Usiku wa kuamkia tarehe 10 Septemba 2011, meli ya Mv Spice Islander iliondoka kisiwani Unguja kuelekea Pemba ikiwa imejaza kupita uwezo wake halisi.
Inasemekana kuwa ndani yake mulikuwa na abiria zaidi ya 3,000 badala ya 645 iliotakiwa kisheria. Ilikuwa pia na shehena kubwa ya mizigo.
Majira ya saa saba za usiku ikazama kwenye Mkondo wa Nungwi na hadi sasa, miaka saba baadaye, watu waliopatikana wakiwa hai ni 620 tu, hiyo ikimaanisha kuwa ndani ya usiku huo mmoja tu, Zanzibar ilipoteza roho takribani 2,500.
Kwa taifa lenye raia milioni 1.3, hii ni idadi kubwa kabisa kupotea kwa wakati mmoja, tangu wale waliopotea wakati wa mavamizi ya Januari 1964. Takribani kila familia, hasa kisiwani Pemba, ilikumbwa na msiba huo. Aliyekuwa hakupoteza jamaa yake wa moja kwa moja wa damu, basi alipoteza jamaa wa jamaa yake, na kwa mjengeko wa kijamii na kitamaduni wa Zanzibar ulivyo, kwa hakika huu ulikuwa msiba wa taifa zima.
Ripoti iliyotolewa baadaye na Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo ilithibitisha kuwa hasara hiyo kubwa kwa roho na mali ilisababishwa na uzembe na ukosefu wa uwajibikaji. Hapana shaka, palikuwa na mkufu mrefu wa waliopaswa kuwajibishwa kwa uzembe huu – kuanzia maafisa wa bandari, wamiliki wa meli yenyewe hadi maafisa wa usalama.
Bahati mbaya, hivyo sivyo ilivyokuwa hadi sasa, miaka saba baada ya mkasa wenyewe. Lakini hilo huenda likawa ni dogo sana kuliko upande mwengine wa suala hili. Nalo ni ukweli ni kuwa taifa la Zanzibar limeamua kuzidharau kabisa hisia kali zinazoambatana na msiba huu mkubwa.
Mwaka 2012, mwaka mmoja baada ya tukio lenyewe, nilizungumza na waziri aliyekuwa na dhamana ya usafiri wa baharini kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Rashid Seif, na nilipomuuliza serikali ilikuwa na mpango gani wa kuwawekea kumbukumbu wahanga wa ajali ile, jawabu yake ilikuwa: “Zanzibar ni nchi ya Waislamu na Waislamu huwa hawana kawaida ya kuikuza misiba yao.”
Nilimkumbusha ukweli kuwa Zanzibar ina sanamu ya kumbukumbu ya Abeid Karume na hadi leo sanamu hilo na kaburi lake ni miongoni mwa alama za historia ya nchi, pamoja na pia kuifanya siku yake aliyouawa, tarehe 7 Aprili, kuwa siku ya mapumziko kitaifa.
Msimamo wake, ambao ndio uliokuwa msimamo wa serikali, ulikuwa kwamba hitima zilizosomwa na matanga yaliyowekwa na familia pamoja na siku tatu za maombolezo ya kitaifa zilikidhi haja yote. Hapakuwa na chengine cha kufanya.
Wakati huo nilidhani kuwa jawabu hiyo ingelikuwa ya muda tu, na baadaye hali ingelibadilika. Moyoni mwangu mulikuwa na imani kwamba hatuwezi kupoteza watu wengi kwa wakati mmoja kama wale, kisha tukawasahau milele kama kwamba hakuna kilichotokezea ndani ya nchi.
Huu ni mwaka wa sita sasa na alichokisema Waziri Rashid wakati ule ndicho ambacho kimesimama hadi leo, na imani yangu imeanguka na kuzikwa mchangani. Hii haimaanishi kuwa msimamo huo wa serikali ulikuwa sahihi, wala kwamba wangu ulikuwa sio. Hapana. Bali tuliyaangalia mambo kutoka vipembe tafauti.
Wakati huo, na hadi leo, mimi nilitaka Zanzibar iuchukulie msiba huu kwa uzito mkubwa zaidi, maana haikuwahi kutokezea kabla ya hapo, ajali ya baharini, angani na wala ardhini kuondoka na watu wetu wengi kwa wakati mmoja kama ajali hii.
Ni kweli ajali si jambo la fahari hata kidogo. Lakini kuwakumbuka wahanga wa ajali yenyewe hakuna maana ya kuionea fahari ajali hiyo. Kulikuwa, na bado, kuna maana ya kuwajali wenzetu waliotangulia mbele ya haki na kujifunza kwa mkasa wenyewe uliosababisha ajali hiyo.
Hadi leo, waliohusika na ajali yenyewe hawakubebeshwa dhanama yao wanayostahiki kuibeba, badala yake suala lenyewe limebambanywabambanywa na kuvungwavungwa hadi limefutika kwenye vitabu vya kumbukumbu kama kwamba roho zilizopotezwa hazikuwa za binaadamu.
Kulikuwa, na bado, kuna maana ya kuliwekea taifa letu kumbukumbu ya mazuri na mabaya yetu, ili vizazi vijavyo viige mazuri tuliyofanya sisi watangulizi wetu na vijifunze kwa mabaya yaliyotutokezea.
Ni kwa kuwa hatukuonesha tangu awali uzito unaostahiki kwenye jambo hili, ndio maana si ajabu kuwa miezi minane tu baadaye, meli nyengine iitwayo MV Skargit nayo ikazama mkondoni ikielekea Dar es Salaam, ikiondoka na roho nyengine za maelfu ya watu wetu. Chanzo kikiwa ni kile kile – uzembe wa wenye dhamana.
Kulikuwa, na bado, kuna maana ya kuwaenzi waliobakia hai baada ya mkasa wenyewe. Kwanza wale 620 walioripotiwa kuokolewa, kwa kuwapatia msaada wa kisaikolojia, kisheria na kiuchumi ili kuyaanza tena maisha baada ya kupitia njia ya mauti na kunusurika. Pili kwa wanafamilia ambao waliwapoteza ndugu na jamaa zao.
Kuna ambao ajali hii iliondoka na takribani familia nzima, mfano wa yule bwana wa Gando, ambaye alibakiwa na paka wake tu nyumbani, lakini mke na wanawe wanne wote walikwenda.
Hadi leo, hakuna taasisi wala mfuko ulioanzishwa kwa ajili ya wahanga hawa. Wenye misongo ya mawazo wameendelea kuwa nayo. Na si hasha kuwa wengine wamewafuata wapendwa wao makaburini, maana majonzi waliyoyabeba bila msaada wa kitaalamu kufarijiwa, yaliwafanya nao kufa vifo vya mapema.
Namjuwa rafiki yangu mkubwa ambaye alipoteza mke wake aliyekuwa ndio kwanza wameoana mwaka mmoja kabla ya ajali hiyo. Mwaka wa sita sasa huu amekataa kuoa tena, na bado hadi leo anaomboleza kama ndio kwanza mkewe amekufa jana jioni.
Namkumbuka mama ambaye aliwapoteza watoto wake watatu na wajukuu wanne, akibakiwa nyumbani na mtoto mmoja tu sasa, na hadi leo akimuita yule mmoja, kwanza hutaja majina ya wote waliotangulia mbele ya haki. Wala hakusudii. Lakini akili yake imetikisika, moyo wake umeganda.
Hawa wote walistahili jawabu nzuri zaidi kuliko ile ya kuambiwa tu kuwa Zanzibar ni nchi ya Waislamu na Waislamu hawana kawaida ya kuitukuza misiba yao. Jawabu ambayo sio tu ni kinyume na Uislamu wenyewe, maana vyenginevyo Qur’an isingejaa visa vya majanga yaliyowapata waliotangulia, bali pia haitatuwi ukubwa wa tatizo lililosababishwa na ajali hii.
Lakini kama kweli sisi ni taifa la watu wenye fikira, bado hatujachelewa kupatengeneza pale tulipoharibu. Ni miaka sita tu sasa imepita tangu ajali hizi mbili – ya MV Spice Islander na MV Skagit. Hata miaka kumi haijafika.
Yako matukio makubwa duniani ambayo kuanza kwake kukumbukwa na kupewa nafasi inayostahiki, kulianza miongo kadhaa baadaye, baada ya jamii kutulia na kutazama zilikopita ili kujenga mbele ziendako. Nasi tunaweza kufanya hivyo.
Kuelekea kuwapa hishima yao wahanga hawa, hata hivyo, tunapaswa kujipanga kwa tafiti, kwa maandishi, kwa rikodi za picha, vidio na sauti. Tunapaswa kuanzisha sasa vuguvugu maalum kwa ajili ya wahanga wa ajali hizo na kulipa sura na nguvu ya kuhifadhi tareikh yetu.
Tufanyeni hivyo kama jamii, kama nchi na kama taifa, maana taifa lisilowaomboleza wahanga wake, halina uthubutu wa kuwatukuza mashujaa wake.
Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: ajali, msiba, Mv Spice Islander, Zanzibar
