Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all 854 articles
Browse latest View live

Tusiruhusu kutawaliwa na mademagogi

$
0
0

BAADA ya mkasa uliomkuta Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, wiki iliyopita, nimekumbuka kwa uchungu, mazungumzo yangu na waandishi wa habari tarehe 12 Februari 2017, ofisini kwangu Mwanza, anaandika Ansbert Ngurumo kwenye mtandao wa MwanaHalisi Online. 

Siku hiyo, niliwaeleza kuwa nchi yetu sasa inaongozwa kidemagogi. Niliomba wananchi waamke kuomba, kukemea, kushauri, kupinga na kufanya lolote ambalo litachangia kuiepusha nchi yetu na maangamizi.

Kabla ya waandishi kuniuliza demagogi ni nani, nilifafanua kwa kifupi maana yake. Na leo nitafanya hivyo.

Demagogi ni kiongozi anayejitafutia sifa kwa kuumiza wengine au kwa kutumia hofu za kijamii kujijengea umaarufu wa kisiasa.

Katika historia ya dunia, wamekuwepo mademagogi mashuhuri kadhaa, lakini wanaolaaniwa zaidi ni Huey P, Long, Joseph McCarthy, Fr. Charles Coughlin na Lewis Charles Levin.

Nilieleza kuwa udemagogi huu ulizaa pia kitu kingine kinachojulikana kama umakathi, kutokana na jina la McCarthy demagogi wa Kimarekani, aliyekuwa Seneta wa Wisconsin mwaka 1947 mpaka 1957.

Kwa muktadha wa uchambuzi huu, nitamwita Makathi. Mnamo Februari 9, 1950, Makathi alifanya kituko. Kwa kujua kwamba jamii ya Wamarekani walichukia mno Ukomunisti, aliamua kujitafutia umaarufu kwa kutuhumu raia wenzake kuwa ni wakomunisti.

Kuitwa Mkomunisti nchini Marekani kulikuwa sawa na kuitwa mhaini. Aliita vyombo vya habari, hasa televisheni, akatuhumu watu mashuhuri – wakiwamo watumishi waandamizi katika wizara nyeti ya mambo ya nje, Ikulu, Redio Sauti ya Marekani (VOA), Jeshi na kadhalika. Alisema walikuwa wanaandaa mapinduzi dhidi ya serikali.

Kutokana na hofu iliyokuwa imejengeka, na kwa kuwa haikuwahi kutokea kiongozi yeyote kufanya hivyo, na kwa kuwa waliotajwa walikuwa watu maarufu na vigogo; na kwa kuwa mkomunisti ni adui wa umma, wananchi walimuona Makathi kama shujaa wa kitaifa.

Mwanzoni waliamini alichokuwa anafanya, wakidhani kinalenga kuokoa nchi. Machoni mwa wengi, Makathi alionekana kiongozi mzalendo anayepiga vita ufisadi na uhaini.

Naye kwa kujua alicholenga kufanya, na kwa kujua wananchi hawajatambua nia yake, aliongeza kasi na mbwembwe. Hakujali katiba inasema nini kuhusu haki za hao aliokuwa anawatangaza kwenye vyombo vya habari.

Kwa kutumia vyombo vya habari, hasa katika matangazo mubashara ya televisheni, alihoji watuhumiwa, akawadhalilisha na kuwafedhehesha maofisa wa jeshi na wanasiasa.

Miongoni mwa watuhumiwa wake walikuwa wasanii mbalimbali. Baadhi yao waligoma kuhojiwa. Lakini hakuwaacha salama. Kwa kuwa watuhumiwa karibu wote walikuwa watumishi wa serikali, waliogoma kutoa ushirikiano walifukuzwa kazi.

Baadhi ya watuhumiwa, kwa sababu ya mateso, walilazimishwa kukiri hadharani, kutubu, na kutaja watu wengine kuwa ni watuhumiwa wenzao katika kashfa ya ukomunisti, ili waachiwe huru.

Hata hivyo, walijitokeza watu wachache katika jamii, wakaanza kushtuka. Wakatilia shaka mbinu alizotumia. Wakatilia shaka weledi wake wa upelelezi katika suala alilokuwa anasimamia moja kwa moja.

Miongoni mwa walioshtukia udemagogi wa Makathi ni Dwight Eisenhower, ambaye wakati utesaji huo unaendelea, alibahatika kuwa rais wa 34 wa Marekani (1953-1961).

Alichukua uamuzi mkali. Akamkana Makathi hadharani. Akamwamuru kuacha kusingizia watu na kuwafedhehesha hadharani.

Jamii nayo ikashtuka, ikaanza kumlaani Makathi na mbinu zake za kuchafua watu kwa tuhuma za kutunga. Makathi akapata anguko la kijamii na kiafya. Hakuishi miaka mingi tena, alifariki dunia akiwa amechanganyikiwa, akiwa kijana wa miaka 48.

Kutokana na jina lake, matendo na hatua za kikatili za aina hii vilizaa mtihani mpya katika lugha ya Kiingereza – McCarthyism(Umakathi).

Miaka 67 baadaye, baada ya kiongozi mmoja kijana kutembelea Marekani na kurudi, mapema mwaka huu, umakathi umeanza kuota mizizi nchini. Aliyosababishia wasanii, wanasiasa, wafanyabiashara, viongozi wa dini na wengine, na kumpa ushujaa wa muda yanafahamika. Na anakoelekea kijamii na kisiasa panaonekana.

Bahati mbaya, jamii yetu imechelewa kushtuka. Mwanzoni, baadhi ya wabunge walishtuka, lakini sauti zao hazikusikilizwa kwa kuwa wasaidizi wa kiongozi huyo walifurahia alichokuwa anafanya.

Kama ilivyokuwa Marekani, vyombo vya habari vya hapa navyo havikushtuka mapema. Viliendelea kumsaidia kusambaza ukatili huu hadi alipotenda kituko kingine dhidi ya vyombo vya habari vyenyewe.

Jeshi la Polisi, kwa bahati mbaya, nalo liliingizwa katika mkumbo; likamsaidia kukamata na kutisha raia kinyume cha utaratibu, hadi hali hiyo ilipokuja kurekebishwa baada ya watuhumiwa wanaojitambua kuchukua hatua za kisheria.

Ilichukua muda kiasi kabla ya wananchi kukumbuka kuwa demagogi huyu amezoea kupanda vyeo kwa kutendea wengine yasiyofaa.

Kwa mfano, mwaka 2013 aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya kurusha matusi dhidi ya Edward Lowassa na wengine mbele ya vyombo vya habari. Mwaka 2015 aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya baada ya kumzaba kibao Jaji Joseph Warioba katika mdahalo wa katiba mpya.

Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa baada ya kutukanana, kuzozana na kuburuzana mahakamani na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo. Yumkini alikuwa anawinda nafasi kubwa zaidi kwa kituko hiki kilichoibua umakathi wake.

Bahati mbaya ninayoona ni kwamba wakuu wake na baadhi ya vijana wenzake, wamekuwa wanafikiri njia nzuri ya kujulikana na kupata sifa ni kuumiza raia. Kwanini? Wametambua kuwa mkuu wao anawafurahia pale wanapotoa matamko au wanapochukua hatua za kuumiza wale wanaodhaniwa kuwa wabaya na washindani wao.

Ndiyo maana kumekuwapo matukio ya kushangaza yanayofanywa na baadhi ya wakuu wa wilaya. Halikuwa jambo la kiungwana kwa mkuu wa wilaya ya Ubungo kuagiza polisi wamkamate na kumtia ndani kwa saa 24 Boniface Jacob, Meya wa Ubungo, eti kwa kualika viongozi wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutembelea miradi ya maendeleo katika Manispaa anayoongoza.

Kitendo hiki, hata kama kilifurahisha wakuu wake, hakikumbakizia heshima DC huyo katika jamii ya Watanzania. Kabla siku hazijapita nyingi, mkuu wa wilaya ya Kinondoni naye akaagiza polisi wamkamate Mdee na kumweka ndani kwa saa 48.

Kisa? Alizungumza na waandishi wa habari akatetea haki ya watoto wa kike kupata elimu hata kama ikitokea wakapata mimba shuleni; akakosoa kauli ya Rais John Magufuli aliyetangulia kusema kuwa katika utawala wake watoto hao hawana haki hiyo.

Hadi naandika haya, mbunge wa Kawe alikuwa amekaa ndani kwa saa zaidi ya 70. Katika nchi ya kidemokrasia, matendo kama haya ni ya kikatili, na yanapaswa kupingwa.

Tukilea tabia hizi za kidemagogi, tutajenga jamii ambayo inazima uhuru wa wananchi kujieleza, na hivyo kuzima mawazo mbadala, ubunifu, na ndoto za maendeleo.

Tukiendekeza udemagogi huu, na tukaulea kwa woga wa jamii, tutajenga siasa za kutafutana uchawi, kuzushiana, na kuviziana. Tusipokemea mambo haya, tutajenga na kukuza hofu ya mabadiliko chanya. Zaidi, tutaharibu sifa na maisha ya watu wengine.

Nini kifanyike? Ninapendekeza. Kwanza, wananchi washtuke, waache woga, na wahimize serikali kuzingatia katiba na sheria za nchi pasina kuonea watu.

Pili, rais akubali kushauriwa. Apunguze kufoka na kutisha watu ili aweze kuletewa asiyoyajua, anayonyimwa na wasaidizi wake kwa sababu wanaogopa kupoteza madaraka.

Rais ahimize wasaidizi wake waache kujipendekeza kwake na anapogundua wanatesa watu ili wapate sifa, achukue hatua kali kama iliyochukuliwa na Rais Eisenhower niliyemtaja mapema.

Tatu, viongozi wa kiroho nao waache woga. Watambue kuwa wapo juu ya viongozi wa kisiasa. Waoneshe unabii wao kwa kukemea maovu yanayosababishwa na watawala.

Nne, wanasiasa wafanye kazi yao bila hofu, wakemee tabia hizi, hata kama kwa kufanya hivyo wanatishwa na kukamatwa. Tano, wafanyabiashara washikamane, wajitetee. Umoja wao ndiyo nguvu yao, na ndio uhai wa Watanzania.

Sita, wasanii watunge nyimbo za kuombea taifa, kuhamasisha demokrasia, ujenzi wa uchumi imara, na utetezi wa haki za raia. Huu ndio wakati wa wasanii kujitambulisha rasmi kama kioo cha jamii.

Saba, vyombo vya habari visiandike tu na kutangaza ajenda za watu kwa woga, na kulisha wananchi sumu; bali vishtuke na kuokoa taifa kwa kufanya uchambuzi wa kina wa masuala yanayoendelea.

Itakumbukwa mwaka 2011, kwa bahati mbaya, vyombo vya habari ndivyo vilikuza suala la kikombe cha Babu wa Loliondo, kwamba ana dawa ya kutibu magonjwa yote ukiwamo Ukimwi.

Miongoni mwa waliokimbilia Loliondo “kupata kikombe” ni Rais Jakaya Kikwete, mawaziri kadhaa – William Lukuvi, John Magufuli na wengine – wabunge, na wananchi wengine.

Nguvu iliyotumika kutangaza “neema” ya kikombe cha Babu, ingeweza kutumika kufanya uchambuzi wa kina kuhusu haja ya serikali kuimarisha miundombinu ya afya ili wananchi watibiwe kwa ufanisi.

Tusipofanya hivyo, tunaweza kujikuta tumejenga jamii ya walevi wa madaraka kama walivyokuwa watawala wa kale kama Lavrentiy Beria wa Urusi, Ivan The Terrible, Mfalme Commodus, Mfalme Caligula, Christian VII, Heliogabalus, Nero, Hitler, Stalin, Mussollini, Idi Amin, Mobutu Seseseko.

Hatutaki kulea watawala wa aina ya Yoweri Museveni, Paul Kagame, Paul Nkurunziza, na wenzao waliochafua sifa ya bara la Afrika kwa matendo ya kikatili yatokanayo na ulevi wa madaraka. Tukiwahi, hatutafika huko.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ansbert Ngurumo na kuchapishwa kwenye mtandao wa gazeti la MwanaHalisi Online. 


Filed under: SIASA Tagged: CCM, CHADEMA, demokrasia, haki za binaadamu, Halima Mdee, madaraka, Magufuli, Tanzania

Ngeleja, shujaa au fisadi aliyeogopa?

$
0
0

Makala hii imeandikwa na Julius Mtatiro, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) kwenye ukurasa wake wa Facebook ikiwa na kichwa cha habari “William Ngeleja, shujaa wangu!” Zanzibar Daima inaichapisha tena hapa ikiwa na kichwa cha habari kipya, kwani mhariri ameona kuwa ndani ya makala yenyewe ushujaa wa mtajwa unaning’inizwa baina ya uhalisia, mashaka na matazamio. Sasa endelea… MHARIRI

Kaka yangu mpendwa, William Ngeleja amefanya uamuzi wa kishujaa sana. Ameamua kujitakasa kwa kurejesha fedha za wizi ambazo aliyempa alituibia huko nyuma na jambo hili lilishafanyiwa maamuzi na bunge lakini hayakutelezwa.

Hata hivyo, namkumbusha Ngeleja kwamba makosa ya jinai hayafi milele. Ukiuwa mwaka 1970 halafu ukaombwa ujitokeze, ukakataa, halafu mwaka 2017 (miaka 47 baadaye) ukajitokeza na maburungutu ya pesa au roho na mwili wa mtu mwingine ili uwakabidhi ndugu wa mtu uliyemuua kwa maana ya kuwalipa fidia, vitu vyako vitapokelewa lakini havifuti jinai.

Ukiiba hela za walalahoi mwaka 1950, halafu miaka 67 baadaye ukajitokeza na hela mara milioni elfu moja ya zile ulizoiba, zinaweza kupokelewa kwa mbwembwe kubwa, lakini hiyo haifuti jinai. Hata kama leo ungelikuja na viwanda vyote vya Mo na Bakhressa na vya Dangote uwakabidhi uliowahi kuwaibia senti tano huko nyuma, hiyo haifuti jinai!

Ukishatenda jinai, makosa ambayo humaanisha umeshindwa kuwa mwaminifu kama hili la kina Ngeleja, wewe ni mtenda jinai na dunia yote sheria ziko wazi kabisa. Jinai haijadiliwi, haitafutiwi ufumbuzi, haifanyiwi maridhiano. Jinai ni makosa yenye adhabu kwa mujibu wa sheria na adhabu hizo hazina mjadala.

Na Julius Mtatiro

Kama tungelikuwa na serikali iliyo makini na inayokata kotekote, baada ya mkutano na waandishi wa habari wa kaka yangu Ngeleja, ilipasa maafisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) wamsubirie geti la HABARI MAELEZO na asionekane hadharani hadi awe mahakamani, kama akina James Rugemarila!

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Happi, ni juzi tu hapa alitumia ile sheria ya kikoloni, kibaguzi na ya kitumwa, akaamuru Halima Mdee akamatwe mara moja na kusota rumande, kwa sababu tu Halima alizungumza na vyombo vya habari na akaonya juu ya mienendo ya Rais John Magufuli.

Ni juzi pia wale viongozi karibu 50 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa kwenye kikao halali cha ndani huko Geita, walizingirwa na polisi na kukamatwa kwa nguvu kubwa sana. Kisa walikuwa wanatimiza haki yao ya kikatiba kama chama cha siasa.

Undumilakuwili kwenye uchukuwaji hatua

Huwa najiuliza, hivi tuna dola ngapi Tanzania? Hivi tuna serikali zinazofanya kazi kwa kutumia sheria zipi kuhusu wale wa Geita au zipi kwa mbunge wa Kawe inapolinganishwa na hii ya Ngeleja?

Godbless Lema alipotangaza ile ndoto yake. Aliishia gerezani miezi minne, lakini Ngeleja ametangaza hadharani kuwa amerudisha fedha za wizi, hadi sasa yuko kwake! Tunataniana?

Unawezaje kumshughulikia mtu aliyetabiri mambo ya kufikirika tu ambayo umeamua kuigiza kuwa mambo hayo ni kinyume na sheria, na wakati huo huo ukamuacha huru mtu ambaye ameeleza mambo halisi ambayo ni makosa ya jinai yasiyo na mjadala?

Rugemarila pia ni binadamu jamani, kama yeye yuko gerezani kwa sababu ya fedha alizoiba, vipi kuhusu wale waliopokea fedha hizo za wizi na tena wengine wakasema ni hela za mboga?

 

James Rugemarila (kushoto) akiwa mahakamani anakoshitakiwa kwa makosa kadhaa likiwemo la kuiibia serikali.

Kama Rugemarila yuko gerezani kwa kukwapua fedha za umma, vipi wale watendaji na viongozi wa serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) walioidhinisha fedha zile zitoroshwe wako huru mitaani? Yaani unamkamataje mwizi aliyeiba fedha halafu wale waliomfungulia geti na kumhesabia fedha kwa hiyari na wale waliowatuma wakiwemo hadi watendaji wa ikulu, wako mitaani salama?

Kama kweli taifa langu lingekuwa na sheria zinazokata kotekote, unamshughulikiaje Rugemarila na kuwaacha watendaji wa Benki ya Stanbic na Benki ya Mkombozi ambao walizitumia benki zao kutakatishia fedha hizo bila kujali kuwa kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za fedha na sheria za nchi?

Tunakumbuka kuwa bunge liliazimia fedha zile zirejeshwe kwa kulipiwa kodi. Ilikuwa mwaka 2014, lakini akina Ngeleja hawakurudisha fedha hizo, akina Chenge, Askofu Methodius Kilaini na wenzao waliendelea kuwa na misimamo kuwa zile ni fedha halali. Nini kinachotokea hii leo? Wanawezaje tu kuzirudisha kienyeji namna hii?

Askofu Kilaini ni askofu wangu, maana mimi ni Mkatoliki. Huku Marekani, wapo wachungaji, maaskofu, mapasta, mapadre wako gerezani, walishtakiwa na kufungwa, kama watu wengine. Siwezi kuwatetea watu walioshiriki kuliibia taifa, hata kama angelikuwa Papa wa Kanisa!

Unamshughulikiaje Rugemarila kwa wizi wa fedha zile kama mwizi mkuu, halafu ukamuacha jaji wa mahakama kuu ambaye alipokea fedha za umma kama rushwa au fedha haramu? Jaji unamstaafisha kwa maslahi ya umma, yeye hawezi kukaa jela! Kwamba Jaji ana mke mzuri na muhimu kwake kuliko Ruge? Undumilakuwili!

Chenge naye, pamoja na kushiriki kwenye masakata yote makubwa ya wizi kuanzia ule wa rada na bado kupokea shilingi bilioni 1.6 za rushwa kutoka kwa Rugemarila, bado ameendelea kuwa mtu muhimu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na nchi, na leo hii Chenge ni Mwenyekiti wa Bunge. Hivi tuko makini kweli? Yaani Rugemarila yuko gerezani kwa makosa makubwa, lakini walionufaishwa na fedha zinazomponza Rugemarila wanapeperusha bendera za serikali mitaani?

Yaani inaingiaje akilini kuwa umuweke Mdee ndani kwa masaa 120, umuweke Lema gerezani miezi minne, lakini Chenge yeye yuko mtaani tu! Hakika tunadanganyana sana! Hivi kati ya Chenge na Lema, nani ameihasidi nchi hii? Hivi kati ya Chenge na Mdee nani ameichafua nchi hii? Yaani hawa wanaotoa maoni yao, na kushauri na kuonya serikali, wao wanaishia jela. Yale majizi makubwa yanadunda mtaani na bado kuna watu wanakwambia nchi imebadilika kwelikweli. JPM ameinyoosha!

Wote wanawania kumridhisha Mtukufu Rais 

Na kichekesho kikuu kinaweza kuwa kwamba hata hao wanaochukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani, TAKUKURU haifanyi hivyo kwa weledi wao, bali wanamtumia ishara Rais Magufuli na kuona kama angelipenda mtu fulani afikishwe mahakamani. Sote tunajua kuwa kwa utawala wa sasa hakuna anayefanya maamuzi. Kila kitu watu wanasubiria kupima upepo, ikiwa kina madhara kwao (kitamfurahisha Rais au la!) Maana kwa sasa unaweza kufanya maamuzi mazuri, lakini Rais asiyapende, utatumbuliwa, na ukifanya maamuzi mabaya akayapenda unaweza kubaki (na kinyume cha kila moja), kwa hiyo ponapona yako ni kutokufanya lolote hadi uwe na uhakika kuwa litamfurahisha Rais.

Andrew Chenge, mmoja wa viongozi waliotuhumiwa takribani katika kila kashfa kubwa ya hivi karibuni ya ufisadi serikalini.

Unaweza kukuta TAKUKURU wana ushahidi dhidi ya Askofu Kilaini, kwamba anastahili kushtakiwa, lakini unaweza ukashangaa wakubwa wanawaambia, “huyo mwacheni, huyo ni Askofu!” Kwa kweli hili ndilo taifa tunalojenga, taifa linaloongozwa na utashi wa mtu mmoja mmoja katika uongozi kuliko kuongozwa na taasisi ambazo zinafuata viwango.

Nchi zinazofuata viwango, askofu akibaka na mvuta bangi akibaka, wote watashtakiwa na wote watafungwa ikiwa wana hatia. Lakini kwa Tanzania, Ruge na Chenge wataiba pesa na kugawana, kisha Ruge atakwenda gerezani na Chenge atabaki mtaani, na bado Watanzania wanapiga makofi kuwa hatua zinachukuliwa! Tutasubiri milele, kama hakuna viwango katika hatua zetu hatutapiga hatua. Kama tukisubiri kuongozwa na sauti ya mtu mmoja hatutakwenda mbele.

Tunaendelea kujenga taifa lenye ubaguzi mkuu na lenye aibu. Ndiyo maana leo Rais anakwenda Sengerema anahutubia mkutano wa chama chake kwa kigezo cha urais wake lakini vyama vingine vimezuiliwa kufanya mikutano, hata ya ndani, na wapo watu wanashangilia kuwa “ngoja awakomeshe wapinzani, 2020 wawe wamemalizika” na anayesema hayo ni Mtanzania masikini ambaye hata bima ya afya ya uhakika hana.

Nani amesema kuwa kwa hatua hizi za undumilakuwili za sasa eti Freeman Mbowe anakomeshwa? Eti Maalim Seif Sharif anakomeshwa? Eti James Mbatia anakomeswa? Eti Zitto Kabwe anakomeshwa? Hivi hata hiyo 2020 ikiwa Watanzania wataichagua CCM kwa asilimia 100, Zitto ataathirikaje? Mbatia ataathirikaje? Maalim ataathirikaje? Mbowe ataathirikaje?

Yaani tunakisia kuwa wote siyo wabunge na wako mitaani tu, wataathirikaje kukushinda wewe ambaye hadi leo hujui utaajiriwa lini na nani? Au wewe ambaye umeajiriwa na mshahara wote unatumika kupandia daladala na kula mlo wa mchana?

Bila viwango, mbele kuna giza

Nchi yetu inapoendeshwa kwa undumilakuwili wa kuchukua hatua dhidi ya watu fulani na siyo wengine kwenye jambo lile lile, nchi hiyo haiwezi kupiga hatua, itakuwa inarudi nyuma kweli kweli.

Inaonekana kila afisa serikalini na kwenye chama tawala anataka kutenda jambo la kumridhisha Rais John Magufuli na sio kujenga taasisi imara za nchi.

Kwenye masuala ya viwango masuala ya msingi yanayohusu nchi na sheria zake, askofu ana wajibu ule ule alionao mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Rais ana wajibu ule ule alionao mama kule kijijini Kiabakari, mwenyekiti wa chama cha siasa kinachoongoza dola ana haki na wajibu ule ule wa yule mwenyekiti wa chama ambacho hakina dola, sheikh ana wajibu ule ule ambao anao mfanyakazi au mkulima. Sote tuna wajibu katika viwango vyetu.

Tukiendelea kwenda mbele bila viwango, tutaona baadhi ya watu wanakomeshwa na wengine wakila bata! Kwangu mimi, Rugemarila ana haki sawa sawa na Chenge, na Ngeleja, na Anna Tibaijuka na kadhalika, maana naye ni binadamu pia. Ana watoto, mke, na ndugu na wana uchungu naye.

Hakuna namna yoyote kwamba kwamba eti askofu, waziri, au mbunge fulani ni muhimu katika nchi kuliko na ana utaratibu tofauti mbele ya sheria na haki tofauti na mtu wa kawaida. Ndiyo maana kila siku nasema na nakumbusha maneno ya Barack Obama alipokuwa Ghana: “Afrika haihitaji watu imara, inahitaji taasisi imara!”

Mfano huu wa Obama kwa baadhi ya watu wanaofikiri kinyume chake, nawapa changamoto. Wale wanaoamini kuwa JPM ni Rais bora sana, anapambana na rushwa na ufisadi, nataka niwaambie kuwa kama huo uimara wa JPM hatautumia kujenga taasisi imara, na akaendelea kujilimbikizia madaraka na amri na kila kitu, baada ya miaka yake mitano au kumi kuisha, Tanzania itabakia na bunge dhaifu, mahakama dhaifu, serikali dhaifu, TAKUKURU dhaifu na kila kitu dhaifu. Na hapo ndipo wale watetezi wa hoja kuwa ujenzi wa taasisi imara unahitaji watu imara, wataelimika kwamba kiongozi imara asiyejenga taasisi imara ni sawa na mtu anayechota maji kwa kutumia tenga.

Kitendo cha kaka yangu Ngeleja nakiita cha kishujaa kwa sababu kimeivua nguo serikali nzima, kwamba mwizi anaweza kusimama hadharani na kutamba kuwa anarudisha fedha za wizi na baada ya tambo zake akarejea hadi kwake na kulala huku wezi wenzie waliomuibia fedha hizo wako gerezani. Yaani ni sawa na mmeibiwa ng’ombe, kisha mwizi halisi mkamkamata na huku mkiwajua wale ambao mwizi alikwenda kuficha ng’ombe huyo kwao na wao wakijua ng’ombe ni wa wizi na wakakaa na ng’ombe kwa miaka kadhaa, kisha siku moja wanamrudisha bila hofu na mnampokea na mnawaacha watunza ng’ombe wa wizi wakirejea makwao huku mwizi mkuu yuko gerezani!

Nakushukuru sana kaka Ngeleja, shujaa wangu wa leo!


Filed under: SIASA Tagged: Escrow Tegeta, Tanzania, ufisadi, william ngeleja

Kama kichwa cha treni

$
0
0

Naendeshwa, kama kichwa cha treni
Hidogoshwa, kama yaya wa nyumbani
Hichezweshwa, kama vile punguani

Hiamka, ni mbio kutwa ni njiani
Hekaheka, za kutisha insani
Hivunjika, wananitupa jaani

Niendako, huwa mimi sikuoni
Mara huko kushoto na kuliani
Kwangu mwiko, kusema ni hilakini

Hisimama, huwa dereva yu ndani
Sijahema, keshashika usukani
Na kugoma, haingii akilini

Najihisi, ninaumia jamani
Kwenda kasi, nikawa sipati kyeni
Kwa wepesi, huruma nioneeni

Mussa Shehe
Zanzibar


Filed under: KISWAHILI KINA WENYEWE

Maalim Seif anaringia uadilifu wake

$
0
0

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, ana sifa ya kuuthibitisha ukweli anaouamini hata akiueleza kwa namna ya kubashiri kinachoweza kuja mbele ya safari.

Sifa hii inaendana sana na mazoea yake ya kupenda kutembea na maneno yake. Akisema, anamaanisha. Akiahidi jambo, hulisimamia, akalitekeleza. Ni mambo yanayomsababishia kujivunia asili yake ya kujiamini na kuaminika.

Anajiamini kuwa kiongozi shupavu na muadilifu aliyeijenga CUF kufikia kuwa tishio lisilo mbadala mbele ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachovuta pumzi kwa kutumia visaidizi. Lazima kibwebwe na dola ndipo kiishi.

Karibu wiki mbili zilizopita, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutangaza jambo jipya linaloongeza uzito katika mwenendo ule ule wa kuthibitishia ulimwengu kuwa yeye si rahisi kushindwa kwa dhulma.

Na Jabir Idrissa

Amefichua tukio jingine baya linaloumbua watawala kwa vile walivyojitoa haya na kuamua kutumia taasisi za kidola kutekeleza mkakati wa kudhoofisha jitihada zake za kuwaongoza wananchi wa Zanzibar kuikamata serikali kutokana na ushindi wao ulioporwa wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Katika mkutano huo, Maalim Seif alibashiri kuwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini mwenye dhima ya kusimamia haki kwa usimamizi wenye ufanisi wa kumbukumbu muhimu za maisha ya binadamu, ufilisi na udhamini, naye ataingia mtegoni kama walivyoingia wengine na kukoleza mgogoro wa uongozi wa chama hicho uliopandikizwa.

Alisema wazi tayari uongozi wa RITA ulishaanza kushinikizwa kutekeleza matakwa ya watawala ya kuvuruga CUF, ili kuwavunja moyo viongozi wake katika jitihada wanazozifanya za kupigania haki ya Wazanzibari kupata uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wa ridhaa yao kama walivyoamua katika uchaguzi uliohujumiwa kwa kutangazwa umefutwa wote tarehe 28 Oktoba 2015.

Maalim Seif alisema Bodi ya Wadhamini ya CUF iliyopendekezwa kupitia ofisi yake, baada ya kuandaliwa kwa mujibu wa taratibu zote za kisheria zikiwemo zinazoelekezwa na Katiba ya chama hicho, itapigwa na chini, na penye sehemu yake, kuidhinishwa Bodi iliyopendekezwa na Profesa Ibrahim Lipumba, anayeongoza genge la waliofukuzwa uongozi pamoja naye baada ya kusaliti chama hicho.

Hakupotea na kweli hakukosea kitu. Ndivyo ilivyotokea. Wakala wa Usajili alikabidhi barua rasmi ya kuidhinisha bodi ya kundi hilo la Prof. Lipumba, mwanasiasa aliyejiuzulu uenyekiti kwa hiari yake tarehe 5 Agosti 2015, akitoa sababu ya kutoridhika na anavyochukuliwa na viongozi wake katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani pamoja na ule wa Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani wa Zanzibar.

Kwa hatua hiyo ambayo Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson aliikiri mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari waliokutana mjini Morogoro kwa semina ya kujenga mahusiano mema ya kikazi wiki moja baada ya kukubali kumridhisha kibubusa Prof. Lipumba kwa kumuidhinishia bodi aliyoelekezwa kuipendekeza, taasisi hiyo ilijiongeza kwenye orodha ya washiriki wa uchafu wa kuvunja sheria na katiba ya nchi kuhusu suala la upanuzi na uimarishaji wa demokrasia na utawala bora.

Viongozi wa CCM Zanzibar kwa kutambua mafanikio ya Maalim Seif kisiasa, baada ya kujikuta kimeadhibiwa kwa kukataliwa na umma, wameamua kujipakatisha mapajani mwa viongozi wenzao wa Tanganyika na kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama na kama inavyozidi kuthibitishwa hata na taasisi za kijamii ili kumhujumu.

Alipokutana na waandishi wa habari mara ya kwanza tarehe 9 Aprili 2017, alisema “si siri tena sasa kwamba kile kinachoitwa ‘mgogoro wa uongozi’ ndani ya CUF si chochote bali hujuma zilizopangwa na zinazoendeshwa na dola (serikali na vyombo vyake) kupitia njama ovu na mbinu chafu zilizolenga kuua upinzani makini nchini ikiwa ni sehemu ya kinachoonekana ni mkakati mpana wa kunyamazisha kila sauti inayothubutu kuwakosoa watawala.”

“Nataka ifahamike lengo la njama ovu na mbinu chafu hizi siyo CUF… ni upinzani na hasa UKAWA; na lengo pana zaidi ni kuua demokrasia inayokua Tanzania kwa kuhujumu na kuziua taasisi zote zinazoonekana ni nguzo za demokrasia (Tanzania).

Maalim Seif anatanua wigo wa kuzitathmini jitihada ovu za dola ya Tanzania chini ya CCM, kwa mgongo wa “mgogoro wa uongozi ndani ya CUF” na bila ya aibu wala haya, watawala hawajishughulishi kuamini kuwa wamekaa uchi na ni muhimu wakajifunika ili wasizidi kuadhirika.

Ni nini kama sio dola ya CCM kujidhalilisha inapothibitika kuwa RITA, baada ya kushikwa shingo, wamejiachia na kuidhinisha bodi ambayo haikupatikana kwa utaratibu wa kisheria na unaoelekezwa na Katiba ya CUF wa kuteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT)?

Kweli kabisa CCM hawapendi kuona CUF inabakia taasisi imara ya kuongeza nguvu ya ushawishi kwa kushirikiana na vyama vingine vitatu chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kweli nchini baada ya kuondoa mfumo uliooteshwa na watawala.

Sasa RITA, huyu wakala wa usajili, ufilisi na udhamini, anajikuta hana namna isipokuwa kuandaa mawakili wa kuisimamia katika kesi mpya iliyofunguliwa na CUF ikitaka itamkwe kuwa kilichofanywa na wakala huyo kuidhinisha bodi ya Prof. Lipumba ni udanganyifu unaostahili kuadhibiwa kisheria.

Shuruti ieleweke waziwazi hapa kwamba kwa kuidhinishwa Bodi iliyopendekezwa na Prof. Lipumba, kupitia msaidizi wake mkuu Magdalena Sakaya, aliyemteua kaimu Katibu Mkuu, akidharau hata uamuzi wake wa kupigania kuwa mwanachama baada ya kufukuzwa tarehe 26 Septemba 2016, watawala wanataka CUF isitulie na upinzani usishikane kuisumbua CCM.

Kwa maneno mengine, viongozi wa CCM wanafurahi kila wanapoona CUF wanavutana kwani hawatapata nafasi tena ya kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi kuwakurupusha watawala nje ya madaraka.

Ndipo Maalim Seif akatoa tahadhari kwamba kwa hali iliyofikiwa ya mkakati wa dola ya CCM, jamhuri inapelekwa katika kukabiliwa na mgogoro mkubwa usiowahi kushuhudiwa katika historia yake. Panahitajika mshikamano kuepusha hatari hiyo.

Tangu Maalim Seif alipokaza kamba ya kushawishi ulimwengu ikiwemo Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague, nchini Uholanzi, kuhusu kuhujumu maamuzi ya wananchi kuchagua viongozi wawatakao Zanzibar, na jamhuri yenye mamlaka na vikosi vya ulinzi na usalama, CCM haijasimama kutapatapa.

Swali la msingi kwa nukta hii ni mwisho wa kutapatapa huko kwa CCM utakuaje? Wanaodhulumiwa wanaamini kuwa wataishinda tu CCM na itaanguka chini.

Hili amelisema wazi mwenyewe. “Nawaambia watawala walio nyuma ya njama na hujuma dhidi ya CUF msitulazimishe kutusukuma ukutani. Tutailinda CUF kwa gharama yoyote. mlio nyuma ya hujuma hizi mtabeba dhamana ya mnayoyaandaa. Wazanzibari na Watanzania wote wanaotuunga mkono na wapenda demokrasia ya kweli watasimama imara kulinda haki yao; ni wakati wa kulinda demokrasia ya kweli Tanzania.”

CCM wanaamini wakimhujumu Maalim Seif, watatawala daima. Hata sasa, wanatawala miili tu ya wananchi, si nyoyo zao maana walishaikataa CCM.


Filed under: SIASA Tagged: CCM, cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, uchaguzi Oktoba 2015, Zanzibar

Pale serikali inapoboresha maslahi wasio Wazanzibari ndani ya Zanzibar na kuwasahau Wazanzibari

$
0
0

Tarehe 2 Julai 2017, kwa nia wizara ya kazi, uwezeshaji, wazee, vijana, wanawake na watoto ilitangaza kima kipya cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi Zanzibar kupitia Waraka wa Sheria Nambari 69 (Legal Notice no. 68), ambacho kiliamuriwa kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2017.

Mabadiliko hayo yanawafanya wafanyakazi wenye hadhi ya kuwa na mikataba ya maandishi, mishahara yao kuongezeka kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 145,000/- hadi kufikia 300,000/-, ambapo ongezeko hilo ni zaidi ya asilimia mia moja. Mabadiliko hayo yamefanyika chini ya Kifungu cha 97 (1) cha Sheria ya Ajira nambari 11 ya mwaka 2005.

Mbali kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa katika kanuni kimeongezeka kutoka kiwango cha sasa cha shilaingi 145,000/- hadi kufikia 180,000/- kwa mwezi. Alisema kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi vibarua wa kutwa wenye ujuzi, kimeongezwa kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 10,000/- hadi 30,000/- kwa siku. Aidha alisema kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka shilingi 7,000/- wanazolipwa hivi sasa hadi kufikia 25,000/- kwa kutwa. Kwa maamuzi hayo ya kisheria kabisa yaliyochukuliwa na wizara hiyo, hakika yangestahiki kupongezwa sana na Wazanzibari, lakini kwa mtazamo wangu kidogo napata ukakasi kuyapongeza maamuzi haya, unaweza kujiuliza kwa nini niwe na nafsi yenye kusitasita katika kuyapongeza maamuzi haya wakati hili jambo la nyongeza ya mshahara ni faida kwa wafanyakazi wa chini.

Lakini niseme jawabu la suala hilo ntalijibu kama ifuatavyo, tarehe 5 Mei 2015 niliandika makala kama hii ambayo ina lengo la kutetea maslahi ya Wazanzibari katika sekta za ajira, hususan, katika sekta binafsi ambapo makala hio niliipa jina “Sera ya Ajira ya Zanzibar Ndiye Adui wa Vijana”.

Katika makala hii nilionyesha jinsi Sera ya Ajira iliyotungwa mwaka 2009 jinsi inavyokosa utekelezaji wake kutokana na kwamba sera inapingwa na sheria zetu za ajira zilizopo, ambapo sheria hizo hadi leo hazijabadilika wala kurekebishwa katika sehemu muhimu ili ziwabebe Wazanzibari katika masuala ya ajira kupitia sekta binafsi.

Kwa muktadha huo basi vivyo hivyo waraka huu nambari 68 (The Legal Notice No. 68) bado haujamnufaisha Mzanzibari hata kwa asilimia 50, nikiwa mdau wa ajira Zanzibar bado sheria zetu hazijaruhusu Wazanzibari waliowengi wapate fursa za ajira katika sekta binafsi hususan katika sekta ya utalii hasa hasa sekta ya mahotelini.

Sitaki nionekane kama labda kuna upande fulani naubagua, la hasha, lengo ni kuisaidia serikali na taasisi husika ili ziweke mazingira ya kisheria ambayo yatamuwezesha mzawa kupata fursa kwanza na baadae mgeni afuatie, na nafanya hivi kwa sababu usipompa nafasi ya ajira mzawa unadhani atakwenda wapi aajiriwe?

Kuna sababu tofauti ambazo zinamfanya Mzanzibari asinufaike katika kupata ajira katika sekta binafsi ambapo zinamzuia kutofaidika na kima hichi kipya cha mshahara kwa sekta binafsi, ambapo ni jambo la historia katika nchi yetu:

  1. Kutokuwepo watendaji wa juu wa kizanzibari katika makampuni binafsi. Hii ni sababu moja wapo kuu na ya msingi sana, naweza kusema asilimia zaidi ya 90 katika mgawanyo wa madaraka kwa nafasi za juu za usimamizi katika sekta binafsi, basi waekezaji wengi wamewapa watu kutoka nje ya Zanzibar, ambapo nafasi za juu aidha hupewa raia wan chi za Ulaya, Asia, Kenya na Uganda, nafasi za katikati hupewa watu kutoka Kenya na Tanzania Bara, panapokuwa na mahitaji ya ajira mara nyingi watu wa nafasi za kati hufanya ushawishi kwa viongozi wao ili walete marafiki na ndugu zao ambapo huwa si Wazanzibari.
  2. Ruhusa ya sheria zetu. Kuna haja ya kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria zetu zinazosimamia ajira, kwani sera ya kila nchi duniani ni kuhakikisha inawapatia ajira wananchi wake, ili kupunguza umasikini, lakini sheria zetu zinazosimamia ajira zinatoa mwanya wa kuzidisha umasikini kwa raia wazawa kwa sababu wazawa wengi hawapati fursa ya ajira katika sekta binafsi, jambo ambalo linawafanya Wanzaibari wengi kurundikana ofisi za Tume ya Utumishi wa Umma kusubiria ajira za serikali, takribani sheria zetu zote zinazosimamia ajira visiwani Zanzibar hazitoi fursa ya kisheria inyohakikisha Mzanzibari kuwa ni mtu wa mwanzo kupewa ajira. Katika sheria nambari 11 ya mwaka 2005 kifungu nambari 36 (1) kinasema: “Hakuna Muajiri atakayeruhusiwa kuajiri mgeni isipokuwa: (a) endapo hakuna Mzanzibari mwenye sifa zinazotakiwa katika nafasi hiyo.”

Wakati kifungu hichi kinatungwa na kuwekwa katika sheria hii, nakubali kwamba zama zile kweli hakukuwa na Mzanzibari aliyekuwa na uwezo wa kuajiriwa katika nafasi nyingi hasa katika sekta ya hoteli na utalii, lakini kwa sasa kifungu hichi kimepitwa na wakati, wahitimu wapo isipokuwa kizuizi kipo katika sababu nambari moja ambayo nimeieleza hapo juu na kizuizi chengine ni ruhusa ya kisheria ambayo muajiri amepewa ruhusa na sheria yetu ya Vitega Uchumi ya mwaka 2004 ambapo muajiri pia amepewa ruhusa kuajiri mtu aneyemtaka kwa sababu za kiufanisi na imani ya kibiashara.

Endapo tuna nia ya dhati kumnufaisha Mzanzibari katika masuala mbali mbali yakiwemo haya ya ajira binafsi na mishahara na tuna imani na kuitakidi kwamba ndiye raia muhimu wa Zanzibar na mwenye haki namba moja, basi kuna haja kuzifumua sheria zetu zote zinazosimamia ajira na kusifuma upya, kwa kuweka vipengele katika sheria hizo vitakavyolazimisha kila muekezaji kwa uchache awe ameajiri mzanzibari kwa asilimia 60 tu, na asilimia 40 zilizobakia iwe kwa watu kutoka nje ya Zanzibar.

Pia kuwe kuna utaratibu wa hawa viongozi wa juu wawe wanaajiriwa katika Sekta binafsi kwa muda mchache na sio muda mrefu kama ilivyo sasa, ili kuwapa fursa na Wazanzibari kufanya kazi za kiungozi katika makampuni binafsi, kwani naamini kwa Zanzibar ya sasa kila fani Wazanzibari wapo, kinyume na hivyo Serikali ya Wazanzibari itaendelea kuwaboreshea maslahi wasio Wazanzibari ndani ya Zanzibar yao.


Filed under: JAMII Tagged: castico, Zanzibar

SMZ iondowe utata kima cha mishahara sekta binafsi

$
0
0

Nimelichukuwa tena na kulisoma kwa makini zaidi agizo la serikali lililochapishwa katika Waraka wa Sheria Nambari 68 (The Legal Notice No.68) kuhusu ongezeko la mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi, zikiwemo taasisi zote ambazo zinamilikiwa na watu binafsi wa nchini na wageni, wawe wakubwa au wadogo, likitokana na Sheria Nambari 11 ya mwaka 2005, Kifungu Nambari 97 (1) lililosomwa na waziri mwenye dhamana ya kazi katika serikali ya Zanzibar, Maudline Castico, mbele ya waandishi wa habari mnamo tarehe 2 Julai 2017, aliagiza kwamba utaratibu huo wa mishahara ulitakiwa kuanza tarehe 1 Julai, yaani siku moja nyuma.

Katika waraka huu wa kisheria nimegundua kwamba kuna baadhi ya changamoto katika agizo lile, lakini nilikuwa na imani ya hali ya juu kwamba wengi wa waajiri wetu si wapingaji wa sheria mpya na hata zile kongwe ambazo zinaongoza makampuni yao.

Hapa nimeonelea ni vyema nizieleze changamoto hizi ili kama wahusika wataafikiana na mimi zitatuliwe na mapema. Kwa mfano, katika agizo hilo, Kipengele Nambari 1 kinawataja: “employees with written contracts – 300,000/-“, yaani waajiriwa wenye mkataba – bila ya kuianisha mkataba wa muda gani wala kwa taasisi zipi, kubwa, ndogo au ya kati – wote walipwe mshahara wa shilingi 300,000/-.

Na Ali Mohammed

Ni wazi kuwa baadhi ya waajiri wataingia makosani kwa kutotekeleza agizo hili kwa sababu tuchukulie mfano muajiri ana kioski pale Kwa Mchina kilicho rasmi na ameajiri wafanyakazi wawili na wote wana mikataba, lakini mtaji wake ni shilingi 2,000,000/-, sasa atawezaje kulipa 300,000/- na bado juu ya kima hicho pia aongeze na asilimi nyengine 13 kumlipia kila mwajiriwa wake mafao ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF)? Je, akifanya hivyo si atakuwa ameshaiuwa biashara yake?

Katika Kifungu Nambari 2 cha agizo hilo imeandikwa: “Emplyees with with written contracts for small institutions established under regulations – 180,000/-“. Labda ungelifikiria kuwa hofu na utata uliopo katika Kifungu Nambari 1 unaweza kupatiwa mwarobaini wake katika kifungu hichi, lakini bado kifungu hichi nacho kinazidi kukipinza Kifungu Nambari 1 na kisha kujipinza chenyewe, kwa sababu kifungu kinasema, “waajiriwa wenye mikataba ambao wanafanyakazi katika taaasisi ndogo zilizoainishwa katika kanuni watalipwa 180,000/-”.

Lakini hadi naandika makala hii, ikiwa ni tarehe 15 Julai 2017, hiyo kanuni iliyotajwa inayoainisha ni ipi taasisi ndogo, haipo hewani na haijawahi kuwepo na kama ipo basi waajiri haijawahi kuwafikia.

Kwa upande wa vifungu nambari 3,4 na 5 vinavyoelezea ajira za vibarua, hakuna tatizo katika utekelezaji, bali lipo kwenye zile fursa za ndugu zetu ambao wao hawapendi kuajiriwa moja kwa moja, ambao daima wanapenda kuwa vibarua, yaani ajira za kutwa. Kwa ungezeko hili la malipo ya kibarua la asilimia 200, wasitegemee kwamba fursa hiyo itakuwepo. Hata ikitokea, basi haitakuwa ya muda mrefu, mana ikiwa muajiri atakuajiri kama kibaruwa, kwa muda wa siku 26, atatakiwa kukulipa 780,000/-, wakati akikupa mkataba, atakulipa 300,000/- pekee. Hivyo muajiri atakhiyari akuajiri ili mshahara wako wa siku 26 alipe watu wawili na chenji ibakie.

Wakati naandika makala hii, mmoja miongoni mwa wadau wa ajira amenipasha habari kwamba Jumiya ya Waekezaji katika Sekta ya Utalii (Zanzibar Association of Tourism Investors – ZATI), wamemuandikia waziri husika juu ya changamoto mbalimbali zilizomo katika waraka huo na hata kulalamikia wizara kwamba wamekwenda mbali sana kwa ongezeko hilo la mshahara kwa zaidi ya asilimia 100% kwa waajiriwa wenye mikataba na kwa asilimia mia 200% kwa waajiriwa wa vibarua.

Kabla ya kutangazwa kwa kima kipya cha mshahara, mwaka jana Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) ilifanya mkutano katika ukumbi wa Kiwanja cha Kufurahishia Watoto cha Kariako, ambapo mkurugenzi wa jumuiya hiyo, Bwana Salah Salim Salah, aliwaelezea wajumbe lengo hilo la serikali kupandisha mshahara na waajiri wakasema bayana kwamba hawana uwezo wa kulipa kima hicho cha mshara na wakaitahadharisha wizara kwamba endapo ingesimamia maamuzi hayo, basi kwa kuwa wataathirika kimapato kutokana na kwamba bili ya mshahara itapanda na faida yao kushuka, basi wao waajiri watatekeleza kifungu cha sheria ya kupunguza wafanyakazi.

Makala hii haina lengo la kuwatetea waajiri wasilipe kima kilichowekwa na serikali, lakini lengo ni kuzishauri pande zote hizi kukaa tena pamoja kwa maridhiano na kutoka na kitu kitakachoondowa hali hizi za utata, hofu na mifarakano inayotarajiwa kutokea kuanzia tarehe 1 Agosti 2017, ambapo waajiri watakuwa wameshafanya maamuzi aidha kutekeleza agizo hilo au kulitupilia mbali na kujifichia kwenye utata nilioueleza hapo awali.

Tukizidharau changamoto hizi na tuking’angang’aniza bila ya kulipitia upya agizo lenyewe la serikali na endapo waajiri watatumia haki yao ya kupunguza wafanyakazi iwe kwa kutowapa mikataba mipya wale wanaomaliza mikataba yao au kwa kutumia sheria ya punguzo la wafanyakazi, tutakuwa hatukuwatendea haki wafanyakazi ambao ni ndugu na jamaa zetu, na zaidi tutakuwa tumekwenda kinyume na agizo la Mkataba wa Kimataifa Namba 131 wa (ILO Minimum Wage Fixing Convention, 1970 No. 131), ambapo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla tumetia saini kuuridhia kikamilifu.

Mkataba huo wa kimataifa unasema katika Kifungu Nambari 3 kuwa ongezeko la mshahara wa kima cha chini lizingatie mambo yafuatayo:

  • Ukuaji wa kiuchumi
  • Engezeko la ajira
  • Kuangalia uwezo wa Muajiri

Sasa kwa mambo hayo matatu yafaa tujiulize:

a) Je, uchumi umekuwa kwa kiwango gani kumuezesha muekezaji kumudu kulipa kima hicho?
b) Endapo waajiri wakiamuwa kupunguza wafanyakazi, je ajira itaengezeka au itapunguwa?
c) Je, waajiri wote wanalingana kiuwezo kuweza kumudu kima hicho?


Filed under: JAMII Tagged: ajira, kima cha chini, mishahara, uwekezaji, Zanzibar

Watanzania ni wajinga si wapumbavu

$
0
0

KAULI chafu za Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, kila mara anapofungua kinywa chake kuzungumza dhidi ya wale anaowahesabu kuwa wapinzani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaudhi, lakini hazishangazi.

Kwa hivyo, haikushangaza aliporejelea kauli kama hizo hivi karibuni wakati akiwa Chato mbele ya mwanafunzi wake wa kauli kama hizo, Dk. John Magufuli.

Hakikuwa kitu kigeni pia kuwa aliwafurahisha waliokuwapo jukwaa kuu na wanachama wa kawaida wa CCM waliohudhuria shughuli ya kukabidhi nyumba 50 za watumishi wa umma katika sekta ya afya.

Hata hivyo, tukiacha ukweli kwamba miongoni mwa mambo mema aliyofanya Rais Mkapa ni kuondoka madarakani muda wake wa kikatiba ulipokwisha, tofauti na jirani zake wanaobadili katiba ili waendelee madarakani, ilitarajiwa kauli gani njema kwake?

Mkapa aliyeingia madarakani kwa mgongo wa Mwalimu Julius Nyerere kwa kudhani kwamba mwanafunzi wake huyo angeendeleza kile alichokiamini yeye, alianza awamu ya utawala wake kwa kuhubiri alichokiita “Ukweli na Uwazi.”

Wakati huo, alitaka nchi imwamini yeye ndiye “Bwana Msafi” aliyeaminiwa na Mwalimu Nyerere, kwamba angeweza kuwa mpigavita rushwa kwelikweli. Alinza fungate hiyo kwa kutaja mali alizokuwa nazo, akawashawishi mawaziri wake, kina Waziri Mkuu Frederick Sumaye, wafanye vivyo.

Hakuishia hapo. Akawataka wananchi wamuamini yeye ni mpambanaji kwelikweli dhidi ya ufisadi. Akaunda Tume ya kuchunguza mianya ya rushwa na kumteua Jaji Joseph Warioba kuiongoza. Lakini kutaka kujua alivyokuwa hakuwa akimaanisha akisemacho, angalia kilichotokea baada ya tume kukamilisha kazi yake.

Kwanza, baada ya kupelekewa majina ya “wala rushwa” katika serikali yake, aling’aka kwamba watu wana wivu wa kike na eti, “badala ya kuangalia maendeleo yao, wanaendekeza choyo cha kuona kila mwenye mali basi ameipata kwa rushwa.”

Akasema watu wasimpelekee majina tu, bali wampelekee ushahidi, hali anajua fika katika kutoa na kupokea rushwa, kila jitihada huchukuliwa kufuta ushahidi.

Pili, ripoti ya Tume ya Jaji Warioba iliishia kapuni. Ikachapwa, bila ya shaka, katika magazeti, lakini mambo yakaenda taratibu mno. Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU) aliyoiunda ikawa kama mbwa mkubwa anayetisha lakini kibogoyo asomeno ya kutosha kuwang’ata walarushwa.

Wengine tunaamini kuwa kihoro kilichomuingia Mwalimu Nyerere kwa kuangushwa na chaguo lake, kiliharakisha mauti yake Oktoba 14, 1999. Haikuwa kazi nyepesi, kwa mtu wa heshima kama yeye katika umri ule, kuzunguka nchi na kumnadi mtu wake, kisha mtu huyo akaja kumwangusha kwa kiwango kile.

Mwalimu Nyerere hakumuunga mkono tena Rais Mkapa tangu alipoanza kutekeleza madaraka yake kwa kusabilia mali za nchi kwa wawekezaji.

Kuna suala la ununuzi wa rada na ndege ya rais, ambayo baadaye uchunguzi wa polisi ya Uingereza uligundua kuwa ulitandwa na kashfa kubwa ya rushwa. Waziri wake wa Fedha, Basil Mramba, alitwambia ilikuwa heri wananchi wale nyasi lakini ndege ya rais inunuliwe.

Kuna mkasa kama ule wa kina Jenerali Twaha Ulimwengu ambaye, licha ya kuwa mpiga debe wake mkubwa katika siku za kampeni, alipoanza kumuona anakwenda mrama, naye akamsema kwa hilo, mara akatangazwa si raia.

Hatua hiyo ilichukuliwa huku uongozi ukisahau kuwa Ulimwengu aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mbunge wa taifa na Mtanzania aliyeongoza Umoja wa Vijana wa Afrika uliokuwa na makao makuu yake nchini Algeria.

Hata sakata la uraia wa mwandishi mwingine mkongwe wa habari, marehemu Ali Nabwa, lilianza katika siku za mwisho mwisho za utawala wa Mkapa na kwa hakika alilijua vyema, lakini akaondoka na kuliacha kama lilivyo.

Kuna mauaji ya Mwembechai ya mwaka 1997 ambayo pamoja na serikali yake kuwafanya ilivyowafanyia waumini wa Kiislamu ndani ya msikiti, bado alikataa kuunda tume ya uchunguzi. Hata alipotokea msomi Dk. Hamza Njozi, kuandika kile hasa kilichotokea katika kitabu chake cha The Mwembechai Killings (Mauaji ya Mwembechai), serikali yake ilikipiga marufuku kitabu hicho.

Kuna kasheshe la Bulyanhulu lililotandwa na malalamiko ya mauaji, watu kufukuzwa makaazi yao na wengine kufukiwa migodini. Si tu kwamba serikali yake ililikanusha, bali pia ilizuia vyanzo vyovyote vya habari kutoa taarifa hizo popote na kukamata wanaharakati waliokuwa wakichunguza madhila hayo.

Likaja suala kubwa la mauaji ya Januari 2001, Zanzibar, ambalo mwenyewe aliwahi kusema eti liliwahi kumkosesha usingizi na karibuni na mwisho wa utawala wake, alipokuwa ziarani Marekani, akasema lilimsononesha hadi siku anamalizia muhula wake madarakani.

Lakini wakati anazungumza na Tim Sebastian wa BBC wakati huo, alimwaga kiburi chake kuwa hatua ya serikali yake kuua watu ilikuwa sahihi.

Alikuwa anaamini zaidi nguvu ya vyombo vya dola katika utawala. Sio nguvu ya wananchi. Mdomoni, alikuwa akisema watu ndio wenye nguvu, katika vitendo alikuwa akionesha yeye na vyombo vyake vya dola ndio mwanzo na mwisho.

Ndiyo maana niliwahi kupendekeza utawala wake uitwe Mkapakrasia. Ndio uliozaa mauaji yale ambayo yalithibitishwa na Tume ya Hashim Mbita aliyoiunda. Ndio uliowafanya dada zetu wabakwe, na ndugu zetu waikimbie nchi yao. Mkapa hakuwa aina ya rais anayekubali changamoto katika utawala wake.

Alipenda na kuhusudu mataifa ya magharibi na waandishi wa huko. Akiwa kule, akitoa maneno ya kistaarabu na kidemokrasia. Lakini alipogeukia wananchi wake, akitoa kauli za ujuba na kebehi.

Sote tunakumbuka kauli zake za kuapa kutumia nguvu za dola kuzima nguvu ya umma iwapo baada ya uchaguzi, watu wangeandamana kupinga matokeo yaliyotangazwa na tume zake za uchaguzi.

Mifano ya kuendesha ovyo nchi haihesabiki. Na yote inamharamishia haki ya kuita wengine “wapumbavu,” maana mwenye akili hasa asingeitendea Tanzania alichokitenda, na nafsi yake ikabakia salama.

Leo Tanzania inachukua jitihada za kurekebisha majanga mengi ya kiuchumi, aliyoyaumba. Ni bahati mbaya kwamba wakati Rais Magufuli anasafisha uchafu ulioasisiwa na Mkapa kwenye uchumi, anautukuza ulimi wa mwanasiasa huyo anayeamini ndiye aliyemjenga kisiasa na kumbeba kumfikisha kileleni mwa ulwa.

Pamoja na ukweli kwamba Watanzania wengi wanaweza kuwa wajinga kielimu, wana akili ya kutambua haki na batili. Wao si wapumbavu.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017


Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: Benjamin Mkapa, CCM, John Magufuli, Mauaji ya Januari 2001 Zanzibar, Tanzania, wajinga, wapumbavu, Zanzibar

Je, Tanzania yaweza kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kubaka demokrasia?

$
0
0

Shutuma kwamba utawala wa awamu ya tano wa Rais John Magufuli unaibinya roho demokrasia changa ya taifa hili kubwa kabisa Afrika Mashariki zina mashiko yake kwa kuangalia rikodi ya yale yanayotendwa dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi wao, asasi za kijamii na hata vyombo vya habari, viwe vipya ama vikongwe.

Lakini wale wanaokosoa kwamba utawala huu unafanya mambo bila ya kuwa na itikadi au falsafa maalum inayouongoza, nao pia wanakosea. Ukweli ni kuwa kinachofanywa sasa na Rais Magufuli na timu yake kina mashiko yake kwenye mojawapo ya matapo makongwe kabisa kwenye taaluma ya uchumi wa kidola.

Tapo hilo ni lile linaloamini kwamba, kwanza, maendeleo yana tafsiri ya ukuwaji wa uchumi kupitia miundombinu na ubanaji matumizi na, pili, maendeleo hayo yanawezekana pale tu ambapo pana mfumo wa kirasimu na utawala wa mkono wa chuma. Ushahidi wa wanaoamini hayo wanautoa kwenye mifano ya Rwanda na baadhi ya mataifa ya Amerika Kusini na Asia, ambayo ni kigezo cha namna udikteta unavyofanikiwa kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.

Wasomi akina Walter Galenson, Karl De Schweinitz na Samuel Huntington wanahoji kwamba demokrasia inajikita zaidi kwenye mahitaji ya muda mfupi ambayo yanagharimu uwekezaji na ukuwaji wa uchumi. Kwa maoni yao, “demokrasia inatishia faida na, hivyo, kupunguza uwekezaji na basi haiendani na maendeleo ya kiuchumi.“ Watetezi hao wanahoji kwamba udikteta una uwezo mkubwa zaidi wa kulazimisha upatikanaji wa akiba na hatimaye kuanzisha ukuwaji mkubwa wa uchumi.

Akitetea mtazamo huo, Vaman Rao aliandika maneno haya mwaka 1984: “Maendeleo ya kiuchumi ni mchakato unaohitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu, vitu na fedha. Mipango ya uwekezaji kama huo inahusisha makato kwenye matumizi ambayo yanaweza kuwa machungu sana kwa watu wa chini ambao ndio wengi wao kwenye mataifa yanayoendelea. Serikali zinapaswa kuchukuwa hatua kali kabisa na kulazimisha zitekelezwe kimabavu ili kuweza kuzalisha ziada inayohitajika kwa uwekezaji. Endapo hatua hizo zitapigiwa kura na wananchi, hapana shaka zitashindwa. Hakuna chama chochote cha siasa kinachoweza kutegemea kushinda uchaguzi wa kidemokrasia kwa kutumia hoja ya kuwataka wananchi wajitowe muhanga leo ili wawe na maisha mazuri kesho.” (Tafsiri ni yangu).

Na Mohammed Ghassani

Hadi hapo, kwa wale wanaodhani kuwa chini ya Rais Magufuli, Tanzania inaendeshwa mzobemzobe huku mkuu akiwa hajuwi aendako, wanapaswa kuhakiki upya wanayoyaamini. Inawezekana muda wa kuwepo kwake madarakani usitoshe kumfikisha anakolunga, lakini haina maana kuwa hakujuwi – angalau kwa kuzingatia tapo hili la kitaaluma ya uchumi wa kidola.

Ubakaji demokrasia hauwezi kuwa dawa ya ukuwaji uchumi

Lakini je, kwa kuungwa kwake mkono na wasomi kama hao niliowataja, kunaufanya mtazamo wa kuyachagua maendeleo kwa gharama ya kuiua demokrasia kuwa sahihi? Jibu langu ni hapana. Mtazamo huu si sawa hata kidogo, kwa sababu sio tu kwa kuwa una fasili finyu sana ya maendeleo (kwa kusisitiza ukuwaji wa uchumi kupitia uwekezaji wa miundombinu pekee), bali pia unapingana na hata ushahidi wa wazi na tafiti kadhaa za kisayansi duniani, zikiwemo zile zilizofanywa kwenye mataifa yetu ya Dunia ya Tatu na yale yaliyojikwamua kiuchumi yaitwayo sasa Dunia ya Kwanza.

Wasomi Douglass C. North na Barry R. Weingast, kwa mfano, waliandika hivi mwaka 1989: “Dola ya kikandamizaji kila siku inakuwa tayari kuigeuza jamii kuwa windo lake kwa kisingizio cha kujenga uchumi. Ni taasisi za kidemokrasia pekee ndizo zinazoweza kuizuwia dola hiyo kwa maslahi ya umma. Udikteta wa aina yoyote ile ni chanzo kikuu cha ukosefu wa ufanisi, maana serikali ambayo jukumu lake la msingi ni kuweka mfumo wa kulinda uwekezaji, uzalishaji na usambazaji inajigeuza kuwa ndio mtendaji wa pekee wa kila kitu.”

Dunia ni shahidi wa kupinduka kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kibinafsi kwenye mataifa yaliyoujaribu udikteta hata katika yale ambayo leo hii utawala wa Rais Magufuli unayachukulia kuwa ni kigezo cha kufuatwa. Kuanguka kwa uchumi wa Nicaragua chini ya dikteta Somoza, wa Jamhuri ya Dominik chini ya Trujillo, Ufilipino chini ya Marcos na Ulaya ya Mashariki chini ya tawala za kikomunisti si mambo ya kuigwa.

Athari za ubakaji wa demokrasia ndani ya ‘Tanzania ya Magufuli’

Ndani ya kipindi hiki kifupi cha utawala wa awamu ya tano unaoikanyaga misingi ya kidemokrasia, Tanzania imo kwenye wakati mgumu sana kimaendeleo. Hali ya maisha imezidi kuwa ngumu, imani ya wananchi kwa mfumo inapotea na imani ya wawekezaji wa kati na wa juu inatikisika, licha ya ripoti za kutunga zitolewazo na taasisi za kidola kuonesha kuwa mambo yako shwari.

Bei za bidhaa muhimu kwa matumizi ya kila siku kama vile unga, mchele, sukari na madawa ni ya juu sana, vituo vya afya havina madawa, mashuleni kuna msongomano na ukosefu wa vifaa.

Hoteli kadhaa zimeripoti anguko la asilimia hadi 60 la mauzo yao ndani ya kipindi hiki cha utawala wa Rais Magufuli, huku kukiwa na wimbi la wafanyabiashara wanaohamishia biashara zao nje ya nchi kwa sasa, si kwa kuwa ni wakwepaji kodi kama inavyotakiwa iaminike, bali kwa kuwa hawana hakika ya mitaji yao nchini kutokana na staili ya matamko ya kuripuka na kutaka sifa ya mkuu wa nchi.

Yote haya ni kwa kuwa utawala usiohishimu misingi ya kidemokrasia hukaribisha ghasia – ghasia kwenye nafsi za watu, ghasia kwenye maisha yao, ghasia kwenye mifumo ya kiuchumi na kisiasa. Hizi ni ghasia za kimyakimya lakini zina mahusiano ya moja kwa moja na ukosefu wa maendeleo. Tanzania ya Magufuli – kama mwenyewe anavyopenda kuiita – sasa inapitia kwenye kipindi hicho cha ghasia.

Dawa ni kuimarisha viwili kwa pamoja

Mwaka 1972, muongo mmoja baada ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere aliuvunja mfumo uliotoa mamlaka kwa serikali za mikoa kwa minajili ya kuimarisha madaraka na nguvu za serikali kuu iliyopo Dar es Salaam, lakini wakati akikaribia mwisho wa utawala wake, alinukuliwa akisema kwamba: “Kuna mambo ambayo nisingeliyafanya endapo ningeweza kuanza upya. Mojawapo ni kuvunja mamlaka ya serikali za mikoa.”

Hili linatuzinduwa kuwa daima kwenye utawala, jambo la busara ni kutoa uhuru zaidi wa kidemokrasia kwa wananchi na sio kuubana. Ushiriki wa wananchi kwenye uendeshaji wa mambo yao ni jambo la muhimu sana kama jamii hiyo inataka kweli kuyafikia maendeleo.

Ingawa miaka 25 ya siasa za vyama vingi haikuwa na ukamilifu, ikizongwa na matatizo mengi na wakati mwengine ya kuvunja moyo, lakini Tanzania ilikuwa inapiga hatua kidogo kidogo. Hatua hizo zilipaswa kuendelezwa na sio kurejeshwa nyuma kama ambavyo inaonekana wazi hivi sasa.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina serikali isiyohishimu mgawanyo wa madaraka, isiyohishimu uhuru wa kimsingi kama vile uhuru wa mawazo, uhuru wa kujieleza, na uhuru wa kujiunga na kujikusanya na pia utawala wa sharia, ni taifa lenye utawala uliopoteza uhalali wake wa kidemokrasia, hata kama awali uliingia madarakani kwa kushinda uchaguzi.

Kama kweli tunataka kuwa na maendeleo, tunapaswa kuziunganisha dhana hizi mbili pamoja, kwani kimsingi maendeleo na demokrasia duniani yameungana na uimarishaji wa thamani ya maisha ya binaadamu.

Serikali ya Rais Magufuli inapaswa kuifahamu na kuihishimu mifumo ya kikatiba, vyombo huru vya habari na vyenye kujumuisha wote, asasi imara za kijamii na dhamira ya kweli ya kuelekea utangamano na majadiliano ya kijamii.

Hii ndiyo misingi mikuu ya kufikia lengo la maisha bora. Demokrasia inaweza tu kudumu kama inaonesha, muda wote na mwahala mote, kwamba ni njia bora kabisa ya kufikia lengo hilo.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kabisa na gazeti la Mwelekeo la tarehe 18 Julai 2017.


Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: demokrasia, maendeleo, Magufuli, Tanzania, ukuwaji wa uchumi

Ubaguzi ni asili ya serikali dhalimu

$
0
0

TUKIO la Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Mwinyi Usi Makame kufika hospitalini kumjulia hali kijana anayefanya kazi ya utingo wa daladala aliyejeruhiwa na wahuni akiwa kazini, linajadilika.

Mwinyiusi amekwenda katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kumjulia hali Khamis Juma Mgaya, ambaye alipigwa na kundi linalofaa kuitwa machokoraa, maarufu kwa jina la Ubayaubaya, ambao ni mfano wa wale vijana wakorofi wa jijini Dar es Salaam waitwao Panya Road.

Ni vijana waliopigika kimaisha na kwa sababu shida yao kubwa ni kupata mkate wa siku, wanavamia wananchi popote wanamopita na kuwanyang’anya walichonacho. Katika harakati zao, hupora fedha taslimu, simu za mkononi na vinginevyo.

Mmoja wa machokoraa wa Ubayaubaya alipanda daladala akiwa hana nauli. Alipodaiwa nauli na utingo, au kondakta, kama anavyoitwa upande wa Bara, alibisha na kuzusha tafrani. Aliposhushwa kwa nguvu, akapanga njama kumhujumu utingo. Aliwajulisha wahuni wenzake na kumvamia na kumshambulia utingo mpaka kumjeruhi.

Na Jabir Idrissa

Kundi hili la Ubayaubaya si la leo. Limekuwepo kwa muda mrefu hata kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Likijikusanya na kufanya operesheni zake maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar. Hakuna taarifa za kuwa kundi hilo lilidhibitiwa.

Wala haikushangaza kutodhibitiwa. Serikali haijali wananchi. Inaridhia viongozi wajali tu maslahi yao na familia zao. Inajali zaidi kudhibiti madaraka kwa kujua haikuingia kwa ridhaa ya watu.

Katika huko kudhibiti madaraka, kinachofanyika kingine ni kwa wenye nafasi za maamuzi serikalini kujiingiza katika kufisidi mapato ya serikali kwa kiwango watakacho. Ufisadi serikalini unatokomezwa kwa maneno matupu.

Wanachumia matumbo yao. Ndani ya Baraza la Wawakilishi lililojadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, baadhi ya wajumbe walilalamikia vitendo vya viongozi kutosimamia dhamana walizopewa na rais. wanachokifanya ni kujihusisha na miradi ya kifisadi kwa kutumia mgongo wa ofisi za umma.

Serikali iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kufanikiwa kuyahujumu maamuzi ya wananchi kupitia uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, iliendesha harakati nyingi za kuwabana wananchi hata kwa shughuli halali za kujitafutia kipato cha kuendesha maisha yao.

Shughuli za ufugaji zilizuiwa kwa kisingizio cha kuuweka mji katika mazingira safi. Yalitokea matukio mengi ya jitihada za askari wa serikali kupambana na wananchi wenye mifugo kama ng’ombe, mbuzi na punda. Ng’ombe na punda hutumika kwa ajili ya kubebea mizigo, moja ya shughuli maarufu zinazotegemewa kimaisha na wananchi wengi wa Unguja na Pemba.

Tukio la kijinga mwisho linalokataa kutoka kwenye kumbukumbu za wananchi, ni lile la Uwanja wa Magereza, ndani ya Shehia ya Tomondo. Askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), maarufu kwa kushiriki matukio ya kuhujumu wananchi, kama inavyoonekana kwa Mazombi, walidiriki kufyatua risasi za moto ili kukamata ng’ombe.

Picha za tukio hili zilienea mitandaoni. Milio ya risasi za moto kutoka bunduki za serikali zilizoshikwa na askari wa serikali wanaolipwa mishahara na posho kutokana na kodi za wananchi, ikirindima kuwalenga ngombe ambao yumkini walielewa wanaandamwa na wasiokuwa wafugaji wao.

Utadhani labda ng’ombe walikuwa wamevamia shamba la migomba au muhogo, walikuwa wanakimbia kuhujumiwa na askari wa serikali. Walikataa kukamatwa na kuondolewa kwenye himaya ya mabwana wanaowafuga.

Ulikuwa ni wakati ambao wafugaji walificha mifugo yao kwenye mabanda maalum. Nilishuhudia baadhi yao wakiwa wamewaficha ng’ombe kwenye vyumba vya kulala watu.

Ilikuwa ni matukio ya kihistoria ambayo hayajawahi kutokea Zanzibar – askari wenye bunduki za moto kupambana na mifugo ya wananchi iliyofungwa mabandani karibu na nyumba za wamiliki.

Haijapata kutokea zama zilizopita. Bali ilitokea mwaka jana, huku viongozi wa serikali wakitamba kuwa hakuna mfugo utakaosalimika hata ukifichwa namna gani. Inakokatazwa mifugo ni maeneo ya wilaya ya Magharibi ambayo yanajulikana kwa watu wake wengi kujishughulisha na ufugaji na kilimo.

Mifugo mingi ilikamatwa. Ikapelekwa maeneo ya vikosi vya ulinzi vya serikali. Ikahifadhiwa na wenyewe kutakiwa kwenda kuikomboa. Ukombozi huo wa mifugo ya wananchi ulifanywa kwa ngawira sio maneno.

Kwa sababu ukamataji ulifanywa holela, hata hifadhi yao ilikuwa holela. Hakukuwa na mpangilio kujua ng’ombe X ni wa nani? Alikamatwa wapi? Haikujulikana nani ana ng’ombe yupi hasa.

Ni katika uholela huo, wasimamizi wa hifadhi ya mifugo, waliruhusu malipo ya fedha kwa wenyewe waliotaka kugomboa. Lakini hakukuwa na utulivu wa mtu kupata ng’ombe wake hasa. Baadhi ya watu walilipa fedha na kuondoka na wasiokuwa ng’ombe wao. Ilikuwa ni utaratibu wa rushwa kwenda mbele. Walinzi, kwa niaba ya viongozi waliowatuma, walivuna wasichopanda. Ni rushwa iliyovunda ikinuka.

Ni matukio yaliyoenda pamoja na ya Mazombi kushambulia wananchi majumbani kwao usiku na mchana. Haya yangali yanaendelea leo. Mazombi wakitoa amri watu kulala hata saa 2 usiku. Wakipita wanatoa amri ya watu kuingia ndani.

Na pamoja na mashambulizi yao kusababisha madhara makubwa, ya watu kuumizwa ikiwemo kuvunjwa viungo vya miili yao, na kulazimika kulazwa hospitali, hakuna kiongozi hata mmoja wa serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein aliyepata kuzungukia kwenye hospitali kukagua wananchi waliojeruhiwa.

Wengi wa waliojeruhiwa walipata matibabu kwa kificho na pasina kupata fomu za kutibia (PF3) zinazotolewa kwenye vituo vya polisi. Walihofia kushughulikiwa kwa kuwa iliwahi kutangazwa kuwa wale wanaoshambuliwa wakamatwe wakifika kwenye hospitali za serikali au vituoni kuomba fomu hiyo. Wakubwa walijiaminisha kuwa anayeshambuliwa ni mpinzani.

Uendeshaji huo wa chuki katika serikali iliyowekwa madarakani kwa mabavu, ulidhuru wananchi wema waliokuwa wanaamini maamuzi yao ya kuchagua viongozi wawatakao yamehujumiwa kwa mkono wa dola kwa matakwa ya CCM.

Sasa pale serikali isiposhughulikia uovu unaofanyiwa wananchi, tena ikiwa na vyombo vya dola vinashiriki, unakwepaje kusema uovu huo ukipaliliwa na serikali? Hapa ndipo ilipo asili ya serikali dhalimu – vitisho kwa nia ya kundamiza sauti za wanyonge; hila na ubaguzi.

Basi, yule DC Mwinyiusi hakubahatisha kufika hospitalini kumkagua Khamis. Alizivaa hisia za kada mwenzao wa CCM, baba wa Khamis, Mzee Mgaya Juma. Anajulikana ni kada. Makada wa CCM hawatupani. Serikali ya CCM huwalinda kama wanavyolindwa askari wastaafu waliojiundia umoja uitwao UMAWA.

Tukio hili limenigusa kwa sababu nalichukulia kama mahsusi linalojenga picha kubwa na pana ambayo ninapoiweka kwenye pimamaji, naiona kuwa ni picha inayoifedhehesha serikali isiyo ridhaa ya haki.

Ni serikali ambayo imeingia madarakani kwa ubavu wa vyombo vya dola na kuashiria kuvunja msingi muhimu wa serikali kushika uongozi kupitia ridhaa ya wananchi kwa njia ya kidemokrasia kama inavyoelekezwa na Katiba ya Zanzibar ya 1984, inajisifu kuongoza kisheria.

Lakini, ipo kwenye rekodi ya kuwa serikali poa mbele ya vikundi vya ulinzi vinavyopita kwenye mitaa na kuvamia watu na kuwashambulia hadi kuwajeruhi miili.

Maeneo ambamo wahuni hao wanapita na kushambulia wananchi yanajulikana kuishi zaidi watu wenye mtizamo wa kuunga mkono upinzani na hasa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kwa kuwa kinapigania haki ya kuunda serikali kutokana na ushindi walioupata katika uchaguzi mkuu, kinasakamwa ili kifilie mbali.

Sema hakifi. Kigumu kama kimetengenezewa kangiriti. Wanaokiamini hawafi moyo. Wapo bega kwa bega na viongozi wa chama hicho kusubiri ifike siku haki irudishwe mikononi mwao.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017


Filed under: SIASA Tagged: CCM, ubaguzi, udhalimu, Zanzibar

Lissu atiwa nguvuni

$
0
0

SIKU moja baada ya polisi kumhakikishia Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema kuwa yupo huru na hakuna mpango wa kumkamata, hatimaye leo Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam limemkamata akiwa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JKNIA), anaandika Charles William.

Lissu amekamatwa akiwa uwanjani hapo tayari kwa safari ya kuelekea jijini Kigali, Rwanda kuhudhuria kikao cha halmashauri ya vyama vya mawakili wa Afrika Mashariki (EALS).

“Nipo uwanja wa ndege, najiandaa kuelekea Kigali kwenye kikao cha halmashauri ya EALS kinachoanza kesho. Watu waliojitambulisha kama maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa upelelezi Dar wamekuja kunikamata ili kunipeleka Kituo Kikuu cha Polisi,” amesema Lissu kupitia ujumbe alioutoa kupitia mitandao ya kijamii.

Taarifa ya polisi kumsaka Lissu kwa lengo la kumkamata zilizanza kusikika tangu Jumatano, ambapo Lissu akiwa katika kazi zake za uwakili mkoani Dodoma alielezwa kuwa maofisa wa Polisi walikuwa wakimsubiri nje ya chumba cha mahakama ili wamkamate.

Hata hivyo, Lazaro Mambosasa Mkuu wa Polisi Mkoa wa Dodoma alimfuata katika chumba hicho cha mahakama ambacho Lissu alieleza kuwa asingetoka nje na kumtaarifu kuwa jeshi la polisi mkoani Dodoma na hata makao makuu halina mpango wa kumkamata.

“Mimi sina maagizo ya kukukamata na wala IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi), hajatoa maagizo ya kukukamata…. upo huru,” alieleza Kamanda Mambosasa.

Masaa 24 baada ya kauli hiyo ya polisi, Lissu amejikuta yupo nguvuni huku Lucas Mkondya, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam akiueleza mtandao wa MwanaHALISI online kuwa Lissu amekuwa akitafutwa ili kuhojiwa.

“Sasa hivi sipo ofisini, sijajua kama tumempata lakini tulikuwa tunamtafuta kwa ajili ya mahojiano, kuna vitu tunataka atuambie. Hatuwezi kukwambia kwa sasa ni vitu gani tunataka tumhoji, lakini tukimpata na kumhoji tutakwambia,” ameeleza kwa njia simu.

Kukamatwa kwa Lissu, kunaweza kuhusishwa na kauli alizozitoa Jumatatu ya wiki hii tarehe 17 Julai, 2017 katika mkutano wake na wanahabari Kinondoni, jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine alimtuhumu Rais John Magufuli kuwa anaendesha nchi kidikteta.

“Nani anayeweza kutuambia, uwanja wa ndege wa Chato unajengwa kwa gharama gani na ilipitishwa na nani. Nani anayejua ndege za Bombadia zimenunuliwa kiasi gani na ziliidhinishwa na nani na kwa utaratibu gani?

“Leo hii, nani anayeweza kubisha kuwa Rais Magufuli anaendesha nchi kwa misingi ya upendeleo wa kifamilia, kikabila na kikanda? Amemteua Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye ni mtoto wa dada yake ili anapotaka fedha, mpwa wake ambaye ni mlipaji mkuu wa serikali awe anatoa kiurahisi,” alisema Lissu.

CHANZO: MWANAHALISI


Filed under: HABARI Tagged: CCM, CHADEMA, demokrasia, Lissu, Magufuli, Tanzania

Kwani upinzani wa kisiasa ni adui wa maendeleo?

$
0
0

ZIMEKUWEPO  hisia miongoni mwa nchi za Kiafrika kuwa upinzani wa kisiasa ni kama njia ya kuzorotesha maendeleo! Hisia hizo zinatolewa na serikali zinazokuwa zimeingia madarakani kwa njia ya kudai demokrasia na baada ya kuukalia usukani zikatamani kuiziba njia hiyo ili isije kutumiwa na wengine, pamoja na serikali zilizodumu madarakani muda wote bila kuonesha maendeleo chanya.

Mfano, tumeshuhudia serikali ambazo zimelazimika kushika usukani kwa kupitia misituni, kwa maana ya kuendesha vita katika jitihada za kuzing’oa serikali zinazokuwa madarakani huku zikiweka vikwazo vya kuondoka madarakani kidemokrasia.

Cha kushangaza ni kwamba serikali hizo zinazokuwa zimepita misituni kutokana na njia za kidemokrasia kuwekwa vigingi, badala ya kuzisafisha njia za kidemokrasia ili ziweze kupitika kiurahisi nazo zinazidi kuweka vigingi kana kwamba njia za misituni ndizo pekee  zilizobarikiwa!

Ikumbukwe kwamba harakati zote za kutaka kuchukua madaraka, hususan katika nchi za Kiafrika, ziwe za kiupinzani wa kawaida au hata zile za kupitia misituni, zinaongozwa na neno demokrasia. Kwamba serikali zinazokuwa madarakani zinapuuza sana demokrasia.

Kwahiyo zinakuwepo ahadi lukuki za kujenga na kuimarisha  demokrasia ya kweli pale wapinzani wakiingia madarakani. Lakini kimaajabu, ikishatokea wapinzani wakaingia madarakani ahadi zinabadilika, demokrasia inazidi kuminywa kuliko hata mwanzo.

Kisingizio kikubwa ni cha maendeleo. Kwamba wapinzani wakiingia madarakani watazorotesha au kukwamisha kabisa maendeleo yaliyokwisha kupatikana na yanayoendelea kutafutwa! Ambapo kwa lugha nyingine inajitafsiri kuwa upinzani ni adui wa maendeleo.

Mifano ni mingi. NRM ya Uganda kwa kutumia jeshi lake la NRA ilipigana vita vya msituni kwa zaidi ya miaka mitatu kwa madai ya kuitafuta demokrasia na baadaye maendeleo ya nchi. Lakini baada ya kuchukua madaraka neno demokrasia halitakiwi kusikika tena nchini Uganda, isipokuwa demokrasia nchini humo ni NRM. Zaidi ya hapo ni uchochezi na vurugu!

Inadaiwa nje NRM maendeleo ya nchi hiyo yatavurugika, kitu kinachoonesha kwamba upinzani dhidi ya NRM ni sawa na upinzani dhidi ya maendeleo! Vivyohivyo nchini Burundi, Rwanda na hata DRC.

Ila namshukuru na kumpongeza sana rais msitaafu wa Kenya aliyepewa uprofesa wa siasa, Daniel Toroitich arap Moi, kwa kukubali bila mizengwe kuikabidhi nchi kwa upinzani baada ya yeye kusitaafu. Bilashaka yeye aliamini kwamba maendeleo ya Kenya yangeweza kuendelezwa na wapinzani kuanzia pale alipoyafikisha yeye, ilmradi nao walikuwa ni Wakenya wazalendo.

Kitu pekee cha kutia simanzi ni pale mrithi wake, Mwai Kibaki, aliposhindwa kuwaamini wapinzani wake kuwa nao wangeweza kuyaendeleza maendeleo hayo pale alipokuwa anawania kipindi cha pili cha uongozi wa nchi hiyo na kuifanya Kenya izame kwenye gharika la damu!

Lengo la makala haya ni kuangalia upinzani na maendeleo. Ni kweli upinzani ni adui wa maendeleo kama inavyofanywa ieleweke na walio madarakani katika nchi nyingi za Kiafrika?

Mimi naamini kwamba kitu chochote kisichotaka upinzani, kwa maana ya mabadiliko, hudumaa. Na katika udumavu maendeleo hakuna. Kilichodumaa hakiendelei, maana hakikui.

Tatizo la udumavu katika Afrika limesababishwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la kuuhofia upinzani. Tumebaki kukiri tu kuwa sisi ni nchi changa kana kwamba uumbaji wa dunia ulianzia kwa nchi zilizoendelea na sehemu yetu ikaja kuumbwa baadaye!

Lakini tukiyaacha mawazo hayo ya kufikirika na kuamua kuutazama ukweli tutaona kwamba kwa namna ya pekee upinzani ndio umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika nchi hizo zinazoitwa za dunia ya kwanza.

Mfano tukichukulia taifa kubwa duniani ambalo kwa miaka mingi limeonekana kuwa mbele kwa karibu kila kitu, Marekani, tutaona kwamba tangu lianzishe upinzani wa kisiasa kwenye miaka ya 1850, limekuwa likipiga  hatua za maendeleo kwenda mbele bila kukwama.

Kila kukitokea aina za mkwamo wananchi wanabadilisha serikali kwa njia za kidemokrasia, wanakiondoa chama kimoja na kukiweka kingine. Kwahiyo kila chama kinachokuwa madarakani kinaelewa kabisa kwamba kikifanya mchezo katika maendeleo ya nchi kinarudishwa kwenye upinzani.

Hilo ndilo linalonifanya niamini kabisa kwamba upinzani upo kuyalinda maendeleo ya nchi tofauti na inavyooneshwa huku kwetu kwamba upinzani unaweza kuyavuruga maendeleo.

Kwahiyo nadhani tusingekuwa watu wa kuomba misaada peke yake katika nchi kama hiyo ya Marekani huku tukiwa tunakiri kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo, bali pia tungetakiwa kujifunza mbinu ilizozipitia kuyafikia maendeleo hayo.

Maana ni busara kwa mtu mwenye njaa kumpa jembe akalime kuliko kumpa chakula cha masimango kila siku. Kwa mantiki hiyo hatupaswi kuyaangalia tu maendeleo zilizonayo nchi kubwa na kubaki tunayahusudu tu bila kujiuliza maendeleo hayo ziliyapataje na kujaribu kuziiga mbinu hizo.

Kama nilivyoeleza hapo juu, mbinu mojawapo kubwa ya maendeleo ni demokrasia na upinzani wa kisiasa. Hivyo ni vitu ambavyo tunavyo au niseme vimo ndani ya uwezo wetu. Lakini badala ya kuvitumia ili vikachochee uwezo wa kupata maendeleo tunavifanyia “figisu” za kutaka kuvizima visiwepo huku tukiziangalia nchi hizo zinazovitunza vitu hivyo kiumakini jinsi zilivyoendelea na kutuacha sisi udenda ukitutoka!

Mapinduzi ya Ufaransa, 1789 – 99, yaliyouondoa utawala wa kifalme na kuiweka nchi hiyo kwenye utawala wa kidemokrasia ndiyo yaliyoifanya nchi hiyo iwe hivi jinsi ilivyo kwa wakati huu. Pamoja na kuuondoa ufalme mapinduzi hayo yalijenga upinzani nchini humo.

Ikumbukwe nchi hiyo ilifikia wananchi kukosa chakula huku mke wa mfalme akiishangaa hali hiyo na kuuliza kwamba kama wananchi wamekosa mkate kwa nini wasipewe keki?

Hiyo yote kwa sasa inadhibitiwa na upinzani ambapo wananchi wakikosa mkate hawasubiri keki ila wanauondoa utawala uliopo na kuweka mwingine. Upinzani ni rafiki wa maendeleo.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo, anayepatikana kwa anwani ya barua-pepe: prudencekarugendo@yahoo.com na au simu nambari +255784989512

 


Filed under: SIASA Tagged: Afrika, CCM, CHADEMA, cuf, siasa, Tanzania, upinzani

Guantanamo isifananishwe Segerea

$
0
0

SI sahihi sana kumuingiza Rais John Magufuli katika chungu kimoja tu cha kuukosoa utendaji wake wote. Yapo ambayo anapatia, na kwa nionavyo, kwa hayo, amekuwa mfano kwa viongozi wengine.

Mapambano yake dhidi ya ufisadi, ni mfano, ingawa kiutekelezaji zipo kasoro hizi ni na zile. Kuonesha jinsi gani yapo mazuri, wakati mwengine husababisha aibu na fedheha isiyosemwa kwa tawala zilizopita.

Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya mambo, rais hatendi vizuri. Hii dhana ya kutambua na kuheshimu “uhuru wa kutoa maoni” na baadhi ya haki za binaadamu ipo shidani.

Kauli yake ya hivi karibuni akiwa katika ziara ya Mkoa wa Pwani, alichokizungumza zaidi akimlenga mwanasiasa Edward Lowassa na ya wale Masheikh na kutoka Bara na Zanzibar walioko ndani kwa karibu miaka minne sasa, inachanganya na kuogofya.

Na Rashid Abdallah

Namna anavyoendelea kukoroga katika baadhi ya mambo, unaweza kusema ni kama vile mtu anayevaa kinyago na kukivua; akikivua huonesha ubora wa uongozi wake lakini akikivaa, huwa mtu mwingine.

Anasema, “Niwaombe wanasiasa wajifunze kuchunga midomo yao… unakuta kiongozi anasema waondolewe lock up (mahabusu), hajui kuna wengine wale wabaya walikaa Guantanamo Bay kuliko hata mwaka mmoja.”

Ukiichambua kauli hii kiudadisi unauona utata. Anawatisha wanasiasa wengine, hasahasa wa kambi ya upinzani. Ni vitisho vinavyolenga moja kwa moja kuubinya uhuru wa kutoa maoni na kuzikaidi haki za binaadamu.

Amewahi kuwaonya waache kuropokwa. Kilichowazi anawatisha wasitumie uhuru wao wa kuzungumza, kwa sababu huko nyuma pameshuhudiwa marufuku ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Suala la maonyo ya namna hii si kingine ila ni uleule muendelezo wa ubabe. Anaelekea kutaka kuyamazisha wasiokuwa upande wake kifikra na kimaono. Kwa muda sasa, ndani ya uongozi wa awamu ya tano, kumekuwa na dhiki iliyoambatana na hofu katika watu kutoa maoni.

Bali Tanzania ni jamhuri iliyo huru. Hata katiba yake – Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 – na ile ya Zanzibar – Katiba ya Zanzibar ya 1984 – zinaelekeza uhuru wa watu kutoa maoni na kuwa huru katika kujishirikisha kwenye maongozi ya nchi yao.

Ni desturi ya wanaadamu kutofautiana maoni. Na si lazima mtu kukubaliana na kauli ya mwanasiasa fulani, au hata raia tu. Hata hivyo, kutokukubaliana hakuifuti haki ya kuzungumza kwa namna ya kutoa maoni binafsi.

Pia katika kauli nyengine isiyovutia ni pale aliposema: “Wanashikwa hawa wanaohusika na mambo ya ajabu katika nchi.” Hivi hapo wanalengwa wananchi waliozuiwa na vyombo vya dola kwa miaka minne sasa? Kama ni hivyo, basi picha inayopatikana ina maana wamehukumiwa.

Masheikh wanaotambulika kuwa miongoni mwa viongozi na walimu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (UAMSHO), walikamatwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2012, kwenye mazingira ya mji wa Zanzibar.

Wakafunguliwa kesi Mahakama ya Vuga, Zanzibar, lakini baadaye wakaunganishwa na kesi iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Tangu hapo hakujatolewa ushahidi wowote dhidi yao.

Yumkini ndio sababu hasa ya Lowassa – kama wanavyolalamika na kushauri wanasiasa na wanajamii wengine mbalimbali nchini wakiwemo watetezi wa haki za binaadamu – akalisemea suala hili. Kwa maoni yake hayo, anaendelea kuripoti makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Amehojiwa.

Sibishani na kiongozi. Hata kidogo. Mimi ninahofu tu kwamba hivi ikitokea mahakama imeamuru waachiwe kwa kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani, hapo kesi itakapokuwa imesikilizwa, itakuaje?

Jambo jingine hapa ni kwamba siioni sababu nzuri ya kufananisha mahabusu za Tanzania na ya Guantanamo inayodhibitiwa na Marekani. Hazifanani kwa asili na dhamira. Labda kama ndio dunia inapelekwa kuamini hivo.

Inajulikana gereza la Guantanamo, lilivyo na sifa ya kuvunja haki za binaadamu ikianzia na kushilikilia watu pasina kuwashitaki, hadi kuwatesa kupitiliza mpaka. Hivi ni sifa jamhuri kujifakharisha kwa hayo?

Mamia ya watu wamekuwa wakishikiliwa Guantanamo tangu 2002 baada ya gharika ya Septemba 11, 2001 au (9/11) ya mashambulizi ya ndege za Marekani katika miji ya Washington lilipo jengo la Pentagon yalipo makao makuu ya Wizara ya Ulinzi, na New York penye Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTC).

Wengi hawakupelekwa mahakamani kushitakiwa. Wapo idadi fulani wameachiliwa kwa shinikizo za serikali za kigeni zenye raia zake huko.

Afadhali ninaojadili wanapelekwa mahakamani hata kama kesi zao zinasuasua. Basi huo si mfano mzuri wa kuuchagiza kama jamhuri inautashi wa kuendelea kuaminisha ulimwengu kuwa inafuata katiba, inatambua na kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama, alitaka kulifunga Guantanamo kwa kuanza kuwaachia wafungwa waliokuwepo. Aliamini kisheria haikubaliki kumshikilia mtu bila ya kumshitaki halafu serikali ikajinasibu inaongoza kwa kufuata utawala wa sheria.

Mmoja wa maafisa katika utawala wa Rais wa 43 Marekani, Geroge W. Bush, anasema: “Wengi wa walioshikiliwa Guantanamo Bay walikuwa ni watu wasio na hatia, walisombwa na Jeshi la Marekani, pale waliposhindwa kutofautisha kati ya maadui na raia wasiokuwa na silaha.”

Ule msemo wa vita havina macho, ndio hasa kilichotokea kwa mujibu wa maelezo ya afisa huyu. Watu walibebwa na kupelekwa magerezani kwa sababu tu jeshi lilishindwa kutofautisha raia na adui waliokuwa wanapambana nao.

Mwanasiasa wa Chama cha Republican, Lawrence B. Wilkerson, aliliambia Shirika la Habari la Associated Press (AP) la Marekani: “Guantanamo Bay bado wapo watu wasio na hatia wanashikiliwa. Baadhi wako kwa miaka sita au saba.”

Kwa hivyo, walichokifanya Marekani, ni kama kuwa na nyavu, ukaipitisha mtoni. Unashika kambare wadogo kwa wakubwa, mikunga wanene na wembamba, hadi tope na uchafu navyo vinakuwemo. Hiyo ndiyo elimu kuhusu suala hili.

Haistahili magereza ya Tanzania kufananishwa na Guantanamo. Masheikh wa Zanzibar waliwahi kutoa tuhuma kuwa ndani ya kukamatwa kwao Zanzibar na kusafirishwa Dar es Salaam, mpaka kuhifadhiwa gerezani Segerea, wamepata kudhalilishwa, ikiwemo kupigwa na kuteswa, lakini haraka na kwa sauti nzito serikali ilikanusha.

Masheikh waliopo gerezani bila ya kuhukumiwa tangu hapo, wakiwa wanapelekwa mahakamani kila baada ya wiki mbili hivi, kuwataja kuweza kuhusika na mauaji yanayoendelea mkoani Pwani, ni hatua inayojenga picha isiyoeleweka na isiyoaminika.

Wakati natambua mchango wa Rais katika kudhibiti ufisadi, ni muhimu ashauriwe kuwa inastahili kuongoza huku akiamini wananchi kufaidi uhuru wao. Waseme walionalo. Inasaidia kuwatumainisha kuwa nao ni sehemu ya watoa mamlaka inayoongoza.

Wananchi wanahitajika kukuza uchumi kupitia shughuli zao mbalimbali. Ndio walipa kodi wakubwa, kodi ambayo ndio nguzo kuu ya kuiwezesha serikali kuhudumia jamii. Maendeleo ni hatua, ambazo lazima zipigwe kwa kushirikisha kila mtu. Serikali peke yake haiwezi kufanikisha maendeleo.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017. Mwandishi wake anapatikana kwa simu nambari +255 657 414 889


Filed under: SIASA Tagged: Guantanamo, haki za binaadamu, Magufuli, Tanzania, Uamsho, Zanzibar

Kiburi kinachoelezea shibe hakifai

$
0
0

KIBURI ni uovu uliokatazwa na maandiko matakatifu. Mwenye nacho amedharau utu. Ni kwa maana hiyo hata wahenga walifikia hitimisho la kuwa na methali ya Kiswahili inayosema ‘kiburi si maungwana.’

Methali hii ina maana kuwa mtu mwenye heshima na busara hatakiwi kuwa na kiburi. Ni methali inayotumika kusisitiza kuwa mtu muungwana sharti awathamini wenzake na kuwatendea haki na sawa.

Katika maisha ya binadamu, wapo watu wanaoaminika kuwa viongozi kwa kuchaguliwa na wananchi, siyo wa kujitwalia madaraka kwa nguvu za mtutu wa bunduki, aghalabu hujifunza uungwana.

Hujiepusha na kiburi, kwa kuwa kiburi kinajenga umimi, jeuri, ubabe na kupuuza wengine. Kiburi kinajenga na kuushibisha moyo wa binadamu ganzi ya kukosa utu, huruma. Kiburi ni mama na baba ya uharibifu wote kwa mwanadamu.

Katika historia ya viongozi wa Tanzania waliopata kukaa Ikulu kwa ridhaa ya wananchi, wapo watano. Kwa sasa yupo Rais John Magufuli. Kabla yake, alikuwapo Jakaya Kikwete (2005-2015), ambaye aliachiwa kiti na Benjamin Mkapa (1995-2005).

Mkapa akiwa rais wa tatu alipata madaraka baada ya Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) aliyempokea kijiti Muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere (1961-1985).

Katika orodha hii, ukiweka pembeni aliyepo madarakani na kwa maana hiyo si haki kumjadili hapa kwa sababu hajamaliza ng’we yake, waliobaki wanne, hakuna wa kufananishwa na Mkapa kwa kiburi.

Mkapa ni kiongozi pekee mstaafu wa ngazi ya urais mwenye ujasiri wa kutukana wananchi. Kuwatusi wale anaoamini wana mawazo tofauti na yake. Kwake, anayetofautiana naye ni ‘mpumbavu na lofa.’

Akiwa wilayani Chato wiki iliyopita, Mkapa alirejea maneno aliyoyatamka mwaka 2015 viwanya vya Jangwani, kwenye mkutano kuzindua kampeni za kusaka urais za mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Magufuli.

Alisema wanaosema habari ya ukombozi wa nchi ni ‘wapumbavu na malofa.”

Pamoja na kuwako na shutuma nyingi dhidi yake kutokana na kauli ya ‘upumbavu na ulofa’ takribani miaka miwili baadaye, bado kiburi hakimuachii kutambua kuwa anatumia lugha ya kuudhi na kudharau wananchi.

Dhidi ya walipakodi wanaomwezesha kuishi maisha ya raha na amani. Anaamini kila anayesema ambayo hataki kusikia ni mpumbavu na lofa.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaelezea lofa kama mtu anayezururazurura, asiye na kitu wala kazi. Mpumbavu anatajwa kuwa mtu anayeshindwa kuelewa jambo hata akielezwa. Kwa meneno mengi anaitwa juha, zuzu, nyange, banghami, bahau, fala, hambe, jahili, mbumbumbu na mengine mengi.

Ungeliweza kuelewa na kuvumilia kwamba mwaka 2015, huenda Mkapa alihemuka kama wahemukavyo wanasiasa wengine wanapoona umati kama uliokuwa umejitokeza kushiriki fungua kampeni ya mgombea urais wa CCM.

Lakini miaka miwili baadaye anasema maneno yaleyale, tena safari hii mbele ya yule aliyekuwa anamnadi Jangwani. Kitu pekee kinachotoa ujasiri huo kwa kiongozi mstaafu wa aina yake ni kiburi. Kiburi tu.

Wapo watu wamejiuliza maswali mengi juu ya kiburi cha Mkapa. Kwamba kinatokana na nini? Wapo wanaonasibisha kiburi hicho na tabia, makuzi na hulka yake. Wengine wanasema ni matokeo ya shibe na kinga ya kutenda bila kujali nini kitampata kwa sababu ya kuzama kwenye kichaka cha sheria na mifumo ya kulindana uliowekwa na CCM.

Mifumo yenyewe inawasukuma washika madaraka kuamini hata wakitoka, watakuwa tu salama hata kama walikosea walipokuwa wanatenda.

Hivi, kama kiongozi aliyekaa ikulu kwa miaka 10 na akiwa ameshikilia nafasi za uwaziri, ubalozi na hata utumishi wa ngazi nyingine serikalini kwa zaidi ya miongo minne, si tu alitarajiwa kujifunza kuwa mnyenyekevu, bali mwalimu kwa wengine. Uongozi ni utumishi.

Kwa nini anaona Watanzania hawana kitu -malofa? Mkapa anaposema “watu wenye mawazo tofauti na watawala ni malofa” anakusudia kuwadhalilisha kwa sababu wanahoji ambayo yeye Rais Mstaafu amekuwa sehemu ya uwajibikaji wake.

Malofa hawa wamefikishwa walipo. Ni kweli hawana kitu. Ni vipi mwananchi hohehahe atakuwa sawa na rais mstaafu anayeishi na kugharamiwa kila kitu kwa kodi za wananchi?

Ni vipi mwenyekiti wa chama cha siasa kisicho hata ruzuku ya serikali, apate maisha mazuri sawa na rais mstaafu? Ni vipi mwananchi wa aina hiyo atakuwa na walinzi kadhaa wa kumlinda kila aendako; ni vipi atakuwa na nyumba inayogharimiwa na serikali kila kitu.

Huyu rais mstaafu analipwa mshahara wa asilimia 80 ya mshahara wa rais aliyeko madarakani; nyumbani ana wapishi watatu; mtunza bustani; anabadilishiwa gari kila baada ya miaka mitatu na anagharamiwa angalau safari mbili nje ya nchi kila mwaka na anatibiwa kwa kodi za wananchi.

Kwa mfumo wa maisha na stahili za rais mstaafu hawezi kuwa lofa. Lakini kitu kimoja cha msingi malofa ambao Mkapa anawakejeli yumkini wapo wanaoendesha maisha kwa kujikimu kwa kilimo, wanalipa ushuru na kodi nyingine ambazo serikali huchukua na sehemu yake ndizo zinatumika kumpa yeye maisha ya ukwasi.

Lakini kitu kingine anachosahau ni kwamba hao malofa anaowakejeli hawakupata fursa na hawakuwa sehemu ya mpango wa miaka 10 wa serikali yake wa kuuza na kukwapua mali za umma- mashirika, nyumba na rasilimali nyingine nyingi. Kwa hiyo wanufaikaji wa sera za kupora mali ya umma chini ya kivuli cha ubinafsishaji, ndio wenye jeuri ya kuwaita wengine malofa.

Hakuna lofa aliyepewa nyumba ya serikali kwa bei ya bure kwa kisingizio cha kuwa mtumishi wa umma katika sakata la karne la watumishi wa umma kuamua kilaghai chini ya Mkapa kuuziana nyumba za serikali kwa bei ya kutupa. Kwa kuwa hawana nyumba za kupeana bure, ndio waitwe malofa?

Kikubwa zaidi ni malofa kwa sababu hawakushiriki kuandaa mikataba ya kilaghai iliyowapa wawekezaji umiliki wa raslimali ya madini, gesi, vitalu vya uwindaji na mapande ya ardhi yasiyoendelezwa.

Kwa hiyo, Mkapa kama mtu mzima wa umri na uelewa, kinachomsumbua ni kiburi cha ukwasi unaotokana na rasilimali za taifa. Ni kiburi kinachochangiwa na ulinzi wa sheria na mifumo walioiasisi kwamba wana haki ya kutenda makosa pasina kuadhibiwa – utamaduni wa kulindana (culture of impunity).

Kwa matusi yake ya rejareja anazidi kuthibitisha kuwa ameshindwa kuwa kiongozi wa taifa (statesman), badala yake anajiona kuwa salama yake ni kutetea mifumo ya ovyo ya kupora rasilimali za taifa; kupiga vita uwazi, uwajibikaji na demokrasia.

Ameshindwa kujielewa kuwa kwa nafasi alizowahi kushika ingempasa sasa kuamini – maana anatambua – kuwa kiburi si uungwana na ni vibaya mtu aliyeshiba kulala mlalo wa kumwonyesha Mungu tumbo lililofura. Ajue, shujaa muungwana huacha asili.

TANBIHI: Makala hii iliyoandikwa na Chris Alan ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017.


Filed under: HABARI Tagged: kiburi, Mkapa, Tanzania, ufisadi

Riziki Shahari: Mamlaka ya Bunge kikatiba siyaoni

$
0
0

UKIJUA historia ya ujanani kwake alivyokuwa akisoma hadi alipohitimu elimu ya kidato cha tano katika Shule ya Wasichana ya Korogwe mwaka 1980, ndio utaelewa ni kwa nini leo Riziki Shahari Mngwali ametokea kuwa mwanamke mkakamavu asiyeyumba kimsimamo.

Nimebaini kuwa hivyo ndivyo alivyo Bi Riziki, mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na mbunge wa Viti Maalum.

Mama huyu, mzaliwa wa mwaka 1960, ni kiongozi shupavu aliyejijengea heshima kubwa tangu akiwa katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) lililodumu kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2013 mpaka 2014.

Bi Riziki ni mwingi wa maelezo yenye maneno mazito ambayo huachi kufikiri mara mbili ukiyasikia. Wala hana muhali akijisikia kusema.

Akiipata nafasi ya kusema jambo analolijua na kuliamini, husema hasa. Hafichi kitu na hana sababu ya kudanganya. Huwa anajitoa na kusema ukweli mtupu kinagaubaga.

Katika mahojiano mahsusi na MwanaHALISI yaliyofanyika Jumatano wiki iliyopita kwenye ofisi ya wabunge wa CUF jijini Dar es Salaam, mbunge huyo anasema ukakamavu wake ni wa asili tangu akiwa shule.

Anakumbuka visa mkasa vitatu vilivyomsukuma kuingia kwenye siasa. Mosi, anasema wakati akisoma kidato cha tano na sita katika shule ya wasichana Korogwe ya mkoani Tanga, walifundishwa somo la siasa iliyoelekeza namna ya kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pia jioni walipata mafunzo ya siasa ya lazima kutoka CCM yaliyojumuisha hata wale wanafunzi ambao hawakupangwa kusoma somo la siasa.

“Sikuona umuhimu wa kurudia kufundishwa kitu kimoja mara mbili. Nilihoji kuhusu hili na wakati wa mahafali ya kidato cha sita tukalazimishwa kufanyiwa sherehe pamoja na waliosoma mafunzo kuhusu CCM ambao hawakuwa wahitimu.

“Tulipohoji, tukanyimwa kadi ya uanachama ya CCM,” anasema Riziki.

Kadi hiyo anasema ndiyo iliyotumika kama kiambatanisho cha kujiunga na chuo kikuu na hata mafunzo ya kijeshi jambo amabalo anasema lilikuwa linawanyima haki ya kupata elimu kwa sababu tu ya kukosa kadi.

Kisa cha pili, anasema, ni wakati akituma maombi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, katika fomu za maombi ilitakiwa pia maelezo ya wajumbe wa CCM wa mtaa alioishi kuhusu ushiriki wake katika kujenga chama.

“Basi mama yangu akachukua zile karatasi na kuzipeleka kwa wajumbe. Wale wajumbe wakata niende mwenyewe. Mama akawambia kwa kuwa wananifahamu fika wangeweza tu kunijazia bila ya mimi kuwepo; wakagoma kujaza, nikashindwa kutuma maombi, badala yake nikaomba nafasi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nikapata,” anaeleza Riziki.

Je, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakukuhitajika maelezo ya wajumbe wa shina wa CCM? Anasema, “Chuo Kikuu Dar es Salaam sikupata shida, wao walitaka tu kadi ya CCM ambayo nilikuwa nayo.”

Kisa cha tatu ni kilichomhusisha kada wa CCM. Alikuwa kiongozi ila hana uhakika ni ngazi ipi lakini anahisi alitoka wilayani. Anamkumbuka kuwa na kiburi. Alifika shuleni kwao Korogwe na kuitisha mkutano na kuanza kuwatisha.

Anasema kiongozi huyo aliwatisha kwamba angewaweka ndani kama wangehoji chochote kuhusu utawala au serikali na akawapa mfano namna alivyomweka ndani kijana mmoja baada ya kuhoji kwa nini walilazimishwa kusema “zidumu fikra za Mwalimu Nyerere.”

Kijana huyo alisema kwa mujibu wa Kiswahili fasaha, si sahihi kusema “zidumu fikra za Mwalimu Nyerere” wakati mwalimu alikuwa bado hai. Kauli hiyo ingefaa kutumika kama mwalimu angekuwa amekufa. Akaswekwa ndani.

“Hivi visa vitatu vilitosha kunifanya kuuchukia utawala wa CCM kwa kuwa niliona haukutoa uhuru. Ulikuwa kandamizi… nilitamani siku moja niingie kwenye siasa nitetee haki hata kama nisingekuwa kiongozi katika siasa,” anasema Riziki.

Kwa sasa Riziki ni mbunge, nafasi aliyoipata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kupitia utaratibu uliowekwa na chama chake. Japo si mara yake ya kwanza kuwania nafasi hiyo. Mwaka 2005 aliomba lakini hakubahatika.

Anasema matarajio yake na anachokiona bungeni ni tofauti. Anavyoamini, uhuru na demokrasia pana ni muhimu ili nchi kufikia maendeleo.

Anasema “niliingia bungeni kwa hamu kweli nikidhani ni chombo kikubwa kinachowakilisha wananchi na kinachofanya maamuzi kwa kujitegemea. Lakini ni tofauti.”

“Nilitarajia sisi wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wasimamizi wa serikali. Yale mamlaka ya kikatiba ya Bunge siyaoni katika bunge hili,” anasema.

Anatoa mfano kuwa wabunge wa upinzani wanapoihoji serikali au kuishauri, mara nyingi wanazuiwa. “Kiti cha spika au wabunge wa CCM wanatumika kuitetea serikali. Sio wajibu wao,” anaeleza Riziki.

Mbali na Bunge kutumika kama wakala wa serikali, Riziki anaona mbunge mmoja mmoja hapewi hadhi inayotakiwa kama mwakilishi wa mamilioni ya wananchi. Badala yake, hata hukumu dhidi yake zinatolewa kama mtu binafsi.

“Lakini bado sijakata tamaa. Vichwa makini vya wapinzani vilivyopo mle ndani (bungeni) vinanitia moyo. Hata wananchi nao wananitia moyo. Wanaelewa kila kitu kinachoendelea bungeni. Si wajinga,” anasema.

Akieleza hali ya demokrasia nchini, anasema “Ni mbaya. Huwezi kuwa na demokrasia bila ya kuruhusu midomo kuzungumza. Kinachofanyika sasa ni hofu, na makatazo ndiyo yametanda. Siasa ni maisha ya kila siku. Hakuna kipindi maalum cha kufanya siasa.”

Anasema utendaji wa serikali si mzuri. Unaweza kuwa na nia na mambo mazuri, lakini haufuati utaratibu, sheria na kanuni ambazo imejiwekea.

Riziki haachi kueleza athari za mgogoro wa uongozi ndani ya CUF, anaoamini uliasisiwa na Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, kwa msaada wa vyombo vya serikali, ikiwemo ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Mgogoro huu unatuathiri kiasi chake. Fedha za ruzuku zimezuiliwa kwa sababu ya suala hili. Wabunge na chama tunashindwa kuendesha shughuli za maendeleo katika majimbo ipasavyo. Tunalazimika kuchangishana mfukoni,” analalamika.

Riziki ni mtaalam wa Sayansi ya Siasa, elimu aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ngazi ya Shahada mwaka 1982 hadi 1985. Pia ana Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Kimataifa aliyoisomea katika Chuo Kikuu cha Colombia, Marekani.

Elimu ya sekondari alisoma shule ya wasichana Kisutu na elimu ya msingi aliipatia Shule ya Msingi Ilala Bungoni, Dar es Salaam mwaka 1967 hadi 1973.

Mwaka 1985/86 alifundisha Shule ya Sekondari ya Masjid Quba ya jijini Dar es Salaam. Riziki alifundisha masuala ya diplomasia mwaka 1986/2015 katika Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam, na baadhi ya aliowafundisha ni wabunge Nape Nnauye (Mtama), Marry Mwanjelwa (Viti Maalum) na Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini).

TANBIHI: Makala hii iliyoandikwa na Pendo Omary ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi katika toleo lake la tarehe 17 Julai 2017. 


Filed under: JAMII Tagged: bunge la tanzania, cuf, riziki shahari, Tanzania

Escrow ichunguzwe upya

$
0
0

KASHFA ya kuchotwa fedha zilizokuwa zikibishaniwa na washirika wawili wa kibiashara hapa nchini – Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya IPTL – Akaunti ya Tegeta Escrow – imeibuka upya kwa nguvu kubwa safari kuliko wakati mwingine wowote.

Tangu mjadala wake ulipofungwa baada ya Bunge kuazimia mapendekezo 13 ambayo lilitaka Serikali iyatekeleze, kashfa hiyo iliyohusu ufisadi wa zaidi ya Sh. 320 bilioni, haikuwahi kujadiliwa kwa hisia kali kama ilivyo sasa.

Kwa namna inayosikitisha na kuonesha jinsi gani utawala unavyodharau maoni ya umma na mihimili mingine ya dola, likiwemo Bunge, kwa kutoheshimu kiudhati ushauri wake, hata vyombo vya kiuchunguzi vilivyokuwa na wajibu wa kuchukua hatua thabiti vilinyamaza.

Kimya kikubwa kilipita huku serikali ikijivuta, isitekeleze kwa uzito uliostahili mapendekezo ya Bunge baada ya mjadala mkali wa wabunge ilipobainika kuwa fedha zilizokuwa zikisubiri uamuzi wa mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara ya nchini Uingereza, zimechotwa isivyotarajiwa.

Si Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa wala Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) walioinua sauti kusema wanaendelea kutafuta ukweli. Kwa hakika, wakuu wa taasisi hizi za kiuchunguzi waliufyata.

Bila ya shaka walibaki kimya kwa hofu. Kilichokuwa kikiendelea ni utata. Kwamba je umma umuamini rais aliyetoa msimamo kuwa fedha zilizochotwa kutoka akaunti iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), si za umma?

Au Watanzania wafuate msimamo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyesema “Ndani ya fedha zile kulikuwa na kodi. Kodi ni mali ya umma. Hivyo kwenye eneo hilo la kodi, fedha za umma zipo?”

Alisema historia ya kuanzishwa kwa akaunti hiyo ni kuwa IPTL na Tanesco walikuwa na mzozo kuhusu malipo ya capacity charge. Mgogoro ulikuwa mkubwa na wakaamua kuhifadhi fedha za malipo hayo kwenye akaunti ya Escrow, wakisubiri shauri lao katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

“Ikitokea ni kweli Tanesco ilikuwa inatozwa kiwango kikubwa kuliko ilivyopasa, si sehemu ya fedha ingekuwa ni zake na hivyo ni za umma?”

Kitendo cha mmoja wa waliogawiwa fedha na aliyekuwa sehemu ya umiliki wa IPTL, kujitokeza kurudisha alichogawiwa, Sh. 40 milioni, kimeibua hisia upya, na kwa nguvu kubwa zaidi. Wapo wanaotaka kila aliyeguswa akamatwe na kushitakiwa.

Leo hata TAKUKURU wameibuka na kusema wanaorudisha hawajasafishika. Ni msimamo mpya baada ya kimya kizito. Kwa bahati mbaya, TAKUKURU hawasemi walichochunguza ni kipi hasa – zile zilizokuwa kwenye akaunti ya Benki ya Mkombozi tu au na hata zile ambazo serikali haikuthubutu kumkabidhi CAG achunguze?

Ni rai yetu kwamba kashfa ya Escrow ichunguzwe upya na kitaalamu zaidi. Siasa na utashi wa kulinda wakubwa viachwe.

TANBIHI: Hii ni tahriri ya gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017.


Filed under: MAGAZETINI LEO Tagged: Escrow, Tanzania, ufisadi

Nguzo ya pili ya mitaji ya mafanikio ni fikra

$
0
0

Katika makala ya juma lililopita niliweka bayana kwamba nguzo ya kwanza ya mitaji ya mafanikio ni Afya Njema ya Mwili. Mwili wenye afya njema ndicho chombo cha kutekelezea mawazo yako endapo ni mazuri, murua na ikiwa yamechujwa na kupimwa. Kila uamkapo asubuhi, kichwani kwako unafikiria cha kufanya, mahali kwa kwenda na namna ya kwenda huko. Mwili wenye afya njema unakuwezesha kuwaza cha kutenda. Na kwahiyo, nguzo ya pili ya mitaji ya mafanikio ni “Fikra” au “Mawazo.”

Kila kitu kinachofanyika kwa vitendo huanzia kichwani – kinatokana na fikra au mawazo (ideas) ya vichwani mwetu. Wengine huenda mbali zaidi na kusema vitu vyote vinavyotuzunguka na kuonekana kwa macho, kugusika au kushikika (tangibles), chimbuko lake ni vitu visivyoonekana (intangibles), yaani fikra au mawazo. Amini usiamini, hata kuwepo kwa sayari ya dunia na zinginezo, pamoja na ulimwengu mzima, wa vitu hai na visivyo hai, kulitokana na mawazo! Uumbaji huanzia kwenye mawazo, na hadi sasa tunaendelea kuumba au kutengeneza vitu kwa kuanza navyo kichwani.

Na kwa kusema hivyo, lazima niweke wazi kuwa zipo fikra mbovu au potofu na fikra pevu. Zote ni fikra au mawazo, lakini tutajikita zaidi katika fikra pevu – zilizopikwa kichwani na kuiva, zenye faida ya kutuletea maendeleo ya mtu binafsi, jamii na ulimwengu kwa ujumla. Bila fikra, tunabakia watupu kama makopo au mapipa yaliyowazi. Fikra ni mwanga wa giza na zinaweza kubadili chochote kutoka kutokuwa na faida kwenda kwenye mafanikio. Ilimradi una afya njema ya mwili na akili, tayari una nguzo muhimu za kukupatia mafanikio katika maisha.

Fikra ni ubunifu alionao mtu kichwani au akilini mwake. Hata fedha ulizonazo mkononi, mfukoni, kwenye pochi yako au benki, ni sarafu au makaratasi tu yanayochapishwa na kutupwa au kubadilishwa baada ya kutumika. Lakini fikra au mawazo yaliyosababisha upate hayo makaratasi unayoyaita fedha taslimu ndio msingi au nguzo muhimu ya mafanikio yako. Hakuna anayepinga ukweli huu, na kwahiyo nami napata fursa nzuri ya kujadili kwa kina kuthibitisha kuwa fikra au mawazo ni mtaji tosha.

Mchango wa fikra na mawazo katika maendeleo ya watu

Angalia maandishi mbalimbali yenye maelezo (information), maelekezo (instructions) na miongozo (guidelines) mbalimbali. Sikiliza sauti kwenye vyombo mbalimbali vya kutunzia na/au kunasia sauti. Ni kama mchanga wa bahari ya mawazo kutoka vichwani mwetu. Hata mtu akifa bado ataendelea kuishi nasi kupitia mawazo yake yaliyoandikwa au kurekodiwa (audio), na pengine hata picha zake mnyato (video) tutaendelea kuishi nazo daima.

Aidha, fikra ni ndoto au maono ya mtu anayoyafanyia kazi yeye mwenyewe au wengine ili yatimie. Kuna watu wengi wametupa maono pevu na kuleta mafanikio makubwa sana katika jamii. Dkt Martin Luther King alikuwa na ndoto ya jamii inayojali utu, haki na usawa nchini Marekani.

Ndoto alizoota na kutamka Dkt King, ziliandikwa, zikarekodiwa na kutimia kwa mtu mwenye asili ya Afrika, Barack Hussein Onyango Obama, alipokuja kuapishwa rasmi mnamo Januari 20, 2009 kuwa rais wa Marekani. Ilipita miaka zaidi ya 40 baada ya Dkt King kufariki. Mwili wake ulikufa lakini mawazo yake yaliendelea na yanaendelea kuishi nasi – yuko hai pamoja na Wamarekani na wapenda haki duniani kote kupitia fikra zake za ukombozi.

Nelson Mandela alikuwa jela, lakini fikra zake za ukombozi zilirindima duniani kote na zikaja kufungua milango ya gereza na hatimaye akawa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini.

Fikra alizokuwa nazo Dkt Martin Luther King zimesaidia sana kuibadilisha Marekani

Fikra za ukombozi za Nelson Mandela zilisaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa ukaburu Afrika Kusini

Nisisitize kuwa tuliumbwa kwanza ili tufikiri na ndipo tuishi, hatukuumbwa kuishi ndipo tufikiri. Tuko hivi tulivyo kutokana na jinsi tunavyofikiri. Bila kufikiri tunakuwa si watu, tunabaki kama vyombo vya kutumika na kutumiwa na wengine. Kama kuna utumwa mbaya na jela mbaya kuliko zote, basi ni kubinywa kufikiri. Naamini kabisa kikwazo kikubwa cha maendeleo yetu si kukosa rasilimali, bali kukosa fikra za jinsi ya kuzitumia rasilimali zetu kwa faida yetu. Ufukara mbaya kabisa na adui mkubwa kuliko maradhi na umaskini ni kukosa fikra.

Tukikosa ubunifu kichwani tunakosa kila kitu – hata kilicho chetu! Na kamwe tusiruhusu watu wengine au mataifa mengine yawaze kwa niaba yetu, kwa kuwa watakuwa wanawaza kwa faida yao. Tuwe makini sana katika kila tunachowaza ili kiwe na faida kwetu na jamii tuliyomo. Kama kuna urithi bora na udumuo kwa familia na jamii yetu basi ni fikra. Ni muhimu sana kuziandika au kuzirekodi ili tusije kufukiwa nazo kaburini.

Ulimwengu mzima unaendeshwa na kuendelezwa na mawazo. Watu wanatafakari na kukuna vichwa vyao kila siku. Hata Mungu katika misahafu hakutupa fedha au vitu, bali mawazo ya kutusaidia namna bora ya kuishi kistaarabu katika maisha haya na yajayo.

Magari, ndege, maghorofa, simu, umeme, kompyuta, viwanda, nk.; vilianza na wazo na kisha kuendelezwa. Jaribu kufikiria dunia ya wakati wa bila simu wala umeme, kisha angalia mafanikio yake sasa. Msingi wa jambo lolote lile, katika kila nyanja na fani kutoka siasa hadi teknolojia, ni fikra.

Baba wa sayansi ya kileo Galileo Galilei (1564-1642) alikuna kichwa na kugundua anga lilivyojaa sayari mbalimbali na namna zinavyovutana na/au kuzungukana. Alexander Graham Bell alikuna kichwa namna rahisi ya kuwasiliana kwa sauti tukiwa mbali, akagundua simu. Michael Faraday na wengineo, waliwaza na kugundua nguvu za sumaku na elektroni tukapata umeme na mkondo wake wa hasi na chanya.

Tukumbuke ugunduzi wa Archimedes na Isaac Newton unavyotusaidia katika ufundi makenika wa vyombo vya ardhini, majini na angani. Tunastaajabu kila wakati akina Grace Hooper, Charles Babbage, Ada Lovelace, Steve Jobs, Bill Gates (aliyehai hadi sasa) nk.; walivyokuna vichwa katika ugunduzi wa kompyuta na simu za mkononi.

Tumkumbuke Albert Einstein aliyegundua ukweli muhimu sana katika atomi na molekuli na kutuletea kanuni muhimu ya E = mc2. Fikiria aliyekuna kichwa chake na kugundua dizeli na petroli. Mnaoishi sehemu za joto kaali, fikiria waliokuna vichwa vyao na kugundua jokofu na kiyoyozi. Fikiria tunavyofaidika na waliogundua madawa mbalimbali, ya asilia na ya kisasa, pamoja na vifaatiba. Orodha ni ndefu sana!

Nasi tukune vichwa kwa kuwa hakuna ukomo wa ugunduzi madhali Mungu alituumba kufikiri. Kamwe tusijidharau maana inasadikika kuwa kuna mambo mengi sana hayajagunduliwa, ikiwa pamoja na jinsi ya kutibu mwili bila kunywa vidonge au kudungwa sindano. Unatibu tu kwa kutamka maneno yanayomfanya mtu apone. Kwa taarifa tu, zaidi ya asilimia 70 ya tiba bora ya mwili ni maneno yenye faraja, si vidonge wala sindano!

Tunasema haiwezekani. Ni sawa, lakini mbona pia tunasema haiwezekani kutembea kwa miguu juu ya maji? Tayari kuna mtu alishatembea juu ya maji zaidi ya miaka 2000 iliyopita! Tusikate tamaa, tuendelee kukuna vichwa kisha tutagundua jinsi ya kutembea juu ya maji, na kwahiyo tutaacha kujenga madaraja au kuvuka kwa mitumbwi.

Bila mawazo au fikra hakuna maendeleo, hakuna mabadiliko, na hapawezi kuwepo mafanikio yoyote yale popote pale. Nihitimishe kwa kusema kila unapotaka kufanya jambo lolote, tulia, tafakari kwa makini, yapime vizuri mawazo yako ndiposa ufanye maamuzi. Usikurupuke!


Filed under: JAMII Tagged: fikra, mafanikio, martin luther king, mawazo, nelson mandela

La Zanzibar kufukuzwa CAF, tuangalie tulipojikwaa

$
0
0

Ijumaa ya tarehe 21 Julai 2017 itachukuwa muda mrefu kwangu kusahaulika. Kwenye ukurasa wa Facebook, mtumiaji mmoja alikuwa ametuma taarifa iliyoandikwa na dawati la michezo la mtandao wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusu nchi yangu, Zanzibar, kuvuliwa uwanachama wake iliokuwa imeupata siku 128 hapo kabla kwenye Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Kwanza niliipita habari hiyo ghafla kama siijui, lakini kisha nikarudi kuisoma kwa kina neno kwa neno. Ilikuwa taarifa fupi na nzito. Licha ya kuwa kwangu mhariri na mtangazaji wa shirika la habari la kimataifa kwa takribani miaka saba sasa na kwamba BBC yenyewe ni shirika la habari la kimataifa, nilijikuta siiamini habari hiyo.

Nikaenda kwenye mtandao wa CAF, kisha kwenye akaunti binafsi ya Twitter ya mkuu wake, Ahmad Ahmad wa Madagascar, na mote humo sikukuta taarifa hizo. Hadi muda huo, bado kwenye mtandao wa CAF kulikuwa na bendera na jina la Zanzibar kwenye orodha ya wanachama, tena chini ya bendera na jina la Tanzania.

Hata hivyo, nikaituma tena ripoti hiyo ya BBC kwenye ukurasa wangu wa Facebook, nikiambatanisha na wasiwasi na matarajio yangu. Niliomba na kupenda ile iwe ni habari ya uzushi tu, ambayo punde ingelitamkwa kuwa si kweli.

Na Mohammed Ghassani

Siku hiyo pia, nikiwa mhariri wa zamu, nilikuwa nimefikiwa mezani pangu na habari ya wafanyakazi wa kigeni wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia nchini Tanzania kutakiwa kuondoka mara moja. Muda mchache baadaye, mkurugenzi wa Acacia jijini London akakanusha ripoti hiyo ya shirika la habari la Reuters, akisema kilichotokea ni kuhojiwa kwa wafanyakazi wake wawili tu, na sio kufukuzwa nchini Tanzania.

Kwa hivyo, nikawa naomba kimoyokimoyo na hii ya Zanzibar kuvuliwa uwanachama wa CAF itamkwe kuwa haikuwa ya kweli. Lakini hadi siku ya pili yake mchana, habari ilikuwa imebakia hivyo hivyo, huku wahusika wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wakitajwa kutokuwa na habari ya jambo hilo. Ikimaanisha kuwa aidha hawakuwa wamearifiwa kwa taratibu rasmi au walikuwa wanadanganya. Na bado, moyoni mwangu nikawa nataka kuamini kuwa kutokuwa kwao na taarifa kunamaanisha kuwa jambo lenyewe halipo.

Sijui kama unazielewa hisia hizi, lakini mchangiaji mmoja wa ukurasa wangu wa Facebook aliniandikia faraghani akizifananisha na za mzazi aliyepotelewa na mwanawe katika mazingira ya kutatanisha. Mzazi huyu huwa haamini kuwa mwanawe hatapatikana tena. Hata kama miaka mingi itapita, bado huwa anadhani kuwa kuna siku mwanawe atarejea akiwa mzima, salama usalimini.

Ndizo hisia zangu ambazo hadi naandika makala hii, masaa 24 baada ya kupokea taarifa ya kupotea Zanzibar kutoka ramani ya CAF. Kuna kitu kinanifanya nisitake kuamini ukweli kuwa tumeshatolewa. Hisia tu.

Naam, ni hisia tu. Hisia si lazima ziwe uhalisia. Ingawa baadhi ya wakati, sadfa huzigeuza hisia zetu kuwa ukweli. Hayo ndiyo yale yaitwayo makarama. Bahati mbaya kwangu ni kuwa miye si mja wa makarama, na hivyo mara kadhaa hisia zangu hazikumbwi na rehema ya sadfa zikawa ukweli. Zanzibar yangu imeondoshwa kwenye CAF.

Huo ndio uhalisia uliopo mbele yangu na ndio ambao nitaujadili hapa, baada ya kuipata barua rasmi Rais wa Chama cha Soka cha Zanzibar, Ravia Idarus Faina, na Kaibu Katibu Mkuu wa CAF, Essam Ahmed, siku hiyo hiyo ya tarehe 21 Julai. Nitaachana kabisa na hisia zangu binafsi za mzazi aliyepotelewa na mwanawe.

Uhalisia namba moja ni kauli ya Ahmad Ahmad inayosema hivi: “Zanzibar imeondolewa kwenye uwanachama wa CAF kwa kuwa ni wanachama wa FIFA tu ndio ambao wanaweza kuwa pia wanachama wa CAF.”

Uhalisia namba mbili ni sababu ya ziada iliyomo kwenye Kifungu Na. 4(4) cha Katiba ya CAF ambacho kinalilazimisha shirikisho hilo “kukitambua chama kimoja tu cha kitaifa kwa nchi.”

Na uhalisia huo namba mbili ndio unaopigilia msumari kwenye wa namba tatu, unaosema kuwa “uwakilishi wa kitaifa uliopo sasa unaotambuliwa na FIFA na CAF ni ule wa Shirikisho la Soka la Tanzania.” Hapo anakusudia Shirikisho la Soka la Tanzania Bara (TFF).

Huo ndio uhalisia uliopo kwenye uamuzi wa CAF iliyokutana Rabat, Morocco, na kuiondolea Zanzibar uwanachama wake ilioupata tarehe 16 Machi 2017 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Sasa tuje kwenye uchambuzi wa uhalisia huu, kuangalia ambapo sisi Wazanzibari tulijikwaa na sio tulipoangukia.

Ukweli ni kwamba vyombo vya kimataifa vinaitambua Tanganyika (ninaiita Tanganyika kwa makusudi, maana ushahidi unathibitisha kuwa ndiyo inayojiwakilisha kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania). Ukweli huu ndilo jinamizi kubwa kwenye nafasi, maslahi na taswira ya Zanzibar ndani na nje ya mipaka yetu, maana siasa ya Tanganyika nje ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Zanzibar ni muakisiko tu wa siasa yake ya ndani.

Nimeandika mara kadhaa – na daima nitaandika hivi hivi madhali hakuna kilichobadilika – kwamba Tanganyika inaamini kwa dhati kwamba ukitaka kuwa na Muungano imara (soma Tanganyika imara), basi lazima uwe na Zanzibar dhaifu. Kinyume chake ni kuwa unapokuwa na Zanzibar imara, basi ujikubalishe kuwa na Tanganyika (Muungano) dhaifu. Huu ni ukweli mchungu, lakini ndio uhalisia ulivyo.

Na wala hili jambo halijaanza leo kwenye la uwanachama wa CAF tu. Limekuwa hivyo ndani ya hii inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na limekuwa hivyo pia nje yake. Chimbuko lake lilianzia hata mwezi mmoja haujatimia tangu kuwekwa saini kwa Makubaliano ya Muungano, pale Mwalimu Julius Nyerere alipoanza kuipopotowa Zanzibar nguvu zake kwa kutunga sheria ya kuzibatiza jina la Muungano shughuli zote za Tanganyika ambazo hazikuwa katika yale Mambo 11 ya Muungano, tunayoambiwa walikubaliana na Mzee Abeid Karume.

Kati ya sheria hizi ni ile iliyoitwa The Transitional Provision Decree (N0. 1) ya mwaka 1964, ambayo iliwapa uhamisho wafanyakazi wote wa serikali ya Tangayika na kuwa wa serikali ya Muungano. Kwa sheria hii, iliyochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la tarehe 1 Mei 1964, ndipo taasisi kama vile Mahkama Kuu ya Tanganyika zilipogeuka kuwa Mahkama Kuu ya Tanzania.

Kisha wiki mbili tu baada ya hapo, yaani tarehe 15 Mei 1964, akachapisha sheria nyengine iliyoitwa The Transitional Provision Decree (No. 2) iliyoelekeza kuwa “kila pale penye neno au kumbukumbu inayosomeka Tanganyika sasa pasomeke Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”

Kwa hivyo, hata lile agizo lililokuwemo katika Katiba ya Muda kwamba “Tanganyika and Zanzibar are one United Sovereign State” baadaye likaja kubadilika na sasa ikawa “Tanzania is one State and is a Sovereign United Republic”, ambayo ndiyo iliyomo hadi sasa, na ndiyo inayotumika kuifanya Zanzibar isiwe na chake mbele ya jumuiya za kimataifa, hata kama ushirikiano wa kimataifa si jambo la Muungano.

Kwa kutumia mwanya huu, kila kitu cha Zanzibar kinakuwa kimsingi na kiutekezaji ni cha Tanganyika kwa jina la Muungano, hata kama kijuujuu kitasemwa na kuoneshwa kinyume chake. Vyote na chochote cha Zanzibar si chake.

Ndio maana ukaona, kwa mfano, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaunda wizara zake, kisha anachanganya mambo yasiyokuwa ya Muungano na ya Muungano kwenye wizara moja, kama hilo la Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Masuala ya Afrika Mashariki, ambamo ndani yake ni Mambo ya Nje tu lililo la Muungano. Ndivyo pia ilivyo pia kwa Wizara ya Mambo ya Muungano na Mazingira, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, na kadhaa wa kadha.

Anaweza pia kuunda wizara isiyohusiana kabisa na Mambo ya Muungano na ambayo, kwa hivyo kimsingi inakuwa ya Tanzania Bara tu, lakini akamteuwa Mzanzibari kuwa waziri, kama vile Dk. Hussein Mwinyi alivyowahi kuwa waziri wa afya na sasa Profesa Makame Mbarawa alivyo waziri wa ujenzi.

Kizungumkuti hiki hakifanywi kwa bahati mbaya. Kipo kwa makusudi, maana kwa jicho la ndani la Dodoma ni kwamba kuna nchi moja tu, kuna serikali moja tu na kuna chama kimoja tu. Hii ndiyo falsafa ya mwasisi wa huo unaoitwa Muungano wenyewe, Mwalimu Nyerere, na ambayo inatekelezwa kivitendo na wafuasi wake, miongoni mwa Watanganyika na miongoni mwa Wazanzibari pia.

Kwa hivyo, kwenye hili la CAF, tulipojikwaa sisi Wazanzibari tunaotaka kuiona nchi yetu ikisimama kwa miguu yake yenyewe kwenye mambo yake yote yasiyokuwa ya Muungano, sio kwenye kiherehere chetu cha kujipeleka CAF kabla ya kutoka FIFA, kama inavyojieleza barua ya kufukuzwa kwetu, bali ni kwenye kutokulimaliza kwanza lililosababisha kila chetu kikawa si chetu wenyewe – kutolimaliza la siasa za Muungano kuelekea nchi yetu.

Kama kweli tunataka kuiona Zanzibar ikiwa mwanachama wa jumuiya yoyote ya kimataifa, kama kweli tunataka kuiona Zanzibar ikisimama kwenye mambo yake yote yasiyo ya Muungano, tunapaswa kwanza kukimaliza kizungumkuti kilichomo kwenye Muungano wenyewe. Je, tuko tayari?


Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: CAF, FIFA, mpira wa miguu, soka, Tanzania, Zanzibar

Kinachowafanya Uamsho waendelee kusota rumande

$
0
0

Serikali zote duniani zinakuwa na nguvu nyingi, ukiacha vyombo vya dola ambavyo siku zote husimama imara vikiwa upande wao, hata ikitokea serekali inaboronga basi wao huendelea tu kusimama nayo.

Ni mara chache sana vyombo vya dola kuwa kinyume na serekali, inatokea lakini ni baada ya mure mrefu wa kuwa bega kwa bega na serekali, hata ikitokea wakiasi basi ni kutokana na maslahi yao zaidi na wala si maslahi ya raia.

Nguvu nyegine kubwa ambayo serekali nyingi wanakuwa nazo, ambayo ndio mzizi wa makala hii, ni hili suala la matumizi ya sheria, wakati mwengine sheria hutoa nguvu kwa serekali.

Ndio maana hutungwa baadhi ya sheria zikitoa nguvu nyingi kwao, hili tumelishudia tangu enzi za ukoloni, pale wakoloni walipokuwa wanatunga sheria zilizowapa wao nguvu.

Sheria ambazo hutungwa makusudi kutoa nguvu kwa serekali na sheria ambazo hazijatungwa makusudi hivyo, kuna wakati hizi zote hutumika kwa ajili ya maslahi ya kiserekali, inapobidi kufanya hiyo. Wakati huo zaidi inakuwa ni maslahi wala sio upatikanaji wa haki.

Na Rashid Abdallah

Wakati vuguvugu la Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI), almaarufu Uamsho, linaanza takriban miaka mitano au sita iliyopita, lilianza kidogo kidogo kisha likakuwa kwa nguvu zilizochangiwa na wafuasi wao kuwaelewa vizuri mno, nguvu zikaanza kuhofiwa na watawala wetu.

Sio kitisho tu cha uimara wa Muungano walichokiweka, pia uimara wa kukubalika serekali zetu hasa upande wa Zanzibar nao ukaanza kutikisika, Uamsho sasa wakaonekana ni watoto wanaochezea ndevu za mzee.

Nguvu za kukusanya watu kutoka pembe zote za visiwa na kujaza wafuasi katika mikutano yao, wakieleza kinaga ubaga hatima ya Zanzibar hasa katika muktadha wa muungano, zilizidi kuihenyesha Serekali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na hasa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Nitakueleza sababu. CCM na viongozi wa kiserekali ndio ambao walikuwa wanapingana na Uamsho wazi wazi, hadi hapo Chama cha Wanachi (CUF) kilikuwa hakijawah kutoa tamko rasmi ikiwa wanapingana na Umasho au wanawaunga mkono, kwahiyo kwao haikuwa tatizo.

Tatizo likawa kwa CCM/SMZ ambao walikuwa wanapingana na watu ambao wameshabeba rundo la wafuasi. Na kuifanya CCM hadi kuanza kupoteza wafuasi. Ndipo hapa sasa ilipotafutwa mbinu ya kuwanyamazisha Uamsho.

Kwa vifungu vyao walivyovitumia, wakaamua kuwapachika kesi ya Ugaidi na kesi nyengine kadhaa, kisha bado wakaona kuwaacha Unguja wataendelea kuleta hatari, ndipo walipowahamishia Dar es Salaam kwa siri na ulinzi usio wa kitoto. Kwa sasa wamekuwa na kesi isiyokwisha, nenda rudi na ushahidi uliokosa kukamilika hadi sasa.

Hofu zote watawala wa CCM waliokuwa nazo, zaidi ilikuwa ni ule uchaguzi ambao tuliuwelekea, waliamini kuwaacha Uamsho nje wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi, wangekuwa ni kikwazo kibuwa kwa mafaniko yao.

Na huo ndio ukweli, Uamsho walikuwa tayari wameshaingia katika damu za Wazanizibar, wengi wa Wazanzibar wanamini Uamsho ndio waliowafumbua macho na kuona upi hasa ni muelekeo wa nchi yao.

Kufunguka macho huku kwa raia kukawa ni tatizo kwa uongozi wa muda mrefu wa CCM, sheria ndio zikatumika kama silaha kuwafumba midomo nyuma ya nondo za vyuma katika magereza ya Tanzania bara.

Uamsho hawakuwa wanavunja sheria, walikuwa wanatumia haki yao kikatiba kukusanyika na kujadili masuala ya nchi yao na kutoa maoni yao juu ya Muuungano.

Uchaguzi ulipoisha mategemeo makubwa Uamsho wangetoka na kuwa huru, kwa sababu lile daraja la hofu CCM walilokuwa wanaliogopa tayari liikuwa tumeshavuuka.

Swali ni kwanini bado Umsho wanasota ndani wakati uchaguzi umeisha? Jawabu ni moja kubwa, siasa za Zanzibar ambazo bado hazijatulizana zinaendelea kuwapa hofu watawala na hivyo azimio lao la kuwaacha Uamsho baada ya uchaguzi linaendelea kukwama.

Ukweli ulio wazi, ingekuwa hali ya kisiasa Zanzibar imeshatulizana hakuna tena mikwaruzano, ni wazi wangeachiwa huru, kwa sababu kilichowafanya wawekwe ndani tayari kilishapita.

Hizi ndio zile nguvu za kisheria serekali nyingi duniani wanakuwa nazo, huzitumia sheria kwa maslahi yao ya kisiasa, kwa sababu kuwakamata watu na kuwaweka tu ndani duinia isingewaelewa hata kidogo.

Lakini ili dunia iwaelewe ni lazima utafute kesi ya kuwapachika, iliyo nzito inayotishia amani kisha ndio sasa uwashike mmoja mmoja uwanyime dhamana kwa kutumia hiyo hiyo sheria, halafu uwatoe kila mwezi mara moja au mbili kwenda mahakamani.

Wakifika huko, ushahidi wa kesi unaendelea kutokukamilika, hii huchukua muda hadi pale lengo lao la kuwaweka ndani litapo malizika, dunia haitopiga kelele kwa hali kama hii.

Kwa sababu inaona kuwa wanayo kesi ya kujibu, wamekamatwana kuwekwa dani na mahakamani wanapelekwa kila siku, hata watetezi wetu wa haki za binaadamu ndio unawakuta wamekaa kimya.

Kwa sababu wamefungwa midomo kikanuni, kila kitu kinakwenda kikiwa juu ya mstari, kimefunikwa makoti ya tuhuma na fulana za sheria lakini kumbe uongo mtupu na usanii usiokwisha.

Hatujui hali ya Zanzibar itatengemaa lini, ikiwa Zanzibar itaendela kutikisika kisiasa watu hawa nao wataendelea kubaki tu ndani, maana kule kwao wanaogopwa wakirudi wataenda kuitikisa hali zadi, na nguvu zao ni kubwa mno.

Miaka minne mumeshika dazeni ya watu mmeshindwa hata mmoja kuthibitisha uhusika wake juu ya mnachokidai! Si usanii ni kitu gani hicho, ni kufanya uhuni tu kwa kutumia sheria.

Kinachobaki sasa anayezungmzia sakata hili, anaanza kutengenezewa mazingira ya kupachikwa kesi ya uhaini. Hakuna upelelezi wowote ila ni maigizo ili kuiridhisha dunia kuwa hawajawashikilia kinyume na sheria.

Lazima niweke wazi jambo moja hapa, mimi sipo kutetea uhalifu wa aina yoyote,hata Uamsho ikiwa kweli wanahusika na hicho serekali wanachokidai, wakiwapata  na hatia bila kuwasingizia wala sina shida.

Lakni kinachoonekana sio hicho, siasa ndio inagubika kwa kiasi kikubwa uhalisia wa kesi hii, masheikh wenywe wanaamini maoni yao juu ya Muungano ndio yamewafikisha pale.

Pia usisahau kuwa viongozi wetu wote hadi huyu wa sasa hula viapo majukwani kuulinda muungano kwa gharama zote, hata kwa wale wanaotoa maoni kisha maoni yao yakaonekana kuwa na nguvu kwa kundi kubwa la watu, hutafsiriwa wanahatarisha muungano.

Ikiwa serekali inataka unyamaze, kukuweka gerezani ndio njia nyepesi na kiungwana kwao, kwani wengine hufutwa na hawaonekani tena, kwasababu baadhi ya serekali  huamini mchakato wa mahakama utakuwa mrefu sana.

TANBIHI: Mwandishi anapatikana kwa simu nambari +255 657 414 889


Filed under: JAMII Tagged: jamhuri ya muungano wa tanzania, Magufuli, Segerea, Tanzania, Uamsho, Zanzibar

Lipumba na ugonjwa wa kutokuwa na uhakika

$
0
0

Ni kitendo kilichowaumiza wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), pale Prof. Ibrahim Lipumba alipotangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwenyekiti wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

Si tu kwa sababu wafuasi hao walishamzowea sana katika harakati zao za kisiasa, bali kilichowaumiza zaidi ni kujiuzulu katika kipindi ambacho moto wa kisiasa ndio ulikuwa unawaka vilivyo.

Kwanza tukubali kuwa haki ya kujiuzulu alikuwa nayo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ingawa haki yake iliumiza watu wengi sana hasa wapenzi, wafuasi, washabiki wa chama hicho.

Kipindi kile Prof. Lipumba alipowakusanya waandishi wa habari kuwaeleza kujiuzulu kwake, sababu aliyoitoa ilifanana na kushuka kwenye gari kwa kuchukizwa na abiria uliyempandisha mwenyewe!

Prof. Lipumba alisema: “Walioipinga rasimu ya katiba ya wananchi ndani ya Bunge maalum la katiba ndio tunaamini wataturahisishia kushinda uchaguzi. Tumeshindwa kuongozwa na maadili.”

Hapa bila ya kutafuna maneno alikuwa anamzungumzia Edward Lowassa (waziri mkuu mstaafu), mara baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumkaribisha mwanasiasa huyo.

Na Rashid Abdallah

Ni wazi kuwa kitendo kile kilikuwa ni unafiki wa kisiasa ambao upinzani ulifanya, walitekeleza ile kanuni ya kutokuwa na adui wa kudumu ila maslahi ya kudumu.

Lowassa ni mwanasiasa aliyegonda vichwa vya habari kwa tuhuma za ufisadi, hata ile “List of Shame” ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliyoitoa mwaka 2007 katika viwanja vya Mwembeyanga, jina la mwanasiasa huyo lilikuwepo katika orodha hiyo.

Kwa  Chadema na viongozi wake lilikuwa si tatizo kumwita Lowassa ni fisadi kabla, aliandikwa sana na kusemwa sana (kama maneno yanatoboa basi angekuwa tenga).  Baada ya kumsema sana, hatimaye wakamkaribisha  kuwa mgombea wao wa uraisi wa Chadema kwa mwanvuli wa Ukawa.

Ingawa Lipumba anakiri kuwa miongoni mwa waliomkaribisha Lowassa,ila katika moja ya mkutano wake na waandishi wa habari alisema: “nami nilishiriki kweli katika kumkaribisha (Lowassa) ndani ya Ukawa, lakini dhamira yangu na nafsi yangu inanisuta”.

Dhamira na nafasi yake inamsuta baada ya kumpandisha katika gari abiria ambaye anaamini kimadili hapaswi kupanda gari ya Ukawa, kisha abiria huyu ndiye akawa dereva wa gari lile.

Yawezekana alimkaribisa mtu ambaye kama angekuwa abiri wa kawaida lisingekuwa tatizo, ila shida ni huyu abiria kushika usukani, yaonekana ndio jambo zaidi liliomuumiza Lipumba, sio ajabu kuwa mahesabu yake ni kuwa usukani ule angeushika yeye.

Baada ya kukutana na waandishi na kutangaza kujiuzulu, kisha Prof. Lipumba akarudi tena, akiamini anayo haki ya kutengua uamuzi wake, pia taratibu za kukamilisha utenguzi hazikukamilika, huku upande mwengine wakiamini hana haki ya kutengua uamuzi wake na taratibu za kumtegua zimekamilika.

Kwa sasa kinachoonekana ni vita kati yake na Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye anajuulika na wengi kuwa ndio Katibu Mkuu wa Chama hicho, vita ambavyo vinaathiri chama kwa kiasi kikubwa.

Kuna jambo moja kubwa naligundua kutoka kwa Prof Lipumba, tangu anamkaribisha Lowasa kisha akajiuzulu, baadae akarudi tena; kumbe ni mtu wa kigeu-geu, mwenye ugonjwa wa kutokuwa na uhakika na ayafanyayo.

Hakuwa na uhakika ikiwa anamkaribisha mtu sahihi katika Ukawa au la, pia hakuwa na uhakika ikiwa uwamuzi wa kujiuzulu ulikuwa sahihi au la. Kwahiyo usishangae endapo atafanya jengine kisha akashidwa kuwa na uhakika ikiwa kalifanya sahihi au la, kwa sababu huu ndio ugonjwa wake.

Ugonjwa wake wa kutokuwa na uhakika ndio unaomfanya  kuwa mchwa wa  kukimeng’enyae chama cha CUF, mmeng’enyo ambao wengi wa wafuasi wanaamini sio wa kheri.

Prof Lipumba angekuwa na uhakika na maamuzi yake, wala tusingekesha kuandaa makala refu za kumsema yeye kila uchao. Labda niulize; Yule Mzee aliyekuwa na uhakika na anayoyafanya yuko wapi kwa sasa?

Namzungumzia Dk Willibrod Slaa, naye alijiuzulu kama Prof Lipumba tena katika majira yale yale ya joto la kisiasa liko juu, hata ukiniuliza kwa sasa anaishi wapi; ukweli sipajui!

Kawa mchache wa kusemwa, katekeleza haki yake ya kujiuzulu, naami kwa sasa anafanya anayoona ni sahihi Zaidi kwake kuliko siasa na anaamini uwamuzi wake ni sahihi na alikuwa na uhakika na aliloliamua.

Hatujamuona kurudi kuwa mchwa wa kuimeng’emya Chadema. Ajabu kwa huyu mwenye ugonjwa wa kutokwa na uhakika na ayafanyayo, amekuwa tatizo kwa chama.

Aliondoka kwa mbwe mbwe mbele ya waandishi wa habari (kama mwanamke amuachae mume kwa shangwe na nderemo), akielekea kuifanyia kazi elimu yake ya uchumi, tena akiahidi kuwa mwanachama tu wa kawaida.

Lakini wapi! Kumbe alipokuwa nje alitamukiwa na mijeledi ya kisiasa, anataka tena sasa.  Uliondoka mwenyewe jamani! Kiherehere hiki cha kuwakosesha watu usingizi cha nini?

Au huku kutokuwa na uhakika na ayafanyao kuna shida ya afya ya akili kuwa mgogoro.  Kwa sababu usimuone mtu kasoma sana, ukaona visumari vya akili  ni madhubuti kila kona! Hapana! Mungu kila mtu humpa uimara na udhaifu katika mambo.

Kwani nani aliyetarajia bilionea ambaye bado anafanya biashara ili awe chizi wa pesa, angetiliwa shaka juu ya afya ya akili yake? Kwa sasa tatifi na wataalamu wengi wa afya ya akili, wamejitokeza kuonyesha wasi wasi wao na afya ya akili ya Rais Donald Trump. Hakuna mtu alitegemea!

Ukweli ni kuwa, hutokosea ukimtuhumu Lipumba kuwa na nia mbaya na CUF, wakati aliojiuzulu ulikuwa ni wakati mbaya na namna alivyorudi kwa mabavu hakuleti picha nzuri, kuna kila namna ya kumfikiria kuwa hana nia njema.

Magdalena Sakaya, katika kinachoonekana ni jibu kwa Maalim Seif, anasema tatizo la msingi mpaka mgogoro wa CUF umeendelea  kuwepo, ni kugoma kwa Katibu Mkuu kukaa kitako na Lipumba na kutomtambua.

Anayoyasema Sakaya upo uwezekano mkubwa kuwa ya kweli, lakini Maalim Seif hawezi kuwa mzizi wa tatizo hili la sasa. Unaanzaje kumuamini mtu aliyekiacha chama wakati mbaya kisha anarudi wakati siasa zimetulia?

Hutokosea ukimtuhumu kuwa hata huko mbele, kama chama kikipitia wakati mwengine mgumu anaweza kukiacha tena, kisha akakisubiri tena mbeleni ili akidandie.

Ikiwa kukaa na Maalim Seif ni jambo la msingi kwa nini Lipumba hakuona jambo la msingi kukubali kuibebea nyadhifa yake hadi uchaguzi upite?

Aliombwa, tena na waliomzidi hadi umri abaki kwenye nafasi yake hadi  uchaguzi utapoisha, lakini akagoma. Kama kujiuzulu na kukataa nasaha za kubaki, aliona ndio njia sahihi ya kutatua tatizo aliloliona kwanini iwe tatizo kwa wengine kugoma kukaa naye kitako?

Prof Lipumba  anasema Katibu Mkuu anahujumu chama. Labda niulize, yule aliyepo katika chama mchana na usiku na huyu ambaye anakifanya chama kama casino kwa ingia-toka; nani hasa ni mhujumu chama?

Yule anayerudi kwenye chama baada ya kujiuzulu kwa khiari yake, lakini ujio wake umekuwa wa matatizo na shida;  inakuwaje anaacha kujihesabu kuwa  mhujumu  chama?

TANBIHI: Makala hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa katika gazeti la Mwelekeo, tarehe 11 Aprili 2017


Filed under: SIASA Tagged: Lipumba, Maalim Seif Sharif Hamad, Tanzania, Zanzibar

Magufuli anawauzia Watanzania tamaa ya maendeleo kwa gharama ya demokrasia yao

$
0
0

Kwa hakika, Rais John Magufuli anaonekana kuwalazimisha raia wake kufanya naye biashara ya gizani. Yeye awauzie maendeleo, nao wamlipe kwa gharama ya demokrasia angalau hadi mwaka 2020 wakati wa kampeni za uchaguzi mwengine.

Lakini je, biashara hii inawezekana kwa taifa ambalo lilishaonja ladha ya demokrasia kwa robo karne nzima mtawaliya? Je, ili kupata maendeleo ni lazima kuitia rehani misingi ya kikatiba, mgawanyo wa madaraka, haki za binaadamu na uhuru wa mtu binafsi?

Akizungumzia dhana ya demokrasia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anasema: “Demokrasia haihusiani pekee na ile siku moja kila baada ya miaka minne au mitano pale panapoitishwa chaguzi, bali inahusiana na mfumo wa serikali unaohishimu mgawanyo wa madaraka, uhuru wa mawazo, wa kidini, wa kujieleza, wa kujiunga na kujikusanya na pia utawala wa sharia. Utawala wowote unaokanyaga misingi hii, hupoteza uhalali wake wa kidemokrasia, hata kama awali uliingia madarakani kwa kushinda uchaguzi.” (Tafsiri ni yangu).

Dk. Chris Sausman, Mkurugenzi wa Chime Communications Group, anayatafsiri maendeleo kwa umbo la pembe tatu. “Kwanza ni mchakato ambao ndani yake muna mkururo wa hatua zinazopelekea – au zinazotegemewa kupelekea – matokeo ya aina fulani makhsusi, pili ni mkakati ndani ya mipango na sera na, tatu, ni matokeo ya mikondo miwili ya kwanza kupitia kiwango cha mtu binafsi – pale anapokuwa na kuutumia uhuru wake, kiwango cha jamii – pale inapoweza kutoka hatua moja ya kimaisha kwenda nyengine na kiwango cha kiuchumi – pale uchumi wa jumla unapoimarika.” (Tafsiri ni yangu).

Na Mohammed Ghassani

Namna dhana hizi mbili za demokrasia na maendeleo zinavyoungana zinatuambia kuwa biashara anayoifanya Rais Magufuli na Watanzania haitakuwa na mwisho mwema, hata kama sasa kunatolewa takwimu za mapambio.

Kama anavyosema Mkuu wa Madhehebu ya Shia Ismaili duniani, Aga Khan, “kimsingi maendeleo na demokrasia vimeungana na kuimarika kwa thamani ya maisha ya binaadamu. Uwezo wa kuifahamu (na kuihishimu) mifumo ya kikatiba, uwepo wa vyombo vya habari huru na vyenye kujumuisha wote, asasi imara za kijamii na dhamira ya kweli katika kuelekea utangamano na majadiliano ya kijamii. Hii ndiyo misingi mikuu ya kufikia lengo la maisha bora. Demokrasia inaweza tu kudumu kama inaonesha, muda wote na mwahala mote, kwamba ni njia bora kabisa ya kufikia lengo hilo.” (Tafsiri ni yangu).

Tanzania inapitia kwenye moja ya vipindi vigumu sana vya historia yake ya hivi karibuni. Baada ya kujaribu kuujenga mfumo wa kidemokrasia kwa miongo miwili na nusu, sasa jitihada hizo zinarudi nyuma kwa kasi ya ajabu.

Misingi mikuu ya demokrasia inashambuliwa kila uchao na serikali ya Rais Magufuli, akiamini kuwa ana uhalali wa kufanya lolote atakalo kwa kuwa tu madaraka ya juu yamo mikononi mwake.

Hata miaka miwili haijatimia vyema tangu ale kiapo cha utiifu kwa Katiba, Rais Magufuli ameshathibitisha kuwa yeye si muumini wa misingi mikuu ya Katiba yenyewe, kama vile mgawanyo wa madaraka na hishima kwa uhuru na haki za binaadamu.

Kwa mfano, mara kadhaa muhimili wa utawala kupitia kwake na wateule wake, umekuwa ukiingilia muhimili wa bunge kuwafunga midomo wabunge, kuzima mijadala yenye maslahi kwa taifa na hata kuzuwia matangazo ya bunge hilo kuoneshwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa, ambayo inaendeshwa kwa kodi ya wananchi.

Wakati akizuwia matangazo hayo kwa kisingizio cha gharama na kubana matumizi ya serikali na pia kuwapa muda wananchi kufanya kazi, shughuli za kisiasa zake na za chama chake, CCM, hupewa nafasi ya kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya umma, vinavyolipiwa kwa fedha ya umma na katika wakati wa kazi.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, wabunge kadhaa wameshakamatwa, kupigwa, kuwekwa vizuizini na hata kufungwa jela, na katika baadhi ya mifano wakiwa ama bungeni au majimboni mwao katika shughuli zinazohusiana na nyadhifa na madaraka yao kama wabunge na au viongozi wa vyama vyao.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, Rais Magufuli ameshatoa kauli kadhaa zinazoingilia moja kwa moja uhuru wa mahakama na vyombo vyengine vinavyohusiana moja kwa moja na upatikanaji haki kama vile ofisi ya mwendesha mashitaka, polisi na idara za upelelezi, kwa kuwatia hatiani hadharani wale wote anaowashuku.

Matokeo yake, kwa kuwa tuna aina ya Katiba inayompa mkuu wa nchi nafasi ya uungu mtu, walio chini yake kwenye vyombo hivyo wanajipendekeza kuigeuza kila “kauli ya rais” kuwa ukweli, hata kama kwa kufanya hivyo wanazikanyaga sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea wenyewe kama taifa.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, Tanzania imejikuta ikirejea kwenye zama za giza – ikitajwa kuwa na matukio ya utekaji nyara, upoteaji watu, ukamatwaji ovyo ovyo unaofanywa na vyombo vya dola, na hata mauaji dhidi ya raia na pia dhidi ya askari wetu, ambao wana jukumu la kuwalinda raia hao.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, kesi kadhaa zimefunguliwa na serikali yake dhidi ya wananchi wa kawaida wanaotumia mitandao ya kijamii kuelezea maoni na mawazo yao kuhusiana na mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya nchi. Sambamba na hilo, magazeti kadhaa yamefungiwa na vyombo vya habari vimevamiwa na waandishi wa habari kushambuliwa, kupigwa na hata kuwekwa ndani, wakati wakiwa kwenye majukumu yao ya kukusanya na kusambaza habari.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, Rais Magufuli ameirejesha Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja kwa kuzuwia shughuli zozote za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na hata ya ndani, sikwambii maandamano na midahalo ya kitaifa hadi mwaka 2020, kwa kile anachodai ni kumpatia muda wa kutekeleza ilani ya chama chake aliyoinadi kwenye kampeni za uchaguzi wa 2015.

Mara kadhaa, polisi yake imewatia nguvuni viongozi wa upinzani wakiwa kwenye shughuli zao za kisiasa, ingawa haifanyi hivyo kwa viongozi wa CCM wakiwa kwenye shughuli kama hizo.

Tumeshuhudia kiwango kikubwa kabisa cha kukosewa hishima taratibu za kinchi kwenye teuzi, utenguwaji, utendaji na hivyo uwajibikaji wa watumishi wa sekta ya umma. Kila mmoja, kutoka raia wa chini kabisa hadi afisa wa juu serikalini, anaishi kwenye khofu ya kulengwa na kuandamwa si kwa sababu ya makosa anayoyatenda, lakini kwa sababu ya ‘hisia’ za mtawala mkuu wa nchi, ambazo nazo hutokana na taarifa zisizo sahihi anazofikishiwa na wale alioamua pekee kuwaamini na kuwakubali ‘ukweli’ wao.

Kila mtu na kila taasisi ambayo ni tishio kwa ‘ukweli wa hisia’ za mtawala, basi haiko salama. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo viliisababisha kwa mara ya kwanza CCM kushindwa kupata asilimia 60 ya kura za urais ndani ya miaka 25 vinanyanyaswa kusudi na vyombo vya dola.

Chama cha Wananchi (CUF) ni mmoja wa wahanga wakubwa wa kipindi hiki kifupi cha utawala wa Rais Magufuli, kwa kuwa kinaonekana kukataa kuwa sehemu ya ‘ukweli wake wa hisia’ kwamba rais pekee ndiye anayemiliki maoni, mawazo, na njia sahihi kwa kila kinachojiri, likiwemo suala tete la ‘uhuni’ uliofanywa na CCM na vyombo vya dola dhidi ya maamuzi sahihi ya wananchi wa Zanzibar ya tarehe 25 Oktoba 2015.

Kwa ufupi, ndani ya utawala huu wa awamu ya tano, misingi ya kidemokrasia, kama ilivyotajwa hapo juu na Kofi Annan, inakanyagwa na utawala wa Rais Magufuli. Yote kwa jina la kumpa yeye nafasi ya kuleta maendeleo aliyoyaahidi kwa wananchi.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 24 Julai 2017.

 


Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: demokrasia, haki za binaadamu, jamhuri ya muungano wa tanzania, John Magufuli, maendeleo
Viewing all 854 articles
Browse latest View live