Mnamo tarehe 15 Mei 2013 aliyekuwa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman, aliweka saini kanuni inayosimamia mikataba ya kazi Zanzibar, si kwa nguvu za kiuwaziri alizokuwanazo Waziri Haruon ndizo zilizomsukuma kutunga kanuni hio, hapana, Waziri Haroun alifanya hivyo kwa kuzingatia sheria ya ajira ya Zanzibar yenye nambari 11 iliyotungwa mwaka 2005, ambayo ilipitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mwaka 2005 ambayo ilikubaliwa na rais wa wakati huo, Dk. Amani Abeid Karume, mnamo tarehe 27 Septemba 2005.
Katika vifungu vya 44(b)(ii), 45(3) na 126 vya sheria hio, ingawa vifungu hivi vina maelezo tofauti lakini maelezo yote tafsiri zake zote zinafanana katika makusudio, ambapo makusudio yake ni kumpa nguvu na uwezo Waziri husika kushauriana na bodi ili kuweka utaratibu mzuri wa mikataba ya ajira, ambapo ni pamoja na kuainisha aina za mikataba, kutunga kanuni itakayoainisha aina za kazi za kutwa (kibarua) na kutunga kanuni juu ya utekelezaji bora.
Kwa hakika, nampongeza Waziri Haroun pamoja na bodi kwa kushauriana na kutoka na maamuzi mamoja ya kutengeneza kanuni hii inayosimamia mikataba ya ajira ya mwaka 2013 ( The Employment Contacts of Service Regulations 2013).
Napaswa kutoa pongezi kwa sababu kabla ya kanuni hii ya mwaka 2013, naweza kusema asilimia kubwa ya waajiri hawakuwa wakilipa kipaumbele suala la kuwafungisha mikataba ya ajira waajiriwa wao au hata wale waliokuwa wakiingia mikataba walikuwa wakipewa mikataba ya muda mfupi, walikuwa wakifanya hivyo si kwa bahati mbaya bali sheria pia ilitowa mwanya kwa waajiri kufanya maamuzi hayo, kupitia kifungu cha 44(a),(b) na (C) vyote hivi vimempa muajiri uwezo wa kuajiri kwa mkataba anaopenda yeye, iwe wa kudumu, muda mfupi (maalum) au hata usio wa maandishi, lakini uwepo wa kanuni hii inalazimisha sasa kila muajiri analazimika kuangalia kanuni hii ni aina gani ya ajira anayotaka kuajiri na analazimika kuingia na muajiriwa wake katika mkataba wa muda gani.
Lakini kama inavyoeleweka kwamba hakuna kitu chenye faida pekee lazima japo hasara ndogo pia itakuepo katika kitu hicho, ingawa makala hii haina lengo la kuonyesha kiwango gani cha faida na hasara vinavyopatikana kwa uanzishwaji na utekelezaji wa kanuni hii lakini lengo ni kueleza hali halisi ilivyo, niseme kuwa hata utaratibu wa mwanzo wa mikataba kabla ya kanuni hii nao pia ulikuwa una faida yake, faida ambayo niseme rasmi imeondoshwa na utaratibu huu mpya.
Kwa mfano kwa wafanyakazi waliokuwa wanaajiriwa kwa mikataba ya miezi sita na mwaka mmoja, kila wakati ambao mkataba unamapomalizika muajiriwa alikuwa na nafasi ya kuomba nyongeza ya mshahara na mara nyingi waajiri walikuwa wakiwafanyia waajiriwa wao engezeko la mshahara, kwa kuzingatia kwamba kuna haja ya kuporesha maslahi ya kimkataba, kwa kuwa tu waliamini makubaliano yale yamemalizika na sasa ni makubaliano mapya.
Sasa kwa kanuni hii mpya ya mwaka 2013 ambayo tangu kutolewa kwake sasa ni mwaka wa nne haikuwahi kufanyiwa kazi kikamilifu hadi pale Dr. Ali Mohammed Shein alipofanya utezi wa Ndugu Fatma Idd Ali kuwa Kamishna mpya wa kazi, ambapo kamishna huyo amewaagiza rasmi kuanzia mwezi Juni 2017, kanuni hii ifuatwe kikamilifu kama inavyoelekeza.
Binafsi yangu nirudie tena kwamba nimefurahishwa na kanuni hii na maagizo ya kamishna wa kazi, lakini hofu yangu inakuja kutokana na mfumo wetu wa maisha ambao haujatulia kutokana na kila uchao ngarama za maisha zinaengezeka, bei za bidhaa zinapanda na zikishapanda hakuna siku ijulikanayo ya kushuka, sasa endapo muajiriwa ataingia mkataba wa kudumu, tuchukulie kwa kiwango cha sasa cha kima cha chini cha mshahara 145,000/-, mfanyakazi huyu atapata wapi fursa kirahisi rahisi kudai engezeko la mshahara wakati amejifunga mwenyewe kwa kukubali kufanya kazi maisha kwa mshahara huo?
Ingawa kanuni hii kiupande mwengine imempa fursa muajiriwa ya kuamua endapo atakataa basi asilazimishwe kuingia mkataba wa kudumu kama ilivyoelezwa katika kifungu nambari 4(2) lakini kwa nini watu wetu wakatae kufunga mkataba wa kudumu wakati ndio unaotoa usalama wa mfanyakazi katika sehemu ya kazi?
Hivyo maoni yangu yanakinzana na maamuzi haya na nahisi yamechukuliwa kwa haraka mno bila ya kuiangalia athari hii, hivyo ni vyema wahusika wazuie mpango huu kwanza, wafanye tena mabadiliko ya sheria hio kwa kuweka kipengele kitakachomlazimisha muajiri kumuengeza muajiriwa wake asilimia fulani ya mshahara kila ifikipa tarehe waliyoingia makubaliano ya mkataba, kama hilo halitawezekana niwashauri kwa ugumu wa maisha na mfumuko wa bei unaopanda bila kushuka ni vyema tuendelee na utaratibu wa zamani ili watu wetu wapate kuengezwa mishahara kwa kipengele cha kumalizika mkataba na kuingia makubaliano ya mkataba mpya.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa anwani ya barua-pepe: msheli@excite.com.
Filed under: JAMII Tagged: ajira, kazi, sheria, Zanzibar
