WIKI iliyopita niliandika kuhusu mazungumzo waliyokuwa nayo viongozi wawili wa kizalendo wa Kiafrika jijini Accra, Ghana Machi 1958. Viongozi wenyewe walikuwa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Ali Muhsin Barwani.
Nyerere alikuwa Rais wa Tanganyika African National Union (TANU), chama kilichokuwa kikipigania uhuru wa Tanganyika, na Barwani alikuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP, au Hizbu), chama pekee kilichokuwa kikipigania uhuru wa Zanzibar kwa wakati huo.
Nilieleza kwamba walipokuwa wakizungumza katika Hoteli ya Aveneda, waliambizana shida zao. Barwani alilalamika kwamba Zanzibar ilikuwa na skuli chache.
Nyerere alimjibu kwa kumwambia kuwa shida kubwa aliyokuwa nayo yeye ilikuwa kupata magari ya kutosha ya aina ya Land Rover ya kufanyia kampeni za uchaguzi Tanganyika nzima.
Nilichozuia kukieleza wiki iliyopita ni kwamba Barwani alitoa rai ya kuziondosha shida hizo mbili kwa mpigo mmoja. Alimshauri Nyerere waende wakaonane na balozi wa Misri ya kimapinduzi hapo Accra.
Barwani alikuwa na hakika wakimueleza shida zao atawasaidia, kwa kumpatia yeye misaada ya elimu na Nyerere magari ya Land Rover.
Nyerere alikubali akamtaka Barwani apange miadi ya kuonana na balozi wa Misri. Agizo hilo Barwani alilitimiza papo hapo kwa kumpigia simu balozi wa Misri na wakakubaliana wakutane siku ya pili saa nne za asubuhi.
Yaliyojiri siku ya pili Barwani ameyaelezea hivi:
“Mapema asubuhi ya siku ya pili rafiki yangu, Nyerere, hakuwako katika chumba chake kilichokuwa kinakikabili changu hotelini. Aliondoka hotelini bila ya kuniachia ujumbe. Kwa hivyo ilinibidi niende peke yangu kwenye ubalozi wa Misri. Nilimwambia balozi kwamba labda rafiki yangu atakwenda mwenyewe, lakini mimi nikihitaji misaada ya masomo ya sekondari na ya baada ya sekondari.”
Sasa tunajua kwamba Nyerere alifanya kusudi kukwepa kwenda kwa balozi wa Misri. Ndiyo maana asubuhi na mapema alimhepa Barwani. Wakati huo Barwani hakuyajua hayo.
Kuna jambo ambalo Barwani alilibania katika kumbukumbu zake alizozimwaga katika kitabu chake “Conflicts and Harmony in Zanzibar.” Ingawa hakulisema wazi jambo hilo, aliliashiria.
Alifanya hivyo alipoandika: “Katika siku zetu zote za mapambano (dhidi ya ukoloni) Nyerere hakuwahi hata mara moja kuhudhuria mikutano ya kupinga ukoloni.” Aliongeza kwamba Nyerere akijua maslahi yake yalikuwa wapi.
Kile ambacho Barwani alibania kukitaja kinaganaga, ni kwamba Nyerere alifanya kusudi asionekane kwa sababu ya woga. Akijua kwamba wakoloni walikuwa wakimuandaa awe kiongozi mtiifu wa Tanganyika huru na hakutaka kuwaudhi.
Labda hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomvua Nyerere na shari ya wakoloni. Alikuwa miongoni mwa viongozi wachache wa Kiafrika wasiofungwa na wakoloni au hata kupata misukosuko yao.
Nyerere hakuwa mwiba kwa wakoloni wa Kiingereza kiasi cha kumfunga jela kama walivyomfunga Jomo Kenyatta wa Kenya au Abdulrahman Babu wa Zanzibar.
Ukweli ni kwamba Nyerere alikuwa akipunwa kisiasa na Waingereza. Kwa hivyo, akichelea asijiharibie jina lake kwa kujipeleka kwa Wamisri kama alivyofanya Barwani. Misri ya siku hizo haikuwa Misri ya leo iliyo chini ya mbawa za ubeberu na ukoloni mamboleo.
Misri ya enzi hizo ikiongozwa na Gamal Abdel Nasser aliyekuwa ameisabilia nchi yake kwa ukombozi wa Afrika. Akichukiwa na wakoloni.
Kwa hivyo, siku Nyerere aliyomkwepa Barwani kwenda kwa balozi wa Misri, Nyerere alifanya hivyo kwa akili zake. Akijua akifanya nini. Magari ya Land Rover akiyahitaji lakini hakutaka kufadhiliwa na Misri, adui wa Waingereza.
Akiwa bado mchanga katika harakati za kupambana na ukoloni, Nyerere hakutaka kujiharibia kwa kushirikiana na Misri ya Nasser. Unaweza kusema alikuwa mjanja. Au unaweza kumtetea kwa kusema akijua namna ya kuzicheza karata.
Kulikuwa na sababu maalum iliyomfanya Nyerere asiwakaribie Wamisri. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel alikuwa mjini. Lililompeleka Accra lilikuwa moja: kukutana na Waafrika wataokuwa viongozi nchi zao zitakapopata uhuru.
Mmojawao alikuwa yeye Julius Kambarage Nyerere. Mwengine alikuwa Ali Muhsin Barwani. Na walikuwapo wengine kutoka sehemu nyingine za Afrika.
Wote walikuwa wamealikwa Accra na Waziri Mkuu Dkt. Kwame Nkrumah kuhudhuria sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa uhuru wa Ghana.
Kulikuwa na sababu nyingine, iliyokuwa imefichwa na Nkrumah kwa kusudi, kama tulivyoeleza wiki iliyopita lakini kuhudhuria sherehe za uhuru ndiyo iliyokuwa sababu rasmi.
Kuwapo kwa Waafrika hao Accra kuliipa Israel fursa nzuri ya kuwarandia na kuwavutia upande wake dhidi ya Waarabu.
Balozi wa Israel aliandaa karamu ili Waafrika hao wakutane na waziri wake wa Mambo ya Nje. Waziri mwenyewe alikuwa Bibi Golda Meir ambaye miaka 11 baadaye aliibuka kuwa waziri mkuu wa mwanzo wa kike wa Israel.
Barwani alialikwa akutane na Meir hapo Accra. Lakini hakwenda kwenye dhifa hiyo. Nyerere alikwenda.
Nyerere na Barwani walikuwa na mitizamo tofauti kuhusu taifa la Israel. Siku hizo wananchi wa Zanzibar tayari walikuwa na mwamko wa kuipinga Israel na itikadi yake ya Uzayuni. Nakumbuka nikiwa mdogo kuziona kuta za Mji Mkongwe, Unguja, zikichorwa maneno yaliyosema “Hatutaki Masahayuni, Hatutaki Masahayuni”.
Mtoto wa umri kama niliokuwa nao siku hizo, hakuweza kufahamu matamshi hayo yalikuwa na maana gani au na historia gani. “Masahayuni” ndilo jina lililokuwa likitumiwa siku zile kuwaelezea Wazayuni.
Ingawa Barwani alisusa kuhudhuria ile hafla ya balozi wa Israel, hata hivyo alipata habari ya yaliyojiri. Rafiki yake, Mallam Aminu Kano, mwanasiasa kutoka kaskazini mwa Nigeria, ndiye aliyempasha habari hizo. Kano alikuwa kiongozi wa kisoshalisti aliyeongoza vuguvugu dhidi ya ukoloni Nigeria.
Kano alimueleza Barwani nani na nani waliohudhuria karamu hiyo na nini kilichosemwa na nani.
Kwa mujibu wa Kano, Bibi Meir aliwaambia waliohudhuria kwamba alikwenda Accra kusudi akutane na viongozi wa siku zijazo wa Afrika. Aliwaeleza kwamba Waarabu walikuwa wakijaribu kuizingira na kuisonga roho ya Israel. Kwa hiyo, Israel imekuwa na shauku ya kuwa na urafiki na nchi za Kiafrika kuwakabili Waarabu.
Meir aliongeza kwamba Israel ni nchi ndogo na mpya, lakini Waisraeli wana uzoefu wa kuviruka vizingiti. Kwa hivyo, nchi yake ina uwezo mkubwa kwa kuzipa ushauri na misaada nchi za Kiafrika zitazopata uhuru na zitazokabiliwa na changamoto kama Israel ilizokabiliwa nazo.
Golda Meir alikuwa na yake; baadhi ya Waafrika kwenye dhifa hiyo nao pia walikuwa na nayo. Pande hizo mbili zilioneshana moyo wa “nipe, nikupe”.
Nyerere hakuondoka patupu. Pamoja na maakulati na vinywaji alivyokirimiwa, alipata jingine: Waisraeli waliahidi kumpelekea magari aliyoyataka ya aina ya Land Rover ili kukisaidia chama chake cha TANU kiendeshe kampeni za uchaguzi kote Tanganyika.
Na yeye, kwa upande wake, hakufanya uchoyo. Magari hayo yalipowasili Tanganyika alikigaia walau gari moja chama cha Afro-Shirazi katika nchi jirani ya Zanzibar.
Nyerere alipokutana na Golda Meir mjini Accra, Machi 1958, ndipo yalipoanza mahusiano rasmi baina yake na Israel na, baadaye, baina ya Israel na Tanzania. Meir aliwahi kusema kwamba akiuthamini sana mchango wa Israel wa kuisaidia Afrika. Safari moja Nyerere alimueleza Golda Meir kuwa ni “mama wa Afrika”.
Tunaweza kuyagawa mahusiano baina ya Nyerere na Israel au Tanzania na Israel katika vipindi viwili. Katika kipindi cha mwanzo kilichoanza Accra 1958, Nyerere alikuwa amevutiwa na viongozi wa Israel na namna walivyokuwa wamejipangia kuiendeleza nchi yao. Siku hizo Nyerere alikuwa mshirika mkubwa wa nchi za Magharibi. Mahusiano yake na nchi za Mashariki yalianza kwa nguvu baada ya kuundwa Muungano baina ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Aprili 1964.
Katika kipindi hicho usoshalisti wa Nyerere ulikuwa ukiuigiza ule wa Israel. Hata dhana ya kuanzisha Vijiji vya Ujamaa aliifikiria na kuiendeleza kwa kuuigiza mfumo wa ujima wa kuishi mashambani katika “kibbutzim.” Mfumo, au utaratibu huo, ulizichanganya itikadi za uzayuni na za usoshalisti. Kadhalika, Nyerere alivianzisha vyama vya ushirika kwa kuvisoma vile vya Israel vya “moshavim”.
Labda Nyerere alivutiwa na viongozi wa Kizayuni wa Israel ambao ingawa walianza siasa wakiwa magaidi, lakini itikadi za takriban wao wote, zilikuwa za kisoshalisti. Viongozi hao ni kutoka David Ben Gurion, waziri mkuu wa kwanza wa Israel, hadi Shimon Peres, aliyekuwa kinyonga wa kisiasa na rais wa tisa wa Israel.
Katika kipindi hicho cha mwanzo cha mahusiano baina ya Tanzania na Israel, Nyerere alipata msaada wa Israel kila pale alipotafuta msaada kutoka huko. Hakuona kuwa ni jambo kubwa, au la aibu au la kushangaza kuwa na mahusiano hayo. Lau angelikuwa hai leo sifikiri kama Nyerere angeona kwamba alikuwa na haja ya kutaka radhi kwa kuwa na mahusiano na Israel wakati ule.
Mahusiano hayo mazuri yaligeuka ghafla baada ya Israel kuzishambulia nchi za Kiarabu katika vita ya 1967. Shambulio dhidi ya Misri lilimkera Nyerere bila ya kiasi. Alihisi kwamba aliwajibika kuyavunja mahusiano ya Tanzania na Israel.
Asitosheke bali akawa mbele kuzishajiisha nchi nyingine za Kiafrika ziwe na msimamo kama wake dhidi ya Israel.
Katika hotuba aliyoitoa mara baada ya kumalizika vita ya Mashariki ya Kati ya 1967, Nyerere alisema kwamba sera ya mambo ya nje ya Tanzania imejengeka juu ya misingi ya haki na uhuru.
Tanzania ilikuwa imekwishajitolea kupigania ukombozi wa walioendelea kutawaliwa na wakoloni Afrika na nje ya Afrika, ikiwa pamoja na kuwatetea Wapalestina wapewe haki yao ya kujitawala wenyewe. Hatua hiyo ilimjengea yeye na Tanzania sifa kubwa kimataifa. Ni msimamo alioushika hadi kufa kwake.
Nyerere wa kipindi hicho cha pili cha kutokuwa na mahusiano ya kidiplomasia na Israel ndiye Nyerere anayekumbukwa na kuliliwa wakati huu ambapo nchi yake imeingia katika kipindi kipya cha mahusiano na Israel.
Katika kipindi hiki ni Tanzania nyingine kabisa inayoyafufua mahusiano na Israel. Ni Tanzania iliouacha msimamo wake wa kutoshirikiana na serikali dhalimu.
Wenye kupinga msimamo wa sasa wa Tanzania juu ya Israel wanavunjwa nguvu na baadhi ya nchi za Kiarabu zenye kushirikiana na Israel, kwa uwazi au kwa kificho. Nchi hizo ni pamoja na Tawala za Kifalme za Ghuba (UAE) na Saudi Arabia, inayoshirikiana na Israel katika mikakati ya kuziangamiza Yemen na Syria na kuitishia Iran.
Wenye mtizamo wa kimaendeleo (progressives) wanaendelea kupigwa na butwaa wanapoizingatia misimamo ya sasa ya Tanzania juu ya Israel na juu ya Morocco, nchi ambayo bado inakataa kuipa Sahara ya Magharibi uhuru wake.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 17 Mei 2017
Filed under: SIASA Tagged: Ali Muhsin Barwani, Israel, Nyerere, Zanzibar
