Wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, niligombea ubunge katika Jimbo la Busokelo kupitia tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo. Endapo ningechaguliwa kwa kura nyingi na kuwa mbunge niliazimia kwa dhati kupeleka muswaada binafsi bungeni kwa ajili ya kuanzisha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Kijamii kwa Wakulima (Farmers Social Security Fund – FSSF). Sikuupata ubunge baada ya kugaragazwa vibaya na mwanaCCM aitwaye Atupeele Mwakibete.
Hata hivyo, wazo la Mfuko wa Hifadhi ya Kijamii kwa Wakulima bado ninalo na nitaendelea kupigania kwa njia zingine hadi wabunge au serikali ione umuhimu wa kuwa na FSSF. Sina hakika endapo wabunge watasoma makala haya na kushawishika kuwa na FSSF, ila nina uhakika watendaji wa serikali wakisoma watapata mantiki na hamasa ya umuhimu wa wakulima katika uhai na maisha yetu ya kila siku. Bila kula hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya kazi yoyote!
Wafanyabiashara, wafanyakazi, na wengineo wanaweza kugoma; na tukaendelea kuishi. Lakini mkulima akigoma kulima na kuuza mazao yake, hata wenye pesa watashindwa kuishi kwa pesa zao. Na ijulikane vema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima na hutegemea kilimo katika maisha yao vijijini. Pia kwa wanaoishi mijini karibu wote hutegemea chakula toka vijijini. Ni chakula kidogo sana huzalishwa mijini, hasa ufugaji wa majumbani, kwa kuwa hakuna pa kulima. Ndio maana wengi wao ni wafanyabiashara na wafanyakazi.
Wafanyakazi wa serikali kuu, serikali za mitaa na wa mashirika na makampuni binafsi wana mifuko ya hifadhi ambayo huwasaidia sana kuishi vizuri wanapostaafu na hupata mikopo wakiwa bado wako kazini. Wakistaafu wanapata penseni au malipo ya uzeeni ambayo mara nyingi tunaita kiinua mgongo. Je, hivi ni nani hasa anayepinda sana mgongo na kuhitaji kuinuliwa kuliko mkulima? Inauma sana kuona mkulima akishazeeka na kupinda mgongo hana kiinua mgongo!
Lakini mifumo ya hifadhi za kijamii ina umuhimu gani?
Mifumo ya Hifadhi za Kijamii (Social Security Systems) ni mifumo ya bima za kijamii inayohusika na bima za mafao ya uzeeni na tiba kwa wafanyakazi. Mifumo hii inahakikisha kuwepo kwa ustawi wa kijamii kwa wasiojiweza, hasa watoto, walemavu na wazee, japo tunalenga zaidi mafao ya uzeeni (pensheni) au kiinua mgongo kwa wastaafu.
Neno hifadhi linatokana na neno la Kiingereza “Security” ambalo humaanisha usalama, uhakika au katika muktadha huu tunalitafsiri kuwa hifadhi. Security nalo lina asili ya neno la Kilatini liitwalo “Se-curus.” “Se” kwa Kilatini likimaanisha ukombozi (liberation) na “curus” kwa Kiingereza ni “uneasiness”; yaani kufadhaika, kukosa raha, kuwa na msongo wa mawazo, nk). Therefore, security means liberation from uneasiness – to be peaceful without any risks or threats: yaani kwa tafsiri rahisi mifumo ya hifadhi za kijamii ni ukombozi katika kukosa raha ili kuwa na amani bila hatari au vitisho.
Hivyo basi, mifumo ya hifadhi za kijamii inapaswa kumwezesha kila raia mwenye uwezo wa kufanya kazi kuishi maisha mazuri na yenye staha katika jamii iliyostaarabika. Mifumo ya hifadhi za kijamii hutoa msaada kwa mtu asiyejiweza kama vile mgonjwa, mlemavu, mfiwa, asiye na ajira na aliyezeeka. Je, mkulima anasaidiwaje akishazeeka?
Wafanyakazi wengi wana elimu, ujuzi au maarifa fulani yanayowapatia ajira yenye mishahara minono. Huendelea kupata mishahara yao hadi watakapostaafu na huondoka na kitita kikubwa kwa mkupuo kiitwacho pesheni au kiinua mgongo, na wengine huendelea kupata mishahara ya kiwango fulani hadi watakapofariki.
Ni kweli wanalitumikia taifa kwa kiwango fulani, lakini si bure kwasababu hulipwa kulingana na utaalamu wao. Ni vema tuwaite waajiriwa badala ya watumishi. Pamoja na mishahara, posho mafao manono ya uzeeni, wengine hupewa nyumba na magari ya kuendea kazini – achilia mbali marupurupu kwa kupitia vyeo au nafasi zao ofisini. Lakini je, vipi kwa wakulima wanaolisha taifa kwa jasho lao?
Je, mkulima akishazeeka nani anampongeza kwa kusaidia kulilisha taifa na kutayarisha malighafi za viwandani? Je, nani anauinua mgongo wake uliopinda kwa miaka mingi kwa jembe la mkono huku akibwia vumbi jingi mashambani?
Nini sasa kifanyike kwa jamii yetu?
Napendekeza serikali ianzishe FSSF kwa kufuata hatua zifuatazo:
- Iorodheshe wakulima wanaomiliki mashamba na wenye uwezo wa kulima kuanzia ekari moja na kuwasajili rasmi.
- Mchango wa mkulima uwe kuanzia gunia moja au kilo 100 ya mazao aliyovuna.
- Umri wa kustaafu kulima uwe miaka 80 au mkulima anapothibitika kuwa na ulemavu au maradhi ya mwili yanamfanya ashindwe kuendelea kulima.
- Mkulima aliyesajiliwa na anayechangia mavuno yake apate kibali cha kukopa FSSF fedha za kuendeshea kilimo chake.
- Penseni au mafao ya uzeeni au kiinua mgongo cha mkuliwa kiwe kinalipwa kulingana na bei ya soko kwa kila gunia au kila kilo 100 za akiba ya mazao yake wakati anapostaafu kulima. FSSF watahesabu idadi ya magunia au kiasi cha mazao alicholimbikiza na kumpa fedha taslimu kwa mkupuo.
Kwa mkulima, kama mifumo hii itaanzishwa, basi atapata faida hizi, pamoja na nyengine:
- Kukopeshwa fedha za kununulia viuatilifu, zana za kilimo na pembejeo za kilimo
- Kukopeshwa fedha za kununulia vifaa vya umwagiliaji
- Kukopeshwa fedha za kununulia mashamba mengine
- Kukopeshwa fedha za kujengea maghala ya kuhifadhia mazao
- Kukopeshwa fedha za kununulia magari ya kusafirishia mazao baada ya kuvuna na kupeleka sokoni au viwandani
- Kukopeshwa fedha za kujengea nyumba ya kuishi baada ya kustaafu kulima.
FSSF, kwa kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, wawe wanakusanya chakula kutoka kwa wakulima waliosajiliwa rasmi na kuhifadhi kwenye maghala ya taifa kwa ajili ya kutumika wakati wa ukosefu au upungufu wa chakula nchini ili kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula. Aidha, akiba ya ziada ya chakula iwe inauzwa nje au kwenye viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.
Ningefurahi sana endapo bajeti ya mwaka 2017/18 iliyosomwa jana ingekuwa mkombozi kwa wakulima wanapostaafu kulima, ili tuwaenzi walivyolilisha taifa na kutuwezesha kufanya kazi za kujenga maisha yetu, familia zetu, jamii zetu na taifa letu kwa ujumla.
TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo Mwakatobe, mchambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa anayeishi Mwakaleli, Busokelo, mkoani Mbeya. Anapatikana kwa anuani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com
Filed under: JAMII Tagged: bajeti, kilimo, mkulima, Tanzania
