Jinichi Kawakami anaelezwa kuwa ndiye ninja wa mwisho kabisa duniani, akiwa mrithi wa moja kwa moja wa sanaa hiyo ya mapigano, ujasusi na mauaji iliyodumu kwa miaka 500.
Maninja wamefunzwa kufanya maajabu kwenye ujasusi na mauaji ya kimyakimya, na kawaida huwa hawaonekani hadi wawe wameshamaliza kazi yao, linaandika gazeti la Daily Mail la Uingereza.
Kiasili, maninja walikuwa wameajiriwa na wababe wa kivita wa Samurai kwa lengo la kufanya ujasusi, kuhujumu na kuuwa, na wanatumia majina, herufi na nambari maalum ambazo sasa zinafifia kutokana na maendeleo ya kisasa.
Hata hivyo zimebakia hadi sasa akilini na mikononi mwa Kawakami, mhandisi mwenye umri wa miaka 63 nchini Japan, akiwa chifu wa 21 wa dola ya kininja ya Ban iliyodumu kwa karne tano nzima.
Amefunzwa kuusikia hata mlio wa sindano inayoanguka chumba cha pili, kupotea kwenye mawingu ya moshi na hata kulikata koromeo la adui yake vipande 20 kwa kutumia ‘nyota ya mauti’ tu yenye ukubwa wa nchi mbili.
“Nadhani naitwa ninja wa mwisho kwa kuwa huenda kukawa hakuna mtu mwengine yeyote aliyejifunza mbinu zote ambazo hutolewa moja kwa moja na machifu wa uninja kwa karne tano zilizopita,” anasema Kawakami. “Maninja halisi hawapo tena!”
Kawakami alianza mafunzo ya sanaa ya mapigano iitwayo Ninjutsu akiwa na umri wa miaka sita kabla hajaanza kusomea chini ya utawala wa chifu Mazaso Ishida wa Kibuddha.
Ili kuweza kuongeza umakinifu wake, alikuwa anatumia masaa kadhaa kuuangalia mshumaa ukiwaka hadi mwenyewe ajihisi yumo ndani ya mshumaa huo.
Alifundishwa kupanda kuta, kujiangusha kutoka majengo au miti mirefu, kuruka angani na hata kupambana na wanyama wakali kama vile simba, chui na nyoka wakubwa.
Filed under: BURUDANI Tagged: Buddha, Japan, Kawakami, Ninja
