Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Riwaya: Safari ya Kumuua Rais – 2

$
0
0

Ilipoishia shemu ya kwanza! Tuliona jinsi Abdull na Talib ambao ni ndugu walivyotoka Dodoma na kufika Dar es Salaam, baada ya mapumziko ya siku chache wakaelekea Zanzibar katika kisiwa cha Unguja. Huko wakaanza maisha, Abdull akiishi km mgonjwa wa akili na Talib akiwa na mtangamano mzuri na jamii inayomzunguka. Yote haya wanayafanya wakiwa na sababu maalum. Ndipo siku moja Abdull akiwa Forodhani akaikumbuka ile safari ya kukimbia Pemba na kukimbilia Mombasa, Kenya akiwa na kaka yake huyo…..Sasa endelea

Walipofika Nyali, Mombasa walianza maisha  kwa kulala pembezoni mwa vibaraza vya nyumba za watu, wakati mwengine hufukuzwa na wenye nyumba hizo. Kula yao walikuwa wanaipata kwa  kuomba omba masokoni au kutafuta mabaki mabaki ya samaki kutoka katika vyombo vya wavuvi.

Baada ya siku chache walipata akili ya kuomba kwa mmoja wa wavuvi awachukue baharini ili na wao wapate chochote kitu cha kutia mdomoni na kuhifadi mfukoni. Mzee Jabir hakuwa mkorofi, kila mmoja alimjua kwa wema wake, aliwakubalia ombi lao na kuanza  kuwachukua katika shughuli zake za kivuvi.

“Hivi mnatokea wapi Mombasa hii?”, ilikuwa ni alfajiri ya awali Mzee Jabir akiwa na ndugu wawili tayari kuondoa nang’a ili kuingia baharini kwa ajili ya kuanza shuguhuli kusudiwa.

“Hatutokei Mombasa Mzee’;

“Kwahiyo mnatokea wapi?

“Kisiwa cha Pemba’

“Aaaa poleni sana, tunayasikia yanayotokea huko kipindi hiki… tumepishana na majahazi mengi tu wengine wakikimbilia Somalia”,alisema Mzee Jabir

Muda ule ulikuwa ni saa kumi na moja za jioni ndipo wavuvi wengi walipendelea kuelekea baharini kwa kipindi kile,kutokana na mahesabu yao ya kivuvi.

Na Rashid Abdallah

Siku zilianza kukatika, na maisha ya uvuvi yaliwawezesha ndugu wawili kupata chumba cha kulala na kujikimu milo yao, lakini hawakuwa wanahifadhi chochote mifukoni mwao. Hali ya maisha bado haikuwa laini kwani uvuvi wao wa dau lililokosa hata  mashine, ulikuwa unawawiya vigumu kwenda kwenye maji makubwa ambako ndiko wangepata samaki wengi.

Baada ya mwezi kadhaa kukatika na hali bado haikuwa nzuri katika shughuli za kivuvi, ndipo walipopewa wazo la kuondoka na kukimbilia katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyopo kaskazini-mashariki mwa Kenya katika eneo la Garrisa.

Walikubaliana na wazo hilo kutoka kwa Mzee Jabir, kwani aliamini wangepokelewa  kwa sababu kila mmoja alikuwa ameshasikia kile kilichotokea Zanzibar hasa katika kisiwa cha Pemba.

“Basi safari njema… huko pengine mtapata msaada mzuri zaidi”, Mzee Jabir alikuwa anawaaga Abdull na Talib, mapema asubuhi ,mara baada ya kuwatafutia gari la mizigo ambalo lingewafikisha Garrisa.

Safari ya kufika huko haikuwa nyepesi lakini hatimaye walifika Garrisa mchana mmoja wa siku ya Jumatano.  Kisha wakapanda gari nyengine ya kuomba  iliyokuwa inaelekea Dadaab.

Kambini walipokelewa mara baada ya maswali mengi mno, maofisa wa pale waliamini hali imekuwa shuari katika visiwa vya Zanzibar, hivyo walikuwa na maswali mengi mno hadi kukubali kuwapokea. Lakini hatimaye walipokelewa na kusajiliwa kama wakimbizi.

Katika kambi ya wakimbizi unafuu wa maisha unapatikana kwakuwa tu mnapata malazi ya bure na chakula cha bure, huduma nyengine pia zikiwa bure, kama afya, elimu na shughuli zinazowazunguka wakimbizi.

Kwa sababu Daadab ni kambi inayohifadhi wakimbizi wengi wa Kisomalia, hata lugha maarufu  kambini pale ilikuwa ni Kisomalia, ingawa na Kiswahili hakikuachwa nyuma kikiwa na wazungumzaji wachache.

Waliishi katika hema moja na vijana wawili wa Kisomalia, ambapo mmoja wao alikuwa anaelewa Kiswahili vizuri tu. Nyakati za usiku kabla ya kulala, zilikuwa ni nyakati za kusimuliana maisha ya kila mmmoja aliyopitia hadi kufika pale.

Mohammed ambaye ndiye alijua Kiswahili vizuri , kabla ya vita havijapamba moto kule Somalia alikuwa anakwenda Mombasa mara kwa mara na Baba yake kwa shughuli za kibiashara.

Mohammed aliwasimulia mkasa wa kukosa familia yake. Ilikuwa ni siku ya jioni ya saa kumi,  akiwa na familia yake wakisubiri chakula kilichokuwa kikiandaliwa na Mama yake katika nyumba yao iliyoko katika mji mdogo ulio nje kidogo ya jiji la Mogadishu, Somalia. Mohammed akiwa amempakata mdogo wake wa kiume aliyekuwa na miaka takribani sita.

Nyakati hizo ndipo kombora ambalo hajui hata lilitokea upande gani, lilipiga nyumba yao na kuifanya familia yote kuwa maiti isipokuwa yeye tu, alikosa mkono wake wa kushoto.

Mikasa kama ya Mohammed ni mingi sana katika kambi ya Dadaab. Abdull na Talib walianza kuzizoeya simulizi za namna ile. Maisha yaliendelea na siku zikikatika. Baada ya kuzoeyana na watu kadhaa na wao hawakuacha kujifunza lugha ya kisomali .

Maisha yalirudi kuwa ya furaha kwa kiasi fulani kwao, walitangamana vizuri na jamii ile, jioni hucheza mpira na kujumuika katika shughuli nyengine za eneo lile. Pia wakapata rafiki mwengine kwa jina la Ismail.

Miezi ilisonga wakiwa na rafiki yule wa Kisomalia. Kwa sababu Mohammed hakuwa mtokaji sana nje, kutokana na ulemavu aliokuwa nao, hivyo Ismail akawa ndiye rafiki yao mkubwa wakiwa nje.

“Pale Mogadishu hali imetulia kidogo sasa hivi, kuna biashara zangu  tutaenda kufanya”, Ismail alikuwa akijaribu kuwashawishi Talib na Abdull, waondoke katika kambia ya Dadaab na  waende Somalia.

Ismail alikuwa anawashawishi vijana hawa muda mrefu tangu kujuana nao, akiwaeleza kwamba maisha hayawezi kusonga mbele katika kambi ya wakimbizi, hivyo ni lazima wapate sehemu watakayo kuwa huru kufanya mambo ya kimaendeleo.

Ni maneno yaliyoingia akilini kwa ndugu wawili na hatimaye wakaamua kung’oa nanga zikiwa zimebaki siku tatu tu kabla ya rafiki yao Mohammed kufunga ndoa na binti mmoja wa Kisomali kutoka pale pale kambini.

Walipanda gari moja ambalo husafirisha   watu kimagendo kuingia Somalia, kikawaida magari haya yalikuwa yanafika tu mpakani mwa Kenya na Somalia, hayakuwa yanavuuka kuingia mpaka wa nchi nyengine kati ya nchi hizo mbili.

Walikaa kutwa nzima katika msitu wakisubiri kiza kiingie ili wavuke mpaka kuingia Somalia, baada ya gari walilopanda kuwashusha na kuondoka. Walisubiri kiza kiingie kwani waliogopa wasije kukamatwa na wanajeshi wa Kenya au Somalia, na  kuwatuhumu wanaingia Somalia kwenda kujiunga na kundi la Alshabab.

Kiza kilipoingia ndipo walipotoka na kuanza safari ya kuvuka mpaka.

“Ismail, wewe Ismail..”, Talib alikuwa anamuita Ismail aliyekuwa wa mwanzo kutoka mbele.

“Shii”,  lakini alitoa ishara ya kidole katika mdomo wake, kumuashiria anyamaze na asiinue sauti. Walikuwa wanapita karibu na kizuizi cha jeshi la Somalia.

Wakiwa na nguo nyeusi  wakitembemba udama udama, wakijificha na miti ya eneo hilo, hatimaye waliweza kupita salama katika eneno lile la kizuizi.

“Ulikuwa unasemaje?, aliuliza Ismail kwa ukali kidogo

“Chakula kinaelekea kuisha sasa tutatembeaje na njaa?

“Baada ya saa moja na nusu tutakutana na kijiji hapo mbeleni…usiwe na wasi wasi”, alieleza Ismail kisha kuwapa ishara wasonge mbele.

Usiku mzima ulikuwa ni wakutembea, lile saa moja na nusu waliloahidiwa lilikatika wala hakukuwa na kijiji chochote karibu.  Hadi ilipofika saa kumi na moja alfajiri ndipo walipofika  katika kijiji kimoja ndani ya Somalia.

Waliomba maji na chakula kutoka kwa wanakijiji hao,  walikuwa wameishiwa na kila kitu.

Ilikuwa ni safari ya kupita katika ardhi isiyo na rutuba wala neema ya miti mingi. Wakati wanaingia kijijini , Ismail aliwaeleza kwamba safari yao imekuwa nzuri zaidi kwa sababu wamekwepa miale ya jua, kama wangesafiri mchana.

Halikuwa tatizo kwa Abdull na Talib kuwasiliana na Wasomali,  walikuwa wanajua Kisomali tangu walipojifunza Dadaab.

Walionana na wenyeji wa kijiji na kuomba kupumzika katika msikiti mdogo ulioezekwa bati chakavu.

Majira ya saa sita za mchana kila mmoja akiwa katika usingizi mzito, walishituliwa na milio mizito ya risasi zilizokuwa zikilia nje kidogo ya kijiji kile, lakini milio ile ilizidi kusogelea kijiji kila dakika zisongapo.

“Vipi tunafanyaje sasa?, aliuliza Abdull kwa hofu kubwa

Ngoja nikaangalie kama kuna upenyo wa kutokea tutaondoka sasa hivi..”, alijibu Ismail huku akitoka na kuwaacha ndugu wawili msikitini pale, mioyo ikiwaenda mbio.

“Anaonekana  haogopi!”, alisema Talib huku anachungulia nje  kupitia dirisha la msikiti.

“Wamezoeya..”

Baada ya dakikia mbili Ismail alirudi na kuwataka wabebe mikoba yao, ili waondoke. Akidai kuna gari nje  inaelekea Mogadishu amewaomba wenye gari na wamekubali.

Waliondoka mbio mbio na kukimbilia katika gari la pick up kisha likaanza kuondoka taratibu kukiwa na watu wengine katika gari, pia kulikuwa na bendera nyeupe imepachikwa ikipepea kutoka katika gari lile.

Iliwachukua takriban siku nne hadi kufika katika mji wa Mogadishu,  njiani walikuwa wanapishana na wabeba silaha, ilikuwa inawabidi wapumzike kwa baadhi ya nyakati ili kukwepa mapigano mbele yao. Wakati fulani walikuwa wanashambuliwa licha ya bendera nyeupe iliyoashiria hawapo katika vita.

Saa mbili za jioni wakaingia Mogadishu, Ismail akiwa na Talib pamoja na Abdull. Muda mwingi wa safari ndugu hawa walikuwa kimya, hadi Ismail akawa anawashangaa, lakini kumbe ilikuwa ni hofu iliyojaa mioyoni mwao.

Ndugu wawili  wakiwa na mwenyeji wao, wakashuka  Xamar Jabjab, katika jiji la Mogadishu, eneo linalopepewa na mawimbi ya bahari kwa ukaribu wake, pia ni dakika chache tu kuifikia bandari kuu ya  Mogadishu.

Je! safari hii ya kuelekea Mogadishu itakuwa na manufaa yoyote kwa ndugu wawili, au ni kujitia katikati ya tanuri la vita? Alichowaeleza Ismail ni cha kweli, pindi wakifika Mogadishu? Kilichowakimbiza Pemba ni kipi? Fartuun ni nani?


Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles