Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Maisha yasiyotathminiwa hayana maana huyaishi

$
0
0

Ulimwenguni kote na katika zama zote jamii inapokuwa chini ya utawala ulioziba masikio na macho na nyoyo, watawala hupenda waachiwe wafanye watakavyo.

Huwa wamejirithisha wenyewe nchi na raia wake. Na kwa hili hawataki muhali, masahihisho, wala mabadiliko.

Anapotokea mtu kuwasahihisha, badala ya kumchukulia kuwa msaidizi, wao humchukulia adui wao nambari moja, na hivyo hujihalalishia kumuadhibu kwa namna yoyote waionayo inafaa.

Si jibu la haki, ingawa ndiyo kawaida ya watawala kumgeuza mkosoaji wao kuwa muhanga wa utamaduni huo mviya wa kutokutaka mawazo tafauti.

Na hiyo ndiyo dhambi ya asili ya watawala wote wa mkono wa chuma – kule kuamini kwao kuwa msaidizi wao ni yule tu anayewaitikia: “Ndiyo Mzee”, na kwamba kila anayewaambia: “ Hapana” ni adui wao.

Dhambi hii ni kubwa na gharama zake ni ghali mno kulipika.

Kuwatawala watu kwa mkono wa chuma kuna matokeo mabaya, lakini hakuvizi khulka ya wanaadamu kupinga walionalo silo.

Na ndio maana, kote ulimwenguni ambako tawala za aina hii zimepata kuweko, upinzani dhidi yake huzidi kukuwa na kukuwa kila kukicha, hata kama kila mbinu ya kuudidimiza hutumika kila saa na kila dakika.

Wakosoaji wa watawala wakizuiliwa njia hii ya kuwakosowa, huzumbuwa njia nyengine. Alimradi kila watawala wakaapo, hawawezi kustaaladhi nafsi zao, maana macho yote ya umma huwakodolea wao na vinywa vyao huhanikiza sauti: “Hivi sivyo, hilo silo!”

Mwangwi wa sauti hizi ni vitu vinavyoudhi sana mbele ya hadhara ya mtawala, lakini si vitu vinavyoweza kuepukika ikiwa mtawala huyo hakubali mwito wa mabadiliko.

Kila mtawala akizidi kuwa muimla, ndipo anapozidi kuzalisha sauti zinazomsuta na macho yanayomkodolea.

Hizi ni sauti na macho ya watu waliojitolea kumuambia mtawala wao makosefu yake na kumuonesha njia.

Lakini, utawala wa mkono wa chuma huambatana na ujigambi na majivuno.

Mtawala hupandwa na kichaa anapoambiwa kuwa ana makosefu fulani na fulani.

Maana, kwa kila hali, huwa kilevi cha madaraka kimeshamlevya na zile andasa zake humdanganya kwamba yeye yu Mr. Perfect – hawezi kuwa na mapungufu yoyote yale.

Basi hapo hucharukwa na kuanza kumuadhibu kila amuhojiye, haidhuru hoja hiyo iwe makini kiasi gani.

Na kila anavyoadhibu, huona bado – na huwa bado kweli! Huadhibu kwa ulimi wake, kwa mikono yake, kwa virungu, kwa jela, hata kwa risasi na kitanzi. Kwa kwa kila kitu.

Na bado wanaompinga huendelea tu. Angalia msuguano baina ya Bi Kirembwe na Mtolewa katika tamthilia ya Kivuli Kinaishi iliyoandikwa na Dk. Said Ahmed Mohammed uone anguko la kishindo la utawala ulioziba milango yake yote ya fahamu.

Dunia imejaa mifano ya visa na mikasa kama hii. Ni juu yetu kufundishika, ikiwa kweli tu watu wa kuzingatia kutokana na maandiko.

Twapaswa kufundishika, maana vyenginevyo tutakuwa miongoni mwa wale waliotajwa “kuwa na macho lakini hawaoni, masikio lakini hawasikii na nyoyo lakini hawafahamu.”

Ubaya ulioje kuwa miongoni mwao!

Mfano mmoja maarufu ulimwenguni ni ule wa Socrates, mmoja kati ya wanaharakati wa kale.

Tunasoma katika vitabu kwamba Socrates aliwaandama watawala wa Athens kwa kutumia mbinu ya udadisi na uchambuzi wa mambo yaliyoonekana ya kawaida tu, lakini muhimu sana kwa maisha ya watu.

Hayo ni kama vile imani juu ya Mungu, uzuri wa matendo, uadilifu, ilimu, maumbile na kadhalika. Mbinu hii iliuvuta umma wa watu, wengi wao wakiwa vijana, ambao walimchukulia kuwa kigezo chao.

Katika Phaedo, kitabu kilichoandikwa na Plato, aliyekuwa mwanafunzi wa Socrates, tunamsikia mwenyewe akijitetea mahkamani: “Wao (watawala) hukereka mno na hili, na si kuwa wanakerwa na udhaifu wao walionao, bali kwa kuwa udhaifu wao umedhihirishwa na kubainika, na basi huishia kunilaumu na kunichukia mimi.”

Khatima ya kukereka huku kwa wakubwa ikawa ni kumtoa muhanga Socrates, ambaye tunaweza kumuita kuwa ni aalimu mkubwa wa wakati wake na mwanaharakati jasiri.

Alishitakiwa kwa makosa mawili. Kwanza ni kusambaza mafundisho ya kumkana Mungu. La pili ni kuwachochea vijana kuipinga serikali yao. Makosa haya mawili yalimuhalalishia adhabu ya kifo.

Naye, licha ya kupewa fursa ya kujitetea ili aisalimishe roho yake na mauti, kwa kuahidi kuwa angeliiwacha kabisa kazi hii, mwanafalsafa huyu alikataa kwa kusema: “Waheshimiwa waungwana, licha ya kuwa mimi ni mtumishi niliyejitolea kwenu, lakini nina jukumu la kuonesha utiifu wa kiwango cha juu zaidi kwa Mungu wangu na sio kwenu nyinyi; na madhali ninaendelea kuvuta upumzi huu na kuendelea kubarikiwa vipawa hivi nilivyonavyo, basi kamwe sitaacha kuifanya kazi hii ya kuufunua ukweli kwa kila mtu nimkutaye…. Na sitaliacha hili, hata kama itabidi nife mara mia moja!”
Maskini, Socrates akafa akiamini kuwa ni bora kuishi siku moja kama mwanaadamu, kuliko kuishi miaka alfu kama dude, maana ‘the unexamined life is not worth living’ – maisha yasiyotathminiwa, hayana thamani kuyaishi.

Maisha yake yalizimwa pale, lakini ukweli ni kuwa ameendelea kutukuzwa hadi leo hii ulimwenguni.

Hiyo ndiyo gharama ya kuwa mwanaharakati, na ndilo lipo la kuwaambia ‘hapana’ watawala wasiopenda kubadilika.

Wala watawala wa aina hii hawahitaji sababu kubwa ili wapate kumvamia raia wake wanayemuhisi kuwa ni hatari kwao.

Vile kuwa tafauti na wao tu, ni sababu inayotosha kabisa kukupambanisha na ghadhabu ya dola.

Kwamba kama unahitaji kuishi salama usalimini chini ya tawala kama hizi, basi ni kukubali kuwa kama vile wakutakavyo wao uwe.

Wanakutaka uitikie wimbo wauimbao, na ucheze ngoma waipigayo. Na katika kufanya hivyo, usioneshe tafauti yoyote ile – hata ile ya kuuimba wimbo huo huo kwa ghuna nzuri zaidi au kunengua kwa minenguo mororo zaidi kuliko wao. Kwao, hilo litahesabika kuwa ni tendo la kiadui.

Dunia imejaa mifano mingi zaidi ya wanaharakati wanaolipia gharama kubwa kwa uwanaharakati wao.

Kuna waolipotea kiajabuajabu. Kuna waliopaswa kuzihama nchi zao. Kuna waliodhalilishwa na kuteswa kwa mateso mabaya mabaya.

Na wote hawa waliteseka kwa kusema kwao: “Hivi sivyo, hili silo!” – kwa kuhojihoji kwao kusikokwisha.

Lakini dunia shimo la sahau. Leo hii, wa wapi wateswa na watesaji? ‘In’da Rabbihim yansiluun! Wameshawasili mbele ya Mola wao, naye ndiye Mbora wa walipaji na Mkali wa kuadhibu!
Basi kupatwa na mazito ni katika kawaida za harakati. Na nadhani wengi wetu, katika sisi watawaliwa, tunalijuwa hilo.

Sote tunajuwa kuwa kuwakosoa wakubwa kuna khatari zake nyingi sana. Tunajuwa kuwa watawala wana nguvu za kila aina na wanaweza kuzitumia nguvu hizo dhidi yetu, pindi wakitaka.

Tunajuwa kuwa wanaweza kutumia nguvu zao kutubambikia mashtaka ya uhalifu au hata uhaini. Wanaweza kuyafanya maisha yetu yawe kitendawili.

Bali wanaweza hata kuwageuza wake zetu kuwa vizuka na wenetu kuwa mayatima. Wanaweza hawa, hakuna linalowashinda, pindi wakiamua.

Lakini kadiri tunavyoyajuwa hayo, ndivyo tunavyozidi kupata ujasiri wa kuzikosoa serikali kandamizi. Kwa maana nyengine ni kuwa kujuwa kwetu huko, hakupunguzi chochote katika dhamira yetu ya kurekebisha hali mbovu iliyopo.

Sisi raia tumeshajifunza na tumeshaielewa. Zilizokuwa hazijajifunza wala kuelewa ni serikali zetu.

Bado hazijajifunza kuwa hakuna utawala wowote ulimwenguni uliodumu katika madaraka yake kwa kutumia mbinu hizi chafu.

Pengine inaziwia vigumu kuamini, lakini ni historia hii hii ndiyo inayotudihirishia kuwa kuinamako ndiko kuinukako, na kuinukako kukainama.

Lini watawala wetu watakuwa tayari kukabiliana na ukweli huu?


Filed under: KALAMU YA GHASSANI

Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles