Vitu vyote tunavyotaka kufanya iwe ni kupumzika, kulala, kutembea, kwenda kazini au kusafiri popote; tumepewa muda maalum. Lakini, hakuna mtaji au rasilimali muhimu inayopotea bure na kila mara kuliko zote hapa duniani kama muda. Na bahati mbaya wengi tunaupoteza mtaji huu wa muda pasina kujua. Wakati wote muda unakatika na kuisha kabisa pasipo kungojea au kurudi nyuma. Tunaweza tukawa tunangojea tukio fulani lakini kamwe muda haumgojei mtu yeyote yule.
Katika rasilimali zote alizotujaalia Mungu, muda ndio rasilimali pekee aliyotugawia watu wote kwa usawa bila upendeleo. Mtu maskini na mtu tajiri wote wana saa 24 (angalizo: Kiswahili fasaha cha uwingi wa saa ni saa, si masaa!). Nenda kwenye nchi tajiri na nchi maskini zote zina saa 24 kwa siku. Hakuna siku yenye zaidi ya saa 24. Sote tuna siku 7 kwa juma, hakuna nchi yenye siku 10 kwa juma. Tofauti pekee tulizonazo ni mbili tu: jinsi tunavyoitumia rasilimali muda kwa tija na ufanisi, na kiasi cha muda wa kuishi hapa duniani. Baadhi wanaishi muda mrefu na wengine muda mfupi.
Linapokuja suala la kufanya kazi kwa muda tuliopewa, kuna watu hutumia saa 6 kwa siku, saa 18 huishia njiani, kupiga soga na kisha kwenda kulala. Wengine hutumia saa 8 kwa siku, saa 16 hutumika kupumzika, kusafiri, kustarehe na kulala. Ofisi zetu nyingi hufunguliwa saa 2 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni. Ina maana theluthi moja tu ya muda tunafanya kazi na theluthi mbili (zaidi ya 66%) tupo njiani, kustarehe na kulala.
Kwa kusema hivyo, mfanyakazi mwenye miaka 60 kazini, anakuwa katumia miaka 20 tu kufanya kazi. Miaka yote 40 ni kwa ajili ya kulala, kustarehe na kusafiri njiani kwenye foleni au msongamano, hasa kwa wanaoishi mijini. Miaka yote 40 hulipwa mshahara wa bure! Hapa tunabaini kirahisi kwanini hatujaendelea inavyopaswa. Upotevu wa mufa ni mojawapo ya sababu kuu za kusuasua kwetu. Watu waliokwisha endelea hawalali! Wanachakarika kucha-kutwa kusaka maendeleo utadhani dunia inaisha kesho. Wengine hukataa kwenda likizo, na wakipata hufanya kazi zingine za kimaendeleo. Wametambua kuwa muda ni mtaji wa kuwaletea maisha yenye mafanikio.
Umuhimu wa muda katika kuleta mafanikio ya kimaisha
Hekima ya Mungu katika misahafu inatuasa tuukomboe wakati na kuutumia vizuri katika kufanya kazi zenye tija katika maisha yetu (Waefeso 5:15). Aidha muda wetu wa kuishi hapa duniani unatofautiana sana baina yetu. Wengine huishi muda mrefu na wengine muda mfupi. Hata hivyo, wanaobahatika kuishi muda mrefu huishi katika mateso ya maradhi ya uzeeni. Tunaambiwa miili yetu ikiwa na afya njema, miaka yake ya kuishi hapa duniani ni 70 au 80 (Zaburi 90:10). Baada ya hapo ni taabu tupu.
Je, tunautumiaje muda tulionao? Ni swali linalotuchenga sana huku tukijisahau mno kutimiza wajibu wetu na ndoto zetu. Watu wachache sana tunauchukulia muda kuwa ni rasilimali muhimu au mtaji adhimu. Tunaupoteza kwa kufanya mambo yasiyo na tija katika maisha yetu.
Mwaka 2002 nilikuwa Ujerumani na timu ya wanaharakati wa Afrika Mashariki kujifunza masuala ya kijamii. Tulitembelea maeneo mengi ya Magharibi na Mashariki. Maeneo ninayoyakumbuka ni Dusseldorf, Cologne, na Bonn katika jimbo tajiri la North-Rhine Westphalia, kisha Hess, Dresden, Saxony (Leipzig) na Berlin. Tulizunguka kwa boti za kifahari katika mto Rhine na Danube na kuishi kwenye hoteli za kifahari na kisasa.
Wakati sisi tukishangaa hatua kubwa ya kiuchumi na kimaendeleo waliopiga Wajerumani, wao walitushangaa jinsi tunavyopoteza rasilimali muda. Kila tulipokuwa tunaingia ukumbini kwenye mafunzo, kuna mtu alikuwa anasimama mlangoni na kuhesabu dakika ambazo kila mmoja kachelewa. Wapo tuliopoteza dakika 2, 10, 20 na wengine nusu saa nzima.
Mwisho wa mafunzo yetu kila mtu alihesabiwa muda alioupoteza kila siku na kwa kipindi chote tulichokaa. Wengine walipoteza jumla ya saa 2, wengine saa 4 hadi 6. Japo hatukukemewa, lakini walitujulisha kazi ambazo tungeweza kufanya kwa mafanikio kwa kutopoteza saa zote hizo bure. Niliumia sana! Lakini nikabaini kwanini wao wameendelea sana Ulaya, huku sisi tukipiga soga vijiweni na kushupalia mizaha, tetesi na umbea.
Inauma zaidi kukuta watu wakipiga soga kwenye ofisi za umma. Wengi hutumia simu zao au kompyuta za serikali kupakua na kupakia udaku mitandaoni. Wengine muda mwingi hukodolea macho tamthiliya kwenye televisheni zilizotundikwa ofisini. Tumegeuza ofisi za umma kuwa vijiwe huku wateja wakisubiri huduma kwa foleni nje. Pongezi nyingi kwa Waziri William Lukuvi aliyekesha akitatua migogoro ya ardhi. Wenzetu Japan wameendelea sana, ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani. Lakini hawaruhusu wafanyakazi wao kuwa na simu ofisini au kutazama runinga.
Aidha kuna haja ya kufanya kazi kwa zamu (shift) kati ya mchana na usiku ili kuondokana na mazoea ya wote kuamka wakati mmoja asubuhi na wote kurudi nyumbani wakati mmoja jioni. Utaratibu huu utapunguza sana foleni. Kwa kuanzia, napendekeza tuwe na zamu mbili za wafanyakazi wanaoanza kazi saa 2 asubuhi na kutoka saa 10 jioni kama ilivyo ada.
Kisha wawepo wanaoanza saa 2 usiku na kutoka saa 10 alfajiri. Tutakuwa tunapishana njiani badala ya sasa ambapo karibu watu wote Dar es Salaam asubuhi huelekea upande mmoja, huku upande mwingine wa barabara ukiwa tupu na mabasi ya abiria matupu. Zamu hizi kwa kiasi kikubwa zitapunguza sana foleni, misongamano na kuukomboa muda tunaoupoteza.
Sambamba na hilo, tutawasaidia sana wazazi wanaotoka asubuhi kwenda kazini watoto wakiwa bado wamelala na kurudi nyumbani watoto wakiwa tayari wamelala. Hawana muda asilani wa kukaa kifamilia. Ikiwezekana, hata masoko makubwa, maduka makubwa (supermarkets and shopping malls), benki, ofisi za mamlaka ya mapato (TRA) ziwe wazi 24/7 – yaani saa 24 kwa juma. Watu watapishana na kujipangia muda wao bila foleni wala msongamano. Kama imewezekana kwenye baadhi ya vituo vya afya, sioni kwanini isiwezekane kwenye ofisi za umma na maeneo mengine.
Muda ni rasilimali muhimu na adhimu, ni mtaji. Ni rasilimali ambayo hupotea na kuisha kila sekunde, dakika, saa, siku, juma, mwezi na mwaka; si rahisi kuirejelea upya. Marafiki zetu wengi wanatupotezea muda au sisi tunapoteza muda wa marafiki zetu na kuleta hasara. Vijana wengi hukaa vijiweni wakipiga soga ambazo haziwasaidii katika maisha yao. Watabishana kucha-kutwa kuhusu wachezaji mpira au timu maarufu za Ulaya wakati wenzao wanacheza na kuingiza kipato kikubwa kwa kila juma.
Wazee watakaa barazani kucheza bao au kweda vilabuni kunywa pombe wakati wenzao wako mashambani au wanajishughulisha na ujasiriamali. Miaka ya hivi karibuni, tumeona watu wengi wakikesha na simu zao wakifuatilia masuala ambayo hayawaingizii kipato chochote au kuwaelimisha. Wako tayari kukosa usingizi wakifuatilia vituko na udaku wa mitandaoni huku wenzao wakikesha kuzalisha mali.
Ukienda nchini China, Wachina na watu wengine wanaoishi huko, muda wote wa mchana na usiku huutumia kuzalisha mali. Kuna baadhi ya watu wameajiriwa sehemu moja kufanya kazi mchana na sehemu nyingine wameajiriwa kufanya kazi usiku. Wanakuwa na ajira mbili tofauti kwa siku moja. Waliojiajiri nao biashara zao ziko wazi saa 24. Hakuna kulala!
Hivi ninavyoandika makala haya, nimeamka saa 10 alfajiri, na najua wengine wameamka kwenda mashambani, kwenda kuvua samaki au kwenda kazini. Lakini kuna wengine pia ambao wanavuta blanketi na huenda wataamka saa 3 au saa 4 asubuhi. Usingizi ni mzuri kwa ajili ya kupumzisha mwili tu, si kwa ajili ya kuulemaza na kupoteza muda wa uzalishaji mali.
Hitimisho
Miaka tulionayo hapa duniani ni michache sana, inatoweka upesi. “However, what significantly matters in life is not the amount of years we put into life, but the quality of life we put into years.” Namaanisha kuwa: “Hata hivyo, thamani ya maisha haiko katika idadi ya miaka tunayoishi, bali iko katika ubora wa maisha katika miaka tunayoishi.”
Kuna watu wanaishi muda mrefu sana hapa duniani lakini hakuna cha maana wanachofanya, wala kumbukumbu zao hatuna. Kuna watu wanaishi muda mfupi lakini hufanya mambo makubwa na yenye faida kwao na jamii. Kila mara tujihoji endapo muda tunaoutumia kufanya jambo fulani unaleta mafanikio katika maisha yetu. Si kila jambo tunalolizingatia lina maana, na si kila jambo lenye maana linapaswa kuzingatiwa. Unaweza ukazingatia sana kuangalia mpira lakini usiwe na maana kwako. Usipate faida yoyote!
Unaweza ukaona kuna maana kupitia kwenye kilabu au baa, lakini ukizingatia sana hilo na kujiwekea ratiba ya kila siku, utapoteza muda muhimu sana kwako na kwa familia yako. Kitu pekee chenye maana na cha kuzingatiwa ni muda tunaoutumia kuzalisha mali au kujenga mahusiano mema ya kifamilia na kijamii.
Nihitimishe kwa kuishauri serikali kuondoa televisheni zote zilizotundikwa kwenye ofisi za umma. Aidha, wafanyakazi wote wa umma wawe wanaacha simu zao nyumbani au mlangoni nje ya ofisi. Zitumike simu za mezani tu.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe, mchambuzi huru wa masuala ya kitaifa na kimataifa, anayeishi Mwakaleli, Busokelo, Rungwe, Mbeya. Anapatikana kwa anuani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com
Filed under: JAMII Tagged: mafanikio, mitaji, muda, ujasiri amali
