Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo (Taifa), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Mstaafu Francis Mutungi, ana chuki binafsi na chama chake na ndio maana amekuwa akikiandama tangu yeye na wafuasi wake walipoamuwa kuhamia chama hicho mwezi Machi 2019.
Akizungumza kwenye mkutano wa ndani huko Tunduru hivi leo (Julai 21), Maalim Seif aliwaambia wanachama na viongozi wa chama hicho kwamba tangu Machi mwaka jana hadi sasa, ACT Wazalendo imeshapokea zaidi ya barua sita za tuhuma na lawama kutoka Ofisi ya Msajili, zikiwa na madai mbalimbali ya ukiukwaji wa kanuni, sharia na taratibu bila kuwa na ushahidi wowote, na hata kwa matukio ambayo yanafanywa pia na vyama vingine ambavyo kamwe havichukuliwi hatua hiyo.
“Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, ni dhahiri hakipendi chama cha ACT Wazalendo. Tangu tulipojiunga chama hichi mwaka jana, tunapokea mlolongo wa barua. Tukiangalia wenzetu wanafanya yale yale au zaidi ya yale, lakini hawaulizi. Yeye ni ACT Wazalendo tu, basi.”
Wiki iliyopita, Ofisi ya Msajili iliwaandikia barua yenye kurasa sita ACT Wazalendo ambayo iliorodhesha yale inayosema ni makosa yaliyotendwa na chama hicho tangu mwaka 2018, huku ikisema kuwa haikuridhika na majibu ambayo chama hicho kimekuwa kikiyarejesha.
Barua hiyo pia inatishia kuwa itakichukulia chama hicho hatua katika siku chache zijazo, onyo ambalo wengi wamelifasiri kuwa ni kitisho cha kukifuta chama hicho ama kukizuwia kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
Maalim Seif amesema sababu kubwa ya Jaji Mutungi kuchukuwa hatua hiyo ni kile alichokiita “nia ovu” kwa chama hicho, akimtuhumu kwamba “anafuata maelekezo ya Chama cha Mapinduzi” ambacho kinahofia ujio wa aliyekuwa waziri wa masuala ya kigeni wa Tanzania, Benard Membe, ambaye tayari ameshatangaza nia ya kuwania urais wa Muungano.
Barua hiyo ya Ofisi ya Msajili kwa ACT Wazalendo ilivujishwa kwenye magazeti na mitandao ya kijamii kabla ya kuwasilishwa rasmi kwenye ofisi za chama hicho.
“Msajili hana uwezo wa kukifuta chama chetu. Sheria inamzuwia. Tena sheria hiyo ameiandika mwenyewe. Njooni kwenye ACT Wazalendo. Asiwatisheni huyu.” Alisema mwenyekiti huyo.