Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Muungano unalindwa kwa nguvu

$
0
0

RAIS Ahmed Abdallah wa Comoro aliyeuliwa Novemba 26, 1989 na askari wa kizungu aliowakodi mwenyewe, anakumbukwa kwa mengi.  Kuna wanaomuona kuwa shujaa kwa kuthubutu kuikabili Ufaransa na kutangaza kuwa Comoro ni taifa huru Julai 6, 1975.

Wapo pia wanaomlaumu kwa kuwa sababu ya kumeguka kwa kisiwa chane cha Mayotte ambacho hadi leo kimo mikononi mwa Ufaransa.

Mara yangu ya kwanza kukutana naye ilikuwa nyumbani kwake jijini Paris, Ufaransa.  Alikimbilia kuishi huko baada ya kupigwa pute na kupokonywa urais na Ali Soilih Agosti 3, 1975. Abdalla alipinduliwa na askari wa kukodiwa waliokuwa wakiongozwa na Mfaransa Bob Denard.

Askari haohao wa Bob Denard ndio waliomrejesha Abdallah madarakani Mei 13, 1978, na ndio hatimaye waliomuua.

Na Ahmed Rajab

Aliyenipeleka kwa Abdallah alikuwa Amin Ali Moumin al Ahmed, aliyekuwa mwanafunzi wa mahusiano ya kimataifa na ambaye baadaye alikuwa balozi wa muda mrefu wa Comoro katika Umoja wa Mataifa. Amin, aliyekulia na kusoma Zanzibar, alikuwa Mzuwani aliyezaliwa kisiwa cha Nzuwani (Anjouan) ambako ndiko alikozaliwa Abdallah.

Tulikuwa na mwenzetu wa tatu aliyefuatana nasi kwenda kwa Abdallah. Alikuwa Nasor Malik, mtangazaji wa BBC niliyekwenda naye Paris kuandaa vipindi maalum vya BBC.

Ingawa ilikuwa ndio mara yetu ya kwanza kukutana, Abdallah akizungumza kana kwamba tukijuana kwa muda mrefu. Dhihaka zake zilivifanya vinywa vyetu vitanuke kwa vicheko.

Pamoja na mizaha Abdallah alikuwa na mazito pia ya kuhadithia.  Kwanza alitupa siri kwamba katika muda wa miezi sita atarudi Comoro.  Hakutuambia atarudi vipi na kusema kweli mimi nilimsikiliza bila ya kumuamini.

Lakini kurudi alirudi, na alirudi mapema zaidi ya alivyotuahidi. Alirudi baada ya miezi mine na si sita. Na siku aliyorudi alinambia kwa simu kwamba anarudi lakini aliniomba niibanie siri hiyo mpaka atapowasili salama Moroni.  Sikumvunja.

Alinikumbusha yaliyowahi kuwafika Wasudan wawili waliokuwa wanarudi Sudan kutoka London baada ya Rais Ja‘ffer Nimeiry kupinduliwa na Wakomunisti Julai 19, 1971. Mmojawao Luteni-Kanali Babakr al Nur Osman alikuwa ndiye aongoze serikali ya kimapinduzi. Wa pili alikuwa Meja Farouk Hamadallah aliyekuwa awe mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, ambalo ndilo lililokuwa litawale.

Wote wawili walikuwa London wakitibiwa Nimeiry alipopinduliwa kwa muda mfupi.  Kosa walilolifanya walipokuwa wanarudi Khartoum ni kutangaza kwenye mkutano na waandishi wa habari London kwamba wanarudi Khartoum kwa ndege ya shirika la ndege la Uingereza la BOAC.

Libya ilipozipata habari hizo iliilazimisha ndege ya BOAC ilipokuwa juu ya anga ya Libya itue Benghazi. Hamadallah na Osman walikamatwa na baadaye wakasafirishwa kupelekwa Khartoum ambako Nimeiry akiwa amerejea madarakani aliwaua.

Abdallah hakutaka yaliyowafika kina Hamadallah yamfike yeye ndipo aliponiomba nisiitangaze safari yake ya kurudi Moroni.

Jambo jengine alilotuambia na lililokuwa likimkera bila ya kiasi ni kuhusu mipango ya hasimu wake Rais Ali Soilih kuifanya Comoro ijiunge na Tanzania. “Hata jina tayari wanalo. Wanataka kuiita nchi hiyo mpya Tanzacomo,” alisema Abdallah.

Baadaye katika tafiti zangu niligundua kwamba kweli Soilih alitaka Comoro ijiunge na Tanzania.  Alimpeleka mjumbe wake muhtasi (jina lake nalihifadhi kwa sasa) kwenda kuonana na Rais Julius Nyerere wa Tanzania kumwelezea pendekezo hilo la Soilih.

Lakini mjumbe huyo aliyekuwa mzaliwa wa Zanzibar alipofika Dar es Salaam alishauriwa na baadhi ya Wazanzibari waliokuwa na vyeo vikuu katika serikali ya Tanzania arudi kwa Soilih na kumtaka aachane na fikra hiyo. (Majina ya Wazanzibari hao pia nayahifadhi kwa sasa hasa kwa vile mmojawao ana azma ya kuandika kitabu kizima kuhusu utumishi wake serikalini na amenieleza kuwa kadhia hiyo ataizungumzia kwa urefu kwenye kitabu chake.)

Kadhia hiyo ya Ali Soilih na Tanzania niliikumbuka Jumamosi iliyopita siku iliyotimu miaka 55 kamili tangu uundwe muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Katika muda wote huo Comoro ya Soilihi ndiyo  nchi pekee iliyokuwa na shauku ya kutaka kujiunga na Muungano huo. Nyingine kama Uganda (chini ya Milton Obote) na Zambia (chini ya Kenneth Kaunda) ambazo ungetaraji zingejiunga na Muungano huo ziliukwepa licha ya usuhuba wa marais wao na Mwalimu Nyerere.

Visiwani Zanzibar mwaka huu hapakuwa hata na kongamano moja juu ya Muungano seuze sherehe za kuutukuza. Kwa ninayoyasikia sidhani kama zingefanywa zingehudhuriwa na watu wengi. Labda kwa kulazimishwa.

Hata Tanganyika ambako wananchi wako tafrani kwa ugumu wa maisha na ukali wa watawala siku hizi watu wanazidi kubadili mawazo  kuhusu Muungano. Hawauungi mkono kama zamani.  Wasomi, wakiwemo Tundu Lissu, Zitto Kabwe na wengineo wameudurusu upya Muungano tangu chimbuko lake hadi sasa na wanakubaliana na Wazanzibari kwamba sio Muungano wa haki.

Suala la Muungano wa Tanzania ni suala lenye kuwaunganisha Wazanzibari wa itikadi na mirengo tofauti ya kisiasa.  Ni wachache mno miongoni mwao wenye kuubariki.  Wengi wanausema kuwa ndio uliosababisha mamlaka ya Zanzibar yaporwe na Tanganyika kwa kisingizio cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Yanayozidi kuwatia hofu ni vitendo na matamshi ya baadhi ya viongozi wa serikali ya Muungano yenye kuashiria nia yao ya kuibadadili rasmi hadhi ya Zanzibar isiwe nchi na badala yake iwe mkoa tu wa Tanzania.

Kwa hakika, kwa hali ya mambo ilivyo Zanzibar imemezwa na Tanganyika.  Ina sifa zaidi za kuwa mkoa badala ya kuwa taifa kamili. Na ukiufanyia Muungano huo uchambuzi wa kina utajikuta unakubaliana na wenye kuhoji kuwa Zanzibar imegeuzwa na kuwa koloni  la Tanganyika.

Suala hilo la Muungano limegeuka. Badala ya kuwa suala la umajumui wa Kiafrika limekuwa suala la kikoloni.  Ndio maana baadhi yetu tulioishi katika enzi za ukoloni hatushangazwi tunapowaona viongozi wa Tanganyika wakiwa na kibri kilekile kama walichokuwa nacho wakoloni katika sehemu mbalimbali duniani.

Viongozi wenye kutumia vitisho na wenye kujinata kwamba wataulinda Muungano kwa nguvu zote wanajikita juu ya mantiki yaleyale waliyokuwa wakiyatumia wakoloni wa kale. Watawala wanaposema kuwa Tanzania ni taifa moja wanaukana ukweli kwamba Tanzania ni Muungano wa mataifa mawili: Tanganyika na Zanzibar. Lakini wanasema hivyo kujaribu kuuficha ukweli ulio wazi. Wanatumai kwamba kwa kusema hivyo Zanzibar itatoweka kama wanavyokusudia.

Kweli Muungano upo na unalindwa. Lakini unalindwa kwa nguvu. Nguvu hizo ni za dola. Haulindwi kwa mapenzi na ridhaa ya Wazanzibari.  Hapo ndipo penye tatizo.

Tunachoweza kukubaliana nao watawala wa Tanganyika ni kwamba kweli wanaulinda Muungano na watajaribu kuendelea kuulinda kwa nguvu lakini madhali wananchi hawautaki na madhali wao watawala wanaendelea kufanya ukaidi wa kutoyasikiliza matakwa ya wananchi pataendelea kuwako migogoro na mivutano kama tulivyoshuhudia sehemu nyingi duniani baina ya watawala wa kikoloni na watawaliwa.

Miongoni mwa hao wachache wengi wao huwa na msimamo wa kuutukuza Muungano kwa maslahi yao binafsi. Na hata hao wachache wakiwa faraghani huwa na msimamo wenye kulingana na ule wa wenzao walio wengi.

Kwa ufupi, Wazanzibari wanaupiga vita Muungano kila upande.  Kila siku zikiendelea kusonga mbele ndipo Wazanzibari wa kila kizazi wanavyozidi nao kuwa na mori dhidi ya Muungano.

Kuna Rashid Salum Adiy na wenzake 40,000 wanaoishitaki serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Afrika Mashariki wakitaka Muungano huo uvunjwe kwa madai ya kuwa hauna uhalali. Kesi hiyo imewasilishwa mbele ya Mahakama ya Afrika Mashariki baada ya Mahakama Kuu ya Zanzibar kushindwa kuisikiliza.

Hii ni mara ya mwanzo kwa suala la uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kufikishwa mahakamani tangu Muungano huo uasisiwe miaka 55 iliyopita.

Wengine wamo mbioni kudai Zanzibar irejeshewe kiti chake cha Umoja wa Mataifa.  Ilikipata kiti hicho baada ya Zanzibar kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa kufuatia Uhuru kutoka Uingereza Desemba 10, 1963.

Wengine wanataka pafanywe kura ya maoni kuamua juu ya hatima ya Muungano kwa kuwauliza Wazanzibari iwapo wanautaka au hawautaki.

Ni wazi kwamba kuna wasioutaka kabisa Muungano uendelee na kuna wengine wenye kutaka muundo wa Muungano ubadilishwe ili Zanzibar irejeshewe mamlaka yake iliyopokonywa na serikali ya Muungano.

Gurudumu la historia likiwa linasukumwa na wananchi haliwezi kamwe kuzuiliwa hata hao wananchi wawe wanakabiliwa na nguvu za aina gani. Hatimaye watashinda tu madhali wanasimamia upande wa haki. Historia ina ushahidi mwingi wa kuyathibitisha hayo. Ndiyo maana inatia moyo kuwashuhudia vijana wasomi wa Kizanzibari wakiungana kuifikiria Zanzibar ijayo.

Katika historia tumeshuhudia mara nyingi jinsi watawala wa kikoloni walivyokuwa wakipitwa na wakati kimawazo. Wao walipokuwa wakijiandaa kuwakandamiza wanaowatawala kwa nguvu zao zote za dola watawaliwa walikuwa wakipanga kwa siri mikakati yao ya namna watavojitawala baada ya kuikata minyororo ya kikoloni iliyowakaba.

Hivi sasa Wazanzibari wana vikao vinavyojadili ni Zanzibar  ya aina gani waitakayo taifa lao litapokuwa katika Muungano wa muundo mwingine au bila ya Muungano. Wanajadili masuala ya utawala wa kidemokrasia, uchumi unaojikita juu ya Zanzibar kurejea tena kuwa bandari huru na pia mafungamano yao na nchi zilizo jirani yawe vipi.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 01 Mei 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab


Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles