Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

La Prof. Kabudi, Zanzibar na Mtego wa Komba – II

$
0
0

Katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa uchambuzi huu, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Othman Masoud, alizungumzia nadharia ya mtego wa komba akiufananisha na namna viongozi wa Zanzibar wanavyoiingia wenyewe nchi yao kwenye maangamizi kwa muktadha wa majibu yao kwa Waziri wa Sheria wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, juu ya hadhi, mamlaka na nafasi ya taasisi ya urais na katiba ya Zanzibar, na pia akagusia wasifu wa Profesa Kabudi kama amjuavyo yeye. Katika sehemu hii ya pili, anaanza kulinganisha kati ya kile walichokipitisha viongozi wa Zanzibar kwenye Katiba Inayopendekezwa na kile wanachojifanya kumsuta sasa Profesa Kabudi. – Mhariri 

Viongozi Wetu na Uchu wa Kipande cha Ndizi

Suala la kujiuliza ni kwamba je, ugeugeu wa wazi wa baadhi ya viongozi ambao wamekua mstari wa mbele kumtuhumu Profesa Kabudi ni wa kiasi gani na je, umekuwa na tija kwa Zanzibar? Au ndio uliompa silaha Profesa Kabudi kugeuka kwa tija ya Tanganyika?

Kwanza, tuangalie mifano michache tu.  Mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kumlaumu Profesa Kabudi, ndiye aliyetoa pendekezo la kuongeza kifungu kinachosema Zanzibar ni miongoni mwa nchi katika nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar. Pendekezo hilo lilikubaliwa baada ya kueleza matukio kadhaa ya jinsi viongozi wa Serikali ya Muungano wanavyoidhalilisha Zanzibar ndani na kimataifa, akitoa mifano iliyomsibu yeye binafsi nje ya nchi.

Na kiongozi mwengine aliwahi kusema ndani ya Baraza la Wawakilishi kwamba laiti Wawakilishi wenzake wangeliisoma Katiba ya Muungano na kuifahamu, basi wangelishukuru kwamba bado angalau Zanzibar ina Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama.  Kwa Katiba ilivyo, alisema, Zanzibar haina chake.

Na Othman Masoud Othman

Pili, wakati wa mchakato wa Katiba Inayopendekezwa kule Dodoma, mmoja wa viongozi wakuu wa sasa wa Baraza la Wawakilishi – kwa kushirikiana na wajumbe wenzake wa Kamati ya Uandishi – aliwahi kupeleka mbele ya kikao kilichoongozwa na mmoja wa viongozi wakuu wa Serikali ya sasa hivi, mambo 17 ambayo walihisi yanaibana Zanzibar katika Katiba Inayopendekezwa, lakini wajumbe wa Tanzania Bara wakiongozwa na Andrew Chenge waliyakataa katakata tena kwa ufedhuli kabisa. Aliwasilisha hoja hiyo kwa masikitiko hadi machozi yakamtoka, akikumbusha jinsi alivyodhalilishwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba wa Tanzania wakati wa mchakato wa “Katiba Inayopendekezwa.“

Baada ya mjadala mrefu, mambo 8 waliyakubali kwa kauli moja kuwa hayo ndio yawe “deal breaker” katika mchakato, yaani kwa vyoyote vile Zanzibar isiyakubali.  Msimamo huo ulipata idhini ya “Serikali” ya Zanzibar.

Cha kushangaza, nadhani kipande cha ndizi kilifanya wajumbe wafatwe usiku kule Dodoma na kubadili upepo.  Yaliyovuma kule Dodoma ni kuwa kumbe kipande cha ndizi chenyewe kilichotumika ni ahadi ya kupewa ugombea mwenza kwa mmoja wa viongozi wa Zanzibar wenye ushawishi na uamuzi uliotoka kutoka kwa mmoja wa wagombea watarajiwa wa Tanganyika.

Kumbe wala haikuwa ndizi bali tojo, wengine huita fumbufumbu.  Wote wakageuka – wakageuka kauli zao, wakageuka misimamo yao na wakageuka hata hisia kwamba walikuwa wamekwenda kule kuwatetea wananchi wa Zanzibar ambao, kama Katiba Inayopendekezwa ingelipita, basi uhuru, historia, mila na hata silka zao zingebaki katika huruma ya mtawala. Zanzibar ikatoswa.

Katiba Inayopendekezwa na Maafa Dhidi ya Zanzibar

Tatu ni vyema tuangalie, kwa muhtasari tu, kile ambacho viongozi ambao leo wanamlaumu Profesa Kabudi walikikubali kiendelee milele dhidi ya Zanzibar kwa kupitia Katiba Inayopendekezwa. Kwa ufupi wao walishakubali kuidhalisha Zanzibar kwa kiwango cha kuiangamiza Zanzibar kwa kukubali Katiba Inayopendekezwa.

Waliyoyakubali dhidi ya Zanzibar kupitia Katiba Inayopendekezwa hayawezi hata kuwekwa katika mizania moja na aliyoyasema Profesa Kabudi, hasa ikizingatiwa kwamba aliyoyasema Profesa Kabudi ni maoni yake ndani ya Bunge, wala sio Katiba, sio Sheria, sio Kanuni wala Muongozo.  Yale waliyoyakubali wao ni Katiba ya Taifa ambayo yasingeweza kubadilishwa isipokuwa kwa utaratibu ambao wao na wananchi wote wa Zanzibar hawana mamlaka nao. Ndio maana, mimi ninasema ilikuwa Katiba ya Kuiangamiza Zanzibar.

Miongoni mwa mambo waliyoyakubali chini ya Katiba Inayopendekezwa ni kama yafuatayo:

Mamlaka ya Rais wa Muungano kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na sehemu nyengine

Kwa mujibu wa [IBARA YA 2(2)] inaposomeka na ibara ya 83 ya Katiba Inayopendekezwa, Rais wa Muungano anakuwa na mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu [wadi na shehia].  Chini ya mamlaka hayo, anao uwezo wa kuongeza na kupunguza mikoa, anao uwezo wa kuiunganisha mikoa na kuwa mkoa mmoja. Chini ya mamlaka hayo, hakuna kinachomzuia Rais wa Muungano kuifanya Zanzibar kuwa mkoa mmoja au hata wilaya mmoja.

Waliokubali hilo walikuwa wakijua historia ya suala hilo. Kwamba Katiba ya Zanzibar ya 1979 iliwahi kuweka kifungu kama hicho kwa sababu ya mfumo wa chama kushika hatamu, ambapo katibu wa mkoa wa chama alikuwa pia ndiye mkuu wa mkoa.  Hivyo Rais wa Zanzibar hakuwa na mamlaka peke yake kuunda mkoa, kwani akiunda mkoa wa kiserikali alikuwa anaunda mkoa pia wa kichama.

Hata hivyo, mfumo huo ulipoondolewa, Katiba ya Zanzibar ya 1979 ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria namba 9 ya 1982 ambayo ilirejesha mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu mikononi mwa Rais wa Zanzibar. Walioikubali Katiba Inayopendekezwa wakati wakijua kuna kifungu kama hicho, sijui walikusudia kumshikisha nani hatamu dhidi ya Zanzibar?

Ukuu wa Katiba ibara ya 9

“[9(1)          Katiba hii ni Sheria Kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba hii.”

Kifungu hichi cha Katiba Inayopendekezwa kinazua masuala kadhaa ya msingi ambayo kwa mtu anayesimamia maslahi ya Zanzibar hawezi kukibali. Maswali hayo ni pamoja na:

  1. Katiba ya Zanzibar nayo ni Sheria sawa na Sheria nyengine kwa madhumuni ya ibara ya 9(2) ya Katiba Inayopendekezwa? Kwa mujibu wa ufafanuzi uliowahi kutolewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Katiba ya Zanzibar ilichukuliwa kuwa sawa na sheria nyengine na hivyo haikutakiwa kupingana na Katiba ya Muungano, yumkini hata katika mambo yasiyo ya Muungano, kama kwamba Katiba ya Zanzibar inatokana na Katiba ya Muungano wakati inatokana na Hati ya Muungano;
  2. Je, Katiba Inayopendekezwa ikipita, kifungu cha 2A cha Katiba ya Zanzibar kinachotamka kuwa Zanzibar ni nchi kitahitaji kurekebishwa au kitabatilika wenyewe kwa kufuata masharti ya ibara ya 9(2)?
  3. Ibara ya 9(4) ya Katiba Inayopendekezwa inaeleza kuwa sheria, mila na desturi lazima zifuate Katiba hiyo [inayopendekezwa]. Je, sheria ni pamoja na Sheria za Kiislamu na je, matumizi ya Sheria za Kiislamu ni suala la Muungano?
  4. Je, mila na desturi za Zanzibar ambayo ndiyo sehemu ya utamaduni wa Zanzibar zinafungwa na ibara ya 9(4)? Kama ni hivyo, mila na desturi za Zanzibar zitaendelea kuwa salama iwapo zitapingana na Katiba Inayopendekezwa?
  5. Kama Katiba Inayopendekezwa ndiyo kuu kwa mambo yote, je, kutakuwa na haja ya kuwa na Katiba ya Zanzibar? Na kama itakuwepo, itakuwa na nguvu ya kikatiba au sheria sawa na sheria nyengine?

Pamoja na hatari hiyo ya kuathirika mno maslahi ya Zanzibar, bado kifungu hicho kilikubaliwa na wale ambao leo wanamlaani Profesa Kabudi.

Itaendelea…


Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles