Chake-Chake, PEMBA: Chama cha ACT-Wazalendo kimeapa kuwachukulia hatua za kinidhamu wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho watakaobainika wakijihusisha na vitendo vya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa leo (Juni 30) na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akizungumza na wanachama wa mkoa wa Chake Chake kichama, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba kuimarisha chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Mwenyekiti huyo, ambaye juzi Jumapili (Juni 28) alitangaza rasmi nia yake ya kuomba ridhaa ya kuwania urais wa Zanzibar kwa mara ya sita mfululizo, amesema misingi ya chama cha ACT-Wazalendo ni ukweli na uwazi sambamba na kutetea demokrasia, hivyo endapo wataacha vitendo vya rushwa vifanyike ndani ya chama hicho, wanachama wenye sifa watakosa haki yao ya kuchaguliwa.
“Nikiwa kama Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, nasema wazi kuwa hatutomvumilia kiongozi au mwanachama yeyote atakayebainika akijihusisha na rushwa. Tutamchukulia hatua ya kumuondoa moja kwa moja,” alisema.
Katika mkutano huo, Maalim Seif alibainisha kuwa tayari ACT-Wazalendo imeshaandika barua na kuzipeleka kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Tanzania Bara (TAKUKURU) na ile ya Zanzibar (ZAECA) ambayo inaeleza ratiba yote ya mchakato wa kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ili taasisi hizo zimulike wagombea watakaojihusisha na rushwa sambamba na kuwachukulia hatua.

ZEC, Wakala wa Usajili matatani
Katika hatua nyengine, Maalim Seif ameilaumu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii kwa kuwanyima wananchi wa Zanzibar vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambavyo hutumika pia kwenye zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Makamu huyo wa zamani wa rais alidai kitendo hicho cha kunyimwa wananchi vitambulisho ni agizo maalum kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kupunguza idadi ya wapigakura, hususan kisiwani Pemba, ili kukwepa kile alichokiita “aibu” ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambapo alisema alimshinda mpinzani wake, Dk. Ali Mohammed Shein, kwa zaidi ya kura 25,000.
“Leo sote tunashuhudia hapa Wazanzibari wengi wamenyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi. Hili halikufanyika bure. Hizi ni njama za muda wote zinazopangwa na kuratibiwa na CCM ili wananchi hususan wa Pemba wasipate haki yao ya kupiga kura kwani mara zote Pemba huambulia patupu,” aliongeza.
Hata hivyo, Maalim Seif amesisitiza kuwa pamoja na njama zote hizo, CCM haiwezi kupata hata asilimia 10 kisiwani Pemba kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020, huku akisisitiza kuwa “safari hii, ACT itaulinda ushindi wake Bara na Visiwani.”
Mapema, Katibu wa Idara ya Habari na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani alisema kufuatia wananchi wengi na wanachama wa chama chake kukosa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, uongozi wa chama ulikutana na Kiongozi Mkuu wa Vitambulisho pamoja na Mwenyekiti wa ZEC na kuwataka watoe vitambulisho hivyo na kuishauri Tume ya Uchaguzi kuacha kuandikisha mpaka pale wananchi wote watakapopata vitambulisho.
“Licha ya mazungumzo yetu kuchukuwa muda mrefu, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahmoud alikataa ushauri wetu na kusisitiza kuwa ataendelea kuandikisha,” alisema Bimani, akiongeza kuwa anashangazwa na ukimya wa Dk. Shein katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, ambapo wananchi wengi wamenyimwa haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa kunyimwa vitambulisho, licha ya yeye kuahidi mwanzoni kuwa angelihakikisha kila mwananchi mwenye sifa ya kupewa kitambulisho, anapewa haki hiyo.
“Siku ya uzinduzi wa utolewaji wa vitambulisho na yeye kukabidhiwa kitambulisho chake, Dk. Shein aliiambia mamlaka inayohusika kuwa wananchi wasihangaishwe bali wapewe vitambulisho vyao, lakini leo hii tunaona hakuna hata moja lilifanyika na yeye yuko kimya,” alisema katibu huyo wa habari na uenezi wa ACT-Wazalendo.
Kuhusu wananchi hao walionyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi hadi sasa, Bimani aliutaka uongozi wa mkoa wa Chake Chake kichama kuorodhesha majina ya wanachama wote wenye risiti na ambao hawajapatiwa vipande hivyo muhimu, ili chama kiweze kuchukua hatua.
Vile vile ameitaka ZEC kwa kuwa inao muda wa kuwapa wananchi vitambulisho na kuwaandikisha, ifanye hivyo haraka ili wananchi wapate haki yao ya kuchaguwa viongozi wanaowataka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Chake Chake, Yussuf Salum Khamis, alisema siku za CCM kubakia madarakani zinahesabika.
“Uongozi hapa umejipanga vyema kuhakikisha tunawashawishi wanachama na wananchi wa Pemba kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji kura ili kuiondoa CCM madarakani.”
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad, anaendelea na ziara yake ya ujenzi wa chama kisiwani Pemba, ambapo Julai 1 atakuwa Mkoa wa Micheweni kichama na Julai 2 atamalizia ziara yake Mkoa wa Wete.