Ukraine imeyaondosha masanamu yote 1,320 ya mwanamapinduzi wa kikomunisti, Vladimir I. Lenin, kufuatia hatua ya serikali kuachana na alama zote za Kisovieti kwenye taifa hilo.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, masanamu ya kiongozi huyo wa Bolshevik yameondoshwa kwenye kila mji na kijiji kinachomilikiwa na serikali ya Kiev ambayo iliuangusha utawala wa Rais Viktor Yanukovych unaoungwa mkono na Urusi miaka mitatu iliyopita.
Mpango huo wa kupingana na Usovieti, ambao pia ulijumuisha kubadilisha majina ya mitaa na miji, ulitungiwa sheria na Rais Petro Poroshenko mwezi Mei 2015, kwa mujibu wa gazeti la The Times la Uingereza.
Chini ya mpango huo, mitaa mingi imepewa majina ya mashujaa wa Ukraine, ingawa mtaa mmoja uliokuwa na jina la Lenin, magharibi mwa nchi hiyo umepewa jina la Lennon, kwa heshima ya Beatles.
Volodymyr Viatrovych, mkurugenzi wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Taifa, alithibitisha kwamba kila sanamu la Lenin limeondoshwa sambamba na mengine 1,069 ya zama za Kisovieti.
Licha ya sheria hiyo, mabaki ya alama za Ukomunisti bado zimesalia kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo, ambalo linadhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 10,000 wamekufa baada ya Urusi kutwaa udhibiti wa mkoa wa Crimea mwaka 2014.
Chanzo: Gazeti la The Independent la Uingereza la tarehe 18 Agosti 2017
Filed under: BURUDANI, HABARI
