Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Magufuli anawauzia Watanzania tamaa ya maendeleo kwa gharama ya demokrasia yao

$
0
0

Kwa hakika, Rais John Magufuli anaonekana kuwalazimisha raia wake kufanya naye biashara ya gizani. Yeye awauzie maendeleo, nao wamlipe kwa gharama ya demokrasia angalau hadi mwaka 2020 wakati wa kampeni za uchaguzi mwengine.

Lakini je, biashara hii inawezekana kwa taifa ambalo lilishaonja ladha ya demokrasia kwa robo karne nzima mtawaliya? Je, ili kupata maendeleo ni lazima kuitia rehani misingi ya kikatiba, mgawanyo wa madaraka, haki za binaadamu na uhuru wa mtu binafsi?

Akizungumzia dhana ya demokrasia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anasema: “Demokrasia haihusiani pekee na ile siku moja kila baada ya miaka minne au mitano pale panapoitishwa chaguzi, bali inahusiana na mfumo wa serikali unaohishimu mgawanyo wa madaraka, uhuru wa mawazo, wa kidini, wa kujieleza, wa kujiunga na kujikusanya na pia utawala wa sharia. Utawala wowote unaokanyaga misingi hii, hupoteza uhalali wake wa kidemokrasia, hata kama awali uliingia madarakani kwa kushinda uchaguzi.” (Tafsiri ni yangu).

Dk. Chris Sausman, Mkurugenzi wa Chime Communications Group, anayatafsiri maendeleo kwa umbo la pembe tatu. “Kwanza ni mchakato ambao ndani yake muna mkururo wa hatua zinazopelekea – au zinazotegemewa kupelekea – matokeo ya aina fulani makhsusi, pili ni mkakati ndani ya mipango na sera na, tatu, ni matokeo ya mikondo miwili ya kwanza kupitia kiwango cha mtu binafsi – pale anapokuwa na kuutumia uhuru wake, kiwango cha jamii – pale inapoweza kutoka hatua moja ya kimaisha kwenda nyengine na kiwango cha kiuchumi – pale uchumi wa jumla unapoimarika.” (Tafsiri ni yangu).

Na Mohammed Ghassani

Namna dhana hizi mbili za demokrasia na maendeleo zinavyoungana zinatuambia kuwa biashara anayoifanya Rais Magufuli na Watanzania haitakuwa na mwisho mwema, hata kama sasa kunatolewa takwimu za mapambio.

Kama anavyosema Mkuu wa Madhehebu ya Shia Ismaili duniani, Aga Khan, “kimsingi maendeleo na demokrasia vimeungana na kuimarika kwa thamani ya maisha ya binaadamu. Uwezo wa kuifahamu (na kuihishimu) mifumo ya kikatiba, uwepo wa vyombo vya habari huru na vyenye kujumuisha wote, asasi imara za kijamii na dhamira ya kweli katika kuelekea utangamano na majadiliano ya kijamii. Hii ndiyo misingi mikuu ya kufikia lengo la maisha bora. Demokrasia inaweza tu kudumu kama inaonesha, muda wote na mwahala mote, kwamba ni njia bora kabisa ya kufikia lengo hilo.” (Tafsiri ni yangu).

Tanzania inapitia kwenye moja ya vipindi vigumu sana vya historia yake ya hivi karibuni. Baada ya kujaribu kuujenga mfumo wa kidemokrasia kwa miongo miwili na nusu, sasa jitihada hizo zinarudi nyuma kwa kasi ya ajabu.

Misingi mikuu ya demokrasia inashambuliwa kila uchao na serikali ya Rais Magufuli, akiamini kuwa ana uhalali wa kufanya lolote atakalo kwa kuwa tu madaraka ya juu yamo mikononi mwake.

Hata miaka miwili haijatimia vyema tangu ale kiapo cha utiifu kwa Katiba, Rais Magufuli ameshathibitisha kuwa yeye si muumini wa misingi mikuu ya Katiba yenyewe, kama vile mgawanyo wa madaraka na hishima kwa uhuru na haki za binaadamu.

Kwa mfano, mara kadhaa muhimili wa utawala kupitia kwake na wateule wake, umekuwa ukiingilia muhimili wa bunge kuwafunga midomo wabunge, kuzima mijadala yenye maslahi kwa taifa na hata kuzuwia matangazo ya bunge hilo kuoneshwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa, ambayo inaendeshwa kwa kodi ya wananchi.

Wakati akizuwia matangazo hayo kwa kisingizio cha gharama na kubana matumizi ya serikali na pia kuwapa muda wananchi kufanya kazi, shughuli za kisiasa zake na za chama chake, CCM, hupewa nafasi ya kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya umma, vinavyolipiwa kwa fedha ya umma na katika wakati wa kazi.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, wabunge kadhaa wameshakamatwa, kupigwa, kuwekwa vizuizini na hata kufungwa jela, na katika baadhi ya mifano wakiwa ama bungeni au majimboni mwao katika shughuli zinazohusiana na nyadhifa na madaraka yao kama wabunge na au viongozi wa vyama vyao.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, Rais Magufuli ameshatoa kauli kadhaa zinazoingilia moja kwa moja uhuru wa mahakama na vyombo vyengine vinavyohusiana moja kwa moja na upatikanaji haki kama vile ofisi ya mwendesha mashitaka, polisi na idara za upelelezi, kwa kuwatia hatiani hadharani wale wote anaowashuku.

Matokeo yake, kwa kuwa tuna aina ya Katiba inayompa mkuu wa nchi nafasi ya uungu mtu, walio chini yake kwenye vyombo hivyo wanajipendekeza kuigeuza kila “kauli ya rais” kuwa ukweli, hata kama kwa kufanya hivyo wanazikanyaga sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea wenyewe kama taifa.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, Tanzania imejikuta ikirejea kwenye zama za giza – ikitajwa kuwa na matukio ya utekaji nyara, upoteaji watu, ukamatwaji ovyo ovyo unaofanywa na vyombo vya dola, na hata mauaji dhidi ya raia na pia dhidi ya askari wetu, ambao wana jukumu la kuwalinda raia hao.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, kesi kadhaa zimefunguliwa na serikali yake dhidi ya wananchi wa kawaida wanaotumia mitandao ya kijamii kuelezea maoni na mawazo yao kuhusiana na mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya nchi. Sambamba na hilo, magazeti kadhaa yamefungiwa na vyombo vya habari vimevamiwa na waandishi wa habari kushambuliwa, kupigwa na hata kuwekwa ndani, wakati wakiwa kwenye majukumu yao ya kukusanya na kusambaza habari.

Ndani ya kipindi hiki kifupi, Rais Magufuli ameirejesha Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja kwa kuzuwia shughuli zozote za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na hata ya ndani, sikwambii maandamano na midahalo ya kitaifa hadi mwaka 2020, kwa kile anachodai ni kumpatia muda wa kutekeleza ilani ya chama chake aliyoinadi kwenye kampeni za uchaguzi wa 2015.

Mara kadhaa, polisi yake imewatia nguvuni viongozi wa upinzani wakiwa kwenye shughuli zao za kisiasa, ingawa haifanyi hivyo kwa viongozi wa CCM wakiwa kwenye shughuli kama hizo.

Tumeshuhudia kiwango kikubwa kabisa cha kukosewa hishima taratibu za kinchi kwenye teuzi, utenguwaji, utendaji na hivyo uwajibikaji wa watumishi wa sekta ya umma. Kila mmoja, kutoka raia wa chini kabisa hadi afisa wa juu serikalini, anaishi kwenye khofu ya kulengwa na kuandamwa si kwa sababu ya makosa anayoyatenda, lakini kwa sababu ya ‘hisia’ za mtawala mkuu wa nchi, ambazo nazo hutokana na taarifa zisizo sahihi anazofikishiwa na wale alioamua pekee kuwaamini na kuwakubali ‘ukweli’ wao.

Kila mtu na kila taasisi ambayo ni tishio kwa ‘ukweli wa hisia’ za mtawala, basi haiko salama. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo viliisababisha kwa mara ya kwanza CCM kushindwa kupata asilimia 60 ya kura za urais ndani ya miaka 25 vinanyanyaswa kusudi na vyombo vya dola.

Chama cha Wananchi (CUF) ni mmoja wa wahanga wakubwa wa kipindi hiki kifupi cha utawala wa Rais Magufuli, kwa kuwa kinaonekana kukataa kuwa sehemu ya ‘ukweli wake wa hisia’ kwamba rais pekee ndiye anayemiliki maoni, mawazo, na njia sahihi kwa kila kinachojiri, likiwemo suala tete la ‘uhuni’ uliofanywa na CCM na vyombo vya dola dhidi ya maamuzi sahihi ya wananchi wa Zanzibar ya tarehe 25 Oktoba 2015.

Kwa ufupi, ndani ya utawala huu wa awamu ya tano, misingi ya kidemokrasia, kama ilivyotajwa hapo juu na Kofi Annan, inakanyagwa na utawala wa Rais Magufuli. Yote kwa jina la kumpa yeye nafasi ya kuleta maendeleo aliyoyaahidi kwa wananchi.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 24 Julai 2017.

 


Filed under: KALAMU YA GHASSANI Tagged: demokrasia, haki za binaadamu, jamhuri ya muungano wa tanzania, John Magufuli, maendeleo

Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles