Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, CUF, kimeungana na wabunge wanaoiwakilisha Zanzibar kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kambi ya upinzani, ambao juzi walitoka nje ya ukumbi wa Bunge hilo mjini Dodoma kupinga hatua ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kuzuia kuzungumzwa masuala ya Muungano.
Mnadhimu wa Kambi ya CUF Bungeni na Mbunge wa Malindi, Ally Saleh, aliwaongoza wenzake kususia kwa muda shughuli za Bunge kuonesha kukerwa kwao na kile walichokiita udhalilishaji dhidi ya hadhi, heshima na maslahi ya Zanzibar kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.
Kwenye waraka wa leo wa CUF uliosambazwa kwa waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Bimani, amesema kwa wabunge wa Zanzibar kuujadili Muungano ndilo jukumu la kimsingi walilotumwa na wapigakura wao.
Soma waraka kamili hapa chini:
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF –Chama Cha Wananchi)
THE DIRECTORATE OF INFORMATION, PUBLICITY AND PUBLIC RELATION
P.O. BOX 3637 Zanzibar, Tanzania
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
Imetolewa leo Tarehe 12/4/2018
MUUNDO WA SERIKALI YA ZANZIBAR YENYE MAMLAKA KAMILI KITAIFA NA KIMATAIFA NDIO SULUHISHO LA MATATIZO YA MUUNGANO TULIONAO SASA BAINA YA TANZANIA BARA (TANGANYIKA) NA ZANZIBAR:
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) Inaungana na Wananchi wote kuwapongeza Wabunge wa Zanzibar ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali itikadi ya Vyama vyao wakiongozwa na Wabunge wa CUF kususia mjadala wa Bunge kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu kutokana na kuzuiliwa na kiti cha Spika wa Bunge (Mwenyekiti wa Bunge) kujadili masuala yanayohusu Muungano.
CUF inampongeza Mheshimiwa Ally Saleh (Mbunge – CUF Malindi, Zanzibar) pamoja na wabunge wenzake kuonyesha kwa vitendo kupinga vitendo na kauli za kuidhalilisha Zanzibar ndani ya Bunge kunakofanywa na baadhi ya Wabunge na Viongozi wa CCM.
Jumatatu ya Tarehe 09 April, 2018, Wabunge kutoka Zanzibar, walitoka nje ya Bunge kuonyesha msimamo wa kupinga vikali na kukemea tabia ya kuidharau, kuikejeli Zanzibar na mamlaka yake Kikatiba na kuzuiwa kujadili Masuala yanayohusu Muungano. Tanzania Bara (Tanganyika) na Zanzibar ni nchi zilizoungana April 26 mwaka 1964 zikiwa zenye hadhi sawa mbele ya sheria.
Zuio hilo la kutojadiliwa kwa Muungano lilitokana na muongozo ulioombwa wa kutaka kuzuia kujadili masuala ya Muungano kulikofanywa na ndugu Jenista Mhagama Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu wa Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) Kinaamini kuwa Matatizo yanayohusu Muungano wetu yanawezekana kabisa kushughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu pale viongozi watakapokuwa tayari kuonyesha nia na dhamira ya dhati kutaka kuyashughulikia matatizo hayo. Kwa bahati mbaya, Viongozi wa Serikali ya Tanganyika hawana nia na dhamira njema kwa Zanzibar na Wazanzibari na badala yake wanaichukulia Zanzibar kama Koloni lake.
Suala la Muungano si la Chama cha Mapinduzi pekee. Uwepo wa Muungano unapaswa kuwa na ridhaa kutoka kwa wananchi wa pande zote mbili. Kwa kipindi cha takribani miaka 15 sasa CCM imekuwa ikifanya hila na mbinu chafu za kudhorotesha Muungano kwa kuunda zinazoitwa Kamati za Kushughulikia kero na matatizo ya Muungano lakini kamati hizo mara zote zimekosa majibu sahihi na ufumbuzi wa kero hizo. Ni jambo la kusikitisha kuwa, Baadhi ya Wahafidhina (WanaCCM) kutoka Zanzibar waliojawa na ubinafsi na ambao wanajinufaisha binafsi na mfumo huu mbovu wa Muungano wameshindwa kuitetea Zanzibar na udhalilishaji huu unaoendelea ndani ya Bunge na nje ya Bunge.
CUF inaamini kuwa Njia Mujarabu wa Kuipatia ufumbuzi dhoruba hii ya Matatizo yanayohusu Muungano wetu ni kuwa na MUUNDO WA SERIKALI YA ZANZIBAR YENYE MAMLAKA KAMILI KITAIFA NA KIMATAIFA. Aidha, Watanzania na Wazanzibari kwa ujumla wake walishatoa maoni na mapendkezo yao mbele ya Tume ya kuratibu maoni ya mabadiliko ya Katiba (Tume ya Warioba) ambapo pamoja na uchakachuaji uliofanywa Tume hiyo ilikuja na RASIMU YA KATIBA YENYE MAPENDEKEZO YA UWEPO WA MUUNDO WA SERIKALI TATU. Mapendekezo ya Rasimu hii yakitekelezwa yanaweza kuwa sehemu muhimu ya kuanzia safari ya kuelekea kupata uzoefu thabiti wa kuona namna ya kushughulikia na kupatiwa kwa ufumbuzi wa kudumu wa KERO NA MATATIZO YAHUSUYO MUUNGANO WETU.
Lazima ifahamike kwamba, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Muungano uliotokana na nchi mbili zilizokuwa huru kila moja ikiwa na mamlaka kamili. Nchi hizo ni Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa Tanganyika kwa makubaliano makhsusi yaliyowekwa katika Hati ya Makubaliano ya Muungano (Articles of Union). Hatukuungana ili Tanganyika iwe mtawala na Zanzibar iwe mtawaliwa. Lazima tuwe na Muungano wenye maslahi mapana, faida na manufaa kwa pande zote mbili za Muungano.
Tabia ya Serikali ya Muungano kila wakati kutaka kuzima mjadala juu ya Masuala yanayohusu Muungano hayaleti afya njema ya ustawi wa Muungano wetu. Bungeni ndipo mahala stahiki pakujadiliwa Mapungufu na kero mbalimbali za Muungano. Kauli za kuidhalilisha, kuidogosha Zanzibar kwa namna yeyote ile HAZIKUBALIKI. Zanzibar ni nchi yenye Taasisi za kiserikali zenye mamlaka kisheria.
KWA MUKTADHA HUU; CHAMA CHA CUF kinatoa wito kwa Serikali ya awamu ya Tano kuurejesha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na wadau mbalimbali hapa nchini na kuzingatia maoni ya Wananchi kama yalivyowasilishwa na TUME YA WARIOBA.
Lengo na madhumuni ya Chama cha CUF kwa mujibu wa Katiba yake Ibara ya 7(10) inaeleza kuwa ni;
“…kudumisha uhuru wa Taifa, amani ya nchi, na UDUGU WA ASILI WA WATANZANIA uliokwisha shamiri pamoja na kuleta maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii nchini kote.”
HAKI SAWA KWA WOTE
……………………..
SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0777 414 112/ 0752 325 227