Hapana shaka, kuwapoteza watoto wetu, walimu na dereva wao kwenye ajali ya hivi karibuni ya Arusha kulilishtua taifa. Tumeumia kama jamii na kupatwa na simanzi kama wazazi.
Lakini wakati joto la majonzi haya likianza kufifia, sasa ni wakati wa kugeukiana na kuulizana maswali magumu. Kwanza na kwa uwazi kabisa, natofautiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliyehitimisha taarifa yake ya ajali hiyo kwenye ukurasa wake wa Facebook kwa kauli ya “BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA”, kauli ya kukariri, kauli ya kimazoea. Yaani Mungu huyu alingoja watoto watoke shuleni, akawasubiri njiani pale, kwenye korongo lile ili awatwae! Hapana, si kweli!
Ni kweli tumeumia, lakini tuache mazoea, kwamba watu watakufa, tutapokea taarifa, tutashtuka, halafu tutaomboleza kwa kusema BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, kisha tuendelee na shughuli zetu tukisubiri Bwana awatwae wengine.
Walikufa watu kwenye MV BUKOBA mwaka 1996, MV SPICE kule Nungwi Zanzibar mwaka 2011, yametokea maajali mengi yasiyo na vichwa wala miguu, nasi kila mara tunalia, tunasema “Bwana alitoa” kisha tunaendelea na maisha! Hatuambiani ukweli wala hatuko tayari kuusikia. Tunamsukumizia tu Mungu.
TUANZE NA COSTA YA ARUSHA
Tunaambiwa walitumia basi dogo aina ya Costa. Hapa tunaweza tusijadili juu ya vifo bali idadi ya vifo. Tunaambiwa wamefariki takribani watu 35, ukimuondoa dereva tutazungumzia abiria 34 kama hiyo ndio idadi ya vifo. Je, hakukuwa na uwezekano wa kupungua vifo hivyo? Je, ni kweli vifo hivyo vilisababishwa na gari kuanguka tu au hata waliokuwa hai walikufa kwa sababu ya kubanana? Angalia gari iliyopata ajali, ni TOYOTA COSTA, kwa hesabu za haraka (ruksa kunirekebisha) ina uwezo wa kubeba abiria (labda) wasiozidi 25-28, akiwemo dereva wakiwa wamekaa kwenye viti. Idadi ni vifo 32, hao wengine 7 walikuwa wamekaa wapi?
Hivi karibuni, nilikuwa natuma taarifa na picha kwenye ukurasa wangu wa Facebook nikieleza namna ambavyo magari mengi ya wanafunzi yanavyobeba watoto wetu kwa kuwarundika kama mizigo humo. Wengine walidhani najifurahisha tu, lakini sikuishia Facebook, bali nilifunga safari mpaka shule moja kwenda kuwakemea (na niliwakemea kwelikweli), na kuwataka waache tamaa. Sasa hapa sisemi kuwa hayo ndio yametokea Arusha, nimesema tutafakari upande wa pili wa ajali hii!
TUSIMSINGIZIE MUNGU
Tusikimbilie kujitetea au kujivua lawama kwa kusema Bwana ametwaa katika kila ajali, inawezekana (inawezekana) ni uzembe na upuuzi wetu kama jamii unatawaa maisha ya watu kwa mambo mengi hapa nchini. Mpaka leo naamini kuna magonjjwa kama kipindupindu ni ya kujitakia huku tukisema Bwana ametwaa. Kwa nini nasema tusimsingizie Mungu?
Kwanza, tuna magari mabovu. Naomba wataalamu waende barabarani wakafanye utafiti, waende kwenye mashule wakafanye utafiti, magari mengi sana ni mabovu, angalia magari (vi-hiace) vinavyofanya safari ndani ya jiji la Mbeya, mengi mabovu, kutembea barabarani hakutoshi vipi kuhusu afya za wasafiri, viti wanavyokalia nk?
Pili, tuna barabara mbovu. Hili halina ubishi hata kidogo. Na sio tu ni mbovu, hata hizo nzima ni nyembamba sana na zingine huwa za shida kipindi hiki cha mvua. Angalia mazingira ya eneo ambalo basi hilo la wanafunzi limepatia ajali. Je, hakuna uwezekano wa kuwa na barabara zinazoweza kupitika wakati wa masika na kiangazi bila shida? Je, kwa hali ya nchi yetu tunahitaji zaidi ndege/treni kuliko barabara?
Kamwe sikosoi maamuzi ya serikali kununua ndege, bali najaribu kuona kipi kingeliweza kutekelezwa mwanzo! Nina uhakika nchi hii inahitaji zaidi madaraja, barabara na upanuzi wa barabara kuliko usafiri mwingine.
Tatu, tuna madereva wasio uwezo. Binafsi sijatembea sana duniani, lakini nadhani nchi hii ina madereva wa ajabu kuliko kwingine kokote. Hivi karibuni nilikuwa nchini Sweden, huko niliambiwa kupata leseni ya udereva ni sawa na kutafuta PhD kwenye Chuo Kikuu cha Mlimani, na kwamba ukija kunyang’anywa kisha kuipata tena utazamie sana kudra za Mungu. Nikajiuliza, hivi hali kwetu hali ikoje.
Angalia madereva wetu wa daladala, wengi ni wababe, jeuri, viburi na sifa zingine zisizo za kiungwana, nina mashaka sana ikiwa hawa ndio wangekuwa madereva wa mabasi ya mikoani. Naogopea hata kufikiria!
Lakini hata hawa wa mabasi ya mikoani nao kwa nini wazingatie alama za usalama barabarani kwa kuogopa tochi za askari barabarani? Kila kitu kiko wazi, kwa nini kama wako sawa hawataki kufuata alama hizo? Kwa nini hawataki kufuata miiko ya kazi hiyo? Rejea ajali ya CITY BOY kule Nzega mwaka jana, rejea ajali mbali mbali, kisha uliza abiria yaliyotokea kabla ya ajali. Kisha watu wakifa, tunasema BWANA AMETWAA!
Nne, tuna askari wala rushwa barabarani. Hapa nitasimulia mkasa ambao sijausahau na nadhani kamwe sitausahau maishani. Mara moja nilikata tiketi Bukoba ili niwahi ndege Mwanza kunileta Dar es Salaam. Wakati huo kulikuwa kumetokea ajali mbaya sana ya basi la MOHAMED TRANS karibu au maeneo ya KATORO. Nilishuhudia kwa macho yangu askari aliyekuwa anakagua magari pale katoro alisimamisha basi letu, ndani lilikuwa chakavu sana, na wakati anapanda ngazi, utingo wa basi hilo alimkabidhi shilingi 2000 bila kusema chochote, na yule askari akarudia mlangoni.
Kama gari ingekuja kuua watu huko mbele, Watanzania wangelisema Bwana Ametwaa, kumbe askari mmoja kauza roho za watu kwa shilingi 2000. Njia ya kutoka Singida mpaka Babati nilikuwa nashuhudia kwa macho yangu askari wakipewa mpaka shilingi 1000 tu, kisha kuachana na madereva waliovunja sheria za barabarani, ikiwemo mwendo wa ‘kasi ya ndege’ ardhini.
Tano ni uoza wa jamii yetu wenyewe. Hapa naweza kudiriki kusema kuwa pengine jamii yetu ina mchanganyiko wa unafiki na ubinafsi. Wakati wale madereva wa CITY BOYS wanafanya ile mizaha ya kifo, kuna abiria walikuwa wanashangilia wasijue wanaaga dunia kwa nderemo, huku tuliobaki tunasema BWANA AMETWAA!
Niliwahi kupanda basi pale Ubungo kuelekea Tanga kikazi. Nilitumwa na bosi wangu ambaye sasa anafanya kazi nchini Ujerumani. Gari lilijaza abiria kiasi kwamba wengine walikalishwa kwenye korido ya basi. Kitendo cha mimi kuhoji nilishushwa kwenye basi mbele ya askari wa usalama barabarani pale stendi ya Maili Moja, Kibaha, na waliochangia zaidi ni abiria wenzangu ambao walisika wakisema kifo ni mipango ya Mungu!
Hitimisho
Nchi hii ina matukio mengi yanayogharimu uhai wa watu wake sio kwa sababu Mungu amependa au Mungu anatwaa, bali kwa kuwa tumejiandalia hivyo. Mfano hai ni UGONJWA WA KIPINDUPINDU. Hivi kweli suala la vifo vya kipindupindu ni Mungu anatwaa watu wake? Kweli?
Sasa kama kilivyo kipindupindu, hata ajali nazo kwa sehemu kubwa sio Mungu anayetwaa. Mengi yanayotokea yanaweza kudhibitiwa tukitaka. Tukipanga na kuweka mikakati na kuamua kutekeleza, Mungu hatatutwaa kinamna hii, maana si yeye anayetutwaa, bali ni makosa yetu wenyewe.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Mchungaji Daniel Mustafa Gingo.
Filed under: JAMII Tagged: ajali, arusha, barabara, rushwa
