China imo kwenye matayarisho ya kuchukuwa vipimo vya vinasaba (DNA) kutoka kwa raia wake waishio katika mkoa wenye Waislamu wengi na ambao umekuwa chini ya msako mkali wa vyombo vya dola, wanasema watetezi wa haki za binaadamu na wataalamu wa kujitegemea.
Polisi kwenye mkoa wa magharibi mwa nchi hiyo, Xinjiang, walilithibitishia shirika la habari la Associated Press kwamba wako njiani kununuwa vifaa vyenye thamani ya dola milioni 8.7 kwa ajili ya kuchambulia vipimo vya vinasaba.
Wachunguzi kutoka shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch wanasema wamepata ushahidi wa kununuliwa kwa vifaa vya ziada vyenye thamani ya takribani dola milioni 3. Shirika hilo limeonya kuwa mpango huo wa jumla jamala unaweza kutumiwa kama njia ya dola kuimarisha udhibiti wake wa kisiasa.
Hatua hii inakuja baada ya serikali ya China kuripotiwa kuwataka wakaazi wa Xinjiang kuwasilisha vipimo vya vinasaba, alama za vidole na sauti ili kuweza kupatiwa paspoti au ruhusa ya kusafiri nje ya nchi.
Mkoa wa Xinjiang unapakana na nchi kadhaa zenye machafuko katika eneo la Asia ya Kati, ikiwemo Afghanistan, ukiwa pia umeshuhudia mashambulizi ya mabomu na visu yanayotuhumiwa kufanywa na waasi wanaotaka kujitenga na China kutoka jamii ya Waislamu wa Uighur, ambao ni wachache nchini China.
Filed under: HABARI Tagged: China, DNA, human rights watch, Uighur, Xinjiang
