Mimi ni Profesa, nina PhD ya Political Science
Na ng’ombe wa maziwa, na magari ya kubeba kifusi
Nyumbani kwangu hakuna vitabu, kuna nyasi
Mara ya mwisho nilisoma Chuo cha Barkley
Waendako watu teule
Nimerudi kwetu, napanda tungule
Mwezangu aliyesomea uganga
Huamka nyumbani hana hata unga
Akisema, huoneka mjinga
Mdogo wangu ni mwalimu wa skuli
Anasomesha watoto mafedhuli
Kipato chake ni sawa na kuli
Profesa mwezangu aliyesoma GDR
Akarudi nyumbani, akiwa na ari
Ana maisha mabaya hatari
Na mwengine aliyekwenda Urusi
Akawa kwa pombe, hana nafasi
Yeye ni mkubwa, apigiwa hata pasi
Mimi profesa wa Milimani
Nishindaye hilala darasani
Mitaani naoneka kama nyani
Wanafunzi ninaowasomesha
Kila siku migomo waitisha
Wakidai posho halitosha
Kusoma kwao ni kwa kukariri
Na mitihani wafanya kwa shari
Kuwasimamia kwataka ujabari
Wakimaliza nje wanakaa
Mitaani tele wamejaa
Ukiwaona wabigwa na butwaa
Mimi profesa sifanyi research
Kwa kuogopa walio na nchi
Watanambia nawaweka uchi
Nikifanya huwa nadanganya
Ili wao wasije kunionya
Au kuninyima fungu la nyanya
Kusema naishi kiujanja
Ili nikwepe yao mikwanja
Au jela kwenda ionja
Nifanye nini, ndio suali
Nijibuni watu wa mbali
Unitoke huu udhalili
Mussa Shehe
24 Mei 2017
Bonn
Filed under: DARASA LA LUGHA Tagged: political science, profesa, uchumi
