Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Akina Mnyaa, Khalifa na wenzao hawatuwakilishi Wapemba

$
0
0

Hii si mara ya kwanza kwa Chama cha Wananchi (CUF) kujikuta kwenye mgogoro unaokimomonyoa ndani kwa ndani na kisha kikainuka imara kusonga mbele, lakini lazima tuseme wazi kuwa mgogoro wa safari hii si kama mingine ya nyuma na kuna wasiwasi kuwa kinaweza kushindwa kuvuuka salama usalimini.

Katika mengi yaliyoibuka ndani ya mgogoro huu mkubwa, leo nataka nizungumzie kitu kimoja tu – nacho ni hawa waliojiunga na timu ya Profesa Ibrahim Lipumba kutokea visiwani Zanzibar, ambapo ukiziangalia sura zote zilizokwishajitokeza waziwazi hadi hivi sasa, unachoweza kukiona ni kisiwa cha Pemba.

Nassor Seif Amour, Mussa Haji Kombo, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Mohamed Shamis, Khalifa Suleiman Khalifa, Rukiya Kassim Ahmed na Thiney Juma Mohamed, wote wanatoka kisiwani Pemba, ambako kunasalia kuwa ngome madhubuti ya CUF na ambako daima kumekuwa kukikiadhibu Chama cha Mapinduzi (CCM).

Na Mohammed Ghassani

Ukimtoa mwanajeshi Thiney Juma Mohamed, waliobakia wote wamewahi kuwa wabunge na au wawakilishi katika nyakati tafauti, huku wengine kama Khalifa wakikaa bungeni tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995. Kwa hivyo, pamoja na kujitolea kwao kukubwa kukijenga chama, kwa hakika wao ndio hasa waliojengwa na CUF.

Pemba, kisiwa ambacho mimi pia ninatokea, kinatambulika kihistoria kwa upinzani wake dhidi ya watawala kisiowakubali, hata wawe na nguvu kiasi gani. Wenyewe Wapemba tuna fakhari ya kuwa kizazi cha wahenga waliopambana na kuushinda utawala katili wa Mreno baada ya karne nzima, tunajivunia kuupinga utawala wa Busaid, na hata uliofuata baadaye wa Mwingereza na kisha wa CCM.

Kwa sababu zinazofanana, kisiwa hiki kimekuwa sehemu ya mapambano ya Zanzibar dhidi ya wanachoamini Wazanzibari kuwa ni utawala wa Tanganyika kwa hadhi ya nchi yao.

Ukweli kwamba CUF iliungwa mkono na kisiwa kizima cha Pemba mara tu ilipoanzishwa, haukutokana pekee na sababu ya kuwa mmoja wa waanzilishi wake, Maalim Seif Sharif Hamad, ni mzaliwa wa kisiwa hicho, bali pia, na zaidi, ni kwa sababu kisiwa chenyewe kilikuwa kinasaka muda mrefu jukwaa la kuonesha upinzani wake dhidi ya mtawala wasiyemkubali.

Kwa nini sasa wanasiasa hawa kutoka Pemba wamekuwa sehemu ya genge linalosimama dhidi ya chama ambacho kimekuwa daima alama ya mapambano ya Zanzibar dhidi ya mtawala aliyeshiriki, kupanga na kuwahujumu wananchi wa Zanzibar kwa miaka-nenda, miaka-rudi?

Kwa nini akina Mnyaa na Khalifa, ambao walikaa muda mrefu bungeni kwa kura za Wapemba wenzao, wakafaidika kiuchumi wao na familia zao, wamegeuka leo dhidi ya maslahi mapana ya watu waliokanyaga mabega yao kujiinuwa?

Kwa nini akina Nassor Seif na Mussa Haji wawe sehemu ya mchakato wa kuipeleka CUF njia ya NCCR-Mageuzi, chama kilichowahi kuwa na nguvu sana mwanzoni mwa mfumo wa vyama vingi na kutikisa nchi kwenye uchaguzi wa 1995, lakini kikapandikiziwa migogoro ya kiuongozi na hatimaye kusambaratishwa, hadi sasa kimesalia na mbunge mmoja tu bungeni?

Kwa nini akina Thiney na Bi Rukiya wawe sehemu ya mkakati wa kuimaliza CUF, ambayo hadi mwaka 2015 ilikuwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar na iliyowahi kuwa ya pili kwa ukubwa bungeni na kusaidia kuikaribisha Zanzibar kwenye ndoto yake ya kuwa na mamlaka kamili ndani ya Jamhuri ya Muungano?

Majibu ya maswali haya wanaweza kuwa nayo zaidi wenyewe, na pengine wataandika kujibu kwa wakati wao, lakini hawawezi kuondosha ukweli uliopo; kwamba, kwanza, wanachokifanya kiko dhidi ya Zanzibar yao na hivyo kisiwa chao cha Pemba walikozaliwa na kukulia na, pili, kwamba wao ni wasaliti dhidi ya Pemba na Wapemba.

Kwa yote mawili, hawa si wawakilishi wa Wapemba, mimi nikiwa mmoja wao. Nimezaliwa, kukulia na kufundwa ndani ya kisiwa hicho. Mbali ya kuutangatanga ulimwengu, bado nabakia sehemu ya Wapemba na Wazanzibari wanaojuwa nini tunakisimamia kwenye taswira ndogo ya Zanzibar na Tanzania, na kisha taswira kubwa ya Afrika Mashariki, Afrika na hata dunia kwa ujumla.

Ukihesabu gharama ambazo hata wao wenyewe zimeshawapata kwenye mapambano haya, ikiwemo kufungwa, kupigwa na hata kuuliwa kwa ndugu na jamaa zao wa karibu, akina Mnyaa na Khalifa hawakupaswa kabisa kuwa mahala hapa tupaitapo kwa Kipemba ‘asfala-safilina’ – yaani chini kuliko walio chini, panapohusika dhamira.

Lakini pengine swali kubwa kuliko yote ni kwa nini CUF yenyewe – kama chama – imefikishwa mahala hapa? Wengine wanasema ni kutokana na kosa la uongozi wenyewe wa CUF kuchelewa kuchukuwa hatua muafaka kutokana na masharti ya katiba yao, pale pale na wakati ule ule Lipumba alipoamua kuwaacha mkono wakati wakimuhitaji sana karibu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwao wao, laiti CUF ingelifuata kikamilifu katiba yake tangu siku Lipumba anajiuzulu mwenyewe na kwenda zake Rwanda, basi kiongozi huyo asingelikuwa tena na nafasi ya kurejea kuivuruga CUF kwa namna ambayo anafanya sasa kwa mafanikio makubwa kupitia mkono wa dola na ushirikiano aupatao kutoka kwa hawa waliaomua kujiunga na usaliti kutokea kisiwani Pemba.

Lakini kwa wanaoujuwa ukweli wa mambo, majibu si mepesi kiasi hicho. Hao wanajuwa kuwa CUF haidhuriwi kabisa na katiba yake, bali inadhuriwa na mambo matatu makubwa kwenye hili: kwanza ni msimamo wake dhidi ya uhuni uliotendeka Zanzibar tarehe 28 Oktoba 2015, siku uliyofutwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

CCM na vyombo vyake vya dola kwenye serikali zote havikuwahi kuisamehe CUF kwa jinsi chama hicho kilivyowaweka uchi katika kadhia hii nzima. Kwa CCM, chama cha CUF kinapaswa kuondoka kwenye uso wa dunia haraka iwezekanavyo kabla ya uchaguzi mwengine wowote ujao, maana aibu ya Oktoba 2015 visiwani Zanzibar hawakuweza kuifidia hadi leo.

Pili, CUF inadhuriwa na msimamo wake wa muda mrefu kuelekea mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwani hiki ni chama pekee cha kisiasa ambacho kimejijenga vizuri mno katika “Siasa za Muungano” katika kiwango ambacho CCM inapoteza kila uchao kutokana na uungwaji mkono unaoongezeka kwa hoja ya CUF juu ya Muungano huo.

Hili halijaanza leo, na daima vyombo vya dola vimekuwa vikisaka njia ya kuimaliza CUF ili kunyamazisha kabisa hoja dhidi ya Muungano wenyewe. Hadi kufikia mgogoro huu mkubwa kabisa wa Lipumba, CUF ilishapandikiziwa mingine mingi huko nyuma kwa mkono wa vyombo vya dola kutokana na msimamo wake huo.

Na, tatu, CUF inadhuriwa na hatua yake ya kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambao uliitikisa sana CCM kwenye uchaguzi mkuu wa 2015, kiasi cha kwamba kwa mara ya kwanza chama hicho tawala kilikosa asilimia 60 ya kura za jumla. Kwenye hili, CUF hailengwi peke yake, bali ni pamoja na mshirika wake mkuu, CHADEMA, ambacho kimekumbwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya viongozi wake tangu kumalizika uchaguzi huo.

Kwa hivyo, Lipumba na wenzake hawapo kwenye nafasi ya kushinda ‘vita’ vinanavyoendelea sasa eti kwa kuwa uongozi wa CUF ulidharau kuitumia katiba yao kwa wakati tu, lakini zaidi ni kwa kuwa CCM na vyombo vya dola vinataka kuona kuwa CUF inasambaratika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020 ili kuyauwa kabisa madai ya chama hicho kwa uchaguzi wa 2015 Zanzibar, kuizika moja kwa moja ajenda ya Zanzibar kuhusu Muungano na ikibidi kuiuwa kabisa UKAWA.

Uongozi wa CUF unalijuwa hili na unasema mara kadhaa kuwa haupambani na Lipumba na genge lake wala haupingani na katiba ya chama chao, bali unapambana na kupingana na dola nzima iliyosimama nyuma ya genge hilo.

Ni jambo la kushangaza sana kwamba, kwa upande wa Zanzibar, genge hilo linaundwa na wanasiasa kutoka kisiwani Pemba pekee, anakotokea Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, tena baadhi yao, muna ambao kupanda kwao ngazi kuliwezeshwa kwa hishima tu ya wanachama kwa Maalim Seif tu, na si vyenginevyo.

Siku wananchi walipoamua kuchukuwa hatua dhidi ya wanasiasa hawa kwa njia zao wenyewe kwenye kura za mchujo huko mashinani na wakaangushwa, akina Mnyaa, Khalifa, Mussa Haji, Rukia na wenzao, ndipo walipojitokeza kwa sura zao halisi. Maslahi.

Ni bahati mbaya kwamba sasa wanatumia sura zao hizo kuiuwa taasisi pekee ambayo ilitegemewa sio tu na wapigakura wa kisiwa chao, bali pia na Wazanzibari na Watanzania wengine kwa ujumla, kama jukwaa la kuisemea na kuitetea Zanzibar kitaifa na kimataifa.

Hawa ndio wale waitwao wa Kipemba: “Nalitote!” Madhali wao wamekosa ulwa ndani ya CUF, basi CUF nayo naife.


Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, mgogoro, Profesa Lipumba

Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles