Kinachoendelea hivi sasa katika siasa za Tanzania, kwa ujumla, hasa kwa upande wa Zanzibar katika Chama Cha Wananchi (CUF) kimenifanya nikumbuke tarekhe za visa vya Mitume na kwa muktadha wa makala hii fupi nitaangalia kazi kubwa ya kiutume iliyofanywa na Nabii Nuh (AS), upinzani aliokumbana nao na mwisho kulitazama Jahazi la Uokozi aililolichonga kwa amri ya Mola wake. Nafanya hivi kwa kufuata maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’an kwamba visa hivi anavyotusimulia ni kwa ajili ya kuchukua mfano na mafunzo ndani yake na kutuongoza.
Nabii Nuh (AS) ni katika mitume wa mwanzo na alifanya kazi kubwa ya kuwalingania watu wake kutaka kuabudiwa kwa Mungu Mmoja. Kazi hii ilimchukuwa zaidi ya miaka 900 kwa ustahamilivu mkubwa. Hata hivyo, Nabii Nuh hakukubalika na watu wake walio wengi. Kama ilivyo desturi za Mitume kukataliwa na jamaa zao wa karibu, Nabii Nuh alikataliwa hata na mwanawe wa kumzaa.
Sio tu kumkataa, jamaa zake hawa walishtadi pia katika kumfanyia vitimbi na maudhi ya kila aina. Hata pale alipoamrishwa na Mola wake atengeneze jahazi, basi waliamuwa kuligeuza choo cha kuweka haja zao kubwa. Mungu akawatia adabu kwa kuwapa ugonjwa mbaya ambao dawa yake ikawa ni kinyesi kile kile walichotia katika jahazi la Nabii Nuh. Wakawa wanakwenda kukichukuwa na kujipaka hadi jahazi likawa safi kabisa.
Mambo yalipofurutu ada, Mwenyezi Mungu Mtukufu Akamuamrisha Nuh apande kwenye jahazi lile yeye na wafuasi wake waliomuamini kama njia ya kuwatoa kwenye vitimbi hivi na kuwaacha wale wafanya vitimbi wakumbwe na gharika itokayo kwa Mola wao. Miongoni mwa waliogharikishwa ni mtoto wake mwenyewe, ambaye alikataa kupanda jahazi pamoja na baba yake.
Maalim Seif wa nyoyo za watu
Clik here to view.

Maalim Seif si Mtume na kattu hatuwezi kumfananisha hata kidogo na kazi za Mitume wa Mwenyezi Mungu. Huyu ni mwanaadamu wa kawaida tu. Hapokei wahyi na wala hakuna miujiza kutoka kwake. Lakini, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, nimekianza kisa cha Nabii Nuh kwani ndani yake muna mazingatio muhimu kwa muktadha wa makala hii.
Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa kwenye siasa kwa zaidi ya nusu ya umri wake sasa. Ni kiongozi wa pekee aliyedumu kwa muda mrefu anayekubalika na watu wa rika lake na kizazi hata cha wajukuu zake.
Siku fulani katika mwezi wa Disemba mwaka 1987, Maalim Seif alikula kiapo mbele ya maelfu ya wananchi waliokusanyika kwenye uwanja wa Tibirinzi, kisiwani Pemba, baada ya mapokezi makubwa ya kihistoria ambayo yalifanyika kwanza Unguja na baadaye Pemba muda mfupi kabla ya kufukuzwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). h
Siku hiyo ambayo imebakia kwenye historia milele, kiongozi huyu aliwaahidi Wazanzibari kuwa angelikuwa nao akiwa ndani ya serikali au nje ya serikali, ndani ya chama au nje ya chama. Wakati huo chama kilimaanisha CCM tu. Kiapo hiki kilimfungamanisha Maalim Seif na umma wa Wazanzibari na mpaka leo hii huwezi kumtenganisha na umma huo kwa namna yoyote ile.
Kazi kubwa aliyoifanya Maalim Seif ya kuwatumikia Wanzanzibari na Watanzania kwa ujumla imemjengea heshima ya kipekee. Ni kiongozi pekee aliyezitembea karibu katika wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar kuonana na wananchi na kulala nao vijijini katika hali ambayo si viongozi wengi tulionao wanaoweza kufanya hivyo.
Hali hii ya mahusiano kati ya Maalim Seif na wananchi ndio iliyopelekea watu kumpenda, kumthamini na kumuamini. Anaishi katika mioyo ya wananchi walio wengi. Hata maadui zake wa kisiasa hawawezi kuipitisha siku bila ya kumuwaza mtu huyu.
Kosa la Maalim Seif kwa maadui zake
Ni imani hii ya wananchi kwa Maalim Seif ndiyo imekuwa kosa lake kubwa mbele ya maadui zake, ambao kila uchao wanahangaika kufikiria namna ya kummaliza.
Clik here to view.

Hata hivyo, kazi ya kummaliza Maalim Seif nayo imekuwa si rahisi hata kidogo. Kazi hii iliyoanza tokea wakati wa Mwalimu Julius Nyerere inaendelea hadi leo zama za Rais John Magufuli, lakini kila uchao ndivyo Maalim Seif anavyowatazama maadui zake wakimalizika na wakimuacha yeye akizidi kung’ara kisiasa.
Wengi wanaweza kudhani kuwa kilichotekea juzi ndani ya CUF, ndio mwisho wa Maalim Seif: kwamba CUF aliyoiunda yeye mwenyewe na kuijenga kwa nguvu zake zote, leo hii inatumika kumbomowa, kwamba wale aliowajenga kisiasa, akiwemo Ibrahim Lipumba aliyemuita na kumpokea katika chama na kupewa nafasi ya kugombea Urais wa Muungano mwaka 1995 na baadaye uwenyekiti wa chama mwaka 1999, eti ndiye sasa anammaliza Maalim Seif! Huku ni kuota mchana.
Khofu imetanda kila pahala hivi sasa. Dhoruba hii sio ndogo, kwa kukiri ukweli, hasa linapohusika jabali la kisiasa kama Maalim Seif. Wakati wafuasi wake – ambao ndio majivuno yake – wapo kimya wakisubiri kauli yake itowe mwelekeo na matumaini mapya ya kisiasa, cha kustaajabisha zaidi ni kuwa hata wale wapishi wa njama hizi za kuihujumu CUF wanaonekana hamkani si shwari tena.
Kwanza, wanastaajabishwa na uvumilivu wa Maalim Seif unaofanana na Nuh. Pili, hivi sasa ndio wanagundua kuwa CUF – kama itikadi na imani iliyowajumuisha kina Maalim Seif na wafuasi wao – bado haijatetereka. Ipo madhubuti na sasa inawatia khofu sana hasa juu ya mwelekeo wanaoweza kuuchukuwa hasa ukiongozwa na Maalim Seif mwenyewe.
Maalim Seif kuwavuusha wafuasi wake?
Kwenye magazeti yanayotumikia watawala hivi sasa habari na makala za uchambuzi zote zinaelekezwa kwa Maalim Seif, zikijaa kila aina ya propaganda. Hii ni dalili ya khofu kubwa kutawala katika nyoyo zao. Kama Maalim Seif amekwisha na wamefanikiwa kummaliza kama wanavyodai, si wamuache tu wasubiri kumshindikiza katika kaburi lake la kisiasa?
Clik here to view.

Bila shaka, khofu zote zinakuja kwa sababu dalili zinaonesha kuwa wamemchezea simba aliyelala na sasa simba kaamka, khofu ya kujeruhiwa imeshawajaa.
Na naam, wenye macho wanaona kuwa huu ni wakati muwafaka ambao, kama Nabii Nuh alivyotakiwa kutengeneza jahazi na kuwaamrisha wale wafuasi watiifu kwake kupanda pamoja naye ili kukwepa gharika itokayo kwa Mola wao, basi naye Maalim Seif achonge jahazi watu wake waingie.
Kwa mazingira ya siasa za Tanzania hivi leo, mfano wa aliyoyapitia Nabii Nuh ni wazi kuwa anayapitia au anapitishwa Maalim Seif. Kwa sisi tunaomuamini kama kiongozi wetu, tuna imani kuwa vitimbi hivi havitotukatisha tamaa ya kuendeleza mapambano yetu.
Tunajuwa pia kama walivyokuwepo watoto wa Nabii Nuh waloasi, basi watakuwepo pia kina Abbas Muhunzi, Khalifa Suleiman, Mohammed Mnyaa, Nassor Seif, Rukia, Mussa Haji na wenziwao katika zama zetu. Watachupa kwenye jahazi kwa kudhani wataokoka kwa kupanda juu ya jabali, wakati hakuna jabali la kupanda likawanusuru.
Gharika hii ni kubwa. Kusalimika ni kuwa pamoja katika Jahazi la Nuh tu. Tunamsubiri Nuh wetu atuongoze kwenye Jahazi maridhawa la kutuvusha na kututuwa kwenye malengo yetu.
Kama alivyowahi kusema mwenyewe Maalim Seif kuwa endapo watawala wakimpa chama Lipumba, watajuta kitakachotokea. Naona majuto yameshaanza. Nyoyo zinawasuta wasaliti, dola inataharuki kwa kuiona nguvu mpya ya umma itakayosimama pamoja na kiongozi wao kupinga dhulma hii na kupigania haki na demokrasia ya kweli.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kama Mtumbatu.