TUKIO la Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Mwinyi Usi Makame kufika hospitalini kumjulia hali kijana anayefanya kazi ya utingo wa daladala aliyejeruhiwa na wahuni akiwa kazini, linajadilika.
Mwinyiusi amekwenda katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kumjulia hali Khamis Juma Mgaya, ambaye alipigwa na kundi linalofaa kuitwa machokoraa, maarufu kwa jina la Ubayaubaya, ambao ni mfano wa wale vijana wakorofi wa jijini Dar es Salaam waitwao Panya Road.
Ni vijana waliopigika kimaisha na kwa sababu shida yao kubwa ni kupata mkate wa siku, wanavamia wananchi popote wanamopita na kuwanyang’anya walichonacho. Katika harakati zao, hupora fedha taslimu, simu za mkononi na vinginevyo.
Mmoja wa machokoraa wa Ubayaubaya alipanda daladala akiwa hana nauli. Alipodaiwa nauli na utingo, au kondakta, kama anavyoitwa upande wa Bara, alibisha na kuzusha tafrani. Aliposhushwa kwa nguvu, akapanga njama kumhujumu utingo. Aliwajulisha wahuni wenzake na kumvamia na kumshambulia utingo mpaka kumjeruhi.
Kundi hili la Ubayaubaya si la leo. Limekuwepo kwa muda mrefu hata kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Likijikusanya na kufanya operesheni zake maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar. Hakuna taarifa za kuwa kundi hilo lilidhibitiwa.
Wala haikushangaza kutodhibitiwa. Serikali haijali wananchi. Inaridhia viongozi wajali tu maslahi yao na familia zao. Inajali zaidi kudhibiti madaraka kwa kujua haikuingia kwa ridhaa ya watu.
Katika huko kudhibiti madaraka, kinachofanyika kingine ni kwa wenye nafasi za maamuzi serikalini kujiingiza katika kufisidi mapato ya serikali kwa kiwango watakacho. Ufisadi serikalini unatokomezwa kwa maneno matupu.
Wanachumia matumbo yao. Ndani ya Baraza la Wawakilishi lililojadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, baadhi ya wajumbe walilalamikia vitendo vya viongozi kutosimamia dhamana walizopewa na rais. wanachokifanya ni kujihusisha na miradi ya kifisadi kwa kutumia mgongo wa ofisi za umma.
Serikali iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kufanikiwa kuyahujumu maamuzi ya wananchi kupitia uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, iliendesha harakati nyingi za kuwabana wananchi hata kwa shughuli halali za kujitafutia kipato cha kuendesha maisha yao.
Shughuli za ufugaji zilizuiwa kwa kisingizio cha kuuweka mji katika mazingira safi. Yalitokea matukio mengi ya jitihada za askari wa serikali kupambana na wananchi wenye mifugo kama ng’ombe, mbuzi na punda. Ng’ombe na punda hutumika kwa ajili ya kubebea mizigo, moja ya shughuli maarufu zinazotegemewa kimaisha na wananchi wengi wa Unguja na Pemba.
Tukio la kijinga mwisho linalokataa kutoka kwenye kumbukumbu za wananchi, ni lile la Uwanja wa Magereza, ndani ya Shehia ya Tomondo. Askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), maarufu kwa kushiriki matukio ya kuhujumu wananchi, kama inavyoonekana kwa Mazombi, walidiriki kufyatua risasi za moto ili kukamata ng’ombe.
Picha za tukio hili zilienea mitandaoni. Milio ya risasi za moto kutoka bunduki za serikali zilizoshikwa na askari wa serikali wanaolipwa mishahara na posho kutokana na kodi za wananchi, ikirindima kuwalenga ngombe ambao yumkini walielewa wanaandamwa na wasiokuwa wafugaji wao.
Utadhani labda ng’ombe walikuwa wamevamia shamba la migomba au muhogo, walikuwa wanakimbia kuhujumiwa na askari wa serikali. Walikataa kukamatwa na kuondolewa kwenye himaya ya mabwana wanaowafuga.
Ulikuwa ni wakati ambao wafugaji walificha mifugo yao kwenye mabanda maalum. Nilishuhudia baadhi yao wakiwa wamewaficha ng’ombe kwenye vyumba vya kulala watu.
Ilikuwa ni matukio ya kihistoria ambayo hayajawahi kutokea Zanzibar – askari wenye bunduki za moto kupambana na mifugo ya wananchi iliyofungwa mabandani karibu na nyumba za wamiliki.
Haijapata kutokea zama zilizopita. Bali ilitokea mwaka jana, huku viongozi wa serikali wakitamba kuwa hakuna mfugo utakaosalimika hata ukifichwa namna gani. Inakokatazwa mifugo ni maeneo ya wilaya ya Magharibi ambayo yanajulikana kwa watu wake wengi kujishughulisha na ufugaji na kilimo.
Mifugo mingi ilikamatwa. Ikapelekwa maeneo ya vikosi vya ulinzi vya serikali. Ikahifadhiwa na wenyewe kutakiwa kwenda kuikomboa. Ukombozi huo wa mifugo ya wananchi ulifanywa kwa ngawira sio maneno.
Kwa sababu ukamataji ulifanywa holela, hata hifadhi yao ilikuwa holela. Hakukuwa na mpangilio kujua ng’ombe X ni wa nani? Alikamatwa wapi? Haikujulikana nani ana ng’ombe yupi hasa.
Ni katika uholela huo, wasimamizi wa hifadhi ya mifugo, waliruhusu malipo ya fedha kwa wenyewe waliotaka kugomboa. Lakini hakukuwa na utulivu wa mtu kupata ng’ombe wake hasa. Baadhi ya watu walilipa fedha na kuondoka na wasiokuwa ng’ombe wao. Ilikuwa ni utaratibu wa rushwa kwenda mbele. Walinzi, kwa niaba ya viongozi waliowatuma, walivuna wasichopanda. Ni rushwa iliyovunda ikinuka.
Ni matukio yaliyoenda pamoja na ya Mazombi kushambulia wananchi majumbani kwao usiku na mchana. Haya yangali yanaendelea leo. Mazombi wakitoa amri watu kulala hata saa 2 usiku. Wakipita wanatoa amri ya watu kuingia ndani.
Na pamoja na mashambulizi yao kusababisha madhara makubwa, ya watu kuumizwa ikiwemo kuvunjwa viungo vya miili yao, na kulazimika kulazwa hospitali, hakuna kiongozi hata mmoja wa serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein aliyepata kuzungukia kwenye hospitali kukagua wananchi waliojeruhiwa.
Wengi wa waliojeruhiwa walipata matibabu kwa kificho na pasina kupata fomu za kutibia (PF3) zinazotolewa kwenye vituo vya polisi. Walihofia kushughulikiwa kwa kuwa iliwahi kutangazwa kuwa wale wanaoshambuliwa wakamatwe wakifika kwenye hospitali za serikali au vituoni kuomba fomu hiyo. Wakubwa walijiaminisha kuwa anayeshambuliwa ni mpinzani.
Uendeshaji huo wa chuki katika serikali iliyowekwa madarakani kwa mabavu, ulidhuru wananchi wema waliokuwa wanaamini maamuzi yao ya kuchagua viongozi wawatakao yamehujumiwa kwa mkono wa dola kwa matakwa ya CCM.
Sasa pale serikali isiposhughulikia uovu unaofanyiwa wananchi, tena ikiwa na vyombo vya dola vinashiriki, unakwepaje kusema uovu huo ukipaliliwa na serikali? Hapa ndipo ilipo asili ya serikali dhalimu – vitisho kwa nia ya kundamiza sauti za wanyonge; hila na ubaguzi.
Basi, yule DC Mwinyiusi hakubahatisha kufika hospitalini kumkagua Khamis. Alizivaa hisia za kada mwenzao wa CCM, baba wa Khamis, Mzee Mgaya Juma. Anajulikana ni kada. Makada wa CCM hawatupani. Serikali ya CCM huwalinda kama wanavyolindwa askari wastaafu waliojiundia umoja uitwao UMAWA.
Tukio hili limenigusa kwa sababu nalichukulia kama mahsusi linalojenga picha kubwa na pana ambayo ninapoiweka kwenye pimamaji, naiona kuwa ni picha inayoifedhehesha serikali isiyo ridhaa ya haki.
Ni serikali ambayo imeingia madarakani kwa ubavu wa vyombo vya dola na kuashiria kuvunja msingi muhimu wa serikali kushika uongozi kupitia ridhaa ya wananchi kwa njia ya kidemokrasia kama inavyoelekezwa na Katiba ya Zanzibar ya 1984, inajisifu kuongoza kisheria.
Lakini, ipo kwenye rekodi ya kuwa serikali poa mbele ya vikundi vya ulinzi vinavyopita kwenye mitaa na kuvamia watu na kuwashambulia hadi kuwajeruhi miili.
Maeneo ambamo wahuni hao wanapita na kushambulia wananchi yanajulikana kuishi zaidi watu wenye mtizamo wa kuunga mkono upinzani na hasa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kwa kuwa kinapigania haki ya kuunda serikali kutokana na ushindi walioupata katika uchaguzi mkuu, kinasakamwa ili kifilie mbali.
Sema hakifi. Kigumu kama kimetengenezewa kangiriti. Wanaokiamini hawafi moyo. Wapo bega kwa bega na viongozi wa chama hicho kusubiri ifike siku haki irudishwe mikononi mwao.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017
Filed under: SIASA Tagged: CCM, ubaguzi, udhalimu, Zanzibar
