Kuna wanaohoji kwamba mgogoro uliopandikizwa kwenye Chama cha Wananchi (CUF) unaweza tu kumalizika kwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kukaa kitako na aliyekuwa mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, kuyazungumzia wanayotafautiana.
Mtazamo wa mazungumzo ndio unaonekana, kijuujuu, kutajwa pia na Profesa Lipumba mwenyewe, ambaye katika siku za hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa mgogoro uliopo kwenye chama chake hicho cha zamani umalizwe kwa mazungumzo nje ya mahakama, lakini kwa sharti kubwa la, kwanza, Katibu Mkuu Maalim Seif kumtambua yeye, Lipumba, kuwa mwenyekiti wake na, pili, kwenda Ofisi Kuu za CUF zilizopo Buguruni, Dar es Salaam, ili aende akapangiwe kazi na mwenyekiti wake huyo.
Kauli ya mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro inavutia. Inawashawishi wengi waiangalie kama suluhu pekee. Inawaweka wengi hao kwenye bawa la Profesa Lipumba, kumuona kuwa mtu wa suluhu, mtu wa mazungumzo, mtu wa muafaka.
Wanaoshinikiza kuwa Maalim Seif azungumze na Profesa Lipumba wana hoja tatu mkononi mwao. Kwanza, ukweli kuwa njia ya mazungumzo ndio njia bora kabisa ya kumaliza tafauti baina ya wenye uhasama. Msemo wa kifalsafa hutuambia kuwa: “kinachoshindwa kutatuliwa kwa majadiliano, hakiwezi kutatuliwa kwa mapigano.”
Maana yake ni kuwa mapambano, kama haya yanayoendelea sasa kwenye CUF, hayatafanikisha chochote kwa upande wowote, bali mazungumzo – endapo yatafanyika kati ya pande hizo – ndiyo yanayoweza kuumaliza mkwamo uliopo.
Hoja ya pili waliyonayo ni kuwa, hata kama pametokea hitilafu kubwa baina ya Maalim Seif na Profesa Lipumba huko nyuma, basi uhasama wao hauwezi kuwa mkubwa kuliko uliokuwapo baina ya CUF kwa ujumla wake na CHADEMA, kwa upande mmoja, na au CUF na CCM, kwa upande mwengine, ambamo mote humo muwili, Maalim Seif na Lipumba walisimamia na kuongoza juhudi zilizopelekea makubaliano yaliyokuwa na faida kwa pande zote.
Kwa upande wa CUF na CHADEMA, Profesa Lipumba, ambaye chama chake kilishawahi kuitwa CCM B na cha wapenzi wa jinsia moja na CHADEMA, alikuja baadaye mwaka 2014 kushirikiana na CHADEMA, NCCR-Mageuzi na NLD kuasisi Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambao umesalia hadi leo kuwa muungano pekee madhubuti wa vyama vya upinzani dhidi ya chama tawala – CCM.
Kwa upande wa CCM, Maalim Seif alikuja kushirikiana na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Zanzibar mwaka 2009, Amani Karume, kuasisi Maridhiano ya Wazanzibari ambayo nayo yalikuja kuzaa Mabadiliko Muhimu ya Katiba, Kura ya Maoni na hatimaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo ilihudumu baina ya 2010 na 2015 visiwani Zanzibar.
Hoja yao ya tatu ni kwamba, hata kama Profesa Lipumba na genge lake ni wasaliti kama unavyodai upande unaomuunga mkono Maalim Seif, bado ni upande huo wa wasaliti ambao wanapewa nguvu na kila nyenzo na vyombo vyote vya dola – polisi, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ofisi ya usajili na ufilisi, tume za uchaguzi, na kila aliye chini ya dola inayoongozwa na CCM.
Kwa mujibu wa hoja hii, Lipumba na kundi lake watashinda tu hatimaye kwenye vita hivi na watajipatia wanachokitaka, kama ambavyo hadi sasa wanaonekana kufanikiwa kwa kila wanalolifanya.
Wanatoa mfano wa karibuni kabisa wa Lipumba kuwafukuza wabunge wanane na madiwani wawili wa viti maalum, na kisha hatua hiyo kubarikiwa kwa uharaka wa ajabu na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, bunge na tume ya uchaguzi.
Kwa hoja hii, ni kwamba ili Maalim Seif aendelee kubakia salama (ikiwa kweli hadi sasa yupo salama ndani ya CUF), basi ni kumridhia Profesa Lipumba kwa kila analolitaka. Ingawa wenye hoja hii hawahakikishi ikiwa endapo Profesa Lipumba akipatiwa hilo, atasimamia hapo au atataka mengine zaidi.
Nimesema kuwa hoja ya mazungumzo baina ya kambi mbili zilizopo mahakamani hivi sasa ndani ya CUF inashawishi sana. Kama unaiingia kichwa kichwa, unaweza kudhani kuwa upande wa Maalim Seif kwenye mzozo huu ni wapumbavu sana kutokuupokea haraka mkono wa maridhiano unaonyooshwa na Profesa Lipumba.
Lakini ukweli ni kuwa hoja hii imeanza kupotea njia tangu awali kabisa, na hivyo kuamua kuijibu kuangalia mwisho wake hakuna mantiki yoyote.
Kwanza, mgogoro huu uliopandikizwa kwa jina la Profesa Lipumba hauna tafauti hata kidogo na kile kitendo cha Jecha Salum Jecha wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015. Mawili haya yana uhusiano mkubwa kwa asili, njia, lengo na hata muendelezo wake.
Kwa hivyo, kama vile ambavyo huwezi kuyajadili yaliyofuata baada ya tarehe 28 Oktoba 2015, pale Jecha alipochukuwa hatua hiyo, bila kulirejea kwanza hilo tukio lenyewe na kulipima uhalali na uharamu wake, kufaa na kutofaa kwake, ndivyo ambavyo mtu hawezi kulijadili hili la Lipumba bila kwanza kurejelea kwenye chimbuko lake.
Huwezi kuenda popote kabla yakwanya kulijadili na kulimaliza la kujiuzulu kwa Profesa Lipumba kwa hiyari yake, licha ya kuombwa sana na wenziwe akiwemo Maalim Seif kwamba asichukuwe hatua hiyo, na kisha kuja kujirejesha kwenye nafasi hiyo mwaka mmoja baadaye licha ya upinzani mkubwa wa hao hao waliomtaka mwanzo abakie.
Sharti kwanza mwenye kusaka suluhu baina ya kambi hizi mbili, amalizane na hili na uhalali na uharamu wa kitendo hicho, kufaa na kutofaa kwake. Akishamaliza hilo, ndipo sasa aje kwenye meza ya mazungumzo kusaka njia ya kwenda mbele baada ya hapo.
Pili, hoja hii ya mazungumzo baina ya Maalim Seif na Profesa Lipumba imejengwa juu ya upotoshaji kwamba mgogoro uliopandikizwa na ujio huo wa Profesa Lipumba mwaka mmoja baada ya kujiuzulu, ni mgogoro baina ya Maalim Seif na yeye, Profesa Lipumba.
Licha ya wote wawili kurejelea mara kwa mara kwamba wao kama wao wana historia ya miongo kadhaa kama marafiki wa karibu, wajengaji wa hoja hii wanakataa uhalisia huo.
Bahati mbaya ni kwamba baada ya kwishajirejesha madarakani, hata Profesa Lipumba ameazima maneno hayo hayo ya kueleza uhasama baina yake na Maalim Seif, akiwacha kabisa hoja ya msingi inayozozaniwa hapa, ambayo ni matakwa ya katiba, kwa upande mmoja, na ya kimaadili, kwa upande mwengine.
Kuliweka hili kwenye nafasi yake, ni vyema ikafahamika kuwa chimbuko la mzozo huu halimo kwenye ugomvi wa wawili hao, bali limo kwenye katiba na maadili ya kiuongozi. Profesa Lipumba aliondoka kwenye uwenyekiti wa CUF kwa hoja madhubuti ya kimaadili.
Kwamba akiwa kinara wa kupambana na ufisadi, nafsi yake ilikuwa inamsuta kujiona kuwa analazimika sasa kuungana na kumpigia debe mshukiwa mkuu wa ufisadi nchini Tanzania, Edward Lowassa. Akatumia haki yake ya kikatiba, kuiacha nafasi ya kukiongoza chama chake katika wakati ambao, kwa hakika, kilikuwa kikimuhitaji sana.
Maadili na katiba vikafanya kazi yake kwake wakati huo, ikitarajiwa kuwa maadili na katiba hiyo hiyo vingelifanya kazi tena baadaye. Haikuwa hivyo, kwa upande wake. Lakini imekuwa hivyo kwa upande wa waliompinga wakati ule alipoondoka na wanaompinga leo alipojirejesha.
Na ni kwa msingi huo huo wa maadili ya kiuongozi na katiba, ndipo ambapo roho ya dhati ya CUF inasalia hadi leo. Ndipo tamaa ya kuendelea uhai wa roho hiyo ulipo. Na, hapana shaka, hakuna mahala pengine popote ambapo roho ya maadili na katiba inaweza kuhuishwa pasipokuwa kwenye mahakama inayoutambua wajibu wake na inayotenda kazi kiadilifu.
Swali ni kwamba je, idara ya mahakama nchini Tanzania inazo sifa hizo za uhuru, usawa na uadilifu? Mpaka hapo kesi hizi zitakapoamuliwa, majibu ya uhakika hakuna aliyenayo. Hiyo ni kwa sababu, katika mifano kadhaa, muhimili huu wa kugawa haki umeonekana kuchezewa na muhimili wa dola, ingawa ipo pia mifano ambapo ulisimama imara.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 21 Agosti 2017
Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: cuf, demokrasia, Lipumba, maalim seif, mahatma, Tanzania, Zanzibar
