Ufuatao ni mjadala kati ya Wazanzibari watatu – Balozi Ali Karume, Bwana Salim Msom na Wakili Awadh Ali Said – juu ya mada tete ya kuyalinda mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambao ulianza kutokana na mchango wa Bwana Salim katika moja ya majukwaa ya mitandaoni yanayowakutanisha Wazanzibari. Usome kwa kina kisha nawe changia maoni yako kama Mzanzibari:
Tarehe 18 Julai 2018, Bwana Salim Msoma alianzisha mjadala kwa barua yake hii kwenye ukumbi wa mjadala:

“Mimi huwa napata taabu ninaposoma huu usemi unaotamkwa mara nyingi unaodai au kutoa wito kuwa Zanzibar ijitahidi ‘ing’are na sifa yake ya zama za kale kurejea’. Hizo zama za kale ni zipi?
“Mimi kwa maoni yangu Zanzibar kuanzia miaka ya 50 imekumbwa na zama za siasa ambazo zimeambatana na kuenea lugha za fitna zilizosheheni chuki za kikabila na rangi ambazo zilipelekea maisha ya wazanzibari kuangamia kwa umwagaji damu.
“Tuanze na vita vya ‘ng’ombe’ vya 1952 wakati watu wa Kiembesamaki walipigwa risasi na kuuwawa na polisi pale walipojaribu kuwakomboa viongozi wao waliokuwa wanashikiliwa gereza la Kinuamiguu ambako walivunja lango la gereza hilo.
“Halafu yakafuata mauwaji (political assassination) ya mtu maarufu Z’bar, Bw Sultan Ahmed Mugheiry 1954 pale alipokataa kuunga mkono mgomo wa Arab Association kugoma kuhudhuria vikao vya Baraza la Kutunga Sheria.
“Baadae vikazaliwa vyama vya ZNP na ASP ambavyo viligubikwa na mpasuko pamoja na uhasama wa kikabila. Mwaka 1957 kulifanyika Uchaguzi wa mwanzo ambao ulijaa kejeli na jazba za kikabila.
“ZNP walishindwa kwenye uchaguzi ule na ilipofika 1958 makada wa ZNP walishajiisha wakulima wadogo ambao walioonekana kukiunga mkono chama cha ASP wafukuzwe kutoka mashamba na ardhi iliyokuwa inamilikiwa na wafuasi wa ZNP.
“Kitendo hiki kilizaa uhasama mkubwa na watu kugomeana hata kuzikana.Ukaja mwaka 1961 ambao ulikumbwa na ghasia za mauwaji hata ikabidi kutangazwa hali ya hatari na kuletwa Askari wa KAR kutoka Tanganyika na wale wa GSU na hatimae wa Kiingereza kutoka Kenya.Mapinduzi ya 1964 yalikuwa ni kilele cha misukosuko ya harakati za kisiasa kinzani zilizotawala Z’bar.
“Mimi sikuhadithiwa bali nilikuwa kijana mdogo nikisoma shule ya msingi hadi sekondari wakati wa Uhuru wa 1963 na zilzala ya Mapinduzi iliyomwaga damu nyingi. Kaumu ya vijana kama mimi tulizaliwa kwenye miaka ya kumi la 40.
“Kwa hiyo sikumbuki hizo zama za utulivu za kale. Labda kale ya miaka ya 1920s na 1930s! Tusijisifu kwa kutia chumvi kuwa tulikuwa hatuna balaa visiwani. Salim“
Siku hiyo hiyo, Balozi Ali Karume akachangia kuonesha kumuunga mkono:
“Salim: You are right on the ball. Hizo sifa za zamani zinoliliwa ni zipi; mwenye hamu ya Utawala wa Mwinyi-Mkuu, Warenu, Waingereza au Waarabu wa Omani ni nani? Matatizo yetu yote yanatokana na Maradhi ambayo kwa Kiingereza yanaitwa “Condition of Denial”. Naomba wataalamu watafsiri kwa Kiswahili nini maana ya “State of Denial”.
“Wazanzibari wengi wanopinga Mapinduzi, wanaota ndoto za mchana kwamba labda siku moja Mapinduzi ya Zanzibar yatapinduliwa zikipatikana kura za wizi za kutosha. Hilo naliita “Delusional Illusions” (naomba tafsiri ya Kiswahili. Nani asiejua kwamba Zanzibar kulitokea Mapinduzi, na kwamba Mapinduzi ya Zanzibar hayawezi kuchezewa Upatu kwenye uchaguzi wa Kibepari, unaothamini ununuzi wa Kura?
“Mapinduzi ya Zanzibar ni Lazima yatunzwe; yasichezewe Upatu wala Sureti. Umepata kusikia wapi Ushindi wa Mapinduzi uliotokea kwa Risasi, ugeuzwe muelekeo wake kwa wingi wa Karatasi? Katiba ya Zanzibar ibadilishwe na iletwe Katiba ya Demokrasia ya kulinda Mapinduzi ya Zanzibar.
“Waingereza wana Katiba ya kulinda Ufalme wao, vyama vyote vya siasa huko, vimeapa kulinda hiyo Katiba Ufalme wao. Marekani wanayo Katiba ya kulinda Mapinduzi yao na vyama vyote vya siasa vimeapa kulinda Mapinduzi ya Marekani. Cuba walifanya Mapinduzi na wanalinda Mapinduzi yao. Wanayo Dimokrasia kulinda Mapinduzi yao, hawataki kuyapoteza kwa Mabepari wanonunua Kura. Tuwaige WaCuba. Watupatie utaalamu wa kulinda Mapinduzi sio utaalamu wa Madaktari Bingwa Tu. “
Kisha tena Bwana Salim Msoma, akaandika tena kuweka sawa mtazamo wake:

“Ijapokuwa Balozi ali Karume kaonesha kukubaliana nami kwenye hoja yangu iliyosisitiza kwamba Z’bar haikuwa ‘shwari’ kisiasa zama za miaka ya nyuma,maoni yake ya ziada katika mada hii hayawiani wala kukubalika katika muktadha wa leo wa siasa Z’bar. Wito wake wa kuyalinda Mapinduzi ya Z’bar kwa kubana na kuminya demokrasia ya wananchi (people’s democracy) wa visiwani ni mawazo ya siasa kali (extremism) ambayo hayaendani na mwamko wa siasa uliopo.
“Historia inatufunza kuwa hakuna Mapinduzi yeyote duniani ambayo yataweza kutunzwa na kuenziwa kwa kukandamiza demokrasia. Kama tunadai Mapinduzi yalindwe na kutukuzwa basi hatuna budi kukubali na kuenzi haki ya Wazanzibari wote kujichagulia viongozi wao wa kuyaendeleza na kuyalinda hayo Mapinduzi kwa kufanya chaguzi huru kila awamu ya mendeleo yao kisiasa.
“Tabia ya wanasiasa waliopo madarakani kujivisha taji la ufalme wa ulinzi wa Mapinduzi bila ya kuchaguliwa na wananchi kuongoza serikali inayolinda Mapinduzi lazima ikataliwe.Kwani ukweli ni kuwa takriban viongozi wote wanaotawala leo sio tena wale waasisi waliopindua 1964 ambao ni wazee sana au wameshatangulia mbele ya haki.
“Nathubutu kusema kuwa hivi sasa hakuna Waziri wa SMZ alieshiriki, kwa mfano uchaguzi wa mwisho kabla Mapinduzi Juni 1963. Hali kadhalika tabia na khulka ya kumsingizia kila anaehitilafiana na viongozi waliopo madarakani ni mpinga Mapinduzi ya 1964 ni hila na njama ya kukashifu na kupaka matope haki ya kila Mzanzibari kuwa na mawazo na fikra mbadala katika mjadala wa kisiasa.
“La mwisho napenda kueleza kuwa Mapinduzi ya Cuba hayalindwi kwa njia kama hizi za kwetu.Mimi binafsi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mshikamano na Urafiki Kati ya Tanzania na Cuba na ninao uelewa wa mwenendo wa utawala na siasa za kule.Tukitupilia mbali propaganda za Marekani tutabaini kwamba viongozi wa Cuba kuanzia kina Fidel na Che walibuni mfumo wa utawala na uendeshaji serikali ambao haukuwabagua Wakuba kati ya wanachama na wasio wanachama wa Chama cha Kikoministi.
“Fidel siku zote alisisitiza kuwa Wacuba wote ni raia na wanapaswa kuwa na haki ya kushiriki kwenye uendeshaj wa serikali yao.Kwa hivyo kwa mujibu wa Katiba ya kule Cuba Chama Cha Kikoministi hakiingilii kazi za Kamati za Mitaani na Makazini zinazochaguliwa kuendesha zoezi la kupata wagombea wa kuanzia ngazi ya chini ya uwakilishi wa mitaa,mikoa hadi Bunge la Cuba. Chama hakihodhi mamlaka ya kukata au kuondoa majina ya raia wanaotaka kugombea uwakilshi au Ubunge. SI LAZIMA MTU AWE MWANACHAMA WA CHAMA CHA KIKOMINISTI CHA CUBA ILI AWEZE KUWA MBUNGE. Sifa inayomfanya Mkuba apitishwe jina lake na Kamati za Raia za Mitaa na Makazini na kisha achaguliwe ni uzalendo wake na umaarufu wake pamoja na namna anavyoishi na raia huko aliko anakogombea.
“Wengi wetu huku kwetu hatuelewi haya ya mfumo wa Cuba wa uundaji na uendeshaji serikali ya Cuba na siri ya ukomavu wao wa kumudu kuyalinda Mapinduzi yao.Kwa hiyo wazo la Balozi Ali Karume la Wacuba kutufunza namna ya kulinda Mapinduzi yetu halitekelezeki kwasababu sisi na Wacuba tunahitilafiana na kutofautiana katika falsafa na khulka za kisiasa zinazotuongoza.
“Sisi Z’bar tumesheheni kwenye nafsi ya miili yetu DNA za kubaguana.Fidel na Chama cha Kikoministi Cha Cuba walifaulu kubadilisha DNA za ndani ya maumbile ya Wacuba wa rangi na nasaba zote na kukubaliana waendeshe nchi yao na kulinda Mapinduzi kwa kuhamasika na wito wa Fidel wa ‘Venceremos!'”
Wakili Awadh Ali Said naye alikuwa na haya ya kusema kwenye mjadala huu:

“Nimesoma Andiko la Mh. Balozi Ali Karume katika mjadala ulioibuliwa na Shk. Salim Msoma ambaye Yeye ameelezea kwa mtiririko wa kihistoria jinsi ambavyo Zanzibar imekuwa ikigubikwa na mivutano ya kisiasa tokea hizo siasa zilipoasisiwa rasmi.
Baada ya kusoma Andiko hilo la Balozi Ali Karume kuna hoja ambayo ninaamini inahitaji ufafanuzi ili ieleweke kwa ufasaha. Hoja yenyewe ni ile ya “kulinda Mapinduzi” Namnukuu : “Umepata kusikia wapi Ushindi wa Mapinduzi uliotokea kwa Risasi, ugeuzwe muelekeo wake kwa wingi wa karatasi? Katiba ya Zanzibar ibadilishwe na iletwe Katiba ya Demokrasia ya kulinda Mapinduzi ya Zanzibar”
“Ufafafnuzi unaohitajika hapa ni jee hiyo Dhana/Hoja ya “kulinda Mapinduzi” inamaanisha nini?
“Jee inamaanisha kuwa wale waliopindua wanabaki madarakani kwa nguvu za katiba? Au inamaanisha kile Chama kilichopindua ndio kilindwe kikatiba kuwa kiendelee kubaki madarakani? Au inamaanisha Katiba ilinde ile misingi na malengo ya yale Mapinduzi bila kujali Watu waliopindua au Chama kilichopindua? Na Jee ikiwa Katiba ilinde kubaki madarakani wale waliopindua hali itakuwaje Wanamapinduzi watapotoweka, kama ilivyo Zanzibar hivi sasa? Madaraka yatawastahikia Vizazi vyao? Kwa mpangilio na utaratibu upi? Na endapo kulinda Mapinduzi kutamaanisha kuwa Katiba ilinde kubaki madarakani kwa Chama kilichopindua, jee Chama hicho kitapotoweka, kama ilivyo A.S.P hivi sasa; jee itamaanisha Chama kilichoungana na A.S.P ndicho kilindwe kikatiba kubaki madarakani? Au kuyalinda Mapinduzi ni kuhakikisha kuwa zile fikra, misingi na malengo ya Mapinduzi ndio yalindwe Kikatiba ili yoyote ashikae madaraka ayasimamie hayo? Ukitoa hiyo njia ya kulinda ile misingi na malengo ya Mapinduzi kikatiba, ni vipi Katiba hiyo itakuwa ya Kidemokrasia kama alivyodai?
“Sasa kama Katiba italinda wale Waliopindua ama Vizazi vyao ama Chama chao sasa hiyo Demokrasia itakuwa ya aina gani kwa mazingira na muktadha tunaoujadili?
“Kwa mfano ukiwaza zaidi unajiuliza Jee kulinda Mapinduzi ni kuwa pasiwe na Uchaguzi? (Na kwa kweli hili lilikuwepo, tokea 1964 hadi 1995 – miaka 31- hakukuwa na Uchaguzi wa Vyama. Vyama vilipigwa marufuku kwa miaka 28 ili kutoa fursa ya kulinda Mapinduzi) Au pawepo na Uchaguzi lakini kwa kiwango fulani tu, mathalan kwenye Mabaraza ya Uwakilishi na Mabaraza ya Serikali za Mitaa ila Uongozi Mkuu kwa maana ya Rais, pengine na Baraza La Mapinduzi vibaki kwa Waliopinduwa AU Chama kilichopindua? Na ikiwa hali ni hiyo jee huyu Kiongozi Mkuu Mwanamapinduzi mlindwa na Katiba atakuwaje pale Chama chake kitapoambulia patupu katika Uchaguzi au atakuwa na mamlaka ya kuteua Wawakilishi over and above ya wale Waliochaguliwa? Au Yeye atabaki ni Kiongozi Mkuu akiwa ni Alama ya Kuenzi Mapinduzi tu na hatokuwa na nguvu za kimaamuzi katika Uendeshaji Serikali kama alivyo Malkia wa Uingereza na “Constitutional Monarchs” wengineo wa aina yake; na ikiwa ni hivyo hizo nguvu za kulinda Mapinduzi atazipatia wapi?
“Lakini mbali na haja ya Ufafanuzi huo, upo pia mshangao mkubwa. Mapinduzi ni tukio kubwa la kihistoria ambalo lili-shape maisha ya kisiasa ya Visiwa vya Zanzibar hadi leo hii. Yamedumu kwa zaidi ya nusu karne hivi sasa. Waliozaliwa wakati wa Mapinduzi wengi wao wameshajukuu. Na maisha yote imeelezwa kuwa Mapinduzi yale yalilazimika kutokea kwa sababu ya kukithiri kwa hila za kisisa, uonevu, ubaguzi, unyanyasaji, dharau na ukandamizaji uliojaa katika Visiwa vya Zanzibar. Na Mapinduzi yalikuja ili kuondoa uovu wote huo na kujenga jamii yenye haki, usawa, mshikamano na ustawi kwa wote. Sasa kweli baada ya muda wote huo wa kuijenga jamii kwa ile misingi ya Mapinduzi, ni kwa vipi leo Mapinduzi haya yalindwe kwa Silaha ya Katiba? Umma ulioneemeka na mema ya Mapinduzi si utasimama kidete kuyalinda na kuyatetea hata kwa kupitia huo “wingi wa karatasi au mchezo wa upatu” Lililo jema kwa Binaadamu ni wazi litamngia moyoni na katika fikra zake; na ni wazi atalienzi na kulidumisha. Hapatohitajika Lazimisho la Kikatiba. Iweje leo takriban miaka 55 baada ya Mapinduzi yaliyoondoa ile misingi ya dhuluma na ubaguzi bado hayawezi kujisimamia yakajilinda kupitia Umma uliofaidika na neema zake, badala yake tukimbilie kwenye msaada wa Nguvu za Katiba?
“Lakini pia kuna nukta ya kisheria inabidi iangaliwe. Wakati Mapinduzi yanatokea Zanzibar ilikuwa ni Dola kamili “SOVEREIGN STATE” iliyotambulika kama Nchi kamili ikiwa ni sehemu ya Jamii ya Nchi duniani; ilikuwa Mwanachama Kamili wa Umoja wa Mataifa, yenye Kiti chake na ikiwa ina Mabalozi wake wanaoiwakilisha katika baadhi ya Nchi duniani. Miaka 55 leo baada ya Mapinduzi “STATUS” ya Zanzibar Duniani haipo; na hapa Ndani tumefafanuliwa kwa ufasaha na Mahkama ya Rufaa Tanzania (ambayo ndio Mahkama ya Juu kabisa kwa Tanzania) katika kesi ya uhaini ya Machano Khamis Ali na wenzake kuwa Zanzibar SI NCHI. Na wakasema kwa vile Zanzibar si Nchi hakuna kosa la Uhaini unaloweza kufanya. Hujuma kubwa kwa Mapinduzi au Serikali ni kuyapindua Mapinduzi au kupindua Serikali au kudhuru Viongozi. Sasa katika sehemu ambayo huwezi kuyalinda Mapinduzi kwa nguvu za kisheria kwa vile hakuna kosa la uhaini kwa kuws Zanzibar SI NCHI sasa unalindMapinduzi ndani ya nini? Hii ni sawa na kujidhatiti kuwa unalinda NDOA lakini MKE mwenyewe hunaye tena na keshaolewa kwengine. Ila wewe umo na hang-over za kulinda Ndoa. Ndoa ni Mke bila Mke huna ndoa. Mapinduzi ni NCHI bila NCHI ni kiinimacho kusema unalinda Mapinduzi. Kutoa mifano ya Cuba, Marekani na Uingereza jinsi Katiba zao zinavyolinda Mapinduzi na ukafananisha Nchi hizo na Zanzibar ya leo ni kustawisha Barza tu. Zanzibar ya leo haina hadhi ya kuwa Nchi Duniani. Hizo ni Nchi. Labda kama Balozi aliikusudia Zanzibar ile ya wakati Mapinduzi yanatokea. Sio hii ya leo.
“Ninaamini tupo wengi tunaohitaji ufafanuzi ili tujenge uelewa zaidi.
Wakatabahu,
Awadh Ali Said”