SI sahihi sana kumuingiza Rais John Magufuli katika chungu kimoja tu cha kuukosoa utendaji wake wote. Yapo ambayo anapatia, na kwa nionavyo, kwa hayo, amekuwa mfano kwa viongozi wengine.
Mapambano yake dhidi ya ufisadi, ni mfano, ingawa kiutekelezaji zipo kasoro hizi ni na zile. Kuonesha jinsi gani yapo mazuri, wakati mwengine husababisha aibu na fedheha isiyosemwa kwa tawala zilizopita.
Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya mambo, rais hatendi vizuri. Hii dhana ya kutambua na kuheshimu “uhuru wa kutoa maoni” na baadhi ya haki za binaadamu ipo shidani.
Kauli yake ya hivi karibuni akiwa katika ziara ya Mkoa wa Pwani, alichokizungumza zaidi akimlenga mwanasiasa Edward Lowassa na ya wale Masheikh na kutoka Bara na Zanzibar walioko ndani kwa karibu miaka minne sasa, inachanganya na kuogofya.
Namna anavyoendelea kukoroga katika baadhi ya mambo, unaweza kusema ni kama vile mtu anayevaa kinyago na kukivua; akikivua huonesha ubora wa uongozi wake lakini akikivaa, huwa mtu mwingine.
Anasema, “Niwaombe wanasiasa wajifunze kuchunga midomo yao… unakuta kiongozi anasema waondolewe lock up (mahabusu), hajui kuna wengine wale wabaya walikaa Guantanamo Bay kuliko hata mwaka mmoja.”
Ukiichambua kauli hii kiudadisi unauona utata. Anawatisha wanasiasa wengine, hasahasa wa kambi ya upinzani. Ni vitisho vinavyolenga moja kwa moja kuubinya uhuru wa kutoa maoni na kuzikaidi haki za binaadamu.
Amewahi kuwaonya waache kuropokwa. Kilichowazi anawatisha wasitumie uhuru wao wa kuzungumza, kwa sababu huko nyuma pameshuhudiwa marufuku ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Suala la maonyo ya namna hii si kingine ila ni uleule muendelezo wa ubabe. Anaelekea kutaka kuyamazisha wasiokuwa upande wake kifikra na kimaono. Kwa muda sasa, ndani ya uongozi wa awamu ya tano, kumekuwa na dhiki iliyoambatana na hofu katika watu kutoa maoni.
Bali Tanzania ni jamhuri iliyo huru. Hata katiba yake – Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 – na ile ya Zanzibar – Katiba ya Zanzibar ya 1984 – zinaelekeza uhuru wa watu kutoa maoni na kuwa huru katika kujishirikisha kwenye maongozi ya nchi yao.
Ni desturi ya wanaadamu kutofautiana maoni. Na si lazima mtu kukubaliana na kauli ya mwanasiasa fulani, au hata raia tu. Hata hivyo, kutokukubaliana hakuifuti haki ya kuzungumza kwa namna ya kutoa maoni binafsi.
Pia katika kauli nyengine isiyovutia ni pale aliposema: “Wanashikwa hawa wanaohusika na mambo ya ajabu katika nchi.” Hivi hapo wanalengwa wananchi waliozuiwa na vyombo vya dola kwa miaka minne sasa? Kama ni hivyo, basi picha inayopatikana ina maana wamehukumiwa.
Masheikh wanaotambulika kuwa miongoni mwa viongozi na walimu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (UAMSHO), walikamatwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2012, kwenye mazingira ya mji wa Zanzibar.
Wakafunguliwa kesi Mahakama ya Vuga, Zanzibar, lakini baadaye wakaunganishwa na kesi iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Tangu hapo hakujatolewa ushahidi wowote dhidi yao.
Yumkini ndio sababu hasa ya Lowassa – kama wanavyolalamika na kushauri wanasiasa na wanajamii wengine mbalimbali nchini wakiwemo watetezi wa haki za binaadamu – akalisemea suala hili. Kwa maoni yake hayo, anaendelea kuripoti makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Amehojiwa.
Sibishani na kiongozi. Hata kidogo. Mimi ninahofu tu kwamba hivi ikitokea mahakama imeamuru waachiwe kwa kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani, hapo kesi itakapokuwa imesikilizwa, itakuaje?
Jambo jingine hapa ni kwamba siioni sababu nzuri ya kufananisha mahabusu za Tanzania na ya Guantanamo inayodhibitiwa na Marekani. Hazifanani kwa asili na dhamira. Labda kama ndio dunia inapelekwa kuamini hivo.
Inajulikana gereza la Guantanamo, lilivyo na sifa ya kuvunja haki za binaadamu ikianzia na kushilikilia watu pasina kuwashitaki, hadi kuwatesa kupitiliza mpaka. Hivi ni sifa jamhuri kujifakharisha kwa hayo?
Mamia ya watu wamekuwa wakishikiliwa Guantanamo tangu 2002 baada ya gharika ya Septemba 11, 2001 au (9/11) ya mashambulizi ya ndege za Marekani katika miji ya Washington lilipo jengo la Pentagon yalipo makao makuu ya Wizara ya Ulinzi, na New York penye Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTC).
Wengi hawakupelekwa mahakamani kushitakiwa. Wapo idadi fulani wameachiliwa kwa shinikizo za serikali za kigeni zenye raia zake huko.
Afadhali ninaojadili wanapelekwa mahakamani hata kama kesi zao zinasuasua. Basi huo si mfano mzuri wa kuuchagiza kama jamhuri inautashi wa kuendelea kuaminisha ulimwengu kuwa inafuata katiba, inatambua na kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama, alitaka kulifunga Guantanamo kwa kuanza kuwaachia wafungwa waliokuwepo. Aliamini kisheria haikubaliki kumshikilia mtu bila ya kumshitaki halafu serikali ikajinasibu inaongoza kwa kufuata utawala wa sheria.
Mmoja wa maafisa katika utawala wa Rais wa 43 Marekani, Geroge W. Bush, anasema: “Wengi wa walioshikiliwa Guantanamo Bay walikuwa ni watu wasio na hatia, walisombwa na Jeshi la Marekani, pale waliposhindwa kutofautisha kati ya maadui na raia wasiokuwa na silaha.”
Ule msemo wa vita havina macho, ndio hasa kilichotokea kwa mujibu wa maelezo ya afisa huyu. Watu walibebwa na kupelekwa magerezani kwa sababu tu jeshi lilishindwa kutofautisha raia na adui waliokuwa wanapambana nao.
Mwanasiasa wa Chama cha Republican, Lawrence B. Wilkerson, aliliambia Shirika la Habari la Associated Press (AP) la Marekani: “Guantanamo Bay bado wapo watu wasio na hatia wanashikiliwa. Baadhi wako kwa miaka sita au saba.”
Kwa hivyo, walichokifanya Marekani, ni kama kuwa na nyavu, ukaipitisha mtoni. Unashika kambare wadogo kwa wakubwa, mikunga wanene na wembamba, hadi tope na uchafu navyo vinakuwemo. Hiyo ndiyo elimu kuhusu suala hili.
Haistahili magereza ya Tanzania kufananishwa na Guantanamo. Masheikh wa Zanzibar waliwahi kutoa tuhuma kuwa ndani ya kukamatwa kwao Zanzibar na kusafirishwa Dar es Salaam, mpaka kuhifadhiwa gerezani Segerea, wamepata kudhalilishwa, ikiwemo kupigwa na kuteswa, lakini haraka na kwa sauti nzito serikali ilikanusha.
Masheikh waliopo gerezani bila ya kuhukumiwa tangu hapo, wakiwa wanapelekwa mahakamani kila baada ya wiki mbili hivi, kuwataja kuweza kuhusika na mauaji yanayoendelea mkoani Pwani, ni hatua inayojenga picha isiyoeleweka na isiyoaminika.
Wakati natambua mchango wa Rais katika kudhibiti ufisadi, ni muhimu ashauriwe kuwa inastahili kuongoza huku akiamini wananchi kufaidi uhuru wao. Waseme walionalo. Inasaidia kuwatumainisha kuwa nao ni sehemu ya watoa mamlaka inayoongoza.
Wananchi wanahitajika kukuza uchumi kupitia shughuli zao mbalimbali. Ndio walipa kodi wakubwa, kodi ambayo ndio nguzo kuu ya kuiwezesha serikali kuhudumia jamii. Maendeleo ni hatua, ambazo lazima zipigwe kwa kushirikisha kila mtu. Serikali peke yake haiwezi kufanikisha maendeleo.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017. Mwandishi wake anapatikana kwa simu nambari +255 657 414 889
Filed under: SIASA Tagged: Guantanamo, haki za binaadamu, Magufuli, Tanzania, Uamsho, Zanzibar
