KASHFA ya kuchotwa fedha zilizokuwa zikibishaniwa na washirika wawili wa kibiashara hapa nchini – Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya IPTL – Akaunti ya Tegeta Escrow – imeibuka upya kwa nguvu kubwa safari kuliko wakati mwingine wowote.
Tangu mjadala wake ulipofungwa baada ya Bunge kuazimia mapendekezo 13 ambayo lilitaka Serikali iyatekeleze, kashfa hiyo iliyohusu ufisadi wa zaidi ya Sh. 320 bilioni, haikuwahi kujadiliwa kwa hisia kali kama ilivyo sasa.
Kwa namna inayosikitisha na kuonesha jinsi gani utawala unavyodharau maoni ya umma na mihimili mingine ya dola, likiwemo Bunge, kwa kutoheshimu kiudhati ushauri wake, hata vyombo vya kiuchunguzi vilivyokuwa na wajibu wa kuchukua hatua thabiti vilinyamaza.
Kimya kikubwa kilipita huku serikali ikijivuta, isitekeleze kwa uzito uliostahili mapendekezo ya Bunge baada ya mjadala mkali wa wabunge ilipobainika kuwa fedha zilizokuwa zikisubiri uamuzi wa mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara ya nchini Uingereza, zimechotwa isivyotarajiwa.
Si Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa wala Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) walioinua sauti kusema wanaendelea kutafuta ukweli. Kwa hakika, wakuu wa taasisi hizi za kiuchunguzi waliufyata.
Bila ya shaka walibaki kimya kwa hofu. Kilichokuwa kikiendelea ni utata. Kwamba je umma umuamini rais aliyetoa msimamo kuwa fedha zilizochotwa kutoka akaunti iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), si za umma?
Au Watanzania wafuate msimamo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyesema “Ndani ya fedha zile kulikuwa na kodi. Kodi ni mali ya umma. Hivyo kwenye eneo hilo la kodi, fedha za umma zipo?”
Alisema historia ya kuanzishwa kwa akaunti hiyo ni kuwa IPTL na Tanesco walikuwa na mzozo kuhusu malipo ya capacity charge. Mgogoro ulikuwa mkubwa na wakaamua kuhifadhi fedha za malipo hayo kwenye akaunti ya Escrow, wakisubiri shauri lao katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.
“Ikitokea ni kweli Tanesco ilikuwa inatozwa kiwango kikubwa kuliko ilivyopasa, si sehemu ya fedha ingekuwa ni zake na hivyo ni za umma?”
Kitendo cha mmoja wa waliogawiwa fedha na aliyekuwa sehemu ya umiliki wa IPTL, kujitokeza kurudisha alichogawiwa, Sh. 40 milioni, kimeibua hisia upya, na kwa nguvu kubwa zaidi. Wapo wanaotaka kila aliyeguswa akamatwe na kushitakiwa.
Leo hata TAKUKURU wameibuka na kusema wanaorudisha hawajasafishika. Ni msimamo mpya baada ya kimya kizito. Kwa bahati mbaya, TAKUKURU hawasemi walichochunguza ni kipi hasa – zile zilizokuwa kwenye akaunti ya Benki ya Mkombozi tu au na hata zile ambazo serikali haikuthubutu kumkabidhi CAG achunguze?
Ni rai yetu kwamba kashfa ya Escrow ichunguzwe upya na kitaalamu zaidi. Siasa na utashi wa kulinda wakubwa viachwe.
TANBIHI: Hii ni tahriri ya gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017.
Filed under: MAGAZETINI LEO Tagged: Escrow, Tanzania, ufisadi
