Katika hali isiyokuwa ya kawaida na inayoashiria kiwango kikubwa cha kuchoshwa na mateso dhidi yao, wazee kisiwani Pemba wamelipa Jeshi la Polisi masaa 24 kutoka sasa kuhakikisha vijana watatu waliokatwa majumbani mwao huko Mtambwe, kaskazini mwa kisiwa cha Pemba, wawe wameshapatikana wakiwa salama.
Wakizungumza baada ya kutoka makao makuu ya polisi ya mikoa yote miwili ya Pemba magharibi ya leo (Aprili 10), wazee hao wamesema wamelitaka jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake bila kumuogopa wala kumuonea haya mtu, kama ambavyo kila siku limekuwa likidai kufanya “na kuwarejesha watoto wetu!”
Vijana ambao hadi sasa hawajapatikana baada ya kuchukuliwa na watu wanaoaminika kuwa wa vyombo vya usalama usiku wa kuamkia Ijumaa (5 Aprili), ni Thuwein Nassor, Khamis Abdallah na Khalid Khamis.
Wenzao watatu waliochukuliwa pamoja wakiwa na umri wa baina ya miaka 16 na 19 walipatikana siku ya tatu yake wakiwa wametupwa mbali sana na kwao. Walikutikana kwenye kijiji cha Ngwachani, mkoa wa Kusini Pemba wakiwa wamefungwa kamba mikononi na hali zao zikiwa dhaifu ingawa hawakuwa na majeraha mwilini.
“Kama ikifika kesho muda kama huu, watoto wetu hawa waliobakia hawajapatikana, basi tumewaambia polisi kuwa Wapemba wote wataingia kwenye msako kuwatafuta vijana hawa na lolote litakalotokea kwenye msako huo, wao polisi ndio watakaobeba dhamana,” amesema mmoja wa wazee hao.