Katika wiki iliyopita, vyombo vya habari nchini Tanzania vilijawa na habari na tahariri kuhusu marais wawili wastaafu wakiwa kwenye jukwaa la viongozi wastaafu wa Afrika nchini Afrika Kusini.
Katika mkutano huo, ambao marais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete walialikwa kujumuika na wastaafu wenzao barani Afrika kuzungumzia mambo yanayoliathiri bara la Afrika, waliripotiwa kuisemea vizuri demokrasia, utawala bora na uongozi uliotukuka.
Kwa sababu tatu maalum, nitamuwacha Rais Mkapa kwenye uchambuzi wa leo, na nitajikita kwa Rais Kikwete: moja, ni Kikwete ambaye alichukuwa nafasi zaidi kwenye kurasa za magazeti ya nyumbani, na husemwa kuwa nyongeza huenda kwenye fungu.
Mbili – na pengine ndio iliyosababisha hiyo ya awali – Kikwete si mkuukuu sana kwenye uongozi. Huyu ameondoka majuzi tu madarakani kumpisha Rais John Magufuli, na ndio maana hadi sasa pakifanywa mlinganisho, wachambuzi huwapima wawili kwenye mizani moja wakidadisi nani kamzidi nani kwenye nini.
Kuna hata walioona kuwa kauli ya Kikwete ya Afrika Kusini na ile ya Magufuli akiwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni, zilikuwa majibizano ya moja kwa moja. Mmoja akitumia jukwaa la Gauteng kurusha dongo nyumbani dhidi ya utawala unaowachukulia wapinzani kuwa maadui na unaoliminya bunge, huku mwengine akitumia jukwaa la nyumbani kukumbushia uongozi wa ovyo ulioilitia taifa hasara ya matrilioni ya shilingi kwa mikataba mibovu “ya kijinga na kipumbavu”.
Na sababu ya tatu ni kuwa kuna masuala aliyoyazungumzia Kikwete ambayo yanahusu moja kwa moja kesi ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 uliofanyika wakati yeye akiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenyekiti wa chama tawala cha Mapinduzi (CCM) na pia amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Kwa ufupi, akiwa kwenye kilele cha nguvu, madaraka na maamuzi.
Kwenye jukwaa la viongozi wastaafu, Kikwete alizungumzia mambo matatu muhimu aliyoyaita kuwa ni mihimili muhimu kwa demokrasia na utawala bora barani Afrika: vyama vingi, chaguzi, na mabunge. Kwa sababu ya uchache wa muda, nitaepuka kuyajadili aliyoyasema kwenye vyama vingi na mabunge na nitabakia na moja tu – la chaguzi.
Na kwa maslahi ya uchambuzi, naomba hapa niweke tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi ya kile alichokizungumza yeye kwa Kiingereza kwenye jukwaa hilo:
“La pili (muhimu katika demokrasia na utawala bora barani Afrika), ni chaguzi za kawaida za kidemokrasia. Afrika inafanya chaguzi hizo. Hakuna shaka kwenye hilo. Suala sasa ni namna inavyofanya chaguzi hizo. Je, ni chaguzi za kweli, au za aibu, au za mashaka?
“Hapana shaka, daima kunakuwa na wachunguzi wa chaguzi, na tumeona kwenye ripoti zao… ukiwa unafuatilia ripoti hizo, kuna maendeleo fulani. Kwenye chaguzi za mwanzo kunakuwa na matatizo. Waangalizi wa ndani na wa kimataifa wanatoa mapendekezo, tume za chaguzi zinafanya marekebisho.
“Bila shaka, kuna maeneo ambayo kuna matatizo kwenye chaguzi…Kuna tatizo ambalo naliona, na ambalo hatuwezi kujidai kuwa halipo. Kumekuwa na utamaduni wa kutokukubali kushindwa. Hili ndilo tatizo jengine tulilonalo barani Afrika. Katika migogoro mingi tunayozungumzia barani Afrika, ina chimbuko lake kwenye chaguzi. Ni baada ya uchaguzi, ndipo unapoona kuna matatizo kwenye nchi.
“Moja ya sababu ni ukweli kwamba kunakuwa na matatizo kwenye uandaaji wa uchaguzi kwa upande wa tume za uchaguzi (na) kwa upande wa serikali zenyewe. Lakini sababu nyengine ni pale ambapo hata hakuna tatizo lolote. Ni ile dhana tu kwamba uchaguzi ni wa huru na haki ikiwa tu ninashinda. Ikiwa sikushinda, hauwezi kuwa huru na wa haki, na kinachofuatia hapo ni kuiingiza nchi kwenye migogoro.”
Akiwa mwanajeshi aliyegeuka mwanasiasa, au ukipenda kinyume chake, Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005 kupitia uchaguzi ulioandaliwa chini ya utawala wa mtangulizi wake, Mkapa. Huo ulikuwa ni uchaguzi wa tatu wa vyama vingi, tangu mfumo huo urejeshwe nchini mwaka 1992.
Lakini siku chache kabla ya uchaguzi huo, Mkapa alikuwa ameapa kwamba angelitumia kila nguvu aliyonayo, kama kiongozi wa nchi na dola, kuhakikisha kuwa CCM inarudi madarakani kwenye pande zote mbili za Muungano, akimaanisha kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Aliyasema hayo kwenye ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam. Na ndivyo alivyofanya.
Kwa hivyo, uchaguzi uliondaliwa kumuingiza yeye Kikwete madarakani, ulikuwa uchaguzi uliokamiwa na Mkapa kwamba iwe iwavyo, lazima mshindi awe wa chama chake. Uchaguzi wa ushindi lazima, litoke jua ama inyeshe mvua!
Yaliyojiri Zanzibar, ni Mkapa kumimina vikosi vya kijeshi kuliko muda wowote kwenye historia ya nchi yetu hadi wakati huo, na hata alipoulizwa kuhusiana na hilo na Jonathan Power wa jarida la Prospect, jibu lake lilikuwa: “Kwa nini huulizi sababu ya Marekani kupeleka vifaru vyake kule Iraq?”
Huo ndio uchaguzi ambao ulimuingiza madarakani mwanajeshi aliyekuwa wakati huo mwanadiplomasia mkuu wa Tanzania, Kikwete.
Lakini hilo tunaweza kulisema pengine si kosa lake, maana yeye hakuwa rais, mwenyekiti wa chama tawala wala amiri jeshi mkuu wa nchi. Alikuwa waziri tu wa kawaida kwenye baraza la mawaziri la Mkapa na, kwa hivyo, kama kuna lolote baya kwenye kutimiza kiapo cha kuzikabidhisha serikali mbili kwa CCM, lilikuwa ni juu ya Mkapa.
Miaka kumi baadaye ulikuwa ni wakati wa Kikwete kuondoka madarakani na kuachia uongozi kwa wanaomfuatia. Kile kile kiapo alichoapa Mkapa, ndicho alichoonekana kukiapa yeye. Kwamba madhali alikabidhiwa serikali mbili – ya Muungano na ya Zanzibar, naye angelizirithisha serikali hizo hizo mbili mikononi mwa CCM, iwe iwavyo. Piga uwa, kwa Kiswahili cha wenzake wa mjini.
Uchaguzi ulioandaliwa wakati yeye akiwa rais wa nchi, amiri jeshi mkuu, na mwenyekiti wa chama tawala, ulishuhudia mchuano mkali usiopata kushuhudiwa kabla, kwa kuwa kwenye upinzani alihamia Edward Lowassa kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Naye, Kikwete, katika jitihada za kumzuwia rafikiye wa zamani aliyegeuka hasimu asiwe mrithi wake, akakanyaga kila msingi wa utawala bora, sheria na demokrasia kuhakikisha kuwa Lowassa hawi rais na Magufuli ndiye anachukuwa nafasi hiyo. Aliapa na kujiapiza kuwa hivyo ndivyo itakavyokuwa.
Wengi wanakumbuka kuvamiwa kwa kituo cha kukusanyia matokeo ya kura cha UKAWA kilichokuwepo Mikocheni, ambapo waliokuwapo walipigwa na vifaa kama kompyuta kuchukuliwa. Uvamizi kama huo pia ulikikumba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC.
Kabla ya hapo, muda mchache kabla ya bunge kuvunjwa, serikali yake ilipeleka haraka na kuupitisha mswaada wa makosa ya uhalifu mitandaoni, ambayo ilikuwa na imekuwa tangu wakati huo hadi sasa, nyundo ya kuwaangamiza wakosoaji wa watawala kwenye mitandao ya kijamii.
Yote hayo yanaweza kuwa madogo. Tarehe 27 Oktoba 2015, akiwa amiri jeshi mkuu, Kikwete alituma wanajeshi kukiteka kituo cha kutangazia matokeo ya uchaguzi wa urais wa Zanzibar kilichokuwapo Hoteli ya Bwawani mjini Unguja, na siku moja baadaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha, akatangaza kuufuta uchaguzi, ambao waangalizi wa ndani na nje walikuwa wamesema ulikuwa wa haki zaidi na uhuru zaidi kuwahi kufanyika visiwani humo tangu mwaka 1995.
Kwa nini alichukuwa hatua hiyo? Ni kwa sababu ya kile alichokieleza yeye mwenyewe majuzi Afrika Kusini: “Dhana tu kwamba uchaguzi ni wa huru na haki ikiwa tu ninashinda. Ikiwa sikushinda, hauwezi kuwa huru na wa haki, na kinachofuatia hapo ni kuiingiza nchi kwenye migogoro.”
Na, naam, Zanzibar imeingia kwenye mgogoro mwengine mkubwa sana, mgogoro ulioumbwa na mikono ya Kikwete. Sio tu kwamba demokrasia ilizuiwa kuchukuwa mkondo wake kwa maslahi ya kumfanya Kikwete arithishe serikali mbili kwa CCM kama alizoachiwa na Mkapa, bali pia imo kwenye aibu kubwa kwa katiba yake yenyewe, ambayo inaamuru nchi kuongozwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Leo hii serikali iliyopo Zanzibar ni kituko. Ina makamu wa pili wa rais lakini haina makamu wa kwanza. Ina baraza la wawakilishi lisilo na deski la wapinzani. Ina utawala wa chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Huo ndio urithi wa Kikwete, kiongozi anayejipa uthubutu leo hii kukaa jukwaani Afrika Kusini kuzungumzia demokrasia na utawala bora barani Afrika. Ndio maana wengine hupatwa na kichefuchefu tunapomsikia kwenye majukwaa ya kimataifa akizungumzia demokrasia, maana tunamjuwa kuwa anadanganya!
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 29 Agosti 2017.
Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: demokrasia, Kikwete, Tanzania, uchaguzi wa Zanzibar, utawala wa sheria, Zanzibar
