi, maana wakati huo si majeshi wala vifaru huweza kuzuia mabadiliko ya lazima, baada ya serikali kutenda dhambi ya kudharau ukweli.

Riwaya: Safari ya Kumuua Rais – 3

$
0
0

Tuliona sehemu ya pili, Abdull na Talib walipokimbia Pemba wakaishi katika mji wa Nyali, Mombasa ya Kenya, baadaye maisha hayakuwa mazuri wakaelekea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, huku wakapata rafiki wa Kisomali kwa jina la Ismail ambaye aliwashawishi waende Mogadishu kufanya Biashara. Waliwasili Mogadishu jioni pevu baada ya safari ya siku kadhaa. Endelea..

“Karibuni Somalia, hapa ndio Mogadishu”, alisema Ismail huku wakikatiza mtaa mmoja baada ya mwengine. Walikuwa wanaelekea katika nyumba ya Ismail ambayo aliiyacha miezi mitatu tangu aondoke  Mogadishu.

Athari ya vita ilikuwa inaonekana kila wapitapo, ingawa kundi la Alshabab lilikuwa bado halijaudhibiti mji huo moja kwa moja, lakini walikuwa wakiushambulia mara kwa mara.

Licha ya mashambulizi hayo lakini mitaa ilijaa watu usiku ule, vyombo vya usafiri vikizunguka huku na kule ingawa vilikuwa vichache mno,  watu nao wamefunika mitaa kwa shughuli zao za usiku kabla ya kulala.

Baada ya mwendo wa dakika tano, ndipo walipofika katika nyumba moja ambayo iliashiria kuhamwa kwa muda kidogo. Ndiyo nyumba ya Ismail ,  ambayo aliikomea na kuiwacha kisha  akakimbilia Dadaab.

Ismail hakuwa nayo tena ile familia yake,  mke na watoto wake wawili  waliuwawa baada ya kutokea shambulio katika moja ya soko la mji wa Mogadishu,  ambako  mke wake alikuwa anafanya biashara ndogo ndogo.

“Karibuni, hapa ndio nyumbani”, aliwakaribisha baada ya kufungua kufuli iliyokuwa katika reza ya mlango.

Ilikuwa ni nyumba ya kupendeza kwa ndani, ilikosa tu matunzo kwa sababu watunzaji walipoteza maisha wakiwa sokoni.

“Nashukuru Mungu kwamba hawajaiharibu kwa mabomu”, alisema Ismail huku akivua viatu vyake.

Wakati wote huo, Abdull na Talib walikuwa kimya kama kuku wageni walioingizwa katika banda lenye wenyeji wengi. Mioyo yao   ilitafakari  imekuwaje hadi wameishia kujiingiza katika mji wa kifo.

“Kwahiyo bomu linaweza kulipuka hadi hapa?, aliuliza Abdull.

Na Rashid Abdallah

Swali ambalo lilimfanya Ismail aangue kicheko hasa kutokana na aina ya uulizaji wenyewe.  Ismail kabla ya kujibu swali hilo, alimuuliza Abdull ikiwa ameshawahi kuishi katika maeneo ya vita au la. Abdull na  hata kaka yake, hakuna ambaye amewahi kuishi katika maeneno ya vita.

“Usiwe na wasi wasi hapa utazoeya tu baada ya siku chache..”, hiyo ndio iliyokuwa jawabu ya mwisho ya Ismail wakati akiwatoa hofu Abdull na Talib.

Baada ya dakika chache aliwaacha sebuleni akiwaeleza kwamba kuna  duka la mikate mtaa wa pili ambalo huchelewa kufunga, hivyo alitaka kwenda kununua. Ismail alitoka,  nje akisikika akisalimia na mtu  ambaye walikuwa hawajaonana muda mrefu kidogo.

Abdull na Talib walikuwa wamekaa katika masofa, Abdull  amelaza kichwa chake akiangalia juu ya dari ya sebule ile,  Talib akiwa amejiinamia kwa kuweka paji lake la uso  juu ya mikono iliyokuwa juu ya magoti .

“Vipi, tunarudi tulikotoka au tunabaki hapa?, aliuliza Abdull

“Ngoja kwanza hadi jua lichomoze ndio tutapata jibu..”.

Baada ya dakika kadhaa Ismail alikuja akiwa na rundo la mikate na vinywaji kadhaa, baada ya kula ulikuwa ni wakati wa kulala. Ingawa walikuwa katika mitaa ya vita lakini usingizi ulikuja nzito sana ,ni kutokana na uchovu wa safari yenyewe.

Asubuhi kulipokucha, mara baada ya kupata chai walikaa kitako ili kuelezana mustakbali wa maisha yao pale. Wakati wakiwa Dadaab Ismail aliwaeleza kwamba alikuwa na biashara  ameziacha nchini Somalia, lakini asubuhi  aliamua kuwaweka wazi kwamba  uvuvi ndio biashara yenyewe aliyoikusudia.

Talib na Abdull wakabaki wanaangaliana wakiachia midomowazi na  kushangazwa na walichokisikia.

Alijaribu kuzishibisha akili zao  kwamba, kazi ya uvuvi katika mji wa Mogadishu inalipa sana, kwani uhitaji wa samaki ni mkubwa na wavuvi ni wachache.

Walipouliza kwanini wavuvi ni wachache. Ismail aliwaeleza ni kutokana na maharamia huko baharini , licha ya kwamba wanateka meli kubwa kubwa  lakini wakati mwengine huwalenga risasi hata wavuvi wado wadogo kwa madai wanaingilia shughuli zao za utekaji.

“Ukweli kuna mahoteli makubwa yanahitaji samaki kila siku..”

“Hatukatai kwamba kuna uhitaji wa samaki lakini hayo mazingira ya kuvua  sio rafiki”, alisema Talib huku Abdull akitikisa kichwa ishara ya kukubaliana naye.

Baada ya mazungumzo marefu, hatimaye walikubaliana kwamba wangefanya kazi ya uvuvi pamoja, licha ya kuzongwa na hatari nyingi.

Ismail aliwaacha Abdull na Talib nyumbani , yeye akaelekea bandarini kwenda kufatilia boti lake la mashine ambalo alikuwa amelihifadhi kwa rafiki yake .

Si Abdull wala Talib ambaye moyo wake uliwafikiana na maisha yale mapya, lakini walikubali kwa shingo upande   hawakuwa na namna ya kufanya, hawakuwa na uwezo wa kutoka pale Mogadishu na kurudi Dadaab, wakajikuta wanakubaliana na hali bila mioyo yao  kupenda.

Baada ya masaa kadhaa Ismail alirudi akiwa na vifaa vya uvuvi. Baada ya mapumziko ya siku chache, jioni ya siku ya mwisho kabla ya kuingia katika kazi ya uvuvi rasmi. Ismail   aliamua kuwatoa na kuwatembeza katika mji wa Mogadishu, akiwapitisha katika masoko na mahoteli ambayo anaamini biashara yao ya kuuza samaki wanaweza kuifanyia huko.

Hali ya amani inapofunika Mogadishu, mji huo hunawiri kwa uzuri wake, mabinti wazuri wa Kisomali wanaokatisha huku na kule wakiwa katika shughuli zao, hufanya mji huo uzidi kupendeza. Mabinti hao hugeuka na kuwa kama  njiwa  wazuri wanaoupendezesha mji huo.

Uzuri wa mabinti wa Kisomali na rangi zao za mchanganyiko, zilimfanya Abdull akumbuke kwao Pemba, zile shungi na mabaibui hadi chini zilimfanya azame zaidi katika mawazo akidhani anapita katika mji wa Chake Chake na Wete.

Kabla jua kuzama walikuwa wameketi katika fukwe za Sekondo Lido, fukwe maarufu katika mji wa Mogadishu. Walikuwa wanashuhudia uzuri wa jua linavyozama taratibu.

Vijana wa kiume walikuwa wameenea katika fukwe zile wakiogelea, familia za kisomali zilijazana jioni  zikifurahia mawimbi na upepo wa  bahari ya Hindi, pia wakipoza vidonda vya kupotelewa na wapendwa wao.

Adhana, miito kwa ajili ya swala, zilizokuwa zikiita kutoka kila upande ya mji wa Mogadishu ndizo zilizowainua kutoka katika fukwe . Waliporudi nyumbani   Ismail akawakumbusha Talib na Abdull kwamba kesho asubuhi na mapema  ndio siku ya mwanzo wataanza kazi ya uvuvi.

Kazi ya uvuvi na biashara ya kuuza samaki ilianza kwa uzuri sana, kile walichokuwa wanaambwa na Ismail walikuwa wanakishuhudia wenyewe, uhitaji wa samaki ulikuwa ni mkubwa sana, biashara ilinawiri na kustawi kama mgomba unaotiliwa maji.

Miezi kadhaa ilikatika wakiendelea na kazi yao vizur tu, siku moja Ismail aliwachukua ndugu wawili na kuwapeleka katika mgawaha, ilikuwa ni jioni, aliwaeleza kwamba kuna jambo muhimu inabidi walielewe.

“Kabla sijaendelea, Abdull una umri gani?, aliuliza Ismail huku akiinua sharubati iliyokuwa katika glasi nyembamba ndefu.

“22 kwa sasa”,

“Sawa, kwa sababu umri wako bado ni mdogo… ningetoa ushauri mwakani uingie chuo”,

“Hilo tutalitafakari… kwanza tueleze hilo lako”, alidakia Talib

“Ukweli ni kwamba mimi nataka kuondoka na hii kazi nitawaachia muedelee”

Wote walishangazwa na kauli hii, lakini yalikuwa ni maamuzi ya Ismail tangu yupo Daadab, kuimarika kwa maisha ya hawa watu wawili  kupitia biashara ya kuuza samaki, ndio jambo pekee lililomchelewesa asiende  safari aliyokusudia.

Kwa Ismail halikuwa jambo zuri kuwatelekeza katika mji wa Mogadishu bila ya kuwapa msingi wa maisha. Baada ya msingi wa maisha kukamilika, ndipo alipowaaga akigoma kuwaeleza anaelekea wapi.

Abdull na Talib walibaki kupigwa na butwaa, kilichowaumiza kichwa zaidi ni pale waliposhindwa kuelewa anaenda wapi, alikuwa anawaaga kwa kuwaambia kwamba hategemei kurudi kwa miaka ya karibuni hata ikitokezea akirudi basi ni baada ya kipindi kirefu kupita.

Mazungumzo yote yalikuwa yakiendelea katika mgahawa mmoja uliopo karibu tu na bahari ya hindi.

Zilikuwa ni habari za kusikitisha kwa ndugu  wawili, walizokuwa wakizipokea kutoka kwa kaka yao, rafiki yao, mwenyeji wao katika mji ule wa Mogadishu. Licha ya  biashara yao ya kuuza samaki kunawiri, lakini mioyoni waliamini bado wanahitaji uwepo wa Ismail.

Waliondoka katika mgahawa baada ya chakula, siku ikiwa imeharibika kwao.Asubuhi kulipokucha walikubaliana na maamuzi ya Ismail kwa shingo upande, wakati Ismail akikunja nguo zake hawakuwa na uwezo tena wa kumzuiya.

“Ikitokea siku mnataka kurudi nyumbani kwenu,  hii nyumba mtakwenda kuiweka Waqfu ili iwe mali ya Waislamu”, yalikuwa ni maagizo ya mwisho Ismail akayatoa akiwapungia mkono wa kuwaaga.

Aliondoka na kutokemea kusikojuulikana, aligoma hata kusindikizwa, baada ya dakika chache Abdull na Talib walianza maisha wakiwa wawili bila ya  Ismail.

Waliendelea na bishara yao kama kawaida, kwa sababu ya kupata kipato cha kuridhisha waliamua kuikuza na  kuajiri vijana kadhaa wa Kisomalia, hakuna mtu aliyeelewa kwamba wao hawakuwa Wasomalia.

Changamoto za uvuvi katika bahari ya Somalia zilikuwa zinawakumba mara kwa mara lakini hawakukata tamaa. Mwisho wakawa wavuvi na wafanya biashara wa samaki maarufu katika eneno la lote la Jabjab na maeneo mengine ya Mogadishu.

Mwaka ukakaribia kumaliza tangu waingie Somalia. Talib alifunga ndoa na binti mmoja wa Kisomali,  Abdull akaendelea kubaki kuwa barobaro, akisimamia biashara yao kwa kiasi kikubwa.

Lile wazo la Ismail kwamba Abdull aende chuo kusoma, Talib alikubali kulifanyia kazi. Mwaka wa masomo ulipoanza alienda kumpeleka katika Chuo Kikuu cha Simad, kilichopo katika eneo la Jidka Warshadaha, katika mji wa Mogadishu.

Nini kitafuata baada ya Abdull kuingia chuoni? Je, wataelewa Ismail kaenda wapi na kwanini? Sababu ipi hasa iliwakimbiza Pemba? Fartuun ni nan katika maisha ya ndugu hawa wawili? Je, hali ikoje siku Abdull atakapotoka katika dimbwi hili la fikra za maisha yake ya nyumba, na kujikuta yupo Unguja akiwa na kazi ya kutisha mikononi mwake inamsubiri? Tukutane wiki ijayo..

Watoto wenye ulemavu wapatiwa njia nyepesi kujifunza

$
0
0

Katika jitihada ya kuliwezesha kundi kubwa la watoto wenye ulemavu na wale waliotoka kwenye mazingira magumu, Maktaba Kuu nchini Tanzania imeanzisha utaratibu wa kuwapitia mashuleni na mitaani watoto na wanafunzi kwa lengo la kuwafunza masomo mbalimbali kwa njia za kisasa.

 

Viongozi 5 wa Uamsho ‘waachiliwa’

$
0
0

Viongozi watano wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar waliokuwa wametoweka kwenye mazingira ya kutatanisha zaidi ya wiki tatu sasa, wameachiliwa na kurejea majumbani kwao katika mazingira pia ya kutatanisha.

Mmoja wa viongozi hao, Amir Haji Khamis, akizungumza kwa hali ya huzuni na wasiwasi, ameiambia Zaima Media hivi leo kwamba hawawezi kuzungumzia zaidi ya kushukuru kwamba sasa yuko huru na kwamba waliomkamata hawakumuuliza kitu chochote.

“Itoshe tu kuwa tuko salama. Hatuwezi kusema lolote zaidi,” alisema kiongozi huyo ambaye alitoweka tangu mwanzoni mwa mwezi Februari 2018.

ANGALIA VIDIO: Viongozi wengine wa Uamsho watoweka, familia yawasaka, polisi wakanusha kuwashikilia

Jeshi la polisi lilikanusha tangu awali kuhusika na kuwakamata viongozi hao, ambao kwa mujibu wa mke wa Amir Haji waliwahi kuitwa na polisi kutakiwa awache kukusanya michango kwa ajili ya familia za viongozi wenzao walioko mahabusu Tanzania Bara kwa takribani mwaka wa nne sasa.

Akizungumza kwa njia ya simu na Zaima Media muda mfupi baada ya taarifa za kuachiliwa kwa viongozi hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassar Nasser, alirejea kauli yake ya awali kwamba jeshi lake halikuhusika na ukamataji wao na hivyo halijui chochote kuhusu kuachiliwa kwao.

 

Majini wasilimishwa Zanzibar

$
0
0

Katika sehemu hii ya mfululizo wa makala za tiba, mbali ya kuendelea kuchambua mambo yanayoweza kupelekea mtu kukumbwa na hasad, Sheikh Sultan Al Mindhry anasimulia nafasi ya toba na kisa cha yeye kuwasilimisha majini waliomwendea kukiri makosa yao na kutaka kurejea kwa Mungu.

ANGALIA VIDIO: Neema zinazoweza kukusababishia ufanyiwe hasad

Wakaazi Dar walalamikia giza mitaani

$
0
0

Licha ya juhudi kubwa za kuisaidia Tanzania kupitia miradi mbali mbali inayofadhiliwa kimataifa, mingi mingoni mwa miradi hio hufa muda mfupi baada ya kuanzishwa. Mwaka 2005, Benki ya Dunia ilitowa ufadhili wa mabilioni kadhaa kupitia ‘Mradi wa SP’, ambao ulikuwa makhsusi kwa uwekaji wa taa za barabarani kwenye mitaa na wilaya kadhaa jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, taa hizo ziliwaka kwa wiki moja na baada ya hapo hakuna kilichoendelea tena, huku baadhi ya vifaa vikitoweka taratibu. Sasa wananchi wanalalamika.

 

ANGALIA VIDIO: Watoto wenye ulemavu wapatiwa njia za kisasa kujifunza


Mfumko wa bei washuka Zanzibar

$
0
0

Licha ya wananchi visiwani Zanzibar kulalamika kuwa hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kila uchao, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu inasema kuwa mfumko wa bei umeshuka kutoka asilimia 5.2 mwezi Januari hadi 4.8 mwezi wa Febuari 2018, ambapo bidhaa za chakula zimeshuka kwa .5 kutoka asilimia 1.8 kwa Januari hadi 1.3 kwa Februari 2018. Mshuko huo wa bei umeshuhudiwa pia kwenye bidhaa nyengine, na pia pakiripotiwa ongezeko la uimara wa soko.

 

Kesi ya kupinga Muungano kuanza kesho Arusha

$
0
0

Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) imeanza kusikiliza kesi zilizofunguliwa na watu binafsi pamoja na mashirika mbalimbali dhidi ya nchi wanachama wa jumuiya na zinatarajiwa kuuanza kusikilizwa hadi Machi 29 mwaka huu.

Kati ya kesi zinazotarajiwa kuvuta hisia za wengi ni kesi namba 7 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Rashid Salum Adiy na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Muungano itakayosikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Monica Mugenyi.

Majaji wengine ni Fakihi Jundu na Charles Nyawello watatoa uamuzi wa awali wa mpeleka maombi aliyetaka mahakama hiyo ihamishie kwa muda kikao chake Zanzibar ili kuwawezesha wananchi wengi kuhudhuria.

Taarifa iliyotolewa leo kwa waandishi wa habari na Msajili wa Mahakama hiyo, Yufnalis Okubo ilisema pia kesi namba 2 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) itasikilizwa Machi 13 mwaka huu.

Walalamikaji wengine ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) huku mahakama hiyo ikitarajiwa kusikiliza maelezo ya awali juu ya hoja zitakazobishaniwa .

Kesi hiyo ambayo waleta maombi wanadai sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 inaminya uhuru wa kupata na kutoa habari hivyo kukiuka Itifaki iliyoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ibara ya 6,7 na 8 kwa pamoja zinazotoa haki hizo.

Katika hatua nyingine Mahakama hiyo pia imesema Machi 14 mwaka huu itasikiliza kesi namba 15 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Baraza la Serikali ya Kijiji cha Ololosokwan wilayani Ngorongoro na watu wengine watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa na majaji watano wakiongozwa na Jaji Monica Mugenyi, Dk Faustine Ntezilyalo, Fakihi Jundu, Audace Ngiye na Dk Charles Nyawelo. Walalamika wanadai haki zao kukiukwa kwa kuhamishwa kwa nguvu kwenye kijiji chao chenye hati halali za usajili.

Mawakili wawili, Donald Deya na Nicholaus Opiyo wa taasisi ya Pan African Lawyers Union (Palu) wanawawakilisha walalamikaji ambao ni vijiji vinne ambavyo ni Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arash.

Pia kesi namba 7 ya mwaka 2016 inayotarajiwa kusikilizwa Machi 22 mwaka huu iliyofunguliwa na Mhariri Mtendaji wa Mseto & Hali Halisi Publishers Limited dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Chanzo: Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwananchi la tarehe 6 Februari 2018 ikiwa na kichwa cha habari “Kesi nne kutikisa Mahakama ya Afrika Mashariki”

Mahakama ya Afrika Mashariki yaliondoa ombi la kesi ya Muungano

$
0
0

Majaji katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki mjini Arusha wameliondoa ombi la walalamikaji wa kesi inayopinga uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutaka, pamoja na mengine, kesi hiyo isikilizwe hiyo visiwani Zanzibar kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kwenye uwasilishwaji wake.

Akizungumza kwa njia ya simu na Zaima Media akiwa Arusha, mlalamikaji mkuu kwenye kesi hiyo, Rashid Salum Adi anayewakilisha wenzake 39,999, amesema baada ya kesi hiyo kuwasili mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na pingamizi za kila upande kusikilizwa na kujibiwa, imekubalika kuwa uwasilishwaji wa maombi yao ulikosa mambo ya msingi, ambayo yanahitajika kuwepo.

“Tumefika mahakamani lakini mahakama imekataa kuendelea kulisikiliza shauri letu kutokana na mapungufu yaliyotokea kwa wetu,” alisema Adi.

Licha ya kuondolewa kwa maombi yao kwa muda, kesi yenyewe ya msingi ambayo inahoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bado ipo pale pale na Adi aliiambia Zaima Media kwamba kufika kwao kwenye mahakama hiyo na kuwasilikiza wapinzani wao (upande wa serikali zote mbili) kumewasaidia “kuujuwa uzito na wepesi wao na woga wao pia.”

Kwa mujibu wa Adi, wanatazamia kurudi tena mahakamani hapo ndani ya kipindi cha wiki mbili kutoka sasa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza.

“Tuna haki ndani ya wiki mbili kuliwasilisha tena mahakamani, na tunategemea kufanya hivyo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu,” alisema.

 

 

 

Adi afafanua kile hasa kilichotokea kesi ya Muungano EACJ

$
0
0

Kiongozi wa Wazanzibari 40,000 waliofungua kesi ya kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Rashid Salum Adi, amefafanua kwa kina kile hasa kilichotokea jana kwenye mahakama hiyo mjini Arusha, wakati kesi yao ilipotajwa kwa mara ya kwanza kabisa kwa kutanguliza ombi la awali ambalo liliondolewa na majaji wa mahakama hiyo kutokana na mapungufu ya kisheria.

 

Soma taarifa yake rasmi kwa vyombo vya habari hapo chini:

TARIFA RASMI JUU YA MAAMUZI YALIYOTOLEWA NA MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI KUHUSU KESI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR.

Tarehe 09/03/2018

Jana tarehe 08/03/2018 Kesi namba 9/2016 ya madai ya Uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyofunguliwa na Wazanzibari wapatao 40,000 ilisikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Afrika Mashariki – Arusha, mbele ya Jaji Monica Mugenyi, Fakihi Jundu na Charles Nyawello.

Kwa upande wa walalamikaji, Rashid Salum Ady aliongoza timu ya Wawakilishi wa Wazanzibari hao wapatao 40,000 ambapo kwa upande wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hawakuhudhuria Mahakamani hapo na badala yake walipeleka wawakilishi wao.

Katika kesi hiyo, Jana ilikua ni siku ya kusikilizwa kwa Shauri namba Saba (applications no.7) la kesi hiyo ambalo kimsingi, pamoja na mambo mengine Shauri hilo linaiomba Mahakama hiyo ya Afrika Mashariki kuhamishia vikao vyake nchini Zanzibar ili kuendelea kuisikiliza kesi hiyo Visiwani humo. Mahakama ya Afrika Mashariki inayo uwezo huwo na imekua ikisikiliza kesi zake katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki zikiwemo Kenya na Uganda ambazo baadhi Mahakama hiyo imefungua matawi yake.

Ady na wenzake wameiomba Mahakama hiyo kufanya hivyo ili Wazanzibari waliofungua kesi hiyo waweze kuisikiliza kesi yao pamoja na kuweza kuifatilia.

Pia, katika Shauri hilo Ady ameiomba Mahakama ya Afrika Mashariki iwapatie ulinzi kipindi chote cha usikilizwaji na ughairishwaji wa kesi hiyo na kuiomba Mahakama hiyo iweke zuio kwa Serikali ya Tanzania isiendelee kutumia fursa za Muungano, kwavile tayari kuna kesi Mahakamani inayohoji Uhalali wa Muungano husika.

Kwa mujibu wa Ady ni kwamba, kwasasa Serikali ya Tanzania inapaswa kuacha kujishughulisha na maswala yote yanayohusu Muungano mpaka pale kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Hata hivyo, baada ya kupitiwa kwa maombi hayo, kulionekana kasoro ndogo ndogo ambazo Mahakama hiyo iliwaamuru Walalamikaji kwenda kuziweka sawa kasoro hizo na kurudi tena baada ya wiki mbili kwa ajili ya kusikilizwa rasmi kwa Shauri hilo.

NB:
Jana ilikua ni siku ya kusikilizwa kwa Shauri namba 7 tu na sio kesi ya msingi. Kesi yenyewe haijaanza kusikilizwa Hadi yatakapomaliza kusikilizwa maombi ya awali ya pande zote mbili za Wazanzibari na Serikali.

Imetolewa Na:

Rashid Salum Ady,
(Kiongozi wa Wazanzibari waliofungua kesi EACJ).

Uhuru na Raila wafikia muafaka

$
0
0

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga, wamefanya mazungumzo katika ofisi ya rais jijini Nairobi mchana huu, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu ufanyike mwaka uliopita. Wanasiasa hao wameafikiana kuweka kando tofauti zao za kisasa na badala yake kulijenga taifa, baada ya jamii ya Wakenya kugawika kutokana na matokeo ya uchaguzi huku upinzani ukishikilia kutomkutambua Kenyatta kama rais halali.

 

 

Siku ya Jumuiya ya Madola kuadhimishwa Zanzibar

$
0
0

Chama Cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Tawi la Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Wabunge Wanawake wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Zanzibar watafanya maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Madola Duniani hapo Machi 12.

 

 

Kwa nini hupaswi kutumia ushirikina hata unapodhurika kwa ushirikina?

$
0
0

Katika sehemu hii ya mfululizo wa makala za tiba, leo Sheikh Sultan Al Mendhry anakuelezea sababu muhimu za kuepuka kutumia matibabu yanayomshirikisha Mwenyezi Mungu hata pale ambapo umegunduwa kwamba umesibika na matatizo ya kishirikina. Endelea kumfuatilia.


Riwaya: Safari ya Kumuua Rais – 4

$
0
0

Tuliona sehemu iliyoisha Baada ya ndugu wawili kutoka Daadab na kuingia Mohadishu wakiwa na Ismail, wakaanza maisha ya uvuvi hapo, lakini ghafla mwenyeji wao akawaaga na kuondoka bila kusema anaenda wapi, lkn wao waliendelea vyema na uvuvi ambao uliwaingizia kipato kizuri,hadi Abdull akaanza chuo. Endelea…

Akiwa katika Chuo Kikuu cha Simad , Abudull alianza vyema chuo akajipatia marafiki wengi ambao walikuwa ni wanafunzi wenzake.

Idadi ya marafiki iliongezeka. Mmoja wa rafiki zake wakubwa alikuwa ni  Kassim ambaye aliishia karibu tu na Chuo.

Ulikuwa ni urafiki mkubwa mno,  hadi wakutembeleana katika familia zao, wakawa pia hawaachi kufanya mazoezi pamoja kila jioni.

Baba yake Kassim ni mwanajeshi mkubwa katika jeshi la Somalia, hapo ndipo Abdull alipofundishwa kushika silaha kwa mara ya kwanza.

Siku za Jumamosi na Jumapili Baba yake Kassim hutoka nje ya mji wa Mogadishu kwenda kuwinda ndege akiwa na Kassim na Abdull, tangu Abdull  anaogopa silaha hadi akaizoeya na kuwa mlenga shabaha mzuri sana.

Miezi ilikatika, biashara yao na kaka yake bado iliendelea kuwaendesha vizuri kimaisha na yeye akifanya vizuri pia masomoni.

Akafika mwaka wa pili Chuoni akichukua shahada ya Ualimu katika masomo ya Biology na Chemistry.

Kwa sababu ya kushiriki kazi za nguvu baharini na kuanza kupenda mazoezi tangu akutane na Kassim, akaanza kuwa na umbile la kuvutia sana, kifua kilichojaza na mwili mpana.

“Asalam aleykum”, ilikuwa ni salamu kutoka kwa binti mmoja aliyesima mbele ya Abdull. Ulikuwa ni wakati wa jioni, siku ile Abdull alienda kupumzika katika fukwe za Sekondo Lido, ilikuwa ni siku ya mwisho ya mapumziko ya katikati ya mwaka, kabla ya kurudi tena chuoni kwa muhula wa mwisho wa mwaka wa pili.

Licha ya kupumzika pia alikuwa anasubiri boti lao la uvuvi, kwani kundi la wavuvi wakiongozwa na Kaka yake, walienda asubuhi na kuahidi watarudi saa moja za jioni. Akiwa amevaa kaptula lilofunika magoti na fulani nyekundu, Abdull alikuwa ameketi katika jiwe dogo ufukweni pale.

“Waleykum salaam”, alitikia huku macho yake yakigongana na ya binti yule.

“Samahani lakini ni kama nakukumbuka ama nimewahi kukuona sehemu”, alisema binti yule  akitabasamu na kuzungusha kichwa chake huku na kule ishara ya aibu kidogo.

“Umeniona wapi?

“Simad University”.

“Sim..yap yawezekana kweli, nasoma pale, na wewe unasoma pale  pia?

“Ndio nasoma , nimewahi kukuona mara kadhaa..kuna siku nilikusalimia lakini hukuitikia..”.

“Oooh samahani…nadhani sikukusikia huenda mawazo mengi…”.

“Haina shida hata nami nilijipa matumaini kwamba hukunisikia..”

Baada ya kusalimiana hatimaye wakatambulishana majina yao, binti yule alimwambia Abdull kwamba yeye anaitwa Fartuun, alikuja ufukweni siku ile akiwa na marafiki zake.

Aliaga na kuondoka  nyuma akiacha anga yote imefunikwa na harufu nzuri ya manukato ambayo alikuwa amejipulizia.

“Mhh, hawa sio watu ..” ,Abdull alibaki anajisemea moyoni, baada ya dakika chache na yeye akaamua kuondoka eneo lile kwa hofu aliyokuwa nayo.

Alirudi nyumbani  , njia alimuandikia ujumbe mfupi wa simu Kaka yake, akimueleza kwamba watakapo karibia bandarini amjulishe.

Kumbe Abdull aliondoka ufukweni akiwa na hofu kwamba, yule binti aliyemtokezea hakuwa binaadamu, alipofika nyumbani kwao akabaki kumuuliza shemeji yake ambaye ndiye mke wa Talib, maswali magumu

“Kwanini unauliza hivyo sehemeji yangu?

“Yaani leo siamini, jini amenijia uso kwa uso..nilikuwa nimekaa hapo kwenye fukwe za Lido..”.

“Sasa wewe umejuaje kama ni jini?

“Majini wanajuulikana shem…kwanza Masha-Allah anavutia… eti anasema amewahi kunisalimia pale chuoni lakini sikuitikia…

Anadai kwamba siku aliyosalimiwa na Fartuun yeye haikukumbuki kabisa, akisistiza hana tabia ya kudharau salamu za watu, pia hakumbuki kuiyona sura ile sehemu yoyote.

Abdull aliendelea kulalama huku kijasho kikimtoka, mkononi ameshika gilasi ya maji akilainisha koo lake taratibu.

“Usiwe na wasi wasi..”, mke wa Talib aliendelea kumtoa hofu

“..halafu alivyokuwa  ananukia mafuta mazuri balaa yaani jini..nimemshitukia tu..”

Ni maelezo yaliyofanya mke wa Talib kucheka na kutabasamu, akaendelea kumsisitiza apunguze hofu,  akimueleza kwamba katika ufukwe ule watu wengi hufika kwa ajili ya mapumziko.

Baada ya dakika chache Abdulll alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa kaka yake, ulioeleza kakaribia kwao katika bandari ya Mogadishu. Shughuli zote za usiku ule za kumsaidia kaka yake, alizifanya akiwa na mawazo pomoni kichwani mwake.

Hata alipokuwa kitandani kuutafuta usingizi ili aamke siku nyengine, bado mawazo yalimsonga akiamini kwa udhati kwamba kakutana na jini la kike katika fukwe.

Akizikumbuka zile hadithi za utotoni kwake; majini wanapenda sehemu za bahari na fukwe,wanavutia sana,  pia hupenda kunukia. Ni mambo  yaliyozidi kuuchanganya ubongo wa hadi akachelewa kupata usingizi.

Hata baada ya chuo kufunguliwa, aliongeza wiki nzima ya kukaa nyumbani. Baada ya wiki kupita ndipo asubuhi ya Jumatatu baada ya jua kuchomoza,  akajitayarisha na kuelekea chuoni, huku akiwa na hamu iliyochanganyika na hofu moyoni mwake.

Baada ya dakika kadhaa alikuwa tayari ameshawasili chuoni, akiingia kupitia geti kuu, akizungusha kichwa chake upande huu na ule, kana kwamba kuna mtu anamtafuta,  hakuwa mwengine aliyekuwa akimtafuta isipokuwa ni sura ya Fartuun.

Lakini hakufanikiwa kumuona, akaingia darasani alipomaliza kipindi akaelekea katika mjengo mlo wa  chuo ili kupata kifungua kinywa, bado alikuwa akijitahid kuzungusha kichwa chake akitegemea atainasa sura ya binti yule.

Hadi mchana anaondoka chuoni hakumuona , moyo wake ukazidi mashaka, lakini akaamua kulipotezea suala lile kidogo kidogo.

“Vipi umemuona huko chuoni? , mke wa Talib  alimuuliza Abdul,baada ya kufika nyumbani.

“Hutoamini, sijamuona..lakini bora tuache ni kheri tuipotezee hii hadithi sitaki hata kaka ajue..”

Wiki ikakatika  Abdull akienda chuoni wala hamuoni Fartuun,binti aliyemwambia kwamba nayeye anasoma chuo kile. Zile safari za kwenda akipumzika ufukweni akazipunguza pia. Siku mbili za mwanzo wa wiki iliyofuata hakuenda chuo  kwa sababu mafua yalikuwa yanamsumbua , siku ya tatu ndipo alipoingia chuoni tena.

Asubuhi na mapema kabla hajaingia darasani akakutana na rafiki yake Kassim, aliyempa taarifa kwamba kuna binti alikuwa anamuulizia siku mbili ambazo hakuwepo chuoni.

“Anaitwa nani?, aliuliza Abdull

“anaitwa Fartuun..”

Ni jina lililoshitua moyo wake kwa mara nyengine , akabaki akitoa macho bila ya hata neno moja kumtoka kinywani mwake.

“Alitaka nimpe namba yako ya simu lakini nikamzungusha kwanza, si unajua mpaka unambie mwenyewe..”

“Vizuri kwa vile hukumpa..”

“Lakini kanambia  umfate, yeye anasoma madarasa yaliyo karibu na maabara …”

Abdull alibaki anaitika kwa roho ya unyonge taarifa alizokuwa anapewa na rafiki yake, nywele za mikononi zikaanza kumsimama kwa hofu na hamu ya kutaka kuonana naye, ili roho yake ijue moja.

Aliondoka na kuelekea sehemu ya mapumziko hata darasani hakuenda tena, akimuacha Kassim akielekea darasani kwa ajili ya kipindi. Hakukuwa na watu wengi wakati ule, aliamua kutoa moja ya kitabu na kuanza kusoma, ili kurusha mawazo.

Lakini kila mstari anaougusa, kulikuwa na swali linakuja kichwani mwake, akijiuliza kuhusu Fartuun. Hazikupita dakika nyingi ghafla  akamuona binti anakuja upande ambao alikuwa amekaa.

“Fartuun anasema umsubiri ..”, ndio ujumbe aliokuja kuuwacha binti yule baada ya salamu kisha akaondoka na kurudi alikotoka.

Ni ujumbe uliomuacha Abdull akiendelea kutafakari, na kuzama zaidi katika tafakuri hadi akahisi anapotea katika taswira ya mazingira yale.

Lakini baada ya robo saa, macho ya Abdull yaligongana na binti yule yule ambaye alimuona kule fukweni

Na Rashid Abdallah

akivuta hatua kuelekea alipo

“Abdull , hujambo?, aliuliza Fartuun kwa uchangamfu kabisa huku akitabasamu

“Sijambo,  na wewe mzima?

“Mzima, rafiki yako alinambia unaumwa , vipi hali yako..?

“Niko vizur, ni mafua tu”

“Hata taarifa ya kuumwa jamani hatupeyani?, aliuliza huku akimuangali Abdull usoni kwa jicho la kuibia ibia.

“ hakukuwa na namna ya kukufanya ujue..”

“Basi nipe namba yako..wakati mwengine usije kupata sababu..”,  huku akitoa simu yake kujiweka tayari

Hakukuwa na mazungumzo ya ziada baada ya hapo,  Fartuun aliaga akidai  wenzake wanamsubiri kwa ajili ya kufanya kazi ya kundi.

Fartuun ni binti anayevutia kwa rangi yake, mwili wake uliojazia kwa kiasi ulikuwa ni mvuto kwa wanaume wengi, hakuwa binti mwenyewe maringo ingawa familia yake ilikuwa inajiweza.

Abdull alirudi nyumbani,  roho yake ikiwa imemtulia kwa kiasi fulani, lakini hakutaka kulizungumzia suala lile kwa shemeji yake tena.

Siku zikasonga na urafiki wa karibu kati ya Fartuun na Abdull ukaanza, walikuwa ni marafiki wa karibu sana, huku mapenzi yakianza kuchipua katika mioyo ya wawili hawa.

Lakini hadi mwaka unamaliza kila mmoja anaingia mwaka wake wa mwisho chuoni, hakukuwa na cha zaidi kinachoendelea kati yao zaidi ya urafiki tu wa kawaida.

Kwa sababu ya wingi wa mapenzi ya Fartuun kwa Abdull, hata alipokuwa akiwaaga mashoga zake akimfata Abdull kwa ajili ya kwenda mjengo mlo  kupata chakula cha asubuhi au mchana pamoja , alikuwa akiwaambia kwamba anaenda kwa shemeji yao.

Walikuwa hawaachani mara kwa mara wakiwa chuoni hata wakati wa kurudi.

“Umewaambia mashoga zako waniite shemeji yao…?, kwa utani Abdull alimuuliza Fartuun ,  ilikuwa ni jioni moja wakiwa wameongozana wakirudi chuo.

“No! No! No!..hapana kabisa..”, alikataa huku akitabasamu na kuficha uso wake kwa mtandio

Jambo lililomfanya  Abdull naye atabasamu kisha wote wakaanza kucheka,  ingawa walicheka kwa pamoja lakini kila mmoja alikuwa na sababu yake ya kucheka.

“Unanitia aibu na wewe…maswali gani hayo!, alilalama Fartuun akiwa bado anaendelea kucheka.

Kipi kitaendelea kati ya Abdull na rafiki yake mpya (Fartuun)? Safari ya kumuua rais imegeuka na kuwa safari ya mapenzi? Ni kisa gani kilichowakimbiza Abdull na Talib kwao? Nini kitaendelea Unguja? Tukutane wiki ijayo….

Kutana na Ally Hilal 3 ndani ya 1

$
0
0

Ingawa kanuni ya maisha inatuelekeza kuwa kila mwanaadamu amezaliwa akiwa na kipaji cha aina fulani, lakini si kila mmoja anayekigunduwa na kukitumia kwa maslahi yake na wengine. Matokeo yake ni kwamba wengi wetu huzaliwa, kukuwa na kufa na vipaji vyetu tukaenda navyo kaburini, bila hata kufahamika kwamba tulikuwa navyo. Havikutufaa wenyewe wala wenzetu. Hivyo sivyo kwa Ally Hilal Ally. Mmoja kati ya vijana wa Kizanzibari waliojaaliwa vipaji kadhaa – na sio tu kipaji kimoja – maishani, na ambao wamefanikiwa kuvitambua, kuvikuza na kuviendeleza.

‘Kilio cha Usumbufu’: Diwani mpya yaingia sokoni rasmi

$
0
0

Kampuni ya uchapishaji ya mtandaoni, Zanzibar Daima Publishing House, imechapisha diwani mpya ya ushairi wa Kiswahili iitwayo ‘Kilio cha Usumbufu’ iliyoandikwa na mtaalamu wa lugha na fasihi na mwalimu wa siku nyingi, Maalim Ali Abdulla Ali.

Diwani hiyo, ambayo inaanza kuuzwa leo katika mtandao wa Amazon na washirika wake kote ulimwenguni, ina zaidi ya tungo zilizoandikwa kwa mitindo na miundo mbalimbali, ila zote zikifuata kanuni ya kimapokeo ya urari wa vina na mizani.

Akiandika kuhusu diwani hii na mwandishi huyu, bingwa wa Fasihi Andishi ya Kiswahili wa zama hizi, Profesa Said Ahmed Mohammed, ana haya ya kusema:

“Inahitaji sifa nyingi kwa mshairi kuweza kumteka msomaji namna hii! Kwanza, anahitaji kuwa na ukwasi wa lugha, na Ali Abdulla Ali anao wa kumiminika. Pili, ni jinsi mshairi anavyojua kuyatumia maneno yanavyostahiki mwahala mwake – katika miktadha ambayo msomaji angeungama kwamba yasingeliweza kutumika bora pahala pengine popote.”

Ali Abdulla Ali ni mzaliwa wa kisiwani Pemba na muda wote wa maisha yake ya kikazi amekuwa mwalimu aliyefundisha skuli kadhaa Unguja na Pemba, wakati huo huo akiandika kazi chungu nzima za Fasihi ya Kiswahili.

Miongoni mwa hadithi zake fupi kama vile: ‘Machupa’, ‘Mwanamke’ na ‘Mwenye Pupa’ ziliwahi kusikika katika kipindi cha ‘Karibuni’, cha Idhaa ya Kiswahili ya Deustche Welle nchini Ujerumani katika miaka ya 1980′.

Kazi zake za hivi karibuni ni pamoja na ‘Faidika na Methali, Nahau na Vitendawili’ (Phoenix Publishers) na tamthilia ya ‘King’ora cha Mwehu’ (Longhorn Publishers).

Aidha, Maalim Ali amechangia katika mikusanyo ya diwani kadhaa za hadithi fupi zikiwemo ‘Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine’ (Moran Publishers), ‘Homa ya Nyumbani na Hadithi Nyingine’ (Phoenix Publishers), ‘Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine’ (Longhorn Publishers) na nyinginezo.

 

Je, sheria ya ardhi Zanzibar inakupa haki gani?

$
0
0

Miongoni mwa masuala yanayozuwa mizozo mikubwa visiwani Zanzibar ni umiliki na uhaulishaji wa ardhi pamoja na mali nyengine zisizohamishika, ambapo matukio mengi ya kudhulumiana yanaripotiwa. Lakini je, sheria ya ardhi inakulindaje na inawezaje pia kukuingiza mtegoni kama hukuzingatia? Fuatana na Wakili Msomi Omar Said Shaaban kwenye mfululizo huu wa Zaima Sheria, ambapo leo anaizungumzia sheria hiyo na mambo inayoambatana nayo.

 

Polisi yadai Abdul Nondo alijiteka

$
0
0

Mkuu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo, anashikiliwa na jeshi hilo na atafunguliwa mashitaka ya kuzusha uongo kuwa alitekwa, taarifa ambazo zilizusha taharuki nchini. Zaidi msikilize hapa:

 

Viewing all 854 articles
Browse latest View live