NENO demokrasia limekuwa ni mwiba mchungu kwenye nchi nyingi zilizo duni! Nchi hizi ambazo kwa kiasi kikubwa zinashindwa kujiendesha zenyewe bila kutembeza bakuli, ombaomba, kwa mataifa makubwa zimelikataa kabisa neno demokrasia ambalo kwa uharaka ni mfumo wa kuongoza nchi kwa kuwaachia wananchi wajiamlie majaaliwa ya nchi zao.
Bara la Afrika, ambalo ndilo linaloongoza duniani kwa kuwa na nchi ombaomba, kiasi cha kuitwa jina la kebehi la dunia ya tatu, ndilo linaloongoza vilevile kwa kuikataa demokrasia pasipo kutafakari kuwa hicho kinaweza kuwa ndicho kisababishi cha hali hiyo ya uduni.
Kimaumbile bara la Afrika ni tajiri sana kuliko mabara mengine, lakini ukosefu wa demokrasia unajionesha kuwa kirusi kikubwa kinachosababisha ugonjwa wa uduni na ufukara wa bara hili.
Hilo linatokana na watawala walio wengi katika bara hili kutopenda kuwashirikisha wananchi kimaamuzi kwenye majaaliwa ya nchi zao kuhusiana na utajiri zilionao. Mara nyingi, kutokana na ukosekano wa demokrasia, utajiri wa nchi unaishia kuwa utajiri wa watawala hasa kiongozi mkuu.
Mfano mzuri ni wa nchi ya DRC iliyowahi kujulikana kama Zaire. Nchi hiyo imejaaliwa utajiri mwingi sana ambao lakini umeishia kuwanufaisha watawala tu wa nchi hiyo huku nchi na wananchi wakibaki kwenye dimbwi la umasikini unaonuka.
Enzi za kiongozi wa nchi hiyo, Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga, liliwahi kuulizwa swali kupitia kipindi cha Klabu ya Maarifa cha BBC likiuliza ni rais gani tajiri kuliko wote duniani, jibu lake lilikuwa ni Mobutu!
Maana yake ni kwamba utajiri wote wa Zaire ya wakati huo ulikuwa ni wa Mobutu! Marais wa mataifa yote matajiri duniani, kama Marekani, Ufaransa, Ujerumani na mengineyo hawakuwa lolote kwa Mobutu!
Pamoja na mataifa hayo kuhangaikia umasikini wa Zaire marais wa nchi hizo hawakuwa lolote kwa rais wa nchi waliyokuwa wakihangaika kuisaidia! Walikuwa masikini sana kwake!
Ni wazi kwamba ukosefu wa demokrasia nchini Zaire ndio uliomsaidia Mobutu, rais wa nchi masikini sana kuwa kinara wa ukwasi kwa marais hao wa mataifa tajiri sana duniani.
Kwa upande mwingine tutaona kwamba nchi ya Zimbabwe, kipindi inaitwa Rhodesia, ilikaliwa na walowezi wa Kingereza kwa muda mrefu.
Wananchi wazalendo wa nchi hiyo wakapigana kufa na kupona, sababu mojawapo kuu ikiwa ni kuipata demokrasia ambayo ingewawezesha kufanya maamuzi juu ya majaaliwa ya nchi yao. Ikafikia kipindi walowezi wakanyoosha mikono, hiyo ni mwaka 1980.
Lakini badala ya demokrasia iliyotafutwa kwa udi na uvumba Wazimbabwe wakaishia kumpata Robert Gabriel Mugabe. Yanayofanywa na Mugabe nchini humo kwa sasa hayana tofauti na yaliyokuwa yakifanywa na Ian Douglas Smith, kiongozi wa walowezi.
Wakati Smith hakutaka wananchi wazalendo walio wengi washiriki kwenye demokrasia, hakihofia wingi wao kumuangusha katika kuutafuta mustakabari mwema wa nchi yao, Mugabe hataki wazalendo walewale wapige kura ya kumkataa.
Hiyo inajionesha kwamba kuwalazimisha watu wapige kula ya matakwa yake haina tofauti na kuwazuia kupiga kura. Ni bora kuwazuia kupiga kura kuliko kuwalazimisha kupiga kura dhidi ya matakwa yao.
Kama tunakumbuka tutaona kwamba Zimbabwe ya Ian Smith, Rhodesia wakati huo, ilikuwa imenawili sana kulinganisha na Zimbabwe ya wakati huu chini ya Mugabe. Ndiyo maana mara tu baada ya walowezi kung’olewa Zimbabwe ilianza kutoa misaada kemkemu kwa Tanzania kikiwemo chakula.
Lakini Zimbabwe ya wakati huu imedhoofika sana kiasi kwamba utakuwa ni muujiza kusikia ikitoa msaada wa aina yoyote.
Wakati hali ikiwa hivyo, rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe, bado ni mmojawapo wa marais tajiri sana duniani kiasi cha hivi majuzi kutoa dola 60,000 kama zawadi ya siku ya kuzaliwa kwa shemeji yake Junior Gumbochuma!
Kitu cha aina hiyo hakikuwahi kufanywa na Ian Smith, yeye alitaka utajiri wa Zimbabwe uinufaishe Zimbabwe na sio kuwanufaisha tu mashemeji na ndugu wa karibu kama tunavyoona kwa sasa kwa kiongozi aliyesadikika ndiye mzalendo wa nchi hiyo.
Kwahiyo kwa kiasi kikubwa ni kweli kwamba demokrasia inaogopwa katika nchi duni kwa vile inaelekea kuyaondoa maslahi mikononi mwa wachache, hasa watawala, na kuyaweka mikononi mwa umma kitu kinachoonekana kuwakera watawala walio wengi.
Yapo maneno yanayosemwa kinyemela, kwamba kiongozi fulani kafanya vizuri kwenye uongozi wake hivyo anasitahili kuendelea kupewa nafasi yakuongoza kinyume na matakwa ya muongozo wa nchi, Katiba.
Maneno ya aina hiyo yanasikika sana kwenye nchi hizi duni, haijawahi kutokea kwenye nchi tajiri, ambazo kwa lugha nyingine tunaziita nchi zilizoendelea, kwamba kiongozi aliyefanya makubwa na mazuri aendelee kuongoza kinyume cha Katiba ya nchi yake.
Ieleweke kwamba uzuri wa kwanza wa kiongozi, hapa nitoe mfano wa rais, ni kuuheshimu utaratibu alioapa kuulinda. Rais anaapa kulinda Katiba ya nchi. Haijawahi kutokea rais akaapa kuyalinda mazuri atakayofanya, sababu hayo ni mengineyo.
Rais anayekubali kuongezewa muda wa uongozi, hata awe amefanya kitu gani, hapaswi kuonekana ni rais bora. Sababu anakuwa amekiuka kiapo chake, historia inapaswa kumchukulia mtu wa aina hiyo kama kiongozi aliyekuwa hafai hata kidogo.
Nchi kubwa na tajiri sana duniani, Marekani, inakuwa hivi ilivyo kutokana na kuiheshimu demokrasia na Katiba yake. Haijawahi kushawishika kuibadili Katiba kutokana na uzuri wa rais anayekuwepo.
Wamepita marais wengi wazuri kama kina George Washington, Abraham Lincolin, Theodore Roosevelt, Franklin Pierce, JFK, Bill Clinton, Barack Obama na wengineo, lakini Katiba ya nchi hiyo haikubadilishwa ili waendelee kutawala.
Tuiheshimu demokrasia kwa mustakabari mwema wa nchi zetu.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo anayepatikana kwa anwani ya barua-pepe prudencekarugendo@yahoo.com na simu nambari +255 784 989 512
Filed under: SIASA Tagged: demokrasia, kura, nchi, taifa
