KILIO cha wapinzani cha miaka yote kwamba raslimali za nchi zinaibiwa ama kutokana na uzembe wa wale wanaopaswa kuzilinda au kwa wao kuamua kushirikiana na waporaji hao, huku wakiwa wameiangamiza nchi kiuchumi, kwa sasa kimeanza kufanyiwa kazi.
Tumeweza kuona kwamba kwa upande wa sehemu ndogo tu kwa kitu kinachoitwa makinikia, ambayo ni kama mabaki au takataka baada ya vitu vyenye thamani kuondolewa, Tanzania imepoteza matrilioni ya matrilioni ya shilingi. Sasa je, kwenye vitu vyenyewe vyenye thamani hali ikoje?
Kinachojionesha ni kwamba Rais John Magufuli ni kama ameamua kuokoka, kachoshwa na wizi wa kinyama ambao muda wote imefanyiwa nchi yetu chini ya ulinzi wa mfumo anaoutumikia, mfumo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao kwa muda wote kabla hajawa rais na mwenyekiti wa mfumo huo, yeye alikuwa ni mtu mdogo bila uwezo wa kupingana na mfumo uliomtumikisha.
Sasa kawa kinara wa mfumo wenyewe, kaamua kupingana wazi na wizi ambao mfumo wake uliukumbatia bila kujali majaliwa ya nchi na wananchi.
Ikumbukwe wakati Magufuli akiwa bado naibu waziri au waziri, aliwahi kulisemea hilo la mchanga wa madini kwamba nchi inaibiwa pesa nyingi sana. Vingunge aliokuwa nao wakamtania kwamba endapo yeye angekabidhiwa nchi angefanyaje, bila kuuma maneno aliwaambia kwamba angehakikisha wezi wote wanaoliibia taifa kwa kiwango hicho wanaitapika pesa hiyo.
Sehemu ya picha ya mazungumzo hayo inazunguka kwenye mtandao kwa sasa. Kumbe alichokifanya alikuwa nacho moyoni kwa siku nyingi, sio kwamba kakiota mara moja na kukitimiza. Tatizo ni kwamba hakuwa na uwezo wa kukitimiza wakati huo.
Kwa upande wa pili ni kwamba wapinzani walikuwa wanautaja wizi na uporaji huo kwa muda mrefu huku wakibezwa kiushabiki na watu wa mfumo ulioulinda uporaji huo, kwa hapa namaanisha mfumo wa utawala ambao ni wa CCM.
Leo hii baada ya kinara wa mfumo, Magufuli, kuamua kuokoka na kuukana uporaji ambao wapinzani wameupigia kelele kwa muda wote, wapinzani wanaona kama wamenyang’anywa tonge mdomoni! Hivyo wameamua kuruka na kwenda upande wa pili, kule kule walikokuwa wenye mfumo wa uporaji.
Baadhi ya wapinzani, kwa nguvu zote tena bila aibu, wanasema uporaji huo kamwe hauwezi kuguswa sababu tayari uko kwenye mikataba halali na ya kisheria!
Kidogo hiyo imewachanganya wananchi kiasi cha baadhi ya waliokuwa upande wa upinzani kuamua kuhamia upande wa chama tawala wakiuchukulia upinzani kama jitu lililoamua kuendeleza uporaji wa mali za nchi wakati CCM imeamua kuokoka na kuwa chama kilokole kinachojali maslahi ya nchi!
Ikumbukwe mtu akishaamua kuwa mlokole anayataja bila woga madhambi yote aliyokuwa akiyashiriki, huku akiyakemea na kuyalaani kwa nguvu zote. Hakuna awezaye kumuuliza kwamba mbona wewe umeyashiriki? Maana huyu tayari kaishayaacha na kuanza kuyalaani. Njia yoyote ya kupingana na mlokole ni sawa na kuukumbatia uovu kwamba usitoeke.
Kwa hiyo kwa sasa kinachotakiwa kufanyika ni kumpongeza Rais Magufuli kwa nguvu zote baada ya kuyakubali maono ya wapinzani na kuamua kujiunga nao, ambao kwa hapa nawachukulia kama walokole. Swali la kujiuliza ni kwamba kuna tatizo gani mtu akiamua kujitenga na uovu naye kuwa mlokole?

Tundu Lissu, mmoja wa mbunge wa upinzani anayehoji uhalisia wa hatua za Rais Magufuli na dhamira yake.
Isipokuwa kisiasa kuna mtazamo mwingine. Wapo wanaodhani kuwa Magufuli kadhamiria kuufuta upinzani kwa njia ya kuuona ukweli, kuusema na kuutekeleza. Bado mimi sioni kama hilo linawezekana. Upinzani ni lazima uendelee kuwepo.
Sababu bila upinzani haya yote yasingeweza kuonekana na kutekelezwa kama tunavyoshuhudia kwa sasa. Nadhani walio na imani kwa Mungu wanaelewa jehanamu. Insemwa kwamba kule ndiko Mungu anakowaweka waliomkosea, mashetani.
Haijawahi kutokea, kiimani, aliyewekwa jehanamu akabadilika kitabia na baadaye kuruhusiwa kuingia mbinguni. Sababu ni moja, ni kwakuwa kule hakuna upinzani. Wote walioko kule wanakubaliana na jambo moja tu kuuendeleza uovu.
Kwa mantiki hiyo upinzani hauwezi kufutika hapa nchini kwetu, maana hii bado haijageuka jehanamu. Ni lazima tuendelee kupingana na kukosoana katika kuipata Tanzania inayonufaika na neema iliyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Kitu pekee ambacho ningemshauri Rais Magufuli, ni kwamba kwa vile kaamua kuokoka na kuutawanya uovu wote ambao nchi yetu imefanyia kwa muda wote kiasi cha nchi zilizoumbwa zikiwa masikini wa kutupwa kugeuka matajiri wa kutufadhili huku sisi tukionekana ndio masikini wakati utajiri wote umetoka kwetu, watu wote waliohusika na uovu huo, bila kujali walikuwa na nyadhifa gani, wachukuliwe hatua kulingana na walivyoushiriki uovu huo.
Isiwepo sababu yoyote ya kumkingia kifua aliyeushiri uovu huo. Hata zile zinazodaiwa ni kinga zinatakiwa zibomolewe mara moja kusudi wahusika wakafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili ikithibitika walihusika kweli wakakabiliane na adhabu kulingana na uovu walioutenda.
Tanzania haitakuwa ya kwanza kutengua kinga dhidi ya uovu. Nchi ya China kwa mfano, iliwahi kutengua kinga aliyokuwa nayo, Jiang Qing, Mama wa Taifa hilo, mke wa Mao Zedong, akafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa. Nadhani hiyo ni moja ya maamuzi yanayoifanya China iongoze uchumi wa dunia kwa sasa.
Kama hilo litamshinda Rais Magufuli litaendelea kudhihirisha thamani ya upinzani, sababu wapinzani, kama kweli wamedhamiria, watalifikisha kwa wananchi ambao ndio wenye maamuzi ya mwisho, wakalitolee hukumu ya mwisho ya kuuondoa na kuupumzisha mfumo uliowaletea ukiwete ambao tayari mwenyekiti wa mfumo huo kaishaukiri uovu uliotendwa na mfumo wake.
Madai ya kwamba nchi itashitakiwa hayana mashiko yoyote, sababu baadhi ya waliopora utajiri wa nchi yetu tayari wamekuja na kuukiri uporaji huo wakisema kwamba yafanyike mazungumzo ya kukijua kiasi kilichoporwa ili wakirudishe. Upinzani daima.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo anayeishi Dar es Salaam na kupatikana kwa anwani ya barua-pepe prudencekarugendo@yahoo.com, simu nambari 0784989512
Filed under: SIASA Tagged: Accacia, barrick, dhahabu, Magufuli, mchanga wa madini
