MTU mmoja nisiyeelewa yuko upande gani kiitikadi, kama anafuata itikadi za upinzani au za chama tawala, kanipa wazo la kufikirisha kama mojawapo ya changamoto za kisiasa. Kanitumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yangu akisema hivi: “Kwa sasa CCM eti ndipo inakumbuka kero za wananchi!”
Katika kutafakari, nagundua jambo la kushangaza. Kinachonishangaza ni namna baadhi ya watu wanavyolinganisha pande hizi mbili, CCM na upinzani. Maana kuzilinganisha hizi pande mbili ni sawa na kumlinganisha mzee wa miaka 80 na kijana wa miaka 20.
Ni lazima kutakuwepo na tofauti kubwa inayoletwa na kupishana sana kwa umri wa watu hao, mzee na kijana. Mzee ni lazima atakuwa ameyaona mengi, amefanya mengi au kushindwa mengi kuliko kijana anayelinganishwa naye.
Kwa hiyo mzee kukubali kulinganishwa na kijana, hata kama hakutamka, ni lazima atakuwa amekubali kushindwa.
Tukiiangalia CCM na upinzani nchini, tutaziona tofauti za wazi zinazotokana na kupishana sana kwa umri. Ni sawa na tofauti zilizokuwepo kati ya chama cha TANU, kilichokuwa kinapigania uhuru na wakoloni waliokuwa wanatutawala.
Wakati TANU ikionesha athari za kutawaliwa, wakoloni walikuwa wakidai kwamba chama hicho hakijawafanyia lolote wananchi!
Wakati CCM kwa sasa inachezea kwenye umri wa miaka 60, upinzani ndio kwanza unachezea kwenye umri wa miaka 20. Ni tofauti kubwa sana ambayo kwa mtu mwenye aibu ni vigumu kutamani kulinganishwa na mtu aliyemzidi kwa kiwango hicho.
Kwa mantiki hiyo, anayekubali kulinganishwa na mtu aliyemtangulia umri kwa kiasi kikubwa namna hiyo, atakuwa anakiri kushindwa kuitumia vizuri tofauti hiyo ya umri kukifanya kile alichopaswa kuwa amekifanya.
Sababu mbali na uzoefu unaotokana na umri mkubwa ilionao CCM, chama hicho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, lakini upinzani ndio kwanza unataka upewe ridhaa ya kuonesha namna ya kuongoza.
Wakati huu chama hicho tawala kinajinadi kwa wananchi kikitaka kilinganishwe na upinzani huku kikihoji upinzani umewafanyia nini wananchi, kana kwamba kuna wakati kiliwahi kuona upinzani ukiongoza kama chenyewe kilivo!
Chama tawala kinasahau kuwa uzembe wake ndio umeuzaa upinzani. Maana bila uzembe huo sidhani kama kungekuwepo na mwananchi yeyote ambaye angekuwa anaufikiria upinzani kwa vile kila jambo lingekuwa katika mstari wake.
Ni yaleyale yaliyokuwa yakifanywa na wakoloni katika kuzikata makali harakati za TANU za kuwafumbua macho wananchi ili waione, kuitambua na pia kuidai nchi yao toka kwenye makucha yao.
Hivi kama kweli CCM ingekuwanao uwezo wa kuzisikiliza kero za wananchi ingekuwa inazitafuta hivi sasa baada ya miaka 60 ya uwepo wake? Kipindi hicho kisingetosha kuifanya ikawa inazielewa kero za wananchi kama mtu anavyolielewa jina lake?
Tunachoweza kusema ni kwamba CCM haikutaka kutatua kero hizo na sasa imejikuta imekwama, haiwezi tena kuzitatua. Kwahiyo inachokifanya ni kujaribu kukwamisha juhudi za upinzani za kuwafumbua wananchi macho ili kuziona kero zenyewe kiuhalisia.
CCM mara zote imejikita kwenye kauli za kuubeza upinzani na kuutukana. Tunaofuata hoja mara moja tunaelewa kwamba pale mtu anapopungukiwa hoja anaamua kupajazia kwa tusi. Lakini je, tusi linaweza likaziondoa kero zinazotajwa?
Kwa mtindo huo kweli tushawishike na kuamini kuwa CCM inatafuta kero za wananchi? Na kama kweli inazitafuta tukubali kwamba itazitatua kwa kuubeza na kuutukana upinzani?
Kero zilizoishinda kwa miaka 60 kweli itazitatua kwa mtindo uleule ambao umezifanya kero hizo zikarundikana mithiri ya Mlima Kilimanjaro?
Kwa nini tusiamini kwamba upinzani ndio unaweza ukazitatua kero hizo baada ya kupagundua zilikorundikana na kukielewa chanzo cha kuzifanya zikarundikana? Tuseme huyo ni mganga mpya aliyekuja na dawa mpya baada ya kulielewa tatizo.
Tuchukulie kwamba mtu anasumbuliwa na maradhi fulani kwa muda mrefu, mganga ambaye kashindwa kumsaidia kwa muda wote anakuja na dawa ileile iliyoshindwa kuleta nafuu akidai kuwa itasaidia, kusudi mgonjwa asiitamani dawa mpya inayoletwa na mganga mpya. Kukubaliana na mawazo ya mganga aliyeshindwa ni nini zaidi ya kujitakia donda ndugu au kifo?
Ieleweke kwamba huu sio wakati wa kuuziana mbuzi kwenye gunia, hii ni karne ya uwazi. Chama chenye umri wa miaka 60 hakiwezi kusema sasa hivi ndipo kinasikiliza kero za wananchi. Kwa umri kilionao na kwa namna kilivyojijenga, ikiwa ni pamoja na kutumia mabavu kuviondoa vyama vingine ili kibaki peke yake na kuendesha nchi kiimla, kilipaswa kuwa kinazielewa kero za wananchi hata zile ambazo hazijajitokeza.
Kujifanya kinaulizia kero za wananchi kwa wakati huu ni kutaka kukwepa aibu ya kukubali kushindwa.
Upinzani nchini, kama mleta mada alivyotaka iwe, ndio tunaoweza kuufikiria katika utatuzi wa kero za wananchi zilizotamalaki kwa sasa. Sio chama ambacho kimeshindwa kwa miaka 60.
Kwa wakati huu CCM isingekuwa inajifanya kusikiliza kero, ingekuwa inatafuta wapi paboreshwe baada ya kero zote kuwa zimefutika. Imeshindwa. Kwahiyo hayo ya kero za wananchi iviachie vyama vya upinzani ili navyo vioneshe ni kitu gani vinaweza kukifanya kuhusu kero hizi zilizorimbikizwa na CCM kwa zaidi ya miaka 55.
Nimalizie kwa kusema kwamba kinachofanywa na CCM kwa sasa ni sawa na muziki wa zilipendwa, kwa maana ya kwamba sio kitu kipya kinachooneshwa na chama hicho.
Kwa watu wenye kutafakari hiki ni kitu kilichopitwa na wakati na sasa kimekwama, sababu kilianza kufanyika tangu mwaka 1957 kilipoundwa chama hicho wakati huo kikijulikana kama TANU. Kujiunga na chama kingine, ASP, na kubadilisha jina bado havijaleta tija kwa wananchi kwa miaka 40 iliyopita.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii ni Prudence Karugendo, na anapatikana kwa anwani ya barua-pepe prudencekarugendo@yahoo.com na simu nambari +255 784 989 512
Filed under: SIASA Tagged: CCM, demokrasia, maendeleo, siasa, Tanzania, Uhuru, upinzani
