Leo ukienda visiwa vya Zanzibar utashuhudia maghorofa kuanzia Unguja mpaka Pemba, mijini mpaka mashakani, maghorofa hayo yote naambiwa yalijengwa na Hayati Mzee Abeid Karume!
Mzee Karume alijenga maghorofa haya kati ya 12 Januari 1964 baada ya Mapinduzi na 7 Aprili 1972 pale alipokutwa na umauti baada ya kupigwa risasi akiwa katika ofisi za Chama cha Afro-Shirazi maeneo ya Kisiwandui, mjini Unguja!
Mzee Karume alikuwa na kampeni ya kuhakikisha Wazanzibari wanaishi katika nyumba bora, ndiyo maana ndani ya miaka minane alijenga maghorofa kwa ajili ya makazi ya Wazanzibari.
Hayati Mzee Karume alikuwa na mkakati wa kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha utalii na pia alitaka kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha Lugha Afrika Mashariki kama siyo Afrika nzima.
Pamoja na nia njema aliyokuwa nayo Mzee Karume kwa visiwa vya Zanzibar, bado kumbukumbu/kivuli cha uchaguzi wa kwanza visiwani Zanzibar uliofanyika Julai 1957 na kufatiwa na ule wa Julai 1963 na kushuhudia muungano wa vyama vya ZNP na ZPPP vikishinda uchaguzi huu wa pili dhidi ya mahasimu wao ASP na kumchagua Mzee Shamte Mohamed Hamad kuwa waziri mkuu, uchaguzi huu ulibaki kuwa kikwazo kwa utawala wa Hayati Karume!
Kama nilivyotaja, tarehe 12 Januari 1964, ASP walifanya mapinduzi na kuuondoa utawala wa ZNP na ZPPP ambao ASP waliamini kuwa walikuwa bado wana vinasaba na Sultan. Mara baada ya kufanyika kwa Mapinduzi hayo, ili kuimarisha usalama, Hayati Karume alilazimika kwa niaba ya Wazanzibari kwa kushirikiana na Rais wa Tanganyika wakati huyo, Hayati Julius Nyerere, wakaunganisha nchi hizi mbili tarehe 26 Aprili 1964 ikiwa ni miezi mitatu tu toka yafanyike mapinduzi huko Zanzibar!
Historia inasema Hayati Mzee Karume mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar alitangaza kuwa asingependa kuona uchaguzi unafanyika visiwani Zanzibar mpaka baada ya miaka 50, kwa maana hiyo kama hili lilikuwa ni dhamira ya dhati Zanzibar ilitakiwa kufanya uchaguzi wa kwanza mwana 2014!
Pamoja na mapinduzi hayo kufanyika, utawala wa Hayati Karume ulikuwa katika upinzani mkali kutoka kwa wafuasi wa vyama vilivyoshinda uchaguzi wa mwaka 1963 (ZNP na ZPPP), kumbuka matokeo ya uchaguzi wa 1963 yalilalamikiwa sana na ASP waliodai kuwa walishinda kwa asilimia 54, ASP walilalamika kuwa waliibiwa kura! ZNP kwa ushirikiano na ZPPP waliongoza Serikali ya Zanzibar kwa miezi mitano tu (Julai 1963 – Januari 1964).
Taarifa za kichunguzi kutoka kwa wazee na waliofanya kazi na Mzee Karume wanasema baada ya mapinduzi ya Zanzibar, serikali iliweka katazo la kiwaajiri serikalini watu wasio wanachama wa ASP, ilikuwa sharti uwe ASP ndiyo utapata kazi serikalini kwa wakati huo!
Sharti hili kwa mara kadhaa liliaababisha kutokuelewana kati ya Hayati Karume na Hayati Nyerere baada ya Mwalimu Nyerere kuwaajiri ndani ya Serikali ya Muungano baadhi ya Wazanzibari ambao hawakuwa wana ASP,miongoni mwao alikuwa Prof. Abdulahman Babu kutoka chama cha UMMA!
Zanzibar pamoja na kufanya mapinduzi mwaka 1964, hayakuwaunganisha Wazanzibari, maisha ya kutokuaminiana yakiendelea, kifo cha Mzee Karume mwaka 1972 kiliongeza hofu visiwani humo, hata baada ya Mzee Aboud Jumbe kupewa madaraka ya urais wa Zanzibar baada ya Mapinduzi, Zanzibar ilipita kwenye kipindi kingine kigumu kati ya mwaka 1972-1984.
Kwenye kipindi hiki tulishuhudia vuguvugu la kuuvunja Muungano, baadhi ya Wazanzibari walianzisha kampeni za chinichini za kuuvunja Muungano kwa madai yalikuwa makubaliano ya watu wawili (Julius Nyerere na Abeid Karume).
Hata rais wake, Mzee Jumbe, inasemekana aliunga mkono vuguvugu hilo, kiliandikwa kwa siri kitabu kilichoitwa “Partnership”, kitabu hiki hakikuwahi ingia mtaani na kusomwa baada ya kukamatwa na makachero!
Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwatumia makachero zilichunguza vuguvugu hilo na mnamo mwaka 1984, bila kujua kama anachunguzwa, Hayati Mzee Jumbe aliitwa Dodoma na kusomewa mashtaka ya kutaka kuuvunja Muungano. Julius Nyerere alimsomea mashtaka yake mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mzee Jumbe akavuliwa madaraka ya Urais mjini Dodoma na kupelekwa kuishi Kigamboni alipoishi mpaka umauti unamkuta!
Wakati Mzee Jumbe anavuliwa madaraka, CCM ilimuibua Ally Hassani Mwinyi ambaye miaka mitatu iliyopita alilazimika kujiuzulu nafasi ya uwaziri wa mambo ya ndani kwenye serikali ya Muungano na kumteuwa kuwa Rais wa Zanzibar, nafasi aliyoihudumu kwa mwaka mmoja tu, kwani mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Wakati wote huo wa Mzee Jumbe akivuliwa madaraka, Katibu Mkuu wa sasa wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa kwenye Kamati Kuu ya CCM na zipo taarifa kuwa alikuwa kipenzi cha Nyerere aliyekuwa akiaminiwa sana.
Mwaka 1985, Maalim alichukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar akipambana na akina Hayati Mzee Idrissa Abdul Waziri na Dk. Salim Ahmed Salim, ingawa nasikia Salim Ahmed Salim alishawishiwa ajitoe!
Kinyan’ganyiro kilikuwa kikatiba. Maalim Seif alikuwa na mashabiki wengi. Wachambuzi wa masuala ya siasa za Zanzibar wanasema mchuano huu ulikuwa mkali kama ule wa 1957 na 1963, tofauti yake ni moja tu – huu wa mwaka 1985 ulikuwa ndani ya CCM.
CCM walipokaa Dodoma walilipitisha jina la Abdul Wakil, uamuzi huo uliwasononesha baadhi ya Wazanzibari, hususani kutoka Pemba, ambao hawakukubaliana na uamuzi wa kulikata jina la Maalim Seif. Kilichofanyika mwaka 1985, ni kwa baadhi ya Wazanzibari kuichagua sehemu ya kivuli na kutompa kura ya ndiyo Mzee Abdul Wakil.
Baada ya uchaguzi, CCM ilianza kuwasaka wasaliti walioratibu kura za maruhani, msako huu ukawanasa kwenye hatia akina Juma Duni Haji, Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed no a wenzao kadhaa ambao walijikuta wakifukuzwa ndani ya CCM.
Wafukuzwa hawa walianzisha chama chao ambacho hakikuwa kimesajiliwa kisheria. Mwaka 1992, baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza, kundi lililofukizwa visiwani Zanzibar ndani ya CCM liliungana na akina Shaban Mloo na James Mapalala kutoka Bara kuanzisha chama cha CUF, ambacho kimeendelea kuwa chama kikuu cha upinzani huko Zanzibar!
Mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, CUF kimetoa ushindani mkali kwa CCM hususani kule Pemba, mara mbili kuliibuka mtafaruku wa utangazwaji wa matokeo, ambapo mwaka 1995 kituo kimoja cha Televisheni kilimtangaza Maalim Seif kama mshindi na kikajikuta kikifungiwa kwa kukiuka sheria, na mwaka 2015, Maalim Seif aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema atangazwe mshindi hali iliyosababisha uchaguzi kufutwa na uliporudiwa CUF waligoma kushiriki.
Nadhani umeona jinsi siasa za Zanzibar zilizotufikia ngumu, kwamba tangu uchaguzi wa 1957 kumekuwa na malalamiko ya kuibiwa! Mwaka 1963, CCM wakati huo ikiwa ASP ilishindwa uchaguzi wa pili na kulalamika kuwa ilishinda kwa asilimia 54 lakini ikaibiwa kura.
Ugumu huu wa siasa za Zanzibar ndiyo uliowafanya Maalim Seif na Amani Karume kukubali marekebisho ya katiba mwaka 2010 na kuruhusu serikali ya umoja wa kitaifa.
Mpaka Juma Nature na Prof J walitunga wimbo waliouta CCM na CUF!
Mungu vibariki visiwa vya Zanzibar. Mungu ibariki Tanzania!
Tanbihi: Makala hii imeandikwa na Dotto Bulendu kwenye ukurasa wake wa Facebook leo tarehe 25 Juni 2017.
Filed under: SIASA Tagged: CCM, cuf, Dk. Shein, Karume, maalim seif, Zanzibar
