MTU mmoja ambaye sitamtaja jina kwa sasa, kanitumia ujumbe mfupi wa maandishi akishangilia vitendo viwili vilivyotekea kwa wakati mmoja katika siasa za nchi yetu.
Kitendo cha kwanza ni cha baadhi ya madiwani waliojivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro pamoja na sehemu nyingine ambazo bado sijazithibitisha. Kingine ni cha anayejiita mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwavua uanachama wabunge 8 wa chama hicho.
Mtu huyo ambaye anajifanya mweledi wa kila kitu kuanzia usafirishaji wa majini, masuala ya kibalozi, masuala ya kodi na kadhalika, anakosa kuelewa kwamba uchochezi na uchonganishi wa kisiasa ni jambo hatari sana katika mustakabali wa nchi!
Ndiyo, mtu huyo anaweza akawa anayaelewa baadhi ya mambo kwa njia ya kukariri sawa na watoto wa madrasa wawezavyo kuihifadhi Qur’an Tukufu bila uwezo wa kuichambua. Na kwa mtaji huo hataki kukubali kwamba haijui siasa na mambo anayoyashadidia kwenye siasa ni ya hatari kabisa kwa nchi iliyodumu na amani kwa miongo mingi.
Tukianza na suala la madiwani waliovua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM tutaona kwamba kuna mambo kama yafuatayo. Kitendo hicho ni uasi, sio kwa chama tu bali pia kwa wananchi.
Chama kiliwaamini watu hao na kuwapeleka mbele ya wananchi kuwa ndio wanaowafaa, na wananchi wakaridhika nao kwa kuwachagua dhidi ya watu walioletwa kwao na vyama vingine.
Baada ya hapo wachaguliwa hao wakala viapo vya kuwa madiwani wakiwa wanamhusisha Mwenyezi Mungu kwa kushika vitabu vitakatifu, Qur’an na Biblia, kuwa watawatumikia wananchi waliowachagua kupitia njia walizozitumia na kuonekana wanafaa, vyama vya siasa.
Kwahiyo tutaona kwamba kuziruka njia hizo na kuzidandia njia nyingine sio tu kwamba wameziasi na kuzisaliti njia hizo, bali pia wamemuasi na kumsaliti Mungu waliyemuomba awasaidie katika majukumu yao hayo ya kuwatumikia wananchi, ikiwa ni pamoja na kuwaasi na kuwasaliti wananchi waliowachagua kwa ujumla.
Kitendo hicho cha kukiasi kiapo cha aina hiyo ni zaidi ya usaliti, ni kitendo ambacho ni aina mojawapo ya uhaini. Uhaini ni uovu uliopitiliza kutokana na kuyabadili matakwa ya wananchi yanayolindwa na kiapo chini ya Katiba ya nchi.
Kwa hiyo, yeyote anayekishangilia kitendo hicho, hata awe mchumia tumbo tu, mtu asiyejari kinachoweza kutokea ilmradi tu yeye kajaza tumbo lake, anapaswa achukuliwe kama mtu kipofu asiyepaona anakoelekea. Na mtu wa aina hiyo ni hatari sana katika jamii. Maana kwa mtindo huo asiposhituliwa na kukemewa anaweza akaiingiza jamii nzima kwenye gema na kuisababishia maangamizi.
Nasema hivyo nikiwa nimetilia maanani kitendo cha kuapisha, sababu kazi yoyote isiyo ya maana haiwezi kuhitaji uapishwaji. Lengo kuu la kuapisha ni la kumtaka mhusika asilete uasi na usaliti, ili kuwafanya waliompa kazi husika wamuamini.
Kwa hiyo, anayekiuka kiapo na kujiingiza kwenye uasi na usaliti anawezaje kuaminika kwenye jamii aliyomo? Madiwani hao waliojivua uwakilishi wa wananchi wakidhani wanakikomoa chama kilichowasimamia mbele ya wananchi wanawezaje kuaminika kokote waendako?
Hivi kweli CCM inaweza kuwaona hao kuwa ni watu safi au ni ng’ombe waliokatika mikia kama alivyowahi kusema mwenyekiti wao, Dk. Jonh Pombe Magufuli? Kwa mantiki hiyo, tayari hao ni watu wasiofaa, sio kwa wananchi peke yao, hata ndani ya CCM watu hao hawafai kabisa, maana alishaliona hilo mwenyekiti wa chama hicho.
Kwa upande mwingine, ni wabunge 8 waliovuliwa uanachama na anayejiita mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba. Kitendo alichokifanya profesa huyo kinajionesha wazi kilivyo cha usaliti, sio kwa wabunge hao tu, bali pia kwa CUF, upinzani nchini na taifa kwa ujumla.
Sababu kitendo hicho kinaziweka wazi nafasi za wabunge hao, maana yake ni kwamba zikajazwe upya. Kazi ya uchaguzi mdogo kwa ajili ya kuzijaza nafasi hizo, kama ilivyo ile ya kujaza nafasi za madiwani waliojivua uanachama wa Chadema, ni ya gharama.
Pesa itakayotumika sio ya vyama vya siasa, ni pesa ya walipakodi. Kwahiyo mtu aliye mzalendo makini alitakiwa kuliona hilo akiwa anaelewa kwamba kwa sasa nchi imo kwenye msukosuko mkubwa wa kipesa. Isingekuwa rahisi kwa mtu mzalendo kusababisha gharama kwa taifa katika jambo lenye maslahi binafsi kiasi hicho.
Sababu anachokitafuta Lipumba ni kutaka kujisimika vizuri kwenye nafasi ya uenyekiti wa CUF ambayo aliikimbia mwenyewe kiusaliti akidhani angekiyumbisha chama hicho wakati kiko kwenye harakati za Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Lakini baada ya kuona chama hicho hakikuyumba, kwa maana ya malengo yake, Lipumba, kukwama, ndipo akaja kivingine akidai kwamba yeye bado ni mwenyekiti wa chama hicho! Anafanya hivyo bila kujali kwamba anachezea bomu linaloweza kulipuka na kusababisha maafa makubwa kwa nchi na wananchi! Tamaa mbele mauti nyuma!
Tamaa ya maslahi binafsi aliyo nayo Lipumba inamfumba macho asiweze kuona hatari iliyo mbele yake, kwa nchi na wananchi. Maana kama tulivyoona hapo juu, nchi itaigia gharama ya uchaguzi mdogo na pia uwezekano wa wananchi kuvurugana kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo.
Hata kama vyombo vya dola vipo kuhakikisha hilo halitokei, bado vitahitaji gharama kubwa katika kulitekeleza hilo. Sio kwamba vyombo vya dola vinajazwa upepo tu na kuanza kufanya kazi.
Mtu aliyenishangaza zaidi ni Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwahi kuridhia hatua hiyo ya Lipumba na kutangaza kuwa nafasi hizo za wabunge ziko wazi. Mbona hakufanya hivyo kwa Magdalena Sakaya ambaye naye alikuwa amevuliwa uanachama wa CUF?
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo. Anapatikana kwa anwani ya barua-pepe prudencekarugendo@yahoo.com na kwa simu nambari 0784989512
Filed under: SIASA Image may be NSFW.
Clik here to view.
Clik here to view.
Clik here to view.
Clik here to view.
Clik here to view.
Clik here to view.
Clik here to view.
