Swahibu yangu mmoja amenipenyezea taarifa za baadhi ya wasomi vijana waliokuwa wakihudumu sehemu muhimu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupigwa dafrau la uhamisho, wakipelekwa maeneo ambayo hata hawana uzoefu nayo, huku nafasi zao wakipewa wale wanaoonekana kuwa ‘wenza wa watawala’.
Kama kweli linafanyika, hili si jambo kwenye ardhi ya nchi yangu, sehemu muhimu ya utamaduni wa utumishi serikalini, kiasi cha kwamba inapotokezea tafauti ndipo huwa la kushangaza. Katika mifano kadhaa, nafasi za ajira, vyeo, na hata fursa za masomo huambatana na ‘upendeleo’ wa ama mahusiano ya kifamilia, kisiasa, kiuzawa, kimkoa na hata kimapenzi; na sio uwezo wa kitaaluma.
Katika A Man Of the People, Chinua Achebe anamnukuu Chief Nanga, mwanasiasa asiye na uelewa mkubwa wa mambo lakini aliyefanikiwa kupanda ngazi za kisiasa kiujanjaujanja, akimuambia Odili, msomi aliyekuwa ndio kwanza ametoka chuo kikuu: “It doesn’t matter what you know, but whom you know”, yaani sio ukijuwacho, bali umjuwaye.
Achebe alikuwa akiyazungumzia ya Nigeria ya wakati huo, lakini ukweli ni kuwa hiyo ndiyo khulka ya kawaida kwa Afrika nzima, Zanzibar yetu ikiwemo. Kwa hakika, miongoni mwa sababu za kwa nini hivi leo zaidi ya asilimia 60 ya wasomi wa mataifa yetu wako nje wakiyatumikia mataifa mengine, ni hii.
Msomi naye ni mwanaadamu wa kawaida. Ana mahitaji yale yale waliyonayo wengine. Lakini kando ya mahitaji hayo ya kibinaadamu na kijamii, huhitaji pia kupata utambulisho wa taaluma yake angalau kwa maana nyepesi na ya kawaida ya kuachiwa kuutumia utaalamu wake aliousomea.
Bahati mbaya ni kuwa hayo hayapati, maana yetu ni nchi ambayo haijali kipi mtu anakijuwa, bali inajali nani ni jamaa yake katika mfumo wa utawala atakayeweza kumsaidia angalau apate kijisehemu cha kutarazaki, mkono uende kinywani. Anatakiwa asahau kabisa mchango wake kwa watu, asifikirie tena hishima yake, na apuuze ilimu yake.
Siandiki kujitetea mimi ambaye kwa sasa naishi ugenini kwa takribani muongo mzima. Hapana. Mimi siingii kwenye kundi la wasomi hao, kwa kuwa kwanza si msomi na, pili, angalau kwa muda wa miaka minane baada ya kumaliza masomo yangu, nilipata fursa ya kutumia taaluma yangu kwenye sekta ya umma na sekta binafsi. Kwa hivyo, naweza kusema utaalamu wangu ulihishimiwa.
Naandika kwa kuwa mimi mwenyewe niliwahi kufungika na mawazo kuwa msomi anayeihama nchi yake na kwenda kufanya kazi kwengine, huwa ni mpungufu wa uzalendo. Nilipingana na kisingizo kuwa kwetu kuna shida zinazomkwamisha msomi asiendelee, maana niliona huko kulikuwa mbinu tu ya kukimbia matatizo ambako hakusaidii utatuzi wake.
Hisabu yangu ilikuwa ni kiwango cha faida wanachokizalishia nchi wanazofanyia kazi. Ingelikuwa wapi leo Zanzibar, ikiwa faida hiyo ingelikuwa inazalishiwa kwetu? Kwa mfano, vijana wangapi wangemaliza digrii zao kwa kusomeshwa na wasomi wetu wa Kizanzibari? Au miradi mingapi wangeiandika kwa mwezi na kuzalisha mamilioni ya fedha katika kutekelezwa kwake?
Sasa nina maoni mengine kidogo, ingawa bado naamini kuwa mahala bora kabisa kwa msomi kuishi na kufaidika napo ni nyumbani kwao. Nimetanabahi kuwa si kweli kuwa kila anayeondoka kwao hana uzalendo na pia si kwamba kila aliyebakia nyumbani kuwa ndiye mzalendo wa kweli kwa nchi yake. Si kweli pia kuwa kila anayeondoka anazikimbia shida zilizopo na pia si kila aliyebakia anapambana nazo shida hizo. Hakuna uwiano baina ya mawili hayo.
Lakini nimejifunza pia kuwa kuna baadhi ya hawa waondokao wamekimbizwa kwa kuwa ‘hawatakiwi’ makwao. Wanakanwa na nchi zao wenyewe za uzawa, wakati ambao kuna wenzetu wanaowatafuta kwa udi na uvumba.
Kuna mifano mingi ya wasomi walioamua kurudi kwao baada ya masomo, ili waje wafanye kazi kwa ajili ya mataifa yao, lakini walipofika wakakumbana na kejeli za wanasiasa visirani, ambao kwao wao msomi ndiye adui yao nambari moja.
Zanzibar ingali na ugomvi usiokwisha baina ya watawala na wasomi, maana wawili hawa kila siku huyaona mambo kutokea vipembe tafauti. Wakati mtawala huyaona kutokea kipembe cha kisiasa na kutaka kila kitu kifanywe kwa kufuata muono huo, msomi huyaona kutokea kipembe cha kitaaluma na haja yake ni kuyafanya mambo kupitia muono huo.
Wakati mtawala anataka mtu amuendeshe, msomi anagoma kuendesheka na, hivyo, anakuwa khatari kwa nguvu za mtawala huyo. Siku zote watu hawa ni Lila na Fila. Henry Peter aliwahi kusema: “Education makes people easy to lead, but difficult to drive; easy to govern, but difficult to enslave” yaani ilimu huwafanya watu rahisi kuongozeka, lakini wagumu kuendesheka; rahisi kutawalika, lakini wagumu kuwatia utumwani!
Ubaya wa mambo kwa msomi, ni kuwa yeye hana nguvu za kufanya maamuzi ambayo yatafuatwa hapo hapo. Mtawala anazo nguvu hizo. Akisema mashine ya maji ifunguliwe Mjini ikafungwe Shamba ili Mhishimiwa Sana akapate kufunguwa mradi wa maendeleo huko, jambo hilo litafanyika siku hiyo hiyo hata kama ni kinyume na ushauri na matakwa ya kitaalamu.
Msomi akiinuka kulisemea hilo, huyo anaanza kuonekana ‘mpinga maendeleo’, na mchochezi. Na hayaishii hapo tu, huenda siku kumi zijazo akakuta kibarua kimeshaota majani. Kisa? Kukidhi mahitaji ya kitaaluma badala ya mahitaji ya kisiasa!
Akiepukana na hilo, msomi wetu anakumbana na jengine kutoka kwenye mfumo. Kwa mfano, mtu anarudi nyumbani baada ya kumaliza mafunzo ya Uhandisi chuoni, lakini akifika anakabidhiwa chaki akasomeshe Kiingereza kwa wanafumzi wa Darasa la Saba. Mwengine aliyesomea masuala ya kilimo, anapangiwa akawe fundi wa vinu vya maji. Wapi na wapi?
Lakini kwa kuwa watawala wetu wana ugomvi wa kudumu na wasomi hawa, basi si ajabu kuwa wanawafanyia haya makusudi ili washindwe na wapate la kuwadharaulia. Wawaite maprofesa uchwara, madaktari feki na majina mengine kama hayo ya tashtiti. Hiyo ndiyo mbeleko Zanzibar inayombebea msomi wake. Atadumuje?
Hayo ya msomi kupangiwa kazi kinyume kabisa na taaluma yake huenda yakawa madogo, lakini hebu fikiria mtu ambaye amepoteza miaka yake kumi kuchukuwa fani ya udaktari huko nje, anarudi nyumbani na kuamriwa kufunga vidonda wakati aliyechukuwa mafunzo kazini ya unesi ndiye aliyewekwa mkuu wa kitengo cha operesheni kwa kuwa yeye ni mfuasi wa chama kinachotawala, eti ni kumkomoa na usomi wake! Lipi tumfikirie atalifanya msomi huyu?
Lakini adui wa msomi wetu si mtawala pekee, bali hata jamii yenyewe anayokuja kuifayia kazi na kuishi nayo. Wengi wetu huwa tunadhani kupata fursa ya masomo ya juu kulimpa fursa nzuri ya kuyatengeneza maisha na hivyo kumpa pia wajibu wa kutusaidia kwa shida zetu zote za kibinafsi.
Kwetu, kuwa na digrii ya nje, kwa mfano, kunamaanisha kukunja mapesa na kuja nayo nyumbani. Anaporudi mikono mitupu, msomi huyu huonekana kayasaliti matarajio ya watu wake. Na akitaka ayatimize mahitaji hayo, basi lazima afanye kazi kuwatimizia haja zao. Na kazi ipi atakayoifanya hapa petu kuyakidhi mahitaji ya familia zetu kubwa?
Kwa hali hiyo, msomi wetu huwa amesukumwa ukutani, ambapo hana jinsi ya kung’amuka ila ajitolee muhanga kwa kufanya moja kati ya matatu haya: ama akae kupambana na mfumo kwa kucha na meno, au abadilike kwa mujibu wa mahitaji ya mfumo wenyewe au aikimbie nchi yake ya uzawa
Kila moja kati ya matatu haya yana gharama kubwa sana, na lolote analolifanya, hujikuta anajilaumu kwa kutolifanya jengine. Akiamua kubakia na kuukabili mfumo uliopo ni kujiundia maadui wengi na wenye nguvu kuliko yeye kutoka tabaka la watawala; akiamua kujibadilisha na kwenda sambamba na mahitaji ya mfumo uliopo, anasutwa na nafsi na maadili ya taaluma yake; la mwisho – kwa yule asiyeweza kuyastahamilia hayo yote – ndipo hulazimika kupahama pao na kwenda ugenini, anakoweza kufanya kazi na kupata visenti vya kuwasaidia watu wake, huku pia akiilinda hishima yake kitaaluma, lakini nako kunamnyima kwao na kunampotezea kizazi chake.
Bado nyumbani kwetu patabakia mahala pekee bora kwa msomi kuishi na kupafanyia kazi, maana sio tu anakuwa anakirejesha kile alichokopeshwa na jamii yake iliyotumia kila chembe ya nguvu yake kumsomesha, bali pia ndipo ambapo nafsi yake inafarijika akipatumikia. Lakini chini ya utaratibu wa nani umjuwaye na sio nini ukijuwacho, msomi wetu tunamtundika mbichi mbichi!
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 23 Mei 2017
Filed under: UCHAMBUZI
