Tuliona sehemu ya pili, Abdull na Talib walipokimbia Pemba wakaishi katika mji wa Nyali, Mombasa ya Kenya, baadaye maisha hayakuwa mazuri wakaelekea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, huku wakapata rafiki wa Kisomali kwa jina la Ismail ambaye aliwashawishi waende Mogadishu kufanya Biashara. Waliwasili Mogadishu jioni pevu baada ya safari ya siku kadhaa. Endelea..
“Karibuni Somalia, hapa ndio Mogadishu”, alisema Ismail huku wakikatiza mtaa mmoja baada ya mwengine. Walikuwa wanaelekea katika nyumba ya Ismail ambayo aliiyacha miezi mitatu tangu aondoke Mogadishu.
Athari ya vita ilikuwa inaonekana kila wapitapo, ingawa kundi la Alshabab lilikuwa bado halijaudhibiti mji huo moja kwa moja, lakini walikuwa wakiushambulia mara kwa mara.
Licha ya mashambulizi hayo lakini mitaa ilijaa watu usiku ule, vyombo vya usafiri vikizunguka huku na kule ingawa vilikuwa vichache mno, watu nao wamefunika mitaa kwa shughuli zao za usiku kabla ya kulala.
Baada ya mwendo wa dakika tano, ndipo walipofika katika nyumba moja ambayo iliashiria kuhamwa kwa muda kidogo. Ndiyo nyumba ya Ismail , ambayo aliikomea na kuiwacha kisha akakimbilia Dadaab.
Ismail hakuwa nayo tena ile familia yake, mke na watoto wake wawili waliuwawa baada ya kutokea shambulio katika moja ya soko la mji wa Mogadishu, ambako mke wake alikuwa anafanya biashara ndogo ndogo.
“Karibuni, hapa ndio nyumbani”, aliwakaribisha baada ya kufungua kufuli iliyokuwa katika reza ya mlango.
Ilikuwa ni nyumba ya kupendeza kwa ndani, ilikosa tu matunzo kwa sababu watunzaji walipoteza maisha wakiwa sokoni.
“Nashukuru Mungu kwamba hawajaiharibu kwa mabomu”, alisema Ismail huku akivua viatu vyake.
Wakati wote huo, Abdull na Talib walikuwa kimya kama kuku wageni walioingizwa katika banda lenye wenyeji wengi. Mioyo yao ilitafakari imekuwaje hadi wameishia kujiingiza katika mji wa kifo.
“Kwahiyo bomu linaweza kulipuka hadi hapa?, aliuliza Abdull.

Swali ambalo lilimfanya Ismail aangue kicheko hasa kutokana na aina ya uulizaji wenyewe. Ismail kabla ya kujibu swali hilo, alimuuliza Abdull ikiwa ameshawahi kuishi katika maeneo ya vita au la. Abdull na hata kaka yake, hakuna ambaye amewahi kuishi katika maeneno ya vita.
“Usiwe na wasi wasi hapa utazoeya tu baada ya siku chache..”, hiyo ndio iliyokuwa jawabu ya mwisho ya Ismail wakati akiwatoa hofu Abdull na Talib.
Baada ya dakika chache aliwaacha sebuleni akiwaeleza kwamba kuna duka la mikate mtaa wa pili ambalo huchelewa kufunga, hivyo alitaka kwenda kununua. Ismail alitoka, nje akisikika akisalimia na mtu ambaye walikuwa hawajaonana muda mrefu kidogo.
Abdull na Talib walikuwa wamekaa katika masofa, Abdull amelaza kichwa chake akiangalia juu ya dari ya sebule ile, Talib akiwa amejiinamia kwa kuweka paji lake la uso juu ya mikono iliyokuwa juu ya magoti .
“Vipi, tunarudi tulikotoka au tunabaki hapa?, aliuliza Abdull
“Ngoja kwanza hadi jua lichomoze ndio tutapata jibu..”.
Baada ya dakika kadhaa Ismail alikuja akiwa na rundo la mikate na vinywaji kadhaa, baada ya kula ulikuwa ni wakati wa kulala. Ingawa walikuwa katika mitaa ya vita lakini usingizi ulikuja nzito sana ,ni kutokana na uchovu wa safari yenyewe.
Asubuhi kulipokucha, mara baada ya kupata chai walikaa kitako ili kuelezana mustakbali wa maisha yao pale. Wakati wakiwa Dadaab Ismail aliwaeleza kwamba alikuwa na biashara ameziacha nchini Somalia, lakini asubuhi aliamua kuwaweka wazi kwamba uvuvi ndio biashara yenyewe aliyoikusudia.
Talib na Abdull wakabaki wanaangaliana wakiachia midomowazi na kushangazwa na walichokisikia.
Alijaribu kuzishibisha akili zao kwamba, kazi ya uvuvi katika mji wa Mogadishu inalipa sana, kwani uhitaji wa samaki ni mkubwa na wavuvi ni wachache.
Walipouliza kwanini wavuvi ni wachache. Ismail aliwaeleza ni kutokana na maharamia huko baharini , licha ya kwamba wanateka meli kubwa kubwa lakini wakati mwengine huwalenga risasi hata wavuvi wado wadogo kwa madai wanaingilia shughuli zao za utekaji.
“Ukweli kuna mahoteli makubwa yanahitaji samaki kila siku..”
“Hatukatai kwamba kuna uhitaji wa samaki lakini hayo mazingira ya kuvua sio rafiki”, alisema Talib huku Abdull akitikisa kichwa ishara ya kukubaliana naye.
Baada ya mazungumzo marefu, hatimaye walikubaliana kwamba wangefanya kazi ya uvuvi pamoja, licha ya kuzongwa na hatari nyingi.
Ismail aliwaacha Abdull na Talib nyumbani , yeye akaelekea bandarini kwenda kufatilia boti lake la mashine ambalo alikuwa amelihifadhi kwa rafiki yake .
Si Abdull wala Talib ambaye moyo wake uliwafikiana na maisha yale mapya, lakini walikubali kwa shingo upande hawakuwa na namna ya kufanya, hawakuwa na uwezo wa kutoka pale Mogadishu na kurudi Dadaab, wakajikuta wanakubaliana na hali bila mioyo yao kupenda.
Baada ya masaa kadhaa Ismail alirudi akiwa na vifaa vya uvuvi. Baada ya mapumziko ya siku chache, jioni ya siku ya mwisho kabla ya kuingia katika kazi ya uvuvi rasmi. Ismail aliamua kuwatoa na kuwatembeza katika mji wa Mogadishu, akiwapitisha katika masoko na mahoteli ambayo anaamini biashara yao ya kuuza samaki wanaweza kuifanyia huko.
Hali ya amani inapofunika Mogadishu, mji huo hunawiri kwa uzuri wake, mabinti wazuri wa Kisomali wanaokatisha huku na kule wakiwa katika shughuli zao, hufanya mji huo uzidi kupendeza. Mabinti hao hugeuka na kuwa kama njiwa wazuri wanaoupendezesha mji huo.
Uzuri wa mabinti wa Kisomali na rangi zao za mchanganyiko, zilimfanya Abdull akumbuke kwao Pemba, zile shungi na mabaibui hadi chini zilimfanya azame zaidi katika mawazo akidhani anapita katika mji wa Chake Chake na Wete.
Kabla jua kuzama walikuwa wameketi katika fukwe za Sekondo Lido, fukwe maarufu katika mji wa Mogadishu. Walikuwa wanashuhudia uzuri wa jua linavyozama taratibu.
Vijana wa kiume walikuwa wameenea katika fukwe zile wakiogelea, familia za kisomali zilijazana jioni zikifurahia mawimbi na upepo wa bahari ya Hindi, pia wakipoza vidonda vya kupotelewa na wapendwa wao.
Adhana, miito kwa ajili ya swala, zilizokuwa zikiita kutoka kila upande ya mji wa Mogadishu ndizo zilizowainua kutoka katika fukwe . Waliporudi nyumbani Ismail akawakumbusha Talib na Abdull kwamba kesho asubuhi na mapema ndio siku ya mwanzo wataanza kazi ya uvuvi.
Kazi ya uvuvi na biashara ya kuuza samaki ilianza kwa uzuri sana, kile walichokuwa wanaambwa na Ismail walikuwa wanakishuhudia wenyewe, uhitaji wa samaki ulikuwa ni mkubwa sana, biashara ilinawiri na kustawi kama mgomba unaotiliwa maji.
Miezi kadhaa ilikatika wakiendelea na kazi yao vizur tu, siku moja Ismail aliwachukua ndugu wawili na kuwapeleka katika mgawaha, ilikuwa ni jioni, aliwaeleza kwamba kuna jambo muhimu inabidi walielewe.
“Kabla sijaendelea, Abdull una umri gani?, aliuliza Ismail huku akiinua sharubati iliyokuwa katika glasi nyembamba ndefu.
“22 kwa sasa”,
“Sawa, kwa sababu umri wako bado ni mdogo… ningetoa ushauri mwakani uingie chuo”,
“Hilo tutalitafakari… kwanza tueleze hilo lako”, alidakia Talib
“Ukweli ni kwamba mimi nataka kuondoka na hii kazi nitawaachia muedelee”
Wote walishangazwa na kauli hii, lakini yalikuwa ni maamuzi ya Ismail tangu yupo Daadab, kuimarika kwa maisha ya hawa watu wawili kupitia biashara ya kuuza samaki, ndio jambo pekee lililomchelewesa asiende safari aliyokusudia.
Kwa Ismail halikuwa jambo zuri kuwatelekeza katika mji wa Mogadishu bila ya kuwapa msingi wa maisha. Baada ya msingi wa maisha kukamilika, ndipo alipowaaga akigoma kuwaeleza anaelekea wapi.
Abdull na Talib walibaki kupigwa na butwaa, kilichowaumiza kichwa zaidi ni pale waliposhindwa kuelewa anaenda wapi, alikuwa anawaaga kwa kuwaambia kwamba hategemei kurudi kwa miaka ya karibuni hata ikitokezea akirudi basi ni baada ya kipindi kirefu kupita.
Mazungumzo yote yalikuwa yakiendelea katika mgahawa mmoja uliopo karibu tu na bahari ya hindi.
Zilikuwa ni habari za kusikitisha kwa ndugu wawili, walizokuwa wakizipokea kutoka kwa kaka yao, rafiki yao, mwenyeji wao katika mji ule wa Mogadishu. Licha ya biashara yao ya kuuza samaki kunawiri, lakini mioyoni waliamini bado wanahitaji uwepo wa Ismail.
Waliondoka katika mgahawa baada ya chakula, siku ikiwa imeharibika kwao.Asubuhi kulipokucha walikubaliana na maamuzi ya Ismail kwa shingo upande, wakati Ismail akikunja nguo zake hawakuwa na uwezo tena wa kumzuiya.
“Ikitokea siku mnataka kurudi nyumbani kwenu, hii nyumba mtakwenda kuiweka Waqfu ili iwe mali ya Waislamu”, yalikuwa ni maagizo ya mwisho Ismail akayatoa akiwapungia mkono wa kuwaaga.
Aliondoka na kutokemea kusikojuulikana, aligoma hata kusindikizwa, baada ya dakika chache Abdull na Talib walianza maisha wakiwa wawili bila ya Ismail.
Waliendelea na bishara yao kama kawaida, kwa sababu ya kupata kipato cha kuridhisha waliamua kuikuza na kuajiri vijana kadhaa wa Kisomalia, hakuna mtu aliyeelewa kwamba wao hawakuwa Wasomalia.
Changamoto za uvuvi katika bahari ya Somalia zilikuwa zinawakumba mara kwa mara lakini hawakukata tamaa. Mwisho wakawa wavuvi na wafanya biashara wa samaki maarufu katika eneno la lote la Jabjab na maeneo mengine ya Mogadishu.
Mwaka ukakaribia kumaliza tangu waingie Somalia. Talib alifunga ndoa na binti mmoja wa Kisomali, Abdull akaendelea kubaki kuwa barobaro, akisimamia biashara yao kwa kiasi kikubwa.
Lile wazo la Ismail kwamba Abdull aende chuo kusoma, Talib alikubali kulifanyia kazi. Mwaka wa masomo ulipoanza alienda kumpeleka katika Chuo Kikuu cha Simad, kilichopo katika eneo la Jidka Warshadaha, katika mji wa Mogadishu.
Nini kitafuata baada ya Abdull kuingia chuoni? Je, wataelewa Ismail kaenda wapi na kwanini? Sababu ipi hasa iliwakimbiza Pemba? Fartuun ni nan katika maisha ya ndugu hawa wawili? Je, hali ikoje siku Abdull atakapotoka katika dimbwi hili la fikra za maisha yake ya nyumba, na kujikuta yupo Unguja akiwa na kazi ya kutisha mikononi mwake inamsubiri? Tukutane wiki ijayo..