Visiwa vya Zanzibar vimegubikwa na minong’ono na khofu kubwa baada ya Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiagiza Shirika la Ugavi wa Umeme ya Tanzania Bara (TANESCO) kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni makubwa kwa shirika hilo, ikiwemo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Rais Magufuli aliitoa kauli hiyo tarehe 5 Machi 2017, wakati akizungumza kwenye uwekaji wa jiwe la msingi la kituo kipya cha TANESCO mkoani Mtwara, ambapo alisema kuwa tasisi zote za umma zinapaswa kulipa madeni yao, la sivyo zitakatiwa umeme.
“Msiogope mnapaswa kukata huduma hii kwa taasisi yoyote ambayo hailipi bili zake…Ninaambiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijalipa shilingi bilioni 121. Nyinyi (TANESCO) si wanasiasa. Mnapaswa kuzingatia majukumu yenu ya kitaaluma…kata huduma ya umeme. Nimesema hata kama ni Ikulu , polisi, jeshi ama shule , hakuna mwenye deni anayepaswa kuachwa… TANESCO haiwezi kuboresha huduma kwa sababu ya madeni ya serikali yasiyolipwa” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kauli hiyo, ndipo joto la khofu ya kuja kukosekana kwa huduma hiyo likapaliliwa, kumwagiliwa maji na hatimaye likameya na kupanda zaidi baada ya TANESCO yenyewe kutoka hadharani kwanza kwa kusahihisha deni ambalo halijalipwa na SMZ kupitia Shirika lake la Umeme (ZECO) kwamba ni shilingi bilioni 127.8 na sio bilioni 121 bilioni alizosema Rais Magufuli na, pili, TANESCO ikatoa notisi ya siku 14 kuanzia tarehe 8 Machi 2017 kwa ZECO iwe imeshalipa deni hilo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Tito Mwinuka, shirika lake linaidai ZECO pamoja na wateja wengine jumla ya shilingi bilioni 275, ikimaanisha kuwa ZECO peke yake inadaiwa takribani nusu ya deni lote la jumla la TANESCO.
“Tunadai kiasi kikubwa sana cha fedha kutoka kwa wateja wakubwa na wadogo wadogo, mpaka ZECO. Hivyo tunatoa notisi ya siku 14 kuanzia leo (Machi 9), walipe deni lao, kwani baada ya hapo tutasitisha huduma pamoja na kuchukua hatua nyingine za kisheria,” alisema Dk Mwinuka.
Wakaazi wa visiwa vya Zanzibar wana wasiwasi mkubwa sana, kwamba huenda umeme kutoka Tanzania Bara ukazimwa kweli endapo deni halikulipwa. Katika dunia ya sasa ya matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia, licha ya umasikini wa visiwa hivi, huduma nyingi zinategemea umeme.
Ni wasiwasi huu ndio uliokuwamo kwenye suali aliloulizwa Dk. Ali Mohammed Shein, ambaye kama anavyojirejea mwenyewe mara kwa mara kwamba ndiye rais wa Zanzibar, aliporudi ziara ya kikazi nchini Indonesia siku moja baada ya TANESCO kutangaza muda wa mwisho wa serikali yake kulipa deni.
Lakini mimi nimefadhaishwa, kushangazwa na kusikitishwa sana na kauli ya Dk. Shein kujibu hili la kitisho cha kukatiwa umeme na Tanzania Bara. “Serikali yangu haitishiki na tishio la kukatiwa umeme na iko tayari kutumia vibatari na deni linalodaiwa sio la leo wa jana”, alisema Dk. Shein.
Kauli hii ya Dk. Shein haikujibu wala kuondoa khofu na shaka zilizotawala visiwani, bali ni ya mzaha, kukatisha tamaa na inayopalilia zaidi khofu ya wananchi.
Labda Rais ametoa kauli hio kwa kuchukuwa kumbukumbu ya kukaa miezi mitatu bila ya umeme kipindi cha awamu ya mwisho ya Rais Amani Karume. Lakini ikumbukwe mwaka ule ilikuwa ni bahati mbaya, ndio maana raia walikubali kwa shingo upande kukaa miezi mitatu bila ya umeme. Haya ya mara hii ni ya makusudi. Ni serikali anayoiongoza yeye inayodaiwa. Wananchi wanalipia huduma hii kwa wakati na kwa gharama kubwa. Hivyo si busara kwa yeye kutoa kauli hii, ikizingatiwa kwa sasa kila kitu Zanzibar kinategemea nishati ya umeme.
Kwa kuwa anajiita rais, Dk. Shein anapaswa kutambuwa kwamba yeye ndiye mwenye jukumu kuu la kuwahakikisha Wazanzibari na watu wengine wanaoishi katika visiwa hivi wanapata mahitaji na huduma zote muhimu kwa maisha yao ya kila siku zinakwenda mbele bila vikwazo cha aina yoyote, na endapo kutatokea hitilafu yoyote, basi ni yeye mwenye dhamana ya kuhakikisha kwamba hitilafu hizo zinaondoka.
Yote haya ni kwa sababu yeye ndiye aliyekalia kiti cha kiongozi mkuu wa nchi, yeye ndiye aliyekauka kifua akinadi sera za Chama chake cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni za uchaguzi, akiizunguka Zanzibar nzima kuanzia mijini hadi mashamba, na hata aliposhindwa kwenye uchaguzi halali wa tarehe 25 Oktoba 2015, yeye na chama chake wakalazimisha arejee madarakani kwa njia wanazozitaka wao.
Kama nilivyosema, licha ya umasikini wake, Zanzibar ni moja ya nchi zilizopokea ipasavyo wigo wa sayansi na teknolojia na sasa kila jambo lake linategemea nishati ya umeme na hivyo maisha ya watu wengi yamejikita katika shughuli zinazotegemea umeme.
Nakubalina na Dk. Shein kwamba tutatumia vibatali kuweza kumurikia majumbani mwetu, lakini je kibatali hicho kitaweza kuwasha friza kuhifadhia kitoweo? Je, kibatali kitamuwezesha fundi anayechoma mageti kuwasha mashine yake? Je, kibatali kitamuwezesha sekretari kuchapa barua? Je, kibatali kitaweza kuwasha mashine za kuuzia mafuta watu wawahi makazini? Je, kibatali kitatoa baridi sehemu ya kuhifadhia maiti? Je, kibatali kitawasha taa ya sehemu ya upasuaji hospitalini?
Filed under: Masuala ya Kisiasa Tagged: Ali Mohammed Shein, CC;. Zanzibar
