Na AHMED RAJAB
KWA muda mrefu tangu miaka ya mwisho ya 1960 nimekuwa nikizururazurura barani Afrrika nikinusanusa siasa au kusaka habari.
Nimezizuru nchi zilizokuwa na amani pamoja na zilizokumbwa na vita au mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Tangu miaka hiyo hadi leo ni mara mbili tu nilipoingia matatani.
Mara ya kwanza ilikuwa ni kwa kujitakia. Nilivunja amri ya Serikali ya Zambia iliyowazuia watu wasionekane barabarani kuanzia saa 12 za Magharibi hadi alfajiri. Kwa kuonekana barabarani saa 12 na sekunde 30 nilikamatwa pamoja na wenzangu watatu.
Wanajeshi waliokuwa na bunduki walituamrisha tuwafuate hadi kituo kikuu cha polisi mjini Lusaka. Huko walitutumbukiza ndani ya chumba cha mahabusu waliokuwa wamewekwa rumande.
Takriban wote wakikabiliwa na mashitaka ya jinai. Chumba kilikuwa cha giza na kilihanikiza harufu ya mchanganyiko wa mikojo, vinyesi, vikwapa na bangi.
Tulipojaribu kugoma kuingia ndani, wanajeshi walitwambia tushike adabu zetu au tutakabiliwa na mashtaka mazito zaidi.
Ilikuwa wakati wa utawala wa Rais Kenneth Kaunda, “KK” kwa umaarufu wake. Wiki kadhaa kabla mnamo Oktoba 1980 palifanywa jaribio la kumpindua. Ndio sababu ya ulinzi kuwa mkali Lusaka.
Mara ya pili kuingia matatani ilikuwa kwa kuonewa. Baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Luanda, Angola, na pasipoti yangu kupigwa muhuri wa kuingia nchini humo ghafla nilishikwa na watu wa usalama.
Waliipekua pasi yangu na wakaniuliza maswali yaliyokuwa na maana na mengine yasiyokuwa na maana.
Baada ya muda walinisukuma kwenye chumba walikokuwa wameshikwa watu walioshutumiwa kuingia nchini kinyume na sheria. Wengi wao walikuwa ni Waislamu kutoka nchi za Afrika ya Magharibi wenye kufanya biashara ndogondogo Angola.
Kama waliachiwa baadaye basi nina hakika wengi wao walifulizia mtaa wa Martires ulio karibu na hapo. Huko ndiko wanakoishi Waislamu wengi wanaotokea Afrika ya Magharibi.
Kireno hakizungumzwi sana mtaani humo. Huzungumzwa zaidi lugha za Afrika ya Magharibi za ki-Bambara, ki-Wolof au ki-Hausa. Kifaransa na Kiarabu pia huzungumzwa kwa sababu miongoni mwa wakazi wa huko ni wahamiaji kutoka Lebanon.
Na mtaani humo ndiko wanakobughudhiwa mara kwa mara wafanyabiashara wa Kiislamu. Wamebandikwa jina la “kinguila” kwa sababu ya kazi yao kubwa ya kuvunja sarafu za kigeni lakini polisi wanawashutumu kujihusisha na biashara za magendo.
Wengine wanasema kuwa wanaonewa tu kwa sababu ni Waislamu. Angola ina ubaguzi mkubwa dhidi ya Waislamu. Ndio maana pale uwanja wa ndege wengi waliokuwa wameshikiliwa walikuwa Waislamu.
Kilichonichongea mimi zaidi nadhani ilikuwa ziara niliyoifanya miaka michache kabla katika maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi wa UNITA, waliokuwa wakiongozwa na Jonas Savimbi.
Bila ya shaka, watu wa usalama wa Angola wakijua kwamba niliwazuru wapiganaji wa UNITAa kutokana na mahojiano na ripoti zangu kwenye kipindi cha BBC cha “Focus on Africa”.
Bahati nzuri mwenyeji wangu alibishana na kuwabembeleza watu wa usalama na baada ya saa kadhaa, kupindukia usiku wa manane, waliniruhusu niingie mjini.
Jijini Luanda nilikutana na wanadamu wa aina mbalimbali. Nilikumbana pia na maneno mawili ya Kireno yaliyokuwa yakiniandama kila niendako.
Maneno yenyewe yalikuwa “confusao” na “situacao”. La mwanzo tunaweza kulitafsiri kama “mchafukoge.”
Wananchi wa Angola, hususan wale waliokuwa hawanufaiki na mfumo wa utawala, wakikielezea kila kitu kwa kusema “confusao”, mambo mkorogo mtupu, mchafukoge. Walikuwa hawajui wafanye nini kuepukana na “confusao” iliyokuwepo.
Mambo yalikuwa msegemnege; yakenda kama hayendi. “Confusao” ilikuwa ikiwakanganya au kuwachanganya. Hiyo ndiyo iliyokuwa “situacao”, hali halisi.
“Situacao” wakiweza kuimudu, kwa kufanya mbarange, mafamba na kila aina ya hila ili waweze kujikimu kimaisha.
Walikwishazoea kuwaona mawaziri na wakuu wa majeshi wakiishi maisha ya raha na anasa. Wao wakiishi maisha ya ufukara.
Fitina iliyoikoroga Angola ni utajiri wake wa mafuta na madini. Mabilioni kwa mabilioni ya dola za Marekani yakiingia katika hazina za Serikali lakini yakitafunwa na viongozi wachache wa chama cha MPLA, kilichoundwa juu ya misingi ya nadharia ya Kimarx na kilichoporomoka kimaadili na kuwa moja ya vyama vya Kiafrika vilivyokumbwa na ufisadi.
Wananchi wa Angola wamezoea kusikia jinsi mawaziri wao wanavyonunua majumba Lisbon, Paris na London huku wengi wao wakiishi katika vibanda.
Hiyo ndiyo hali halisi, “situacao,” ya Angola. Kwenye kilele cha ufisadi huo yuko Rais Jose Eduardo dos Santos “Zedu” na familia yake, hasa binti yake Isabel, anayesemekana kuwa bilionea wa kwanza wa kike katika Afrika, pamoja na wanawe wengine na jamaa zake.
Pia wako mawaziri, majenerali wa kijeshi na vigogo wa MPLA. Hivi karibuni, miezi miwili tu, iliyopita mahakama moja ya Ureno iliamua kwamba Makamu wa Rais wa Angola, Manuel Vincente, apandishwe kizimbani kwa mashitaka ya kumhonga mshitaki wa zamani wa Serikali ya Ureno.
Inasemekana kwamba alimhonga fedha zenye thamani ya dola za Marekani 810,000 ili afifirishe uchunguzi aliokuwa akiufanya juu ya ufisadi wa Vicente alipokuwa akiliongoza shirika la Serikali la mafuta, Sonangol, baina ya 2009 na 2012. Shirika hilo sasa linaongozwa na Isabel dos Santos, binti wa Rais.
Hakuna mwanamke asiyependwa Angola kama yeye. Ingelikuwa Vicente hakugubikwa na mashitaki hayo inaaminika angelikuwa anaongoza orodha ya wagombea wa MPLA katika uchaguzi mkuu wa leo Agosti 23.
Orodha hiyo sasa inaongozwa na Waziri wa Ulinzi, Joao Lourenco, maarufu kwa jina la “JLo”, mtu mpole asiye na kibri, kinyume na viongozi wenzake wa MPLA. Kwa miaka tunaozifuatilia siasa za Angola tumekuwa tukisema kwamba dos Santos, hatobanduka kwenye kiti cha urais.
Tukiamini kuwa ni mauti tu yatayomuondoa, ama kwa kupigwa risasi au kwa kupigwa na maradhi. Tulikosea. Mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 74, ametimiza ahadi na anampisha mwengine kwenye kiti cha urais achokikalia tangu afariki Rais wa kwanza Dk. Agostinho Neto miaka 38 iliyopita. Inasemekana kwamba dos Santos akitaka mwanawe, Jose Filomeno, amrithi.
Lakini hilo halikuwezekana kwa sababu vigogo wa MPLA walimtilia guu. Ndipo bahati ilipomwangukia Lourenco, aliyekuwa akiumezea mate urais kwa muda mrefu. Safari moja katika miaka ya 1990, dos Santos aliwatania wenzake alipowaambia kwamba anafikiria kujiuzulu. Lourenço alijitokeza na kusema: “Mimi nipo”.
Maneno hayo mawili yalimponza na kwa miaka dos Santos alimtesa kisiasa. Chama cha MPLA hakitojiachia kishindwe katika uchaguzi wa leo. Lakini kinakabiliwa na changamoto kubwa, hasa za kiuchumi.
Angola inapata takriban asilimia 90 ya sarafu zake za kigeni kwa kuuza mafuta. Juu ya utajiri wake wa mafuta, almasi na madini mingine, wananchi wengi wa Angola wanaishi maisha duni.
Kuanguka kwa bei za mafuta katika masoko ya kimataifa miaka miwili mitatu iliyopita kumezidi kuuathiri uchumi wa nchi. Watu wengi wamevunjwa moyo na MPLA.
Uchaguzi wa leo ni wa mwanzo kwa vijana wengi. Ikiwa chama cha MPLA kitashinda na Lourenco akawa Rais, basi dos Santos anatumai ataendelea kuidhibiti Angola kama alivyoidhibiti kwa miaka 38 iliyopita.
Kwa kuwa anaendelea kuwa rais wa MPLA amejipangia awe na madaraka makubwa yatayomwezesha kuwateua wagombea ubunge wa chama chake na maofisa wakuu wa jeshi na polisi. Hata hivyo, mikono ya dos Santos yatafungika.
Kwanza afya yake si nzuri. Halafu anachukiwa ndani na nje ya chama chake kwa jinsi alivyoukabidhi utajiri wa nchi mikononi mwa wanawe, Isabel na Filomeno, ambaye ni mkuu wa Fundo Soberano de Angola (FSDEA), Mfuko wa Utajiri wa Taifa wa Angola, wenye akiba ya dola za Marekani bilioni 5.
Kuondoka kwa dos Santos kwenye urais huenda kukawa na athari nje ya Angola. Kwa mfano, mkwewe, Sindika Dokolo, mume wa Isabel, anakabiliwa na mashitaka Kinshasa, Kongo, kwa kula njama za kumpindua Rais Joseph Kabila. Mwezi Julai mahakama moja ya Kinshasa ilimhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la ulaghai.
Dokolo, Mkongomani aliyezaliwa na mama kutoka Denmark, amesema amehukumiwa hivyo kwa sababu anamuunga mkono mpinzani wa Kabila, Moise Katumbi. Kwa sasa hayuko jela. Anahifadhiwa na mkwewe Luanda.
Muhimu zaidi ni kwamba Lourenco atataka kuonesha kwamba yeye ndiye mwenye nguvu na atafanya mambo tofauti na dos Santos. Dos Santos aliposhika urais 1974 watu wengi walimdharau.
Wakifikiri atakuwa rais wa mpito kwa vile hakuwahi kuwa jeshini wala hakupigana dhidi ya wakoloni wa Kireno.
Ukikiangalia namna chama cha MPLA kilivyokuwa kimepangika siku hizo, mtu ambaye angepaswa kumrithi Neto alikuwa Lucio Lara, aliyekuwa katibu mkuu wa MPLA.
Lakini Lara alikuwa mwerevu. Alijua kwamba angelikuwa rais, isingefika hata miezi mitatu wenzake wangempindua. Sababu iliyomfanya afikiri hivyo ni siasa za “ugozi” za baadhi ya viongozi wenzake wa MPLA ambao akijua wasingemkubali “mulatto” kama yeye, mtu aliyechanganya damu, awe Rais.
Kwa hivyo, ni Lara aliyesababisha dos Santos awe rais. Na alipokuwa rais aliwashangaza waliokuwa wakimdharau kwa namna alivyojenga mtandao wake na kuihodhi Angola, kisiasa na kiuchumi. Aliwapiga chenga wenzake wote hasa wale waliokuwa na itikadi madhubuti ya Kimarx.
Safari hii yeye ndiye aliyesababisha kuchomoza kwa Lourenco anayeweza akawa Rais mpya wa Angola. Nimeandika kusudi “anayeweza” kwa sababu mchuano ni mkali kati ya MPLA na vyama vya upinzani, hasa cha UNITA kinchoongozwa na Isaias Samakuva, na cha Casa-Ce kinachoongozwa na Abel Chivukuvuku.
Utafiti mmoja uliofanywa karibuni kupima jinsi wananchi wa Angola wanavyoelekea kupiga kura umeonesha kwamba MPLA kitashinda kwa asilimia 38, Unita kwa asilimia 32 na Casa-Ce kwa asilimia 26.
Endapo Chivukuvuku ataamua kuungana na wenzake wa zamani wa UNITA ushindi utakuwa wao. Yakijiri hayo hamna shaka kwamba Angola mpya itazaliwa.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 23 Agosti 2017. Mwandishi wake, Ahmed Rajab, anapatikana kwa barua-pepe: aamahmedrajab@icloud.com
Filed under: SIASA
