Vyombo vya ulinzi na usalama vimeelezwa kuwa vinaongoza katika ukiukwaji wa haki za binaadamu katika mikoa mbali mbali nchini Tanzania.
Hayo yameelezwa katika mdahalo wa waandishi wa habari na wadau uliofanyika katika ukumbi wa Kisenga na kuhudhuriwa na wadau na watetezi wa haki za binaadamu.
Wakili Humphrey Mtuy ambaye ni Afisa wa Programu Mwandamizi wa Baraza la Habari Tanzania amesema kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa za haki za waandishi katika kipindi cha mwaka 2018 ambapo jumla ya matukio 46 yameripotiwa katika mikoa mbali mbali ya Tanzania ambayo yanawahusu wanadishi wa habari na vyombo vya habari nchini.
Amesema kati ya matukio hayo Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa uvunjifu wa haki za waandishi. Mikoa mingine inayoonekana kinara wa ukiukwaji huo ni Kigoma, Mtwara, Tanga, Singida, Shinyanga na Njombe.
Akitaja matukio hayo ni pamoja na kunyimwa taarifa, vitisho, mauaji, unyanyasaji, kukamatwa kinyume na sheria, kutekwa, shambulio, faini, kufungiwa na kutolewa kwa mabavu.
Matukio mengine ya ukiukwaji wa haki za binaadamu ambao yameripotiwa kufanyiwa waandishi wa habari wakati wakitekeleza majukumu yao ni uharibifu wa vitendea kazi, mashambulizi ya mtandao na wahariri kuingilia kazi za waandishi pamoja na waandishi na vyombo vya habari au magazeti kujifungia wenyewe kutokana na khofu.
Kwa upande wa vyombo vya habari Mtuy ametaja baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinavyoongozwa kwa kunyimwa taarifa ni magazeti, televisheni, radio na mitandao ya kijamii ambapo waandishi wake huwa wanakoseshwa taarifa na kukataliwa kupewa taarifa wanapofuata wahusika wakiwemo watendaji wa serikali.
Tanbihi: Habari imeandikwa na Loveness Muhagazi & Salma Said