Lile kundi mashuhuri la kihalifu linalotajwa kuhusika na matukio kadhaa mabaya visiwani Zanzibar, ambalo wakaazi wa visiwa hivyo wamelipanga jina la ‘Mazombi’, linaripotiwa kurejea upya kwenye uharamia wao kwa kuwateka vijana nane wakaazi wa Mji Mkongwe usiku wa kuamkia Jumatatu (26 Machi 2018), na kuwapiga, kuwaibia na kisha kwenda nao eneo la Fumba, magharibi mwa kisiwa cha Unguja, ambako waliwatesa. Haya yanakuja ikiwa ni baada ya miezi sita tangu kundi hilo kutajwa kuhusika na mauaji ya Bwana Ali Juma Suleiman, ambaye naye walimteka na kumtesa kabla ya kupoteza akiwa hospitalini Mnazi Mmoja, mkasa ambao ulipelekea kusimamishwa kwa shughuli za kundi hilo kwa muda.