Muda mchache baada ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Naibu Waziri wa Fedha, Aishatu Kijaji, kutoa ufafanuzi wa shilingi trilioni 1.5 ambazo Mkaguzi Mkuu, CAG Juma Assad, alisema hazionekani kwenye mahisabu ya serikali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, ameuokosoa utetezi huo akisema hauna tafauti na ule uliotolewa na Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, hivi karibuni.
Kwenye waraka uliosambazwa katika mitandao ya kijamii hivi leo, Mtatiro amesema “ni aibu kubwa kwa wizara kukopi propaganda za msemaji wa CCM na kuzitumia kufafanua mambo makubwa ya nchi ambayo yana taratibu na taasisi zake”, huku akiituhumu taarifa hiyo ya wizara ya fedha kuwa “haina jambo jipya.”
Akitoa mgawanyo wa fedha hizo, Naibu Waziri Kijaji ameliambia bunge mjini Dodoma kwamba shilingi bilioni 697 zilikuwa ni matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva, shilingi bilioni 687 ni za mapato tarajiwa na ambapo shilingi bilioni 203 zilizobakia ni mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa ajili na kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Hata hivyo, akijibu utetezi huu, Mtatiro ameshangazwa na serikali kuja na majibu haya leo baada ya msemaji wa CCM kuyasema hayo hayo, ilhali “hata CAG alivyowapa muda wa kumpa nyaraka na ushahidi juu ya kutoonekana (nafasi ya mwisho kwa mujibu wa taratibu za ukaguzi) bado walishindwa kumpa maelezo haya.”
Soma waraka kamili wa CUF hapa chini:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI – ( THE CIVIC UNITED FRONT)
Nimeisoma taarifa ya Wizara ya Fedha (yenye kurasa tatu – nimeziambatanisha hapa) juu ya kile wanachokiita “KAULI YA SERIKALI JUU YA TUHUMA ZA UPOTEVU WA SHILINGI TRILIONI 1.5” (Maneno yangu). Taarifa hiyo ya Wizara ya Fedha ambayo pia imesomwa bungeni ni Propaganda na uongo mkubwa.
Kwanza, Wizara imekopi na kupesti yaleyale yaliyosemwa na Ndugu. Humphrey Polepole ambaye ufafanuzi wa kipropaganda alioutoa tumeukosoa vikali kwa ushahidi. i aibu kubwa kwa wizara kukopi propaganda za msemaji wa CCM na kuzitumia kufafanua mambo makubwa ya nchi ambayo yana taratibu na taasisi zake. Kwa hiyo taarifa hii ya wizara haina jambo jipya.
Pili, CAG alipofanya ukaguzi na kuukamilisha na akaibua hoja hizo za ukosekanaji wa fedha hizo (Trilioni 1.5), serikali hii hii ilishindwa kumpa ufafanuzi huu inaoutoa leo baada ya jambo hili kuwa hadharani.
Tatu, hata CAG alivyowapa muda wa kumpa nyaraka na ushahidi juu ya kutoonekana (nafasi ya mwisho kwa mujibu wa taratibu za ukaguzi) bado walishindwa kumpa maelezo haya. Nalisema hili kwa sababu “in STANDARD PROCEDURES, CAG hutoa nafasi kwa mkaguliwa ku-clear doubts zote muhimu.”
Nne, hata kwenye Exit Meetings (Vikao vya Kuhitimisha Ukaguzi) kati ya Serikali na CAG, Serikali ilishindwa bado kutoa ufafanuzi kuwa fedha hizo ziko wapi na zimetumikaje! Vikao hivi hutumiwa na mkaguliwa kurekebisha jambo lolote ambalo alikuwa hajalikamilisha.
Tano, Ufafanuzi huu wa Wizara ya Fedha, sawasawa na ule wa Humphrey ni ushahidi tosha ya kwamba SERIKALI ilijua ikimpa ufafanuzi huu CAG wakati wa ukaguzi, ingeshikwa UONGO na kwa hiyo serikali haikutaka kabisa CAG akague matumizi ya fedha hizi (1.5 Trilioni).
MAPENDEKEZO YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF)
1. Kwa hatua ya sasa, kwa sababu CAG alishamaliza kazi yake na hakupewa ushirikiano wowote na serikali (serikali ikimficha kila kitu kuhusu fedha hizi), ni lazima sasa Bunge liunde Kamati Maalum ili ichunguze fedha hizo zilikwenda wapi?
2. Ikiwa CCM na SERIKALI wanatoa maelezo (baada ya ukaguzi kupita) ya kwamba hizo fedha hazijapotea, bunge lifanye kazi yake, Spika aunde Kamati Maalum kama nilivyosema hapo juu au aruhusu Kamati za PAC na LAAC zikasimiwe jukumu la kufanya uchunguzi maalum wa fedha hizi.
3. Ikiwa Bunge (ambalo Majority ni CCM) na Spika – watakataa kuunda kamati au kuzikasimu PAC na LAAC mamlaka ya kufanya uchunguzi huru, watanzania tujue tumeibiwa, tumeibiwa Shilingi 1.5 Trilioni.
4. Taarifa ya leo ya serikali (sawa na ile ya Msemaji wa CCM) zinamaanisha kuwa serikali imetumia pesa, serikali imemkwepa CAG asikague pesa hizo, na sasa serikali inatutangazia matumizi na ukaguzi wake (imetumia, imejikagua na inatangaza ukaguzi wake). Huu upuuzi haukubaliki hata kidogo.
5. Nawasihi sana watanzania wasi-underestimate masuala haya. Nchi hii ni yetu sote, na mamlaka yetu ya kutaka serikali ichunguzwe na bunge kuhusu jambo fulani si mamlaka tuliyohisaniwa, ni mamlaka tuliyozaliwa nayo kama watanzania. Bunge ndiye mwakilishi wetu, afanye kazi yake.
Kamati ya Bunge itakayoundwa kuchunguza fedha hizi, ikikuta zilitumiwa sawasawa, itueleze! Bunge likikataa kuunda kamati, tumeibiwa! Tuiwajibishe serikali!
#Julius Mtatiro
#Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
#The CIVIC UNITED FRONT (CUF),
#20 Aprili 2018.